read

Aya 101- 103: Swala Ya Hofu

Maana

Swala haiachwi kwa hali yoyote; hata kwa maradhi, vita, au safarini. Anaitekeleza kila mwenye kukalifiwa na sharia kiasi cha uwezo wake; iwe ni kusimama au kukaa; akishindwa ataitekeleza hali ya kulala ubavu. Hata bubu pia ni wajibu kwake kutingisha ulimi wake na kuishiria kwa mkono wake badala ya kutamka. Ufafanuzi uko katika vitabu vya Fiqh.

Na mnaposafiri katika ardhi, si vibaya kwenu kama mkifupisha swala ikiwa mnaogopa kuwa wale waliokufuru watawaletea balaa.

Aya hii imeshuka katika hukumu ya jihadi na hofu; sawa na Aya zilizotangulia, kwani mfumo wa zote ni mmoja. Uwazi zaidi wa kuwa mfumo mmoja ni kauli yake Mwenyezi Mungu: Ikiwa mtaogopa kuwa wale waliokufuru watawaletea balaa. Kwa sababu makusudio ya balaa hapa ni kuua. Ama safari imekuja mahali pa aghalabu, sio kuwa ni sharti.

Ama kauli yake 'si vibaya kwenu' makusudio yake ni wajibu na lazima sio ruhusa na kuhalalisha. Kwa sababu Hadith zimefasiri ulazima; kama vile Aya ya Tawaf: "… Basi anayehiji katika nyumba hiyo, au kufanya umra, si vibaya kwake kuvizunguka (vilima) hivyo viwili." (2:158)

Kwa kuwa Aya imekuja katika Swala ya hofu si Swala ya kupunguza ya msafiri, basi makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu kufupisha Swala ni kupunguza idadi ya rakaa na kugeuza umbo la Swala, kulingana na dharura iliyopo.

Swala ya hofu ina sharti. Sharti lake muhimu ni kuwa upande wa maadui kuna nguvu zinazowawezesha kuhujumu na kuvamia. Ama aina yake, Shahid wa pili amesema katika Lum'a: ni nyingi zinazofikia kumi … inasihi kwa jamaa na kwa mmoja mmoja.

Ifuatayo ni namna ya Swala ya hofu kwa mtu pekee aliyoielezea mwenye Kitab Ash-sharai: "Ama Swala ya hofu ni mfano wa hali ya kufikia kuuana. Ataswali kiasi atakachoweza, iwe ni kwa kusimama, kwenda au kupanda.

Ataelekea Qibla kwa Takbira ya kuhirimia; kisha ataendelea ikiwezekana kuendelea, vinginevyo, ataelekea Qibla kwa itakavyowezekana kwake, na ataswali kwa udhuru wa kuelekea popote patakapomwezekania. Ikiwa hakuweza kushuka, ataswali akiwa amepanda na atasujudu juu ya kiti cha saruji yake; kama hakuweza basi ataashiria, kama atakuwa (anazidi) kuhofia basi ataswali kwa tasbih, bila ya kurukuu na kusujudu. Atasema badala ya kila rakaa "Subhanullah Wal-hamdulillaah wa Lailaha illa Ilah Wallahu Akbar."

Sura hii inatosha kuwa ni dalili kwamba Swala ni laizma, hasamehewi hata katikati ya mapigano na wala wakati wa kukata roho. Na kwamba mtu ataitekeleza kwa namna na hali yoyote atakavyoweza.

Na utakapokuwa kati yao, ukawasimamishia Swala, basi kundi moja miongoni mwao wasimame pamoja nawe na washike silaha zao.

Huu ni ubainifu wa Swala ya hofu ya jamaa. Maana yake, ukitaka Ewe Muhammad kuswali jamaa na wapiganaji, basi gawa makundi mawili: Moja liswali na wewe wakiwa na silaha zao; na la pili lisimame kulinda; kama ambavyo inaswihi jamaa pamoja na Mtume (s.a.w.); vile vile inaswihi pamoja na mtu mwingine.

Watakaposujudu na wawe nyuma yenu.

Yaani watakaposujudu wale wanaoswali na Mtume (s.a.w.), lisimame kundi linalolinda nyuma ya wenye kuswali.

