read

Aya 140 – 141: Msikae Nao Mpaka Waingie Katika Uzungumzi Mwingine

Maana

Na amekwisha wateremshia katika Kitabu hiki kwamba mtakaposikia Aya za Mwenyezi Mungu zinakanushwa na kuchezwa shere, basi msikae pamoja nao mpaka waingie katika mazungumzo mengine.

Aya hii ilishuka Madina, inawakumbusha waislamu Aya iliyoshuka Makka isemayo: "Na unapowaona wale ambao wanaziingilia Aya zetu, basi jitenge nao mpaka waingie katika mazungumzo mengine; na kama shetani akikusahaulisha, basi usikae baada ya kukumbuka pamoja na watu wadhalimu." (6:68)

Ama sababu ya ukumbusho huu ni kuwa baadhi ya Waislamu - kama ilivyoelezwa Katika Tafsiri mbali mbali - walikuwa wakikaa katika vikao vya washirikina huko Makka waliokuwa wakingilia kumtukana Muhammad (s.a.w.) na kuicheza shere Qur'an. Waislamu wakati huo walikuwa wanyonge hawawezi kuwakanya; ndipo ikashuka Aya hiyo (6: 68), kuwahadharisha wais- lamu waepukane na washirikina na kuwaamrisha wasikae nao wanaposikia kufru na kuchezwa shere Aya za Mwenyezi Mungu.

Siku zikapita na waislamu wakahamia Madina; huko nako kulikuwa na mayahudi na wanafiki, waliodhihirisha uislamu na kuficha ukafiri. Baadhi ya waislamu wakarudia mwenendo wao wa kwanza, wakakaa na mayahudi na wanafiki waliokuwa wakiutusi uislamu na Mtume wake; ndipo ikashuka Aya hii, ambayo tunaifasiri, ili kuwakumbusha waislamu Aya ile iliyoshuka Makka na kuwaamrisha kujitenga nao.

Sababu yoyote ya kushuka Aya itakavyokuwa au wanaoambiwa, itakuwa Aya ni ya ujumla inayofahamisha wajibu wa kujitenga na kila mwenye kuingia kati- ka mazungumzo ya batili. Wajibu huu hauhusiki na ambaye alikuwa akikaa na makafiri Makka au na wanafiki Madina tu, ingawaje iko katika kuhusika si kwa ujumla. Hadith inasema: "Upweke ni bora kuliko rafiki mwovu." Nyingine inasema: "Tahadharini na kukaa na maiti." Akaulizwa ni akina nani hao maiti? Akasema: ni kila mwenye imani potofu, dhalimu katika hukumu”. Katika Nahjul Balagha imeelezwa: "Kukaa na watu wapuuzi kunasahaulisha imani na kumkurubisha shetani."

Hivyo hakika nyinyi mtakuwa mfano wao

Mwenye kuridhia ukafiri ni kafiri, na mwenye kurdhia dhambi naye ana dham- bi kwa namna yoyote atakayokuwa; kwa maafikiano ya mafakihi na Maulama. Imekuja Hadith Mutawatir isemayo: Mwenye kufanya dhulma, mwenye kumsaidia na mwenye kuiridhia ni washirika," hasa mwenye kuridhia ukafiri. Katika Nahjul-Balagha imeelezwa: "Mwenye kuridhia vitendo vya watu ni kama mwenye kuingia ndani yake na kila mwenye kuingia ana dhambi mbili: dhambi ya kutenda na dhambi ya kuridhia."

Hakika Mwenyezi Mungu atawakusanya wanafiki na makafiri wote katika Jahannam. Ambao wanawangojea mkipata ushindi kutoka kwa Mwenyezi Mungu husema; Je, hatukuwa pamoja nanyi? Na ikiwa makafiri wamepata sehemu, husema: hatukuwa ni waweza wa kuwashinda tukawakinga na waumin.
Aya hii inachora picha ya hali ya wanafiki wakati wa vita vya waislamu na washirikina. Kwa ufupi picha yenyewe ni kwamba wanafiki walikuwa wakitoka pamoja na waislamu katika kwenda vitani ili wakaharibu na kuchafua safu za waislam.

