read

Aya 135 – 136: Kuweni Imara Na Uadilifu

Baina Ya Dini Na Watu Wa Dini

Sijaona Aya katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu inayoambatana na dini ila ninahisi umbali na tofauti iliyopo baina ya dini kama alivyoipanga katika Kitabu chake na dini kama tunavyoitekeleza sisi. Sisi tunazungumzia dini na kuitolea mwito kuwa imetoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba sisi hatuna lolote katika amri yake na ni watumwa wa dini, kama tulivyo watumwa wa Mungu.

Hayo ndiyo tuyatangazayo na kuyaeleza. Lakini dini tunavyoitangaza na tabia zetu tunazodai ni za kidini ni wapi na wapi! Na ni kinyume waziwazi. Na hii haifa- hamishi chochote zaidi ya kuwa sisi, kwa hakika na hali halisi ilivyo, ni wanafiki. Ni sawa tutambue hivyo au tusitambue.

Lau kama tutaifasiri dini kuwa Mwenyezi Mungu amelipa uwezo baraza la dini litunge sharia za halali na haramu, kama wanavyodai baadhi ya watu wa dini, basi hapo ingelikuwa dini inakwenda sambamba na tabia zetu. Ama tukisema kuwa dini ni ya Mwenyezi Mungu na inatoka kwa Mwenyezi Mungu, kisha tusiende sambamba na hayo katika tabia na vitendo vyetu, basi huo ni unafiki hasa.

Enyi mlioamini! Kuweni imara na uadilifu mtoao ushahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ijapokuwa ni juu ya nafsi zenu au wazazi wawili na jamaa wa karibu.

Katika Aya nyingine Mwenyezi Mungu anasema: " Na msemapo semeni kwa uadilifu hata kama ni jamaa wa karibu, Na tekelezeni ahadi ya Mwenyezi Mungu …" (6: 152)

Maana yake ni kuwa dini inatuhukumu sisi, baba zetu na watoto wetu; na kwamba ikitokea mgongano baina ya masilahi ya kiutu na dini, basi ni juu yetu kutanguliza ya dini; hata kama hili litapelekea kufa; kama alivyofanya Bwana wa mashahidi Husein bin Ali (a.s.)

Lau mtu atalinganisha hakika hii ya Qur'an na tabia zetu ataona kuwa sisi tunaathirika na masilahi yetu na masilahi ya watu wetu, kuliko masilahi ya dini. Na akiendelea kufanya utafiti zaidi ataamini kuwa kiini cha kwanza na cha mwisho cha dini kwetu ni masilahi na manufaa tu, si Kitabu cha Mwenyezi Mungu wala Sunna ya Mtume wa Mwenyezi Mungu.

Hivi ndivyo tulivyo au ndivyo walivyo wengi katika sisi, lakini hatutambui hili wala kulizindukia. Kwa sababu ubinafsi umetawala akili zetu na ukatengan- isha hali halisi zetu na nafsi zetu na kutuziba macho tusione haki. Pia imetupa ndoto ya kuwa dini ya Mwenyezi Mungu ni masilahi yetu hasa, vinginevyo si chochote.

Nayasema haya si kwa kumwekea nongwa yeyote au kuwa na msukumo wowote. Kwani mimi, kwa fadhila za Mwenyezi Mungu, sina haja na yeyote katika viumbe vyake Mwenyezi Mungu. Lakini hivi ndivyo ninavyohisi na wanavyohisi wengine wachunga haki.

Mimi nionavyo ni kuwa hakuna budi kuweko na marekebisho ya hisia hii; kama ambavyo ninaitakidi kuwa hakuna dawa ya ugonjwa huu ila kujituhumu sisi wenyewe; na ninaitakidi kuwa sisi ni wa kawaida tu kama wengine tuna hawaa na mapondokeo ambayo ni lazima tujihadhari nayo na tuyahalifu. Ninasema haya nikijua kuwa ni kama kupiga kelele za kutaka msaada jangwani. Kwa sababu ni kilio kutoka kwa nafsi zetu kwenda kwa nafsi zetu, ambazo ndizo adui mkubwa katika maadui zetu.

Akiwa tajiri au fukara basi Mwenyezi Mungu anwastahiki zaidi.

Kila mtu katika wanadamu ana hali ya kukubali heri na shari wakati huo huo anaumbile la kuchagua heri kuliko shari, kiasi ambacho lau ataachwa na umbile lake, angelifanya lile analoitakidi kuwa ni heri; wala hawezi kuiepuka ila kwa sababu za nje ya dhati yake na maumbile yake.

Wanavyuoni wa elimu ya sifa za Mwenyezi Mungu wametolea dalili hakika hii kwamba mwenye akili lau atahiyarishwa baina ya kusema uongo apewe pesa, basi angelichagua ukweli kuliko uongo.

Kwa hiyo mwenye akili hasemi uongo ila kwa sababu; kama vile hofu, tamaa, kupendelea jamaa wa karibu, kuchukia adui, kuwahurumia mafukara au kujipendekeza kwa tajiri. Na amesema mkuu wa wasemaji; Akiwa - wenye kushuhudiwa - ni tajiri au fukara, basi Mwenyezi Mungu anawastahiki zaidi. Yaani kwamba yeye ni mwenye kurehmu zaidi mafakiri kuliko sisi na ndiye anayejua maslahi yake na maslahi ya tajiri. Sisi wajibu wetu ni kusema haki tu ni sawa iwe itawasaidia au la.

