read

Aya 116 - 122

Maana

Hakika Mwenyezi Mungu hasamehe kufanyiwa mshirika, lakini hum- samehe yasiyokuwa hayo amtakaye.

Imetangulia Aya hii na maelezo yake katika kufasiri Aya 48 katika Sura hii. Hakuna tofauti yoyote kati ya nukuu mbili ila katika kumalizia ambapo huko imesemwa: "Na mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu hakika amezusha dhambi kubwa," na hapa ikasemwa: "Na mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu hakika amepotea upotevu wa mbali," maana ni moja tu.

Tena Kukaririka Katika Qur'an

Tumezungumzia kukaririka Qur'an katika kufasiri Aya 2; 48; sasa tunaunganisha na aliyoyasema mwenye Tafsiri Al-manar katika kufasiri Aya hii; "Qur'an sio kanuni wala si kitabu cha fani kinachotaja suala mara moja, bali ni Kitabu cha mwongozo.

Inakusudiwa uongozi kwa kuyaleta maana yanayotakiwa katika nafsi katika kila mfumo wa maneno unaoukubali maana ya makusudio.

Na hilo litatimia kwa kukaririka makusudio ya kimsingi; wala mwito wa kiujumla hauwi ila kwa kukaririka. Kwa hiyo ndio tunaona watu wa madhehebu za dini na wa siasa ambao wanajua desturi ya kijamii, tabia za watu na hulka zao, wanarudia khutba zao, malengo yao na makala zao wanazozisambaza katika magazeti yao na vitabu vyao."

Hawamwabudu asiyekuwa yeye ila( masanamu ) ya kike.

Waarabu kabla ya Muhammad (s.a.w.) walikuwa wakidai kwamba Malaika ni mabinti wa Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu anasema: Je, Mola wenu amewachagulia watoto wa kiume, na mwenyewe akajifanyia watoto wa kike katika Malaika?" (17:40)

Itikadi yao hii iliwapelekea kufanya masanamu waliyowapa majina ya wanawake; kama vile Lata, Uzza na Manata. Wakiwatia alama za Malaika waliodai kuwa ni mabinti wa Mwenyezi Mungu. Mwanzo walikuwa wakijikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kwa hayo masanamu.

Baada ya kupita vizazi masanamu hayo yakageuka kuwa Mungu anayeumba na kuruzuku. Na hivi ndivyo kulivyogeuka kuzuru makaburu - kwa waarabu na watu wote - kutoka kuwa ni kutukuza alama za Mwenyezi Mungu na kutukuza misingi ambayo amekufia aliyemo kaburuni, na kuwa ni itikadi ya kuwa ni nguvu ya juu inayoleta manufaa na kukinga madhara.

Na hawamwabudu ila muasi.

Yaani ibada ya washirikina kwa masanamu ilivyo hasa ni ibada ya shetani, kwa sababu yeye ndiye aliyewaamrisha hivyo, wakamtii. Yeyote mwenye kumtii mwingine na kufuata njia yake basi yeye ni mtumwa wake mwenye kuamrishwa naye.

Mwenyezi Mungu amlaani. Naye alisema kwa hakika nitajifanyia katika waja wako fungu maalum.
Maana ni kuwa shetani alimwambia Mwenyezi Mungu Mtukufu; Mimi nina fungu katika waja wako uliowaumba, na ukawaambia katika uliyowaambia: "Na sikuumba majini na watu ila waniabudu." (51: 56). Na kwamba fungu hili ni faradhi ya wajibu kwangu wanitii na kukuasi Unaweza kuuliza: Dhahiri ya Aya yaonyesha kwamba shetani ni kiumbe hasa na kwamba yeye anamwambia Mwenyezi Mungu kwa nguvu na kujiamini. Je maneno yako kwenye dhahiri yake au kuna taawili?

Jibu: Mwenye tafsir Al-manar kutokana na ustadh wake Sheikh Muhammad Abduh anasema kwamba kila mtu ana maandalizi ya kufanya kheri na shari na kufuata haki na batili. Maandalizi hayo Mwenyezi Mungu ameyaashiria katika kauli yake: "Na tukamwongoza njia mbili." (90:10)

Na kwamba fungu la wajibu la shetani kutoka kwa bindamu ni kujiandaa kwake na shari ambayo ni moja ya njia mbili. Kwa hiyo tamko la shetani ni fumbo la uandalizi huu.

