read

Aya 114 – 115: Siri Ya Kheri Na Ya Usuluhishi

Maana

Hakuna kheri katika siri zao nyingi, ila mwenye kuamrisha sadaka au wema au kusuluhisha watu.

Baada ya Mwenyezi Mungu kutaja katika Aya zilizotangulia wale wanaokula njama usiku ya kauli asizoziridhia na kuwatetea wahaini, sasa katika Aya hii anasema siri zao nyingi hazina kheri. Kwa hiyo dhamiri ya 'siri' zao' inawarudia hao waliotajwa katika Aya zilizotangulia, kwa dalili ya dhahiri ya mfumo, lakini katika maana inaenea kwa watu wote. Kwa vile sababu inayowajibisha ni ya ujumla, haihusiki na watu maalum wala kundi maalum.

Sadaka ni kutoa mali kwa masikini wahitaji. Kuwasuluhisha watu kunawaokoa na taabu nyingi na kuwaondolea matatizo. Na wema ni kila linalokubaliwa na akili na sharia kwa kuliona kuwa ni zuri. Ikiwemo elimu na mambo yote mazuri kama vile sadaka na kuimarisha udugu. Mwenyezi Mungu amehusisha kuy- ataja hayo mawili kwa kufahamisha umuhimu wake.

Arrazi anaema: "Mkusanyiko wa kheri zote umetajwa katika Aya hii." Na mkusanyiko zaidi umetajwa katika kauli yake Mwenyezi Mungu: "Hakika mwanadamu yumo katika hasara. Ila wale ambao wameamini wakatenda matendo mema, wakausiana haki, wakausiana kusubiri." (103: 2 - 3)

Unaweza kuuliza: Watu huwa wakifanya siri za biashara, kazi, kilimo, na nyinginezo katika mambo ya maisha, sasa je siri hii ni katika mambo yasiyokuwa na kheri?

Jibu: Siri hiyo ni kheri maadam iko katika mipaka ya sharia, na katika yale ambayo ni wajibu kisharia, kikawaida na kiakili. Nayo ni yale ambayo maisha hayatimii bila hayo.

Na Aya imeepuka aina hii ya siri na kuingilia wale wanofanya siri na kuwazungumzia watu; kama kawaida ya wasio na haki; hupoteza muda wao kwa porojo na kujishughulisha na yule ni zaidi na yule ni mchache. Tamko la nyingi katika Aya linafahamisha kuwa siri nyingi za watu hazina heri ila kama itawarudia faida na manufaa kwa namna fulani. Ama siri katika mambo ya maisha, Aya haikuelezea kwa uzuri au ubaya.

Na mwenye kufanya hayo kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, basi tutampa ujira mkubwa.

Kuamrisha mema ni vizuri, hilo halina shaka. Lakini mwenye kulifanya kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu sio kwa kuchuma, na kutaka jaha ni bora kuliko ambaye anaamrisha mema na kuyaletea falsafa kubainisha mazuri yake na faida zake, lakini hayafanyi, bali itakuwa ni hoja yenye nguvu na ya fasaha zaidi kwake. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Hakika sisi hatupotezi ujira wa anayefanya vitendo vizuri." (18: 30) Wala hakusema mwenye kauli nzuri.
Kuamrisha mema kuyatolea mwito ni nyenzo na kuyafanya ndio lengo. Mwenye kuamrisha na yeye mwenyewe akafanya, atakuwa katika waliomsaidia Mwenyezi Mungu kwa kauli yake: "Ni nani asemaye kauli bora zaidi kuliko alinganiaye kwa Mwenyezi Mungu na akafanya vitendo vizuri." (41: 33) Kwa hiyo kauli bora ni nzuri, na inazidi uzuri kama itaambatanishwa na vitendo.

Zaidi ya haya ni kwamba kauli hata kama kwa dhahiri itaambatana na athari za kiislamu; kama vile ndoa na mirathi, haziwezi kufahamisha imani sahihi, ila vitendo vizuri. Amesema Imam Ali Amirulmuminin (a.s.): "Imani inafahamisha mambo mema na mambo mema yanafahamishwa na imani."

Na mwenye kumpinga Mtume baada ya kumdhihirikia yeye uongofu, na akafuata njia isiyokuwa ya wenye kuamini, tutamwelekeza alikoelekea na tumtie katika Jahannam na ndio marejeo maovu.