Ingawaje Mwenyezi Mungu hakutaja sababu zinazosababisha kupotoka zaidi ya kustahiki tajiri au kumuhurumia fakiri, lakini sababu ni ya kiujumla. Haki inapaswa kufuatwa hata kwa maadui wa dini.

Basi msifuate hawaa ili mfanye uadilifu.

Yaani, mtakuwa watu wa uadilifu kwa kuacha hawaa na kwenda kinyume nayo. Imesemekana kuwa tafsiri yake ni kukadiria kuchukia kwa maana ya msifuate hawaa mkaacha uadilifu. Yaani nyinyi mnafuata mapenzi kwa kuchukia uadilifu na kwamba Mwenyezi Mungu amewakataza hilo. Lakini tafsiri ya kwanza ndiyo iliyo karibu zaidi.

Uadilifu

Wamehitalifiana mafakihi katika maana ya uadilifu na wakarefusha maneno. Kuna katika wao mwenye kusema, ni dhahiri ya uislam bila ya kudhihirisha ufasiki, Mwingine akasema, ni tabia iliyomo ndani ya nafsi inayopelekea kufanya wajibu na kuacha haram, wa tatu akasema, ni sitara na kujistahi, wa nne akasema ni kuacha madhambi makubwa na kutoendelea na madogo.

Katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Msifuate hawaa ili mfanye uadil- ifu." Ni kuonyesha kuwa uadilifu ni kuhalifu hawaa. Amirul-muminin Ali (a.s.) alimsifu ndugu yake, kwa Mwenyezi Mungu, katika aliyomsifu kuwa; "Alikuwa akijiwa ghafla na mambo mawili huangalia lipi lililo karibu zaidi na hawaa kisha akalikhalifu."

Na akasema: "Mwanzo wa uadilifu wake ulikuwa ni kukanusha hawaa ya nafsi yake." Amesema Mjukuu wake, Imam Jafar as-Sadiq: "Ama katika mafaqih atakayekuwa anaichunga nafsi yake, mwenye kuihifadhi dini yake, mwenye kukhalifu hawaa yake, mwenye kutii amri ya Mola wake basi ni juu ya watu kumfuata."

Na mkiupotoa au mkaachana nao basi Mwenyezi Mungu ana habari ya myatendayo.

Yaani msicheleweshe au kuacha kutoa ushahidi. Kisha akatoa tisho na kiaga kwamba mwenye kuyafanya hayo Mwenyezi Mungu anamjua na atamwadhibu.
Enyi mlioamini! Mwaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Kitabu ambacho amemteremshia Mtume wake na Kitabu alichokiteremsha kabla.

Mtu anaweza kuamini Muumbaji na kukanusha utume na vitabu vya Mwenyezi Mungu. Na anaweza akakubali utume wa baadhi na baadhi ya vitabu; au kukanusha kuwapo Malaika au Siku ya Mwisho.

Aya hii imebainisha nguzo za imani ambazo ni wajibu kuzikubali kila mwenye kuacha shirki na ulahidi na kuziamini zote sio baadhi ya sehemu zake. Nguzo zenyewe ni kumwamini Mwenyezi Mungu na mitume yake yote, vitabu vyake na Malaika wake na pia Siku ya Mwisho.

Kwa hiyo makusudio ya neno 'wale walioamini,' ni wale walioacha ushirikina na ulahidi. 'Na wale walioamini' la pili ni imani ya uhakika, sio kudumu imani na kuthibiti kwenye imani kama walivyosema wafasiri, Makusudio ya Mtume wake, ni Muhammad (s.a.w.). Na Kitabu ambacho amemteremshia Mtume wake ni Qur'an na Kitabu alichokiteremshia kabla, ni kila Kitabu cha Mwenyezi Mungu alichokiteremsha kabla ya utume wa Muhammad (s.a.w.)

Na mwenye kumkakataa Mwenyezi Mungu na Malaika waake na vitabu vyake na Siku ya Mwisho, basi amepotea upotevu ulio mbali.

Aya hii ni dalili wazi kwamba kuamini ghaibu ni nguzo katika nguzo za Kiislamu na kwamba asiyeamini si Mwislamu. Umetangulia mfano wa Aya hii pamoja na tafsiri yake katika sura 2: 285.

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا ثُمَّ كَفَرُوا ثُمَّ آمَنُوا ثُمَّ كَفَرُوا ثُمَّ ازْدَادُوا كُفْرًا لَمْ يَكُنِ اللَّهُ لِيَغْفِرَ لَهُمْ وَلَا لِيَهْدِيَهُمْ سَبِيلًا {137}

Hakika wale walioamini kisha wakakufuru kisha wakaamini kisha wakakufuru kisha wakazidi kukufuru, hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwaghufiria wala kuwaongozea njia.

بَشِّرِ الْمُنَافِقِينَ بِأَنَّ لَهُمْ عَذَابًا أَلِيمًا {138}

Wape bishara wanafiki kuwa wana adhabu iumizayo.

الَّذِينَ يَتَّخِذُونَ الْكَافِرِينَ أَوْلِيَاءَ مِنْ دُونِ الْمُؤْمِنِينَ ۚ أَيَبْتَغُونَ عِنْدَهُمُ الْعِزَّةَ فَإِنَّ الْعِزَّةَ لِلَّهِ جَمِيعًا {139}

Ambao huwafanya makafiri ndio marafiki badala ya waumini. Je wanataka kwao utukufu? Basi hakika utukufu wote ni wa Mwenyezi Mungu.