read

Aya 144 - 147: Msiwafanye Makafiri Kuwa Marafiki

Maana

Enyi mlioamini! Msiwafanye Makafiri kuwa marafiki badala ya waumini.

Imetangulia Aya hii pamoja na tafsir yake katika (3:28)

Je, mnataka Mwenyezi Mungu awe na hoja iliyowazi juu yenu?

Kila asiyekuwa na ubainifu wa dini yake au kupomoka na njia ya uongofu baada ya kumbainikia, basi yeye mwenyewe amempa Mwenyezi Mungu hoja nzuri juu yake mwenyewe.

Hebu tusome dua hii:"Ewe Mwenyezi Mungu! Hakika sisi tunakiri kwamba wewe huadhibu ila baada ya kusimamisha hoja. Vile vile tunakiri kuwa hoja imetusimamia, bali tunagwaya na kutetemeka kwa kuhofia mashiko yako na tunataka hifadhi yake kwa msamaha wako na utukufu wako. Kwa hiyo haku- na haja ya kusimama mbele zako kwa kuhukumiwa na kuhisabiwa au kuchunguzwa."

Hakika wanafiki watakuwa katika tabaka ya chini motoni. Hutakuta kwa ajili yao msaidizi

Kwa sababu adhabu iko kwa kiasi cha kosa, na hakuna kosa kubwa kuliko unafiki ambao umekusanya ukafiri na uongo. Yote mawili ni mama wa maovu.

Ila wale waliotubu na wakatengeneza (mwendo wao) na wakamtakasia Mwenyezi Mungu dini yao; basi hao watakuwa pamoja na waumini. Na Mwenyezi Mungu atawapa waumin malipo makubwa.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kutoa kemeo na kiaga cha adhabu kali kwa wanafiki, anawaongoza kwenye toba, njia ya uokofu na kuokoka, njia pekee ya kutaka nusura na shufaa kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na hilo liko mikononi mwao na katika uwezo wao. Mwenye kuzembea, basi na ajilaumu mwenyewe. Hii ni hoja nyingine kwa kila mwenye dhambi, anayoiongezea Mwenyezi Mungu Mtukufu kwenye hoja zake sahihi ambazo hazina idadi.

Tumeweka mlango mahsusi wa toba na wenye kutubia wakati wa kufasiri Aya 18 katika Sura hii. Wafasiri wamerefusha maneno katika kubainisha tofauti katika viunganishi vilivyo katika Aya hii waliotubu, wakatengeneza (mwendo wao), wakashikamana na Mwenyezi Mungu na wakamtakasia Mwenyezi Mungu dini yao; Tuonavyo sisi ni kuwa neno toba linakusanya sifa zote hizi kwa ukamilifu wake; wala hatuoni tofauti ya kimsingi baina yao; isipokuwa yamekuja kwa kutilia mkazo kuonyeshwa yale waliyokuwa nayo wanafiki - kubabaika na kuasi, na kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakubali toba yao wala hatawaingiza katika hisabu ya waumini ila wakiwa na uthabiti na kuen- delea na toba; na wao wakirtadi baada ya toba na wakatenda kama wanavyotenda, basi kurtadi kwao kutaongezea ukafiri wao, uzushi wao na ubabaikaji wao. Hakuna malipo ya kurtadi ila kifo duniani na adhabu chungu huko Akhera.

Mwenyezi Mungu Na Unyenyekevu Wa Imam Zainul Abidin

Mwenyezi Mungu ana haja gani ya kuwaadhibu kama mtashukuru na mtaamini?

Kabisa hana haja! Yeye anajitosheleza na kila kitu katika dhati yake na sifa zake vinginevyo basi asingeweza kuumba; isipokuwa anapatiliza na kuadhibu kwa malipo yenye kulingana. Wala hamhitajii kiumbe katika kupatikana kwake na kubaki kwake na katika harakati zake zote.

Sasa msomaji hebu tusikilize unyenyekevu na utukuzo ulio katika munajat huu utokao kwa Imam Zainul Abidin: "Ewe Mwenyezi Mungu! Hakika mimi ni mtu duni na mawazo yangu ni mepesi; wala adhabu yangu haiongezi chembe katika milki yako. Lau adhabu yangu ingelikuwa inazidisha kitu katika milki yako, basi ningekuomba univumilie na ningependa iwe hivyo kwako, lakini ufalme wako ni mkuu zaidi usioweza kuongezewa kitu na utiifu wa wenye kutii au kupunguzwa na maasi ya wenye dhambi."

Munajat huu sio alama tu ya kuonyesha upeo wa mapenzi na shauku juu ya wema wa Mwenyezi Mungu na utakatifu wake; kama wafanyavyo masufi, wala sio dua tu ya kuhofia adhabu ya Mwenyezi Mungu hata kama dhahiri ya maneno inafahamisha hivyo, isipokuwa ni maelekezo kwa kila mwenye nguvu anayetaka kuwakaba wanyonge wasio na uwezo na kwamba lililo bora kwa uwezo wake juu ya wanyonge ni msamaha, na wala sio kuadhibu na kutesa.

Nguvu haziwezi kuwa bora na kamilifu ila kwa kusamehe. Hakika kuhitajia au ukorofi ndio unaosababisha kumtesa asiyekuwa na kimbilio ila kwa mwenye nguvu. Na mwenye nguvu aliye mkamilifu hahitajii wanyonge, ni Mwenye kujitosheleza Mwenye kutakata na upungufu.

Baada ya yote hayo; hakika msamaha ni bora, sisi tuna haja nao na Mwenyezi muweza nao na wala hakuna zaidi kuliko Yeye. Kwa hiyo basi msamaha wake uko. Tunasema haya na sisi tukiwa miongoni mwa wanaomwogopa Mwenyezi Mungu.

Na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kupokea shukrani Mjuzi.

Anamjua mwenye kumtii na mwenye kushukuru na humlipa ujira wa watiifu wa wenye kushukuru. Tumemwamini Mwenyezi Mungu peke yake. Twanyenyekea tukimwambia Yeye s.w.t. atuwafikishe kumshukuru na kumtii.