Tumezungumza kuhusu makusudio ya neno shetani katika juzuu ya kwanza maelezo ya Audhubillahi … sio mbali kuwa kauli hii iliyokuja kwa lugha ya shetani, ‘Nitashika fungu la lazima,’ kuwa ni picha ya matukio ya waasi ambao maandalizi ya shari kwao yameshinda ya heri, na wala sio mazungumzo ya uhakika pamoja na Mwenyezi Mungu (s.w.t.)

Siasa Ya Shetani Na Sayansi

Mmoja aliwahi kusema kuwa fikra ya shetani ilitawala akili za watu pale elimu ilipokuwa ni mazungumzo tu yanayozungumzwa kwenye vikao vya kufundis- hana na misitari tu inayojaza kurasa za vitabu; wala haifikilii kwenye vitendo.

Ama leo fikra ya shetani imekuwa ni uzushi na ngano kwa tafsiri zake zote, baada ya kuwa elimu ni kipimo cha kila hakika, msingi wa kila hatua anayopiga binadamu, nguvu katika nyanja zote na uwezo unaokifanya chuma kipige marefu ya masafa ya mita katika ardhi, kuchimbua miamba ya dhahabu na kuruka angani mpaka mwezini na kwenye Merikh(mars) huku kikizungumza na watu wa ardhini wanoshuhudia safari yake.

Jibu: Hatudhani kuwa kuna yeyote anayeipuza elimu na faida zake na kwamba hiyo ni nguvu na ni utajiri vilevile na kuwa jinsi watu wanavyoihitajia ni sawa na vile mtu anavyohitajia maji na chakula. Lakini hakuna yeyote asiyejua kwamba elimu ni sawa na binadamu; ina maandalizi ya heri na shari na mara nyingine inaelekeza kwenye heri, ikazalisha chakula kwa walio na njaa, kuwavisha walio uchi na kuwatibu walio wagonjwa. Na mara nyingine inaelekeza kwenye shari; ikaua na kuvunja.

Shari ndiyo nguzo ya kwanza ya siasa ya shetani tunayemkusudia na leo elimu katika siasa, imekuwa inaelekeza kubomoa na kutawala na kunyonya. Fungu la shari au shetani - vyovyote utakavyoita - limezidi kwa maendeleo ya elimu (Sayansi).

Zamani wasaidizi wa shari walikuwa na silaha ya nguvu na viungo, ama hivi leo baada ya elimu kuwafikia wakorofi, basi wanachama wa shetani wanatumia silaha za tonoradi, na mabomu na mengineyo yanayotetemesha ardhi kutokea chini.

Kuna mahali nimesoma kwamba Amerika imeweka mpango wa kuwanunua machipukizi wa elimu popote ulimwenguni na kwamba dalali wake anayetembea aliwahi kufika Uingereza katika baadhi ya ziara zake na kukubaliana na wataalamu mia saba wahamie Amerika. Mbinu hizi wanazitumia wanasiasa wa Amerika kutengeneza vifaa vya kupiga ulimwengu wote na kutawala nguvu zake. Hawa ndio shetani adui wa Mwenyezi Mungu na wa binadamu.

Ama mashule ya kisasa yaliyoenea kila mahali, mengi ni katika fungu la shetani hamna chochote chenye mwelekeo wa dini na maadili mema. Hivi ndivyo zilivyoitikia akili kubwa na ndogo mwito wa shetani alioutangaza kwa kusema: Kwa hakika nitashika fungu la lazima katika waja waiko.

Kwa hakika nitawapoteza na nitawatia tamaa.

Shetani kumpoteza mtu ni kumpambia haki aione batili na kheri aione shari, au ampe dhana za kuwa hakuna haki wala heri katika kuwapo kwake wala hakuna pepo na moto na kwamba dunia ni ya mwenye kuimiliki, kama alivyosema Nietezshe1. Kuna hadith isemayo: Ibilis ameumbwa na umbo la kupendeza.

Ama kutia tamaa kwa shetani ni kumpa mawazo ya kupata anayoyatamani kutokana na muda mrefu na kuokoka siku ya hisabu na malipo na mengineyo katika matamanio ya uongo na ndoto za uokofu.

Na nitawaamrisha, watayakata masikio ya wanyama na nitawaamrisha wabadili umbile la Mwenyezi Mungu.

