read

Aya 105 - 113: Kuwatetea Wahaini

Maana

Mwenye kufuatilia tafsir, akachunguza Aya hizi na kufikiri vizuri maana yake atakubali kuwa zilishuka kuhusiana na mwislamu mmoja aliyeiba bidhaa, akamsingizia mtu asiyekuwa na hatia; na kwamba jamaa wa mwizi walimwendea Mtume (s.a.w.) na kujaribu kumkinaisha kwa mbinu mbalimbali wamkinge mtu wao kumwepushia janga la wizi; na kama hakufanya hivyo, basi mtu wao ataangamia.

Karibu Mtume aitikie maombi ya wapotevu hao lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alimlinda mchukuzi mwaminifu wa wahyi wake na mfikishaji wa sharia yake. Akamhifadhi na njama zao na kumfichulia uhakika. Akafichuka mwizi na kusal- imika yule aliyesingiziwa.

Inasemekana pia kuwa aliyesingiziwa alikuwa ni myahudi na mwizi ni ansari; na kwamba yeye baada ya kufichuka alikimbia na kujiunga na washirikina. Dhahiri ya Aya inafungamana kabisa na tukio hili. Ufuatao ndio ubainifu wake:

Hakika tumekuteremshia Kitabu kwa haki ili upate kuhukumu baina ya watu kwa alivyokufahamisha Mwenyezi Mungu.

Tunasema - Tukimwomba msamaha Mwenyezi Mungu - kwamba msemo huu unatoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa Mtume wake mtukufu ukiashiria aina ya lawama.

Kama kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu anamwambia: Nimekuchagua mimi mwenyewe, nikakuteremshia Qur'an ili uhukumu baina ya watu kwa lile unalojua kwa yakini kuwa ni hukumu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Sasa wadanganyifu wamekurubia kukuhadaa, lakini Mwenyezi Mungu amekulinda na walivyokupangia - kumtia hatiani asiye na makosa - kwa kukufichulia uhakika na njama zao.

Hakuna linalofahamishwa na hali hii zaidi ya kuwa kuhifadhiwa na dhambi (Isma) si jambo la kulazimishwa; kama urefu na ufupi; isipokuwa ni wasifu unaomwepusha huyo maasum kufanya haramu, ingawaje anaweza kufanya, na kumpa msukumo wa kufanya wajibu, ingawaje anaweza kuuacha.

Aya hii ni jibu na kubatilisha kauli ya wasemao kuwa Mtume ana hukumu kati- ka baadhi ya masuala kwa ijtihadi yake. Aya inaonyesha wazi kuwa yeye hahukumu ila kwa wahyi utokao kwa Mwenyezi Mungu. Zaidi ya hayo ni kwamba mwenye kujitahidi anapata na kukosa, na Mtume ni mwamuzi wa tofauti za wenye kujitahidi na kubainisha kosa la mwenye kukosea na usawa wa mwenye kupatia.

Wala usiwe ni mtetezi wa wenye kufanya hiyana.

Mtume hakuwatetea, na ni muhali kwa Mtume kuwatetea wanaofanya hiyana. Na kukatazwa kwake kutetea hakulazimishi kutokea hilo kwake, bali ni kwamba kukatazwa haramu kunatokea kabla ya kuifanya. Lau kungekuwa kunakuja baada ya kutokea lengo la kukatazwa basi litabatilika.

Unaweza kuuliza: Ikiwa kufanya haramu ni muhali kwa Mtume kutokana na kuhifadhiwa kwake na dhambi, kwa nini akakatazwa?

Jibu: Mwenyezi Mungu anaweza kuielekeza amri yake kwa Mtume wake kati- ka hali zote. Kwa sababu ni amri kutoka kwa aliye juu kwenda kwa aliye chini yake. Zaidi ya hayo, ni kwamba amri ya wajibu na katazo la haramu mara nyingi huelekea kwa Mitume kwa kuelewesha hukumu tu.

Na muombe maghufira Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.
Anasema Tabari katika Tafsir yake kuwa Mwenyezi Mungu amemwamrisha Mtume wake kuomba maghufira ya kusamehewa dhambi za kumtetea mhaini. Na sisi tunaomba maghufira kutokana na tafsir hii. Kwani Mtume (s.a.w.) - kama tulivyotangulia kueleza - hakumtetea mhaini. Kwa dalili ya Aya itakay- ofuatia (113):

Ama amri ya kutaka maghufira ya dhambi hailazimishi kupatikana dhambi, Tafsiri ya Aya tunavyoiona ni kuwa Mtume (s.a.w.) kwa kuwa ni mtu, anaweza akadhania vizuri jambo lisilostahiki; ikamdhihirikia hakika kwa njia ya wahyi au nyingine kabla ya kuchukua uamuzi wowote wa dhana yake nzuri. Ndipo Mwenyezi Mungu akamwamrisha kuomba maghufira kutokana na ile dhana nzuri iliyomtokea ambayo haikuwa mahali pake. Makusudio ni kujichunga na kujitoa shakani na kutotegemea lolote ila baada ya yakini.

