read

Aya 125 – 126: Nani Mwenye Dini Nzuri

Maana

Na ni nani mwenye dini nzuri kuliko aliyeusalimisha uso wake kwa Mwenyezi Mungu naye akawa mwema.

Makusudio ya kusalimisha uso ni kusalimu amri, Maana ni kuwa, mkamilifu ni yule ambaye anamtarajia Mwenyezi Mungu wala hamtarajii asiyekuwa Mwenyezi Mungu na anafuata desturi alizoweka Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa viumbe vyake katika maisha haya.

Ni kwa hivi tu ndio mja atakuwa karibu na Muumba wake. Ama mwenye kuwanyenyekea waungu wa dunia kwa tamaa ya mali waliyonayo na jaha, basi hana chochote kwa Mwenyezi Mungu: hata kama atasimama kwa ibada usiku na kufunga mchana.

Na akafuata mila ya Ibrahim mwongofu.

Yaani akamfuata Ibrahim (a.s.) ambaye ameachana na kila yasiyokuwa ya Mwenyezi Mungu aliyewaambia watu wake: "… Je, mnanimhoji juu ya Mwenyezi Mungu na hali yeye ameniongoza? Wala siogopi wale mnaowashirikisha naye …" (6: 80)

Unaweza kuuliza Kwa nini Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: "Na akafuata mila ya Ibrahim na wala asiseme mila ya Muhammad?"

Jibu: Kwanza, mila ya Ibrahim na Muhammad ni kitu kimoja "Hakika watu wanaomkurubia zaidi Ibrahimu ni wale waliomfuata, na Mtume huyu na walioamini pamoja naye. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wa waumini." (3:68)

Pili, Utume wa Ibrahim umeafikiwa na dini zote, sio uislamu peke yake. Kwa hiyo kuutolea hoja kwa wasiokuwa waislam kutakuwa na nguvu zaidi, kama sikosei.

Na Mwenyezi Mungu amemfanya Ibrahim kuwa ni rafiki mwandani.

Mwenyezi Mungu amemhusu Ibrahim kwa cheo kikubwa kinakurubia kuwa zaidi ya unabii na utume. Imam Jafar as-Sadiq (a.s.) anasema: "Hakika Mwenyezi Mungu amemfanya Ibrahim ni mja wake kabla ya kumfanya Nabii na akamfanya nabii kabla ya kumfanya mtume na akamfanya mtume kabla ya kumfanya rafiki mwandani."

Na ni vya Mwenyezi Mungu vilivyo mbinguni na vilivyo ardhini.

Yeye ni mwenye kumiliki kila kitu mwenye kukiendesha kila kitu na mwenye kukizunguuka kila kitu.

Unaweza kuuliza kuwa maana haya yamekaririka katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu mara nyingi, je kuna siri gani?

Jibu: Siri ni kumzindua binadamu na kubaki daima kukumbuka kuwa Mwenyezi Mungu peke yake ndiye mwenye kuendesha ulimwengu, na kwamba amri yake ni yenye kupita humo na yeye binadamu daima yuko kwenye ujuzi wa Mungu, uweza na hekima yake. Nafsi itakapotambua hakika hii, itafanya matendo kulingana na aliyeiumba, kwa kufuata njia zake na kutii amri zake.

Zaidi ya hayo, kukaririka kunakuja kwa mnasaba unaohitajia, ambao mara nyingine wafasiri wanaweza kuutambua na mara nyingine wasiutambue. Nao hapa ni kwamba baadhi wanaweza wakafikiria kwamba Mwenyezi Mungu amemfanya Ibrahim rafiki; kama vile sisi tunavyowafanyia marafiki.

Ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akaondoa tuhuma hii, kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye Muumbaji mwenye kumiliki kila kitu na kwamba Ibrahim yuko chini ya milki yake, lakini yeye ni mja aliyechaguliwa, si kama waja wengine.

وَيَسْتَفْتُونَكَ فِي النِّسَاءِ ۖ قُلِ اللَّهُ يُفْتِيكُمْ فِيهِنَّ وَمَا يُتْلَىٰ عَلَيْكُمْ فِي الْكِتَابِ فِي يَتَامَى النِّسَاءِ اللَّاتِي لَا تُؤْتُونَهُنَّ مَا كُتِبَ لَهُنَّ وَتَرْغَبُونَ أَنْ تَنْكِحُوهُنَّ وَالْمُسْتَضْعَفِينَ مِنَ الْوِلْدَانِ وَأَنْ تَقُومُوا لِلْيَتَامَىٰ بِالْقِسْطِ ۚ وَمَا تَفْعَلُوا مِنْ خَيْرٍ فَإِنَّ اللَّهَ كَانَ بِهِ عَلِيمًا {127}

Wanakutaka fatuwa kuhusu wanawake, waambie Mwenyezi Mungu anawapa fatuwa kuhusu wao na yale msomewayo humu Kitabuni kuhusu mayatima wanawake, ambao hamuwapi walichoandikiwa, na mnapenda kuwaoa, na walio dhaifu katika watoto, na muwasimamie mayatima kwa uadilifu. Na heri yoyote muitendayo basi Mwenyezi Mungu anaijua