Na lije kundi jingine ambalo halijaswali, waswali pamoja na wewe na washike hadhari yao na silaha zao.

Yaani baada ya kumaliza kundi la kwanza kuswali, kundi la pili lichukue mahali pa kundi la kwanza katika Swala na kundi la kwanza lichukue mahali pa ulinzi.

Wanataka wale waliokufuru lau kama nyinyi mwasahau silaha zenu na vifaa vyenu ili wawavamie mvamio wa ghafla.

Huu ni ubainifu wa hekima iliyofanya kuwekwa Swala ya aina hii. Hekima yenyewe ni kutopata fursa adui ya kuwavamia wakati wanaswali.

Wala hapana vibaya kwenu ikiwa mnaona udhia kwa sababu ya mvua au mkiwa wagonjwa kuweka silaha zenu.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuwaamrisha walioswali kuchukua silaha, akawapa ruhusa ya kuziacha ikiwa wanaona uzito wa kuzichukua kwa sababu ya mvua au ugonjwa, lakini Mwenyezi Mungu Mtukufu amewalazimisha wajilinde na wawe macho na adui asijewaingilia ghafla.

Mtakapomaliza Swala, basi mtajeni Mwenyezi Mungu kwa kusimama na kwa kukaa na kwa (kulala) ubavu.

Makusudio ya Swala hapa ni Swala ya hofu. Maana ni kuwa kumtaja Mwenyezi Mungu ni vizuri katika hali yoyote si katika Swala tu. Imam Ali (a.s.) amesema: "Amefaradhisha Mwenyezi Mungu katika ndimi zenu dhikri na akawausia takwa na akaijaalia ndio mwishilio wa haja yake kwa viumbe vyake."
Anasema Ibn Al-arabi katika Futuhatil-Makkiyya J.5: "Mwenye kumtaja Mwenyezi Mungu katika kisimamo chake kukaa kwake na kulala kwake, basi amekusanya yote."

Mtakapopata amani, basi simamisheni Swala; Hakika Swala kwa Waislamu ni faradhi iliyowekewa wakati maalum.

Yaani wakati wowote vita itakapotulia na hofu ikiwaondokea basi ni juu yenu kutekeleza Swala kwa wakati wake wala msipuuze.

Tumezungumzia kuhusu Swala na jinsi uislamu ulivyoipa kipaumbele, katika Aya zilizotangulia; kama vile (2: 238- 239).

Unaweza kuuliza: Aya imewajibisha Swala ya hofu, ambapo vita vilikuwa vya panga na mikuki. Lakini hivi sasa kuna maendeleo ya silaha za vita kiasi ambacho hatufahamu katika silaha za kuangamiza. Kwa hiyo si inapasa Swala ya hofu iondolewe kwa vile maudhui yake hayapo?

Jibu:Lililosababisha Swala hii ni hofu, bila ya kuangalia vita na ala zake, ziwe za zamani au za kisasa. Kwa hiyo ikipatikana kwa sababu zisizokuwa za vita, basi imejuzu kuifupiliza Swala kwa idadi ya rakaa na kwa aina.

Mwenye Al-jawahiri anasema: "Kukiwa na hofu ya mafuriko, wanyama, nyoka, moto au mengineyo, basi inajuzu kuswali Swala ya shida ya hofu. Kwa hiyo atapunguza idadi na namna. Kwa kukosekana tofauti katika sababu ya hofu iliyoruhusiwa. Kwani aliulizwa Imam Jafar as-Sadiq (a.s.) kuhusu anayehofia wanyama au wezi ataswali vipi? Akasema: "Atapiga Takbira na kuashiria."

Tunasisitiza tena kuwa Swala haiwezi kumwondokea mtu kwa hali yoyote. Na kwamba kila mtu anaitekeleza kwa namna anavyoweza katika maneno na vitendo. Akishindwa ataashiria, akishindwa kuashiria ataleta picha ya Swala moyoni mwake.

Wala msilegee katika kuwafuatia hao watu. Ikiwa mnaumia basi na wao wanaumia kama mnavyoumia nyinyi. Na nyinyi mwataraji kwa Mwenyezi Mungu ambayo wao hawayataraji. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi mwenye hekima.