read

Aya 127: Wanakuuliza Kuhusu Wanawake

Maana

Mwanzoni mwa Sura Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametaja kidogo hukumu ya mwanamke na yatima, akafuatilia kwa kuwataja watu wa Kitabu, wanafiki na vita.

Kisha akarudi tena kutaja mwanamke na yatima na kutaja baadhi ya hukumu zao kwa kukamilisha hukumu ya familia, aliyoianzia Sura. Hii ndiyo njia ya Qur'an kuelezea jambo kisha kuingiza jambo jingine tena kurudia jambo la kwanza kwa makusudio ya kuathiri katika nyoyo na mengineyo yanayohitajia hekima na kuwachukulia upole waja.

Wanakutaka fatuwa kuhusu wanawake

Fatuwa ni kubainisha mushkeli. Yaani wanakutaka wewe Mtume wa Mwenyezi Mungu uwabainishie hukumu ya wanawake katika urithi, ndoa n.k.

Waambie Mwenyezi Mungu anawapa fatuwa kuhusu wao. Hii inafahamisha kwamba kuweka sharia ni kwa Mwenyezi Mungu peke yake; Mtume hana zaidi ila kufikisha. Imethibiti kwamba Mtume alipokuwa akiulizwa jambo ambalo hajateremshiwa wahyi alikuwa hajibu mpaka ateremshiwe wahyi.

Na yale msomewayo humu Kitabuni kuhusu mayatima wanawake.

Yaani Mwenyezi Mungu anawapa fatwa kuhusu wanawake vile vile Qur'an inawapa fatwa kuhusu hao wanawake.

Unaweza kuuliza kuwa kufutu Qur'an ni kufutu kwa Mwenyezi Mungu hasa. Kwa hiyo kuunganisha kati ya mawili hayo ni kuunganisha kitu chenyewe.

Jibu: Makusudio ya kufutu kwa Qur'an hapa ni yale yaliyotangulia kubainishwa mwanzo wa Sura.

Na makusudio ya kufutu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni yale aliyoyabainisha hapa kukamilisha yaliyotangulia. Kwa dhahiri ni kuwa kuunganisha kunafaa ikiwa kutakuwa na tofauti za mwelekeo fulani kama vile kutofautiana wakati au mahali pa jambo moja.

Ambao hamuwapi walichoandikiwa.

Yaani Mwenyezi Mungu na Qur'an inawabainishia hukumu ya wanawake ambao mliwazuilia fungu lao la urithi na mahari. Waarabu wakati wa ujahiliya walikuwa wakimdhulumu mwanamke na kumfanya kama bidhaa au mnyama.

Na mnapenda kuwaoa.

Mwanamume katika wao alikuwa akijichukulia yatima akiwa mzuri amempendezea humuoa, na kuila mali yake akiwa hakumpen- dezea humzuia asiolewe mpaka afe na achukue mali yake, mara nyingine humuua kwa lengo la kuchukua mali.

Na walio dhaifu katika watoto.

Yaani anawatolea fatwa pia kuhusu watoto wadogo ambao hamuwapi fungu lao la mirathi; na walikuwa hawamrithishi ila anayeweza kushika silaha. Ndipo Mwenyezi Mungu akalikataza hilo na akafanya fungu la mwanamume ni mara mbili zaidi ya mwanamke. Kwa hiyo hii ni kutilia mkazo ubainifu uliotangulia mwanzo wa Sura.

Na muwasimamie mayatima kwa uadilifu.

Yaani pia anawapa fatwa ya kuwasimamia mayatima kwa uadilifu wao wenyewe na mali zao. Kumpa kila mmoja katika wao haki yake kamili, awe mwanmume au mwanamke mdogo au mkubwa.

Na heri yoyote muitendayo - kuwatendea mayatima na wananwake – basi Mwenyezi Mungu anaijua.

Kwa ufupi maana ya Aya ni kuwa waislamu walimtaka Mtume kuwabainishia hukumu ya wanawake. Mwenyezi Mungu (s.w.t) akamwambia Mtume wake: waambie Mwenyezi Mungu amewabainishia sehemu ya hukumu hii na sasa anawabainishia sehemu nyingine, la muhimu kwenu ni kufanya uadilifu na kuitumia hukumu hiyo. Kisha akawabainishia Mwenyezi Mungu (s.w.t.), katika Aya inayofuatia hukumu ya mwanamke, anayehofia unashiza wa mumewe na kuachana na mumewe.

وَإِنِ امْرَأَةٌ خَافَتْ مِنْ بَعْلِهَا نُشُوزًا أَوْ إِعْرَاضًا فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِمَا أَنْ يُصْلِحَا بَيْنَهُمَا صُلْحًا ۚ وَالصُّلْحُ خَيْرٌ ۗ وَأُحْضِرَتِ الْأَنْفُسُ الشُّحَّ ۚ وَإِنْ تُحْسِنُوا وَتَتَّقُوا فَإِنَّ اللَّهَ كَانَ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرًا {128}

Ikiwa mke atahofia mumewe kuwa nashiza au kumtelekeza, basi hapana vibaya juu yao kusikilizana kwa suluhu; Na suluhu ni bora. Na nafsi zimewekewa mbele uchoyo. Na mkifanya wema na mkajihifadhi, basi Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa myatendayo.

وَلَنْ تَسْتَطِيعُوا أَنْ تَعْدِلُوا بَيْنَ النِّسَاءِ وَلَوْ حَرَصْتُمْ ۖ فَلَا تَمِيلُوا كُلَّ الْمَيْلِ فَتَذَرُوهَا كَالْمُعَلَّقَةِ ۚ وَإِنْ تُصْلِحُوا وَتَتَّقُوا فَإِنَّ اللَّهَ كَانَ غَفُورًا رَحِيمًا {129}

Wala hamtaweza kufanya uadilifu baina ya wanawake hata mkikamia. Basi msipondokee kabisa kabisa, mkamwacha (mwingine) kama aliyetundikwa. Na mkisikilizana na mkamcha Mungu, basi Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu

وَإِنْ يَتَفَرَّقَا يُغْنِ اللَّهُ كُلًّا مِنْ سَعَتِهِ ۚ وَكَانَ اللَّهُ وَاسِعًا حَكِيمًا {130}

Na watakaptengana, Mwenyezi Mungu atamtosheleza kila mmoja kwa wasaa wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa Mwenye hekima.