read

Aya 137 - 139: Hawathibiti Kwenye Ukafiri Wala Imani

Lugha

Asili ya neno Bishara ni habari njema za kufurahisha ambazo zinadhihirisha furaha katika ngozi bashar (bashar) ya uso. Mtu akimwambia mwenzake nakupa bishara basi anajua kuwa kuna jambo la kufurahisha. Halitumiwi neno hilo katika jambo la kuchukiza ila pamoja na kukutana na neno jingine, kama vile kauli yake Mwenyezi Mungu: Wape bishara wanafiki kuwa wana adhabu iumizayo.

Maana

Hakika wale walioamini kisha wakakufuru kisha wakaamini kisha wakakufuru kisha wakazidi kukufuru, hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwaghufiria wala kuwaongozea njia.

Mtu anaweza kuamini dini yoyote miongoni mwa dini au itikadi yoyote katika itikadi. Hapo atashikilia na kujadiliana na watu wa dini nyingine au fikra nyingine kwa ajili ya dini yake. Kisha anasoma na kufanya utafiti ikambainikia makosa. Anaachana na fikra yake ya kwanza na kujiunga na watu wema ambao jana walikuwa ni katika maadui zake wakubwa.

Ni juu ya hawa kumkubali na kumpokea; wala hakuna haki yoyote ya kumwaibisha na kupinga mageuzi yake ya kufuata njia sahihi iliyomdhihirikia. Bali ni wajibu kumsifu na kumtukuza, kwa sababu mtu kuacha makosa ni utukufu na kuendelea nayo ni udhalilifu.

Hii ni ikiwa atathibiti na kudumu kwenye imani yake mpya. Ama akigeuka na kurudia sera yake ya kwanza, kisha akarudi tena, akarudia… Akafanya hivi mara nyingi. Huyu ni wajibu kumtoa na kumtupa. Bali ni wajibu kumwadhibu kwa adhabu kali. Hii ndiyo hali waliyokuwa nayo watu wa dini na wakuu wa madhehebu ya kisiasa tangu zamani na sasa. Kwa sababu kugeukageuka kwake huku kunafahamisha tu, kuwa yeye anafanya masihara na vitimbi na ni mzushi mwongo anayejiingiza katika ufisadi na upotevu na kuzidisha dhambi na upotevu kila anapoingia na kutoka.

Huyu na mfano wake ndio wanaokusudiwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu anaposema: "…Walioamini kisha wakakufuru kisha wakaamini kisha wakakufuru kisha wakazidi kukufuru " Kwa sababu ya mchezo huu na kujigeuzagueza, Mwenyezi Mungu hakuwa ni mwenye kuwasamehe maadam wanayumbayumba na kugeukageuka baina ya ukafiri na imani; wala kuwaongozea njia kwa sababu wamepotea njia kwa kuchagua uovu baada ya kuijua njia na kuifuata.

Kwa ufupi ni kwamba muumin ni yule anayethibiti kwenye imani yake hata hali ikigeuka vipi. Ama yule anayertadi mara kwa mara, basi yeye ana hali mbaya kuliko yule aliyethibiti katika ukafiri na ulahidi.

Wape bishara wanafiki kuwa wana adhabu iumizayo.

Razi anasema: "Mwenyezi Mungu ametumia neno 'bishara' kwa adhabu kwa istihzai sawa na msemo: 'salaam zako ni kipigo."

Ilivyo, ni kwamba mfumo wa Qur'an uko mbali na stihzai. La karibu zaidi ni kwamba makusudio ya bishara ni habari tu na inawezekana kulitumia neno hilo katika jambo la kuchukiza kwa kuambatana na jambo lenyewe; kama tulivyotangulia kueleza katika kifungu cha lugha.

Ambao huwafanya Makafiri ndio marafiki badala ya waumini. Je, wanataka kwao utukufu, basi hakika utukufu wote ni wa Mwenyezi Mungu.

Kila mmoja katika sisi anataka atajike katika maisha haya. Baadhi ya watu wanaweza kupupia kutaka umashuhuri kwa kufanya wema au kwa elimu. Lakini wengine hutaka utukufu na umashuhuri kwa kitu chochote kitaka- chokuwa; wanauza dini yao kwa shetani kwa ajili ya kupata umashuhuri; hum- fanya shetani ndio rafiki wa kumsikiliza na kumtii.

Ndipo hapa likaja swali la kusuta na kukanusha kutoka kwa Mola mtukufu kuwa je, wanataka utukufu kutoka kwa shetani na marafiki zake wadhalilifu. Je, utukufu unaweza kupatikana bila ya imani na takua? Uislamu kwa utukufu wake umedhalilisha dini zote, vipi utukufu utatafutwa kwa mwenye kuukanusha?

Waumini waliokusudiwa na Mwenyezi Mungu katika kauli yake "badali ya wau- mini" ni wale ambao uislamu umetukuka kwa ajili yao. Kwa sababu wao wameutukuza na kuuweka juu kwa jihadi yao na kujitolea kwao mhanga. Tumezungumzia kuhusu kuwafanya marafiki makafiri katika tafsir (3: 28)

وَقَدْ نَزَّلَ عَلَيْكُمْ فِي الْكِتَابِ أَنْ إِذَا سَمِعْتُمْ آيَاتِ اللَّهِ يُكْفَرُ بِهَا وَيُسْتَهْزَأُ بِهَا فَلَا تَقْعُدُوا مَعَهُمْ حَتَّىٰ يَخُوضُوا فِي حَدِيثٍ غَيْرِهِ ۚ إِنَّكُمْ إِذًا مِثْلُهُمْ ۗ إِنَّ اللَّهَ جَامِعُ الْمُنَافِقِينَ وَالْكَافِرِينَ فِي جَهَنَّمَ جَمِيعًا {140}

Na amekwisha wateremshia katika Kitabu hiki kwamba mtakaposikia Aya za Mwenyezi Mungu zinakanushwa na kuchezwa shere, basi msikae pamoja nao mpaka waingie katika mazungumzo mengine. Hivyo hakika nyinyi mtakuwa mfano wao. Hakika Mwenyezi Mungu atawakusanya wanafiki na makafiri wote katika Jahannam.

الَّذِينَ يَتَرَبَّصُونَ بِكُمْ فَإِنْ كَانَ لَكُمْ فَتْحٌ مِنَ اللَّهِ قَالُوا أَلَمْ نَكُنْ مَعَكُمْ وَإِنْ كَانَ لِلْكَافِرِينَ نَصِيبٌ قَالُوا أَلَمْ نَسْتَحْوِذْ عَلَيْكُمْ وَنَمْنَعْكُمْ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ ۚ فَاللَّهُ يَحْكُمُ بَيْنَكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ وَلَنْ يَجْعَلَ اللَّهُ لِلْكَافِرِينَ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ سَبِيلًا {141}

Ambao wanawangojea mkipata ushindi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, huseme: Je hatukuwa pamoja nanyi. Na ikiwa Makafiri wamepata sehemu, husema: hatukuwa ni waweza wa kuwashinda tukawakinga na waumin? Mwenyezi Mungu atahukumu baina yenu siku ya kiyama na Mwenyezi Mungu hatawafanyia makafiri njia ya kuwashinda waumini.