read

Aya 104: Msilegee Katika Kuwafuata

Maana

Wala msilegee katika kuwafuatia hao watu. Ikiwa mnaumia basi na wao wanaumia kama mnavyoumia nyinyi. Na nyinyi mwataraji kwa Mwenyezi Mungu ambayo wao hawayataraji.

Lau kama Wahyi ungelishuka hivi sasa katika hali yetu na waisrael, basi usingezidi hata herufi moja ya Aya hii. Haja kubwa iliyopo sasa ya kupambana na adui huyu mwovu na fedhuli na kukomesha dhulma yake, ni kujifunga kibwebwe na kumtegemea Mwenyezi Mungu na sisi wenyewe na kutowasikiliza wakoloni wanaotaka kutunyonya; wanaofanya propaganda ili watudanganye tuache nguvu zetu.

Kumtetemekea adui tu kunampa faida na kunamsaidia, sikwambii kumwogopa. Kwa ajili hii ndipo Mwenyezi Mungu akatukataza kumwogopa adui wa Mwenyezi Mungu na wa ubinadamu kwa hali yoyote ilivyo na itakavyokuwa; na kutuamrisha udhabiti katika kupambana naye.

Vilevile ametuzindua kuwa tunamwumiza adui, kama anavyotuumiza, lakini sisi tuko zaidi kuliko yeye, kwa sababu sisi twamwamini na kumtegemea Mwenyezi Mungu. Ama Israel inawategemea wakoloni na ndugu zao mashetani walioitengeneza; wakawasheheni silaha na mali, wakawahimiza kufanya uchokozi na kuwa- saidia katika Umoja wa mataifa na katika Baraza la usalama.

Hapana shaka yoyote kuwa kama tukijitegemea na kuwa na msimamo imara wa ikhlasi na tukafanya juhudi zetu zote, kama alivyotuamrisha Mwenyezi Mungu Mtukufu, ushindi utakuwa wetu tu. Mwenyezi Mungu Mtukufu, katika Aya nyingine anasema: Wala msilegee na kutaka suluhu na nyinyi ndio mko juu na Mwenyezi Mungu yuko pamoja nanyi. (47:35) Waislamu wako juu kwa itikadi yao historia yao na uwezo wao. Nguvu hizo haziendi wala hazitakwenda bure. Kwa hiyo hapana budi kuwa athari zake zitadhihiri kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, iwe sasa au baadaye.

إِنَّا أَنْزَلْنَا إِلَيْكَ الْكِتَابَ بِالْحَقِّ لِتَحْكُمَ بَيْنَ النَّاسِ بِمَا أَرَاكَ اللَّهُ ۚ وَلَا تَكُنْ لِلْخَائِنِينَ خَصِيمًا {105}

Hakika tumekuteremshia Kitabu kwa haki ili upate kuhukumu baina ya watu kwa alivyokufahamisha Mwenyezi Mungu; wala usiwe mtetezi wa wenye kufanya hiyana.

وَاسْتَغْفِرِ اللَّهَ ۖ إِنَّ اللَّهَ كَانَ غَفُورًا رَحِيمًا {106}

Na muombe maghufira Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira Mwenye kurehemu.

وَلَا تُجَادِلْ عَنِ الَّذِينَ يَخْتَانُونَ أَنْفُسَهُمْ ۚ إِنَّ اللَّهَ لَا يُحِبُّ مَنْ كَانَ خَوَّانًا أَثِيمًا {107}

Wala usiwatetee wale ambao wamezihini nafsi zao. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi aliye haini mwenye dhambi.

يَسْتَخْفُونَ مِنَ النَّاسِ وَلَا يَسْتَخْفُونَ مِنَ اللَّهِ وَهُوَ مَعَهُمْ إِذْ يُبَيِّتُونَ مَا لَا يَرْضَىٰ مِنَ الْقَوْلِ ۚ وَكَانَ اللَّهُ بِمَا يَعْمَلُونَ مُحِيطًا {108}

Wanajificha kwa watu wala hawajifichi kwa Mwenyezi Mungu, na yeye yu pamoja nao walipokula njama usiku kwa maneno asiyoyapenda. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyajua vyema muyatendayo.

هَا أَنْتُمْ هَٰؤُلَاءِ جَادَلْتُمْ عَنْهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا فَمَنْ يُجَادِلُ اللَّهَ عَنْهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ أَمْ مَنْ يَكُونُ عَلَيْهِمْ وَكِيلًا {109}

Nyinyi ndio ambao mnawa- tetea katika maisha ya duniani, basi ni nani atakayewatetea kwa Mwenyezi Mungu siku ya Kiyama au ni nani watakayemtegemea?

وَمَنْ يَعْمَلْ سُوءًا أَوْ يَظْلِمْ نَفْسَهُ ثُمَّ يَسْتَغْفِرِ اللَّهَ يَجِدِ اللَّهَ غَفُورًا رَحِيمًا {110}

Na mwenye kutenda uovu au akadhulumu nafsi yake, kisha akaomba maghufira kwa Mwenyezi Mungu atamkuta Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira Mwenye kurehemu.

وَمَنْ يَكْسِبْ إِثْمًا فَإِنَّمَا يَكْسِبُهُ عَلَىٰ نَفْسِهِ ۚ وَكَانَ اللَّهُ عَلِيمًا حَكِيمًا {111}

Na mwenye kuchuma dhambi, basi anajichumia mwenyewe. Na Mwenyezi Mungu ni mjuzi mwenye hekima.

وَمَنْ يَكْسِبْ خَطِيئَةً أَوْ إِثْمًا ثُمَّ يَرْمِ بِهِ بَرِيئًا فَقَدِ احْتَمَلَ بُهْتَانًا وَإِثْمًا مُبِينًا {112}

Na mwenye kuchuma kosa au dhambi, kisha akamisingizia asiye na kosa, basi hakika amejitwika dhuluma na dhambi iliyo wazi.

وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّهِ عَلَيْكَ وَرَحْمَتُهُ لَهَمَّتْ طَائِفَةٌ مِنْهُمْ أَنْ يُضِلُّوكَ وَمَا يُضِلُّونَ إِلَّا أَنْفُسَهُمْ ۖ وَمَا يَضُرُّونَكَ مِنْ شَيْءٍ ۚ وَأَنْزَلَ اللَّهُ عَلَيْكَ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَعَلَّمَكَ مَا لَمْ تَكُنْ تَعْلَمُ ۚ وَكَانَ فَضْلُ اللَّهِ عَلَيْكَ عَظِيمًا {113}

Na lau si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yako na rehema yake, lingedhamiria kundi katika wao kukupoteza; wala hawazipotezi ila nafsi zao; wala hawatakudhuru na lolote. Na amekuteremshia Mwenyezi Mungu Kitabu na hikima na amekufunza uliyokuwa huyajui. Na fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yako ni kubwa.