Upinzani ni uadui na kila mwenye kumwasi Mwenyezi Mungu ni adui wa Mtume wa Mwenyezi Mungu. Amirul-muminin (a.s.) anasema: "Hakika mpenzi wa Muhammad ni mwenye kumtii Mwenyezi Mungu hata akiwa mbali naye (huyo Mtume) kwa nasabu, na hakika adui wa Muhammad ni yule mwenye kumwasi Mola hata kama akiwa karibu naye (mtume) kwa nasabu."

Adui wa Muhammad hapa ni kila ambaye imemdhihirikia haki, akaikana, akasimamishiwa hoja za kutosha, lakini pamoja na hayo akakanusha kwa inadi na kung’ang’ania mapenzi ya nafsi yake; kama anayejua kuwa uislamu ni haki au kuwa ni uongofu zaidi kuliko dini ya watu wake, lakini pamoja na hayo akang'a ng'ania dini ya mababu zake kwa kupupia masilahi yake ya kiutu au jaha.

Wafasiri wametaja kuwa Aya hii ilishuka kuhusu Bashir bin Ubairiq ambaye alisilimu kisha akartadi na kuungana na washirikina. Inajulikana kuwa ni desturi ya wafasiri kujipachikia sababu za kushuka Aya. Wanataja tukio lolote linaloambatana na zama za kushuka Aya ikiwa linanasibiana nayo.Na Aya hii inafungamana na kurtadi kwa Bashir na kila mwenye kupinga baada ya kum- bainikia uongofu.

Maana ya Tutamwelekeza alikoelekea ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) humtegemezea kila mtu kwenye lile alilolitegemea. Mwenye kujitukuza kwa mali, cheo, siha au ukoo, basi Mwenyezi Mungu huachana naye na kumwachia lile alilojitukuzia. Katika Hadiith Qudsi Mwenyezi Mungu anasema: "Naapa kwa utukufu wangu na enzi nitakatilia mbali matumaini ya kila anayem- tumainia mtu."

Aya hii inatujulisha yafuatayo:

i. Kauli yake Mwenyezi Mungu Tutamwelekeza alikoelekea ni wazi kuwa binadamu ana hiyari, si mwenye kuendeshwa.

ii. Kauli yake Mwenyezi Mungu Baada ya kumbainikia uongofu ni dalili kwamba mwenye kufanya utafiti wa ndani na usimbainikie uongofu basi huyo anasameheka; sawa na ambaye hakufikiliwa na mwito wowote, lakini kwa sharti ya kuwa awe ni mwenye kuelekea kuitafuta haki na kuitumia pale itakapomdhihirikia.

iii. Mtu ni mwenye kukalifiwa na yale anayoyafahamu kutokana na dalili, na wala hana jukumu la hali halisi ilivyo. Kinachotakiwa kwake ni kufanya utafiti tu, mpaka akate tamaa ya kupata dalili. Akipatia hali halisi baada ya utafiti huu, basi atakuwa na malipo mara mbili, na akikosea atakuwa na malipo mara moja; kama ilivyoelezwa katika Hadith.

iv. Yaliyoelezwa katika Tafsiri Razi kwamba Shafii aliulizwa kuhusu Aya ya Qur'an inayofahamisha kuwa Ijmai ni hoja? Akasoma Qur'an mara mia tatu mpaka akapata Aya isemayo: "Na akafuata njia isiyokuwa ya waumini."

Ambapo imefahamisha kuwa kufuata njia isiyokuwa ya waumini ni haramu, kwa hiyo basi kufuata njia ya waumini ni wajibu; na njia yao ni Ijmai yao juu ya jambo.

Hakuna linalofahamishwa na maelezo haya zaidi ya kuwa hakuna chimbuko la Ijmai katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu, kwa vile makusudio ya njia isiyokuwa ya waumini ni njia ya washirikina na wanafiki ambao wanampinga Mwenyezi Mungu na Mtume baada ya kuwabainikia wao uongofu. Kuongezea aliyoyasema Sheikh Muhammad Abduh:

"Ijma wanayokusudia ni kuafikiana mujtahiid wa umma huu baada ya kufa Mtume wake na Aya imeshuka zama za Mtume sio baada ya zama zake."

