read

Aya 142: 143: Wanamhadaa Mwenyezi Mungu Na Atawalipa Kwa Kuhadaa Kwao

Maana

Hakika wanafiki wanamhadaa Mwenyezi Mungu, na hali yeye ndiye menye kuwahadaa.

Makusudio ya kuhadaa kwao ni kule kuonyesha imani kwa Mtume na kuficha ukafiri. Kwa sababu mwenye kumhini Mtume ndio amemhini Mwenyezi Mungu. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Hakika wale wanaokuunga mkono kwa hakika wamemuunga mkono Mwenyezi Mungu…" (48: 10)

Makusudio ya kuwa Mwenyezi Mungu anawahadaa ni kwamba yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu atawaadhibu kwa hadaa yao na unafiki wao.

Na wanapoinuka kwenda kuswali, huinuka kivivu.

Wataichangamkiaje na wao wanaikanusha? Hawatarajii thawabu kwa kuitenda wala adhabu kwa kuiacha; isipokuwa wanaitekeleza kwa kuwinda dunia tu na kuifanya ni nyanzo ya uchumi. Mwenyezi Mungu anasema: "Kwa hakika hiyo Swala ni ngumu isipokuwa kwa wanyenyekevu."(2: 45)

Unaweza kuuliza: Mtu akiswali kwa kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na pamoja na hayo anapenda watu wamuone, ili wamhisabu katika watu wema au asituhumiwe kuwa aniipuuza dini. Je hii itakuwa ni ria?

Jibu: Hapana! Maadamu msukumo wa kwanza ni wa amri ya Mwenyezi Mungu na radhi zake; mengine yanafuatia tu, Imam as-Sadiq (a.s.) aliulizwa kuhusu mtu ambaye anafanya jambo la kheri, kisha akafurahi kwa kuonwa na mtu mwingine akilifanya jambo hili (nini hukumu ya mtu huyo)? Imam akajibu: "Hapana ubaya kwa hilo, ikiwa hakuifanya kwa hilo, kwani hakuna mtu asiyependa Mwenyezi Mungu amdhihirishie kheri mbele ya watu,."

Wanajionyesha kwa watu.

Kwa sababu wao huswali kwa ajili ya kuwinda na kupata faida.

Wala hawamtaji Mwenyezi Mungu ila kidogo tu.

Yaani wakati wa kujionyesha kwa watu. Ama wakiwa peke yao, hawamtaji kabisa. Imam Jafar as-Sadiq (a.s.) anasema: "Mwenye kujionyesha (ria) ana alama tatu: Anakuwa mvivu akiwa peke yake, anachangamka akiwa na watu na hupenda kusifiwa kwa asilolifanya."

Je Watu Wote Hujionyesha

Unaweza kuuliza: Hakuna yeyote anayedhihirisha ukweli wake kwa watu na kuwaambia kila analoitakidi. Ni nani anayeweza kumwambia kila mtu anayoyajua. Na akifanya hivyo, basi atahisabiwa katika wenda wazimu, bali ni nani ambaye - mara nyingine - hafanyi asiyoyapenda na kuyataka? Kisha utaziepuka vipi desturi na maadili ya jamii?

Je, unaweza kumwambia mtu uliyekutana naye, ambaye humpendi, akakwambia 'natamani kukuona,' na wewe umwambie: nachukia kukuona?

Na kama utamwambia hivyo je unavyoona wewe au waonavyo watu utakuwa uko sawa? Mwisho je watu wote wanafanya ria (kujionyesha), kwa sababu hawait- akidi yote wayasemayo; wala hawaamini yote wayafanyao?

Jibu: Kuna tofauti baina ya Ria na Mudarat. Ria ni kudhihirisha unafiki na uzushi ili uwe pamoja na wema na wewe si katika wao.
Na Mudarat ni kuwa mpole na kutowachukilia na kuamiliana na watu bila ya kulenga chochote zaidi ya kutaka kuishi nao katika uelewano na maafikiano.

Ni kweli kuwa mara nyingine unafanya mambo kufuata desturi ya jamii; ukapongeza, kutoa rambi rambi au kutabasamu na kumheshimu mtu kwa jamala tu si kwa kuamini, lakini jambo hili ni salama halina tashwishi yoyote.

Wala halihisabiwi kuwa ni ria maadam kulifanya kwako kunaafikiana na jamii. Vilevile si wajibu juu yako kama utatokewa na kosa - hakuna maasum - kulitangaza kwa watu. Ndio ni wajibu kuwadhihirishia usafi sio makosa.

