read

Aya 123 - 124: Anayefanya Uovu Atalipwa

Maana

Aya mbili hizi zinaelezea msingi wa dhahiri ambao hakuna anayeweza kuutolea mjadala na kuuondoa au kuubadilisha mfumo wake kutokana na mabadiliko ya wakati au hali; wala pia hauhusiki na mwanamume peke yake au mwanamke tu. Msingi wenyewe ni "Mtu atalipwa amali zake ikiwa ni heri basi ni heri na ikiwa ni shari basi ni shari". Maana haya yamekaririka katika kitabu cha Mwenyezi Mungu kwa mifumo mbali mbali; kama vile katika Aya mbili hizi tulizo nazo.

Nyingine ni: "Ili Mwenyezi Mungu ailipe kila nafsi yale iliyoyachuma …" (14: 51) "Ili awalipe wale waliofanya ubaya kwa yale waliyo yafanya" (53:31)

Si matamanio yenu wala matamanio ya watu wa Kitabu.

Wakanushaji waliwaambia wale wanaowalingania kwenye imani kuwa ni sawa tu muwe mmetupa mawaidha au la, haya ni mambo ya zamani tu sisi hatu taadhibiwa. Mayahudi walisema hataingia ila aliye yahudi au naswara. mmoja katika waislamu alisema kuwa moto umeumbiwa wasiokuwa waislamu. Hivi ndivyo walivyo watu wote kufarahia dini waliyo nayo. Ndipo Mwenyezi Mungu akawajibu kwa kusema kwake:

Mwenye kutenda uovu atalipwa kwa uovu huo.

Vyovyote itakavyokuwa Mwenyezi Mungu hana nasaba wala sababu na yeyote, isipokuwa ikhlas na amali njema. Dalili tosha ya hilo ni kauli yake Mwenyezi Mungu: "… Hakika mtukufu wenu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule amchae Mungu zaidi katika nyinyi" (49:13)

Imam Jafar as-Sadiq (a.s.) amesema: "Hatukuwa sisi ila ni watumwa wa ambaye ametuumba na kutuchagua, Wallahi sisi hatuna hoja yoyote kwa Mwenyezi Mungu wala hatuwezi kumwepuka. Sisi tutakufa na tutasimama (mbele ya Mwenyezi Mungu) na tutaulizwa. Mwenye kuwapenda Ghulat ametuchukiza na mwenye kuwachukia ametupenda. Ghulat ni makafiri na mufawadhaa ni washirikina1 ."

Mwanamume Na Mwanamke

Mwenye kufanya mema - mwanamume au mwanamke - hali ya kuwa ni mwenye kuamini, basi hao wataingia peponi wala hawatadhulumiwa hata kitobwe cha kokwa ya tende.

Maadamu mke na mume wako sawa katika taklifa na kuchukua majukumu, basi inalazimika kuwa sawa katika malipo. Kama kuna tofauti kwa namna fulani, basi tofauti hiyo haisihi kwa hali yoyote katika malipo mema na mabaya.

Yametangulia maelezo katika kufasiri (2: 228) kifungu 'Mwanamume na Mwanamke katika sharia ya kiislamu. Kauli yake Mwenyezi Mungu: "Hali ya kuwa ni mwenye kuamini." Ni sharti la kuingia peponi; kama ilivyofafanuliwa katika Aya: "Basi hao wataingia peponi." Lakini sio sharti la malipo mengine ya amali njema. Kafiri akifanya amali njema kwa njia ya kheri kwa fahari au biashara, Mwenyezi Mungu atamlipa kwa sababu Mwenyezi Mungu ni mwadilifu hapotezi malipo ya mwenye kufanya amali njema. Kwa nini isiwe hivyo, na yeye ndiye aliyesema: "Hakuna malipo ya hisani ila hisan." (55: 60)

Si lazima malipo ya hisani kuwa ni pepo, inaweza kuwa malipo duniani au Akhera kwa kupunguziwa adhabu au kwa kutokuwa motoni wala peponi. Tumeyafafanua hayo katika kufasiri 3: 176 kifungu 'Kafiri na amali njema,' Pia katika kufasiri 4: 34.rejea.

وَمَنْ أَحْسَنُ دِينًا مِمَّنْ أَسْلَمَ وَجْهَهُ لِلَّهِ وَهُوَ مُحْسِنٌ وَاتَّبَعَ مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا ۗ وَاتَّخَذَ اللَّهُ إِبْرَاهِيمَ خَلِيلًا {125}

Ni nani mwenye dini nzuri kuliko yule aliyeusalimisha uso wake kwa Mwenyezi Mungu na akawa mwema na akafuata mila ya Ibrahim mwongofu? Na Mwenyezi Mungu amemfanya Ibrahim kuwa rafiki mwandani.

وَلِلَّهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۚ وَكَانَ اللَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ مُحِيطًا {126}

Na ni vya Mwenyezi Mungu vilivyo mbinguni na vilivyo ardhini; na Mwenyezi Mungu ni mwenye kukizunguuka kila kitu.
  • 1. Ghulat ni wale waliopetuka mpaka katika kumpenda Ali na kumfanya ni Mungu. Mufawawwidha ni wale wasemao kuwa vitendo vya binadamu viko chini ya uwezo wake sio wa Mwenyezi Mungu kinyume na Mujabbira waliosema kuwa binadamu analazimishwa na Mwenyezi Mungu katika vitendo vyake. Ama Ahlul-adl wanasema: Hakuna kulazimishwa wala kuachiliwa, lakini mambo yako baina ya mambo mawili.