Wala usiwatetee wale ambao wamezihini nafsi zao. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi aliye haini, mwenye dhambi.

Kwa dhahiri msemo unaelekezwa kwa Mtume (s.a.w.), lakini ulazima wake unamhusu kila aliye baleghe mwenye akili, hasa makadhi na mahakimu.

Ama waliozihini nafsi zao ni wale waliofanya dhambi na kuwasingizia watu wengine wasio na hatia; na mwenye kuwatetea basi yeye ni kama wao. Maana ya mtu kujihini yeye mwenyewe ni kujibebesha mzigo wa adhabu kwa kuharibu mambo ya wajibu na kufanya haramu.

Tumetangulia kueleza kuwa Mtume (s.a.w.) hakutetea wala hatawatetea wahaini, na Aya hii inatilia mkazo kauli yake: Wala usiwe ni mtetezi wa wenye kufanya hiyana; Vilevile inabainisha kuwa mwenye kumdhulumu mwingine amejidhulumu yeye mwenyewe na kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu atamwadhibu kila haini, mwenye kujidhulumu na anayewadhulumu wengine.

Wanajificha kwa watu wala hawajifichi kwa Mwenyezi Mungu, naye yu pamoja nao walipokula njama usiku kwa maneno asiyoyapenda.

Mfanya makosa huficha makosa na kujificha gizani asionekane na watu kwa kutaka sifa au kuogopa shutuma zao. Ambapo ilikuwa afanye kinyume - ajifiche na Mwenyezi Mungu - kama anaweza, na wala asijishughulishe na watu kabisa. Kwa sababu Mwenyezi Mungu peke yake ndiye mwenye kumiliki madhara na manufaa. Asiyekuwa Mwenyezi Mungu hawezi kumtosheleza binadamu na kitu chochote. Sifa za watu na shutuma zao ni maneno yanayok- wenda na upepo. Ikiwa kujificha na Mwenyezi Mungu hakuwezekani, basi kumtii ni lazima, sio pendekezo.

Nyinyi ndio ambao mnawatetea katika maisha ya duniani, basi ni nani atakayewatetea kwa Mwenyezi Mungu siku ya Kiyama au ni nani watakayemtegemeea?

Msemo unaelekezwa kwa watu wa yule mwizi mhaini. Kwa sababu wao peke yao ndio waliomtetea na kumgombea. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu - ambaye limetukuka neno lake - amewafahamisha kuwa kumtetea mhaini hakuwezi kumfaa mhaini siku atakayofichuliwa na Mwenyezi Mungu: "Na jitengeni leo enyi waovu" (36:59)

Na mwenye kutenda uovu au akadhullumu nafsi yake, kisha akaomba maghufira kwa Mwenyezi Mungu atamkuta Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

Huyo ndiye mwenye kutoka katika dhambi mwenye kuikiri na kutubia. Kama ambavyo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni mkali wa adhabu, basi pia ni mwenye kumghufiria mwenye kutubia, mwenye kumrehemu anayekimbilia kwake.

Kuna hadith inayosema: "Hakika Mwenyezi Mungu hachoki, mpaka mchoke; mkiacha naye huacha."

Yaani mkiacha kutubia dhambi naye huacha kusamehe. Kwa hiyo la sawa kwa wale waliomtetea mwenye hatia, ni kumzindua kutokana na kosa lake na kumpa nasaha ya kutubia, kama wangelikuwa ni wanasihi waumin wa kweli.
Katika Aya hizi nne kuna maneno ambayo hapana budi kuyafafanua ili ieleweke tofauti yake ambayo kwa dhahiri inaonekana kama ni moja tu inayokaririka:

Neno la kwanza ni dhambi, lilioko katika Aya ya 107, 111 na 112. La pili na la tatu ni uovu na kujidhulumu, yaliyo katika 111. La nne ni kosa, lililotajwa kati- ka Aya ya 112.

Maneno yote haya yanakusanya maana moja ambayo ni maasi. Tofauti ni kuwa uovu ni ule unaofanyiwa mtu mwingine, kujidhulumu ni kujiingiza katika madhara kwa kuacha wajibu au kutenda haramu na kosa ni lile linalofanywa bila ya udhuru wowote; kama vile mzembe asiyejua anayekosea kutekeleza wajibu kwa kutojua ingawaje ana uwezo wa kujifundisha. Hukumu yake ni kama hukumu ya mwenye kukusudia makosa. Kwa sababu amepuuza kufanya utafiti na kuuliza.