Wakati huo huo wanajionyesha kuwa wao wametoka kuwasaidia waislam; na kungoja, ikiwa ushindi ni, waislamu wakisema 'sisi tuko pamoja nanyi kwa hiyo sisi na nyinyi ni washirika katika ngawira.' Ikiwa ushindi ni wa washirikina husema, "sisi tulikuwa majasusi" Basi yako wapi malipo? Wanaishika fimbo kati kati. Ufasaha zaidi niliousoma kuhusu wasifu wa wanafiki, ni ule aliousema Amirul- mumiinin Ali (a.s.): "Wameiandalia kila haki batili, na kila msimamo upotofu, na kila mlango ufunguo, na kila usiku taa."

Hawa wapo kila siku na idadi yao inaongezeka katika miji ya kiarabu siku hadi siku, tangu ilipojitokeza dhahabu nyeusi (petrol). Wakafanya uzalendo kuwa ni nembo kama walivyojionyesha waislamu wakati wa Mtume. Wapigania ukombozi wakiwashinda wanyonyaji na walanguzi, wanafiki huwaambia: Je, hatukuwa pamoja nanyi? Na kama wanyonyaji wakifanikiwa huwaambia: Je, hatukuwazuia wapigania ukombozi wasiwafikie.

Unaweza kuuliza: Kwa nini Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametumia ushindi kwa waislamu na kupata sehemu kwa makafiri?

Jibu: Ushindi wa waislam ndio ushindi wa haki ambao unadumu na kubaki maadamu watu wake wanafuata desturi ya Mwenyezi Mungu na amri yake katika kujiandaa.

Kwa hiyo ikanasibu kuleta ibara ya ushindi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ama ushindi wa batili ni ushindi wa muda usiodumu, unaondoka mbele ya watu wa haki, kama wakiungana kwa Jihadi. Walikwishasema zamani; "Dola ya batili ni saa moja na dola ya haki ni mpaka Kiyama."

Wala Mwenyezi Mungu hatawafanyia makafiri njia ya kuwashinda waumin.

Mafakihi wameitolea dalili Aya hii kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakuweka sharia inayofanya mamlaka au usimamizi wa asiyekuwa mwislamu kwa mwislamu; Na wameitolea hukumu nyingi; kama vile kuwa baba wa mtoto akiwa mwislamu na mama yake sio mwislamu, mama hana haki ya kumlea. Kwa sababu mtoto hufuata dini iliyo tukufu zaidi anayoifuata mmoja wa wazazi wawili na hukumu yake ni hukumu ya waislamu.

Hukumu nyingine ni kuwa haijuzu kwa mwislamu kuwausia watoto wake wasimamiwe na asiyekuwa mwislmau; na akifanya hivyo basi wasia umebatilika. Hukumu nyingine waliyoitoa katika Aya hiyo ni kuwa, baba anakuwa na usimamizi kwa watoto wake kama wana dini moja.

Ama wakiwa ni waislamu na baba si mwislam hatakuwa na usimamizi juu yao. Nyingine ni kuwa hukumu ya hakimu asiyekuwa mwislamu haitekelezwi kwa haki ya mwislamu, hata kama ni haki na mengine mengi.

إِنَّ الْمُنَافِقِينَ يُخَادِعُونَ اللَّهَ وَهُوَ خَادِعُهُمْ وَإِذَا قَامُوا إِلَى الصَّلَاةِ قَامُوا كُسَالَىٰ يُرَاءُونَ النَّاسَ وَلَا يَذْكُرُونَ اللَّهَ إِلَّا قَلِيلًا {142}

Hakika wanafiki wanamhadaa Mwenyezi Mungu, na hali yeye ndiye menye kuwahadaa. Na wanapoinuka kwenda kuswali, huinuka kivivu. Wanajionyesha kwa watu Wala hawamtaji Mwenyezi Mungu ila kidogo tu.

مُذَبْذَبِينَ بَيْنَ ذَٰلِكَ لَا إِلَىٰ هَٰؤُلَاءِ وَلَا إِلَىٰ هَٰؤُلَاءِ ۚ وَمَنْ يُضْلِلِ اللَّهُ فَلَنْ تَجِدَ لَهُ سَبِيلًا {143}

Ni vizabizabina baina ya huku na huko. Na ambaye Mwenyezi Mungu amemwacha kupotea huwezi kumpatia njia