read

Aya 131 – 134: Ni Vya Mwenyezi Mungu Vilivyomo Mbinguni Na Vilivyomo Ardhini

Maana

Ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini.

Katika juzuu ya kwanza na juzuu hii, tumezungumzia kuhusu kukaririka katika Qur'an. Sasa tutazungumzia kukaririka kwenye Aya hasa hii, kwa sababu ni Aya iliyotajwa na kurudiwa zaidi katika Qur'an.

Kisha tutadokeza kukaririka kwa namna maalum ambayo imetajwa kwa kunakiliwa mara mbili katika Aya moja na kurudiwa mara ya tatu katika Aya inayoifuatia moja kwa moja bila ya kuweko kati kitu kingine.

Ama sababu za kukarika kwake kwa ujumla ni kwamba maudhui yake ni ulimwengu ambao pamoja na vilivyomo ndani yake unatolea dalili kuwapo Mwenyezi Mungu na sifa zake; kama elimu, uweza, matakwa na hekima. Ni dalili inayokusanya aina za dalili zote na vyenye kutolewa dalili. Kwa hiyo kukumbuka Aya hii ni kukumbuka kuwapo Mwenyezi Mungu na utukufu wake.

Ama kutajwa kwake hapa mara tatu, ni ishara ya faida tatu:

1. Mwenyezi Mungu katika Aya iliyotangulia amesema: "… Atamtosheleza kila mmoja kwa wasaa wake" Kwa hiyo dalili hii imenasibiana na wasaa huu kuwa ni vyake vilivyomo mbinguni na ardhini.

2. Amesema: Kama mkikufuru basi ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini. Yaani yeye hamhitaji mwenye kukufuru kwa sababu vilivyomo mbinguni na ardhini ni vyake.

3. Amesema Mwenyezi Mungu: Ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini, na Mwenyezi Mungu atosha kuwa mlinzi. Akitaka atawaondelea mbali, enyi watu na alete wengine.

Makusudio ni kwamba Yeye ni muweza wa kuwamaliza waasi na kuwaleta watiifu; kwa sababu ni vyake vilivyomo mbinguni na ardhini. Kwa hiyo kila moja katika mara hizo tatu ina sababu yake na kukutanishwa na faida mpya.

Anayetaka malipo ya duniani, basi yako kwa Mwenyezi Mungu malipo ya duniani na akhera.

Yaani malipo ya duniani na akhera yanawezekana kupatikana pamoja na imani na takua. Mwenye kudhani kuwa malipo ya duniani hayawi pamoja na takua, basi huyo amekosea.

Kwa sababu hakuna kitu chochote kinachotengeneza vizuri maisha ya hapa duniani ila kitakuwa kinakubaliwa na dini bali kinaamr- ishwa na kuhimizwa na hiyo dini, lakini kwa sharti moja tu; kuwa kufanikiwa kwake kusiwe ni uovu kwa mwingine na utukufu wake usiwe ni utwevu wa mwingine.

Kwa hivyo malipo ya duniani na akhera hayagongani; isipokuwa kugongana kunatokea baina ya dhulma na malipo ya akhera - baina ya ghushi, hadaa na unyang'anyi na vilevile radhi za Mwenyezi Mungu, neema zake na pepo yake.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُونُوا قَوَّامِينَ بِالْقِسْطِ شُهَدَاءَ لِلَّهِ وَلَوْ عَلَىٰ أَنْفُسِكُمْ أَوِ الْوَالِدَيْنِ وَالْأَقْرَبِينَ ۚ إِنْ يَكُنْ غَنِيًّا أَوْ فَقِيرًا فَاللَّهُ أَوْلَىٰ بِهِمَا ۖ فَلَا تَتَّبِعُوا الْهَوَىٰ أَنْ تَعْدِلُوا ۚ وَإِنْ تَلْوُوا أَوْ تُعْرِضُوا فَإِنَّ اللَّهَ كَانَ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرًا {135}

Enyi mlioamini! Kuweni imara na uadilifu mtoao ushahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ijapokuwa ni juu ya nafsi zenu au wazazi wawili na jamaa wa karibu. Akiwa ni tajiri au fukara basi Mwenyezi Mungu anawastahiki zaidi. Basi msifuate hawaa ili mfanye uadilifu. Na mkiupotoa au mkaachana nao basi Mwenyezi Mungu ana habari ya myatendayo.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا آمِنُوا بِاللَّهِ وَرَسُولِهِ وَالْكِتَابِ الَّذِي نَزَّلَ عَلَىٰ رَسُولِهِ وَالْكِتَابِ الَّذِي أَنْزَلَ مِنْ قَبْلُ ۚ وَمَنْ يَكْفُرْ بِاللَّهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا بَعِيدًا {136}

Enyi mlioamini! Mwaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Kitabu ambacho amemteremshia Mtume wake na Kitabu alichokiteremsha kabla. Na mwenye kumkakataa Mwenyezi Mungu na Malaika Wake na vitabu vyake na siku ya mwisho, basi amepotea upotevu ulio mbali.