Makusudio ya wanyama ni ngamia, ng'ombe na kondoo. waarabu wakati wa Ujahiliya walikuwa wakiyakata masikio ya baadhi ya wanyama wao na kuyasimamisha kwenye masanamu halafu wanajiharamisha nao. Utakuja ufafanuzi wakati wa kufasiri (5: 103) Inshallah.

Baada ya kuwa shari au shetani akiwaamrisha wanachama wake wakati wa ujahiliya kukata masikio ya wanyama na kubadilisha umbile la Mwenyezi Mungu, hivi sasa amekuwa akiwaamrisha kutupa mabomu ya sumu (Napalm) kwa wanawake na watoto na kutupa mabomu ya Atomic huko Hiroshima na Nagasaki kwa ajili ya kumaliza viumbe vya Mwenyezi Mungu. Haya ni matokeo ya wanasiasa kutawala akili na elimu.

Na mwenye kumfanya shetani kuwa mlinzi badala ya Mwenyezi Mungu yaani akimtii - basi amehasirika hasara ya waziwazi. Ambapo anakuwa ni mateka wa matamanio na hawaa za nafsi na vilevile mateka wa njozi na uzushi.

Anawaahidi na kuwatia tamaa; na shetani hawaahidi ila udanganyifu.

Ambapo amewawekea kwenye njia ya maangamivu baada ya kuwadanganya kuwa ni uokofu. Kwa mfano, mzinifu au mnywaji pombe anaweza kuwa yeye anastarehe kwa ladha na kumbe ilivyo hasa anajitwisha madhara makubwa ya kidunia na akhera.

Hao makazi yao ni moto wa Jahannam wala hawatapata pa kuukimbia.

Yaani wanachama wa shetani katika washirikina na wafisadi hawataokoka na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Baada ya Mwenyezi Mungu kutaja kiaga kikali, alifuatisha na ahadi kama ilivyo desturi yake ilivyozoelekea - kukutanisha himizo na kitisho. Anasema Mwenyezi Mungu:

Na wale ambao wameamini na wakafanya matendo mema, tutawatia kati- ka pepo zipitazo mito chini yake, watadumu humo milele. Ndiyo ahadi ya Mwenyezi Mungu; na ni nani msema kweli zaidi ya Mwenyezi Mungu?

Katika Aya hii kuna masisitizo matatu: Umiliki, ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kweli na ni nani mkweli zaidi. Lengo la kukaririka huku ni kufahamisha kuwa ahadi ya shetani ni ya uongo, tamaa inayokwisha na amri zake ni batili; na kwamba kauli ya Mwenyezi Mungu ndiyo ya haki na ukweli na twaa yake ni heri na wema.

Unaweza kuuliza kuwa ahadi ya pepo mara nyingi katika Aya hukutanishwa na kudumu milele (Abadan) ambapo Aya nyingi za kiaga cha moto hukutanishwa na kudumu tu, je, kuna siri gani?

Jibu: Kudumu ni kukaa muda mrefu, inawezekana kuwa milele na inawezekana isiwe, mwenye kuingia peponi hatoki kwa hiyo inanasibu kusema milele.

Ama mwenye kuingia motoni anaweza kukatikiwa na adhabu na kuto- ka humo kwa hiyo ndio haikukutanishwa adhabu na umilele ila katika hali maalum; kama vile ushirikina na kuua makusudi.

لَيْسَ بِأَمَانِيِّكُمْ وَلَا أَمَانِيِّ أَهْلِ الْكِتَابِ ۗ مَنْ يَعْمَلْ سُوءًا يُجْزَ بِهِ وَلَا يَجِدْ لَهُ مِنْ دُونِ اللَّهِ وَلِيًّا وَلَا نَصِيرًا {123}

Si matamanio yenu wala matamanio ya watu wa Kitabu. Mwenye kutenda uovu atalipwa kwa ovu huo. Wala hatajipatia mlinzi wala msaidizi zaidi ya Mwenyezi Mungu.

وَمَنْ يَعْمَلْ مِنَ الصَّالِحَاتِ مِنْ ذَكَرٍ أَوْ أُنْثَىٰ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَأُولَٰئِكَ يَدْخُلُونَ الْجَنَّةَ وَلَا يُظْلَمُونَ نَقِيرًا {124}

Mwenye kufanya mema - mwanamume au mwanamke - hali ya kuwa ni mwenye kuamini, basi hao wataingia peponi wala hawatadhulumiwa hata kitobwe cha kokwa ya tende.
  • 1. Mwanafilosofia w Kijerumani (1844 - 1900)