Inzi Kufia Kidondani

Ametaja mwenye Tafsir Al-manar kisa cha anyeathiriwa na hawaa ya nafsi kuliko uongofu. Tutakinukuu kwa faida ya msomaji, anasema: "Mtu mwenye hawa ya nafsi anashawishika na manufaa ya kidunia kwa udhaifu wa nafsi yake.

Kuna kisa kuwa Hajjaj aliandaa karamu ile ya 'nyote mwaalikwa'. Wakawa wanakula huku akiwaangalia, akamwona bedui mmoja anakula kwa umero sana. Lakini mara ilipokuja haluwa aliacha chakula na akairukia. Hajjaj akaamrisha muuaji wake atangaze kuwa atakayekula haluwa atakatwa shingo yake.

Ikawa bedui mara anamwangalia muuaji akipima uchungu wa mauti na ladha ya haluwa. Mara akamwelekea Hajjaj na kumwambia: "Nakuusia uwafanyie vizuri watoto wangu." (akiwa na maana kuwa atauliwa kwa kula haluwa) Akaishambulia haluwa kwa pupa sana kama mtu anayekula mlo wa mwisho maishani! Hajjajakamwachiliambali."

إِنَّ اللَّهَ لَا يَغْفِرُ أَنْ يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَنْ يَشَاءُ ۚ وَمَنْ يُشْرِكْ بِاللَّهِ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا بَعِيدًا {116}

Hakika Mwenyezi Mungu hasamehe kufanyiwa mshirika, lakini humsamehi yasiyokuwa hayo kwa amtakaye.Na anayemshirikisha Mwenyezi Mungu, basi hakika amepotea upotofu ulio mbali.

إِنْ يَدْعُونَ مِنْ دُونِهِ إِلَّا إِنَاثًا وَإِنْ يَدْعُونَ إِلَّا شَيْطَانًا مَرِيدًا {117}

Hamwabudu asiyekuwa yeye ila (Masanamu) ya kike na hawamwabudu ila Shetani Muasi.

لَعَنَهُ اللَّهُ ۘ وَقَالَ لَأَتَّخِذَنَّ مِنْ عِبَادِكَ نَصِيبًا مَفْرُوضًا {118}

Mwenyezi Mungu amlaani shetani. Naye alisema kwa hakika nitajifanyia katika waja wako fungu maalum.

وَلَأُضِلَّنَّهُمْ وَلَأُمَنِّيَنَّهُمْ وَلَآمُرَنَّهُمْ فَلَيُبَتِّكُنَّ آذَانَ الْأَنْعَامِ وَلَآمُرَنَّهُمْ فَلَيُغَيِّرُنَّ خَلْقَ اللَّهِ ۚ وَمَنْ يَتَّخِذِ الشَّيْطَانَ وَلِيًّا مِنْ دُونِ اللَّهِ فَقَدْ خَسِرَ خُسْرَانًا مُبِينًا {119}

Kwa hakita nitawapoteza na nitawatia tamaa. Na nitawaamrisha, watayakata masikio ya wanyama na nitawaamrisha wabadili umbile la Mwenyezi Mungu. Na mwenye kumfanya shetani kuwa mlinzi badala ya Mwenyezi Mungu basi amehasirika hasara ya waziwazi.

يَعِدُهُمْ وَيُمَنِّيهِمْ ۖ وَمَا يَعِدُهُمُ الشَّيْطَانُ إِلَّا غُرُورًا {120}

Anawaahidi na kuwatia tamaa; na shetani hawaahidi ila udanganyifu.

أُولَٰئِكَ مَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ وَلَا يَجِدُونَ عَنْهَا مَحِيصًا {121}

Hao makazi yao ni moto wa Jahannam wala hawatapata pa kuukimbia.

وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ سَنُدْخِلُهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۖ وَعْدَ اللَّهِ حَقًّا ۚ وَمَنْ أَصْدَقُ مِنَ اللَّهِ قِيلًا {122}

Na wale ambao wameamini na wakafanya matendo mema, tutawatia katika pepo zipitazo mito chini yake, watadumu humo milele, ndiyo ahadi ya Mwenyezi Mungu, na ni nani msema kweli zaidi ya Mwenyezi Mungu?