Na dhambi ni kufanya kosa pamoja na kujua na kung'angania kulifanya. Dhambi ni ujumla inakusanya uovu na kujidhulumu. Kwa hiyo maana yanakuwa: ‘Mwenye kutenda uovu au akadhulumu nafsi yake… mpaka mwisho " ni kuwa mwenye kumfanyia uovu mwingine kwa kumtukana au kupiga na mengineyo au kuifanyia nafsi yake tu; kama vile yamini ya uongo kisha akatubia, Mwenyezi Mungu humkubalia toba yake; kama vile hakufanya uovu wowote au kudhulumu.

Na maana ya Mwenye kuchuma dhambi, basi anajichumia mwenyewe. Ni kwamba mwenye kufanya dhambi, basi amejifanyia uovu mwenyewe, ni sawa awe amefanya uzembe kwa uovu huu yeye peke yake au alimfanyia mwingine.

Maana ya Mwenye kuchuma kosa au dhambi, kisha akamsingizia asiye na kosa, basi hakika amejitwika dhuluma na dhambi iliyo wazi, ni kuwa mwenye, kumsingizia mtu mwingine kwa kosa asilokuwa nalo, ataadhibiwa adhabu ya uzushi wa makusudi; ni sawa alifanya kosa hilo akamsingizia mwingine kwa makusudi, (hilo linafahamishwa na neno 'dhambi'), au hakulifanya yeye, lakini akamsingizia mwingine kabla ya kuthibitisha, (hilo linafahamishwa na neno 'kosa') Lengo ni kuwa haifai kwa yeyote kumbandika mtu mwingine jambo lolote, mpaka awe na yakini nalo kama jua.

Na lau si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yako na rehema yake, linged- hamiria kundi katika wao kukupoteza; wala hawazipotezi ila nafsi zao; wala hawatakudhuru na lolote.

Makusudio ya kundi ni wale waliomtetea mwizi; na dhamiri ya katika wao inawarudia watu wake na wasaidizi wake. Makusudio ya kukupoteza ni kukuhadaa kwa maneno ya makosa na masilahi. Wala hawazipotezi ila nafsi zao, kwa sababu kujaribu kupoteza kunalazimisha upotevu; na mwenye kupoteza ni mpotevu na ziada.

Maana kwa ujumla ni kuwa kundi katika wasaidizi wa mwizi na jamaa zake, walikula njama ya kukuhadaa na haki na kujaribu uwe upande wao katika kumwokoa mtu wao nawe ulikaribia kuwakubalia kwa yale mazuri waliyokudhihirishia, lakini Mwenyezi Mungu akakuhifadhi nao; akakufichulia njama zao na kurudisha vitimbi vyao kwao.

Aya hii ni jibu la wazi kwa wale wanaodai kwamba Mtume (s.a.w.) aliwatetea wahaini. Kwani kauli yake Mwenyezi Mungu "Na rehema yake" na "Wala hawatokudhuru na chochote," hazikubali taawili yoyote na shaka yeyote kuwa Mtume hakumtetea mwizi na mhaini. Na kwamba aliyefanya haya ni mwingine.

Na amekuteremshia Mwenyezi Mungu Kitabu na hikima na amekufunza uliyokuwa huyajui. Na fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yako ni kubwa.

Kitabu ni Qur'an na hekima ni utume. Ikiwa Mwenyezi Mungu amewajibisha Muhammad kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumfanya ni mwisho wa Mitume na bwana wa Mitume wote na kumfundisha asiyoyajua, basi ni wajibu kwa waarabu kumshukuru Muhammad kwa kuwa wamekuwa ni wenye kutajika baada ya ujinga wao wa wajinga. Vilevile wamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumjaalia mtukufu zaidi wa viumbe kuwa ametokana na wao sio kwa wengine.

لَا خَيْرَ فِي كَثِيرٍ مِنْ نَجْوَاهُمْ إِلَّا مَنْ أَمَرَ بِصَدَقَةٍ أَوْ مَعْرُوفٍ أَوْ إِصْلَاحٍ بَيْنَ النَّاسِ ۚ وَمَنْ يَفْعَلْ ذَٰلِكَ ابْتِغَاءَ مَرْضَاتِ اللَّهِ فَسَوْفَ نُؤْتِيهِ أَجْرًا عَظِيمًا {114}

Hakuna kheri katika siri zao nyingi, ila mwenye kuamrisha sadaka au wema au kusuluhisha watu. Na mwenye kufanya hayo kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, basi tutampa ujira mkubwa.

وَمَنْ يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِنْ بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَىٰ وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّىٰ وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا {115}

Na mwenye kumpinga Mtume baada ya kumdhihirikia yeye uongofu, na akafuata njia isiyokuwa ya wenye kuamini, tutamwelekeza alikoelekea na tumtie katika Jahannam na ndio marejeo maovu.