read

Aya 128 – 130: Unashiza Wa Mume

Maana

Ikiwa mke atahofia mumewe kuwa nashiza au kumtelekeza.

Unashiza unaweza kuwa kwa mke kwa kumnyima unyumba mumewe au kuto- ka nyumbani bila ya idhini ya mume.Yametangulia maelezo ya unashiza wa mke katika kufasiri Aya ya 34 ya Sura hii.

Pia unashiza unaweza kuwa kwa mume kwa kumuudhi mke na kuacha kumpa matumizi au kumnyima siku akiwa na mke zaidi ya mmoja. Aya hii inaelezea hofu ya mke kwa unashiza wa mumewe au kumtelekeza. Makusudio ya kutelekeza ni kumwepuka kwake kunakoonyesha kumchukia. Ama kwenda kwenye shughuli zake na matatizo yake, lazima mke amvumilie na kumstah- milia madamu hamchukii.

Basi hapana vibaya juu yao kusikilizana kwa suluhu.

Ikiwa mke anahofia kuwa unashiza wa mumewe utasababisha talaka au kuwa katika hali ya kufungika - si kuwa na mume wala kuachwa, basi hapana ubaya kwa mume wala kwa mke kuafikiana wenyewe au kupitia kwa mtu. Waafikiane na kusikilizana, kuwa mume aache kumnyima haki zake, ili abakie katika hifadhi yake na waishi maisha ya utulivu.

Na suluhu ni bora kuliko kutengana na talaka. Kuna Hadith isemayo: "Halali inayochukiza zaidi kwa Mwenyezi Mungu ni talaka."

Ni vizuri tueleze kuwa anachokitoa mke kwa ajili ya talaka si halali ila kwa kuridhia nafsi yake. Mwenyezi Mungu anasema: "… Kama wakiwatunukia kitu katika hayo mahari, basi kuleni kwa raha na kunufaika." (4:4)

Na nafsi zimewekewa mbele uchoyo.

Yaani uchoyo daima uko mbele katika nafsi haumwepuki hata wakati wa kutoa, ile hali ya jaka-moyo anayoihisi mtoaji na kuificha wakati wa kutoa ndio uchoyo wenyewe na makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu "na nafsi zimewekewa mbele uchoyo." Mke haiachi haki yake kwa urahisi wala mwanamume hasamehi badali. Tusisahau kuwa Aya tukufu imezungumzia matatizo ya unyumba. Ama ikiwa unyumba hauna matatizo hakuna lolote la kuwajibisha kutoa kitu bali hakuna kati ya mume na mke anayeona kuwa kitu ni chake.

Na mkifanya wema na mkajihifadhi basi Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa muyatendayo.

Huu ni mwito kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa mume na mke kufanya kila juhudi amfanyie wema mwenzake na ajichunge na sababu za kukosana na kutengana.

Wala hamtaweza kufanya uadilifu baina ya wanawake hata mkikamia.
Kufanya uadilifu baina ya wake kuko aina mbili: Kuna kule kunakowezekana, kama kufanya usawa katika matumizi na mazungumzo mazuri. Na kuna ambako kuko nje ya uwezo wa binadamu, kama vile mapenzi ndani ya moyo na hata kujamii pia. Mume anaweza kusisimuliwa na mke, kiasi ambacho yule mwingine hamsisimui vile.

Uadilifu baina ya wanawake unaotakiwa ni katika matumizi ambao uko chini ya uwezo. Ama uadilifu katika mapenzi na mfano wake, mtu hakalifishwi nao. Na hii ndiyo inayotofautisha baina ya Aya hii na ile Aya ya tatu katika Sura hii isemayo: " Na kama mkihofia kutofanya uadilifu, basi ni mmoja …"

Imam Jafar as-Sadiq anasema: "Ama kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Mkihofia kutofanya uadilifu’ anakusudia kutoa matumizi; na ama kauli yake; 'Hamtaweza' anakusudia mapenzi.” Na sisi ni katika wale wanaoamini kabisa kuwa hakuna kitu kigumu kukipata kuliko uadilifu.

Kwa hakika yake hasa na kiini chake ni kujikomboa na matamanio; kama ilivyoelezwa katika baadhi ya Hadith kwamba mwadilifu ni yule mwenye kuhalifu mapenzi yake na akamtii Mola wake. Wala hawi na haya ila aliyejitakasa.

Basi msipondokee kabisa kabisa.

Kwa mke mnayempenda na mwingine mkamnyima haki zake.

Mkamwacha (mwingine) kama aliyetundikwa akawa si mke aliyeolewa anayepata haki zake, wala si mtalikiwa anayeweza kuolewa na mwingine anayemtaka.

Na watakapotengana, Mwenyezi Mungu atamtosheleza kila mmoja kwa wasaa wake.

Inatakikana kabla ya chochote mume na mke wajaribu kuondoa tofauti zao na mambo yanayosababisha kutengana. Kwa sababu suluhu ni bora. Ikiwa hai- wezekani, basi talaka ni bora kuondoa madhara zaidi; na fadhila ya Mwenyezi

Mungu na riziki yake itawaenea wote, wawe pamoja au watengane. Mwenyezi Mungu anaweza kumpa mtalikiwa mume bora kuliko wa kwanza; na anaweza kumpa mtaliki mke bora kuliko wa kwanza.

Kwa ufupi ni kwamba yote yaliyotangulia yanazunguuka kwenye mzunguuko mmoja tu ambao ni "kushikana kwa wema na kuachana kwa wema." Kushikana ni bora ikiwa hakuna ufisadi na kuachana ni bora ikiwa kuna ufisadi; kama ambavyo Mwenyezi Mungu ameumba dawa ya kuponesha magonjwa ya mwili, vile vile ameweka dawa ya maradhi ya kijamii.

وَلِلَّهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۗ وَلَقَدْ وَصَّيْنَا الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ مِنْ قَبْلِكُمْ وَإِيَّاكُمْ أَنِ اتَّقُوا اللَّهَ ۚ وَإِنْ تَكْفُرُوا فَإِنَّ لِلَّهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۚ وَكَانَ اللَّهُ غَنِيًّا حَمِيدًا {131}

Ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini. Na hakika tuliwaamrisha waliopewa Kitabu kabla yenu na nyinyi kwamba, mcheni Mwenyezi Mungu. Na kama mkikufuru, basi ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na ardhini. Na Mwenyezi Mungu ni mkwasi mwenye kusifiwa.

وَلِلَّهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۚ وَكَفَىٰ بِاللَّهِ وَكِيلًا {132}

Na ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyo ardhini, na Mwenyezi Mungu atosha kuwa mlinzi.

إِنْ يَشَأْ يُذْهِبْكُمْ أَيُّهَا النَّاسُ وَيَأْتِ بِآخَرِينَ ۚ وَكَانَ اللَّهُ عَلَىٰ ذَٰلِكَ قَدِيرًا {133}

Akitaka atawaondolea mbali, enyi watu alete wengine. Na Mwenyezi Mungu ni muweza wa hilo.

مَنْ كَانَ يُرِيدُ ثَوَابَ الدُّنْيَا فَعِنْدَ اللَّهِ ثَوَابُ الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ ۚ وَكَانَ اللَّهُ سَمِيعًا بَصِيرًا {134}

Anayetaka malipo ya duniani, basi yako kwa Mwenyezi Mungu malipo ya duniani na akhera na Mwenyezi Mungu ni mwenye kusikia mwenye kuona.