Vilevile ni kweli kuwa unasema uongo unapomwambia unayemchukia 'mimi nakupenda,' lakini ni uongo ulio katika masilahi na hulka njema. Mwenyezi Mungu anasema: "Na semeni na watu kwa uzuri" (2: 83)

Je hukuona vipi Mwenyezi Mungu alivyopiga mfano wa neno zuri? Ni kama mti mzuri mizizi yake ni imara na matawi yake yako mbinguni." (14:24)

"Nendeni kwa firaun hakika yeye amepetuka mpaka. Kamwambieni maneno laini huenda akaonyeka au akaogopa. " (20: 44 - 45)

Kuna Hadith isemayo: "Tamko jema ni sadaka, hupewa thawabu alisemaye, thawabu za wenye fadhila na ihsan." Hadith nyigine inasema: "Ameniamrisha Mola wangu kuwachukulia watu upole (Mudarat), kama alivyoniamrisha faradhi (wajib)."

Wamekongamana mafakihi kwamba uongo ni wajibu ikiwa utakuwa ni kutetea nafsi isiyo na hatia na kuiepusha na maangamivu. Na kwamba ukweli ni haram katika ufitini na usengenyaji. Kwa hiyo mfitini ni mkweli na msengenyaji ni mkweli, lakini wanashutumiwa mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele za watu1

Baada ya yote hayo ni kwamba ria ya haramu ni ile ya kudhihirisha mambo asiyokuwa nayo mbele za watu; anajionyesha kuwa ana kheri ili apate hadhi ya watu wema na huku mwenyewe ni katika waovu wafisadi.

Ni vizabizabina baina ya huku na huko, Mara wanajidhihirisha wako pamoja na waislamu na mara wako pamoja na makafiri; na wao hasa ilivyo nikuwa: hawako kwa hawa wala hawako kwa wale bali wako kwenye manufaa yao na tamaa zao; wanabusu mkono wowote wenye manufaa kwao uwe mchafu au msafi.

Na ambaye Mwenyezi Mungu amemwacha kupotea huwezi kumpatia njia.

Yaani Mwenyezi Mungu anamwepuka na kumwachia mwenyewe kwa sababu ya inadi yake na kupinga kwake haki. Na ambaye mambo yake yako hivi, basi hatarudi kwenye uongofu.

Na hapana budi kuzingatia kuwa hekima ya Mwenyezi Mungu Mtukufu inasababisha kutomuacha mja wake; kama ambavyo mzazi hamwachi mtoto wake. Ila ikiwa mja mwenyewe ndiye aliyesababisha kuachwa na Mwenyezi Mungu kwa njia ya kumwasi; kama ambavyo mama anaachana na mwanawe kwa sababu ya kumwudhi sana.

Imetangulia Aya kama hii, herufi kwa herufi katika Sura hii. Aya 88 na tumeizungumzia kwa ufafanuzi kama ambavyo tulifafanua mafungu ya uongo- fu na upotevu katika kufasiri (2: 26)

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَّخِذُوا الْكَافِرِينَ أَوْلِيَاءَ مِنْ دُونِ الْمُؤْمِنِينَ ۚ أَتُرِيدُونَ أَنْ تَجْعَلُوا لِلَّهِ عَلَيْكُمْ سُلْطَانًا مُبِينًا {144}

Enyi mlioamini! Msiwafanye Makafiri kuwa marafiki badala ya waumini. Je, mnataka awe nayo Mwenyezi Mungu hoja dhahiri juu yenu.

إِنَّ الْمُنَافِقِينَ فِي الدَّرْكِ الْأَسْفَلِ مِنَ النَّارِ وَلَنْ تَجِدَ لَهُمْ نَصِيرًا {145}

Hakika wanafiki watakuwa katika tabaka ya chini mtotoni. Hutakuta kwa ajili yao msaidizi.

إِلَّا الَّذِينَ تَابُوا وَأَصْلَحُوا وَاعْتَصَمُوا بِاللَّهِ وَأَخْلَصُوا دِينَهُمْ لِلَّهِ فَأُولَٰئِكَ مَعَ الْمُؤْمِنِينَ ۖ وَسَوْفَ يُؤْتِ اللَّهُ الْمُؤْمِنِينَ أَجْرًا عَظِيمًا {146}

Ila wale waliotubu na wakatengeza (mwendo wao) na wakashikamana na Mwenyezi Mungu na wakamtakasia Mwenyezi Mungu dini yao, basi hao watakuwa pamoja na waumini na Mwenyezi Mungu atawapa waumini malipo makubwa.

مَا يَفْعَلُ اللَّهُ بِعَذَابِكُمْ إِنْ شَكَرْتُمْ وَآمَنْتُمْ ۚ وَكَانَ اللَّهُ شَاكِرًا عَلِيمًا {147}

Mwenyezi Mungu ana haja gani ya kuwaadhibu kama mtashukuru na mtaamini na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kupokea shukrani Mjuzi.
  • 1. Maandiko ya Qur'an na Hadith yako kwenye misingi ya kufanya lenye masilahi na kuacha lenye uharibifu. Penya masilahi ni amri na penye uharibifu ni katazo. Kwa hiyo ndio ikajuzu kuse- ma uongo pamoja na masilahi na ikawa haramu kusema ukweli pamoja na uharibifu wenye masengenyo na upeke peke.