read

Aya 24-25: Walioolewa

Lugha

Neno Muhsanat limetoka katika neno Hisni (ngome) likiwa na maana ya Uislam, uhuru, ndoa, na kujistahi. Aya mbili tulizo nazo zinakusanya maana zote hizi nne, ufafanuzi unafuatia.

Maana

Na wanawake wenye kuolewa isipokuwa wale iliyowamiliki mikono yenu ya kuume.

Haya yanaungana na yale ya wanawake walio haramu katika Aya iliyotangulia. Yaani pia mmeharamishiwa wake wenye waume zao.

Yametangulia maelezo katika kifungu cha lugha kwamba neno Muhsanat katika Aya mbili hizi linachukua maana nne: Ndoa, kujistahi, uhuru na Uislam, Makusudio ya Muhsanat hapa ni wanawake walioolewa. Kwa sababu ndoa ni ngome ya mke inayomzuia kufanya yasiyotakikana na ni ngome ya mume, hiyo hiyo. Hadith inasema: "Mwenye kuoa amehifadhi theluthi mbili za dini yake."

Makusudio ya wale iliyowamiliki mikono yenu ni kutokea mwanamke kuwa ni miliki ya mwanamume mwingine. Kwa maana ya kuwa mwanamke akiolewa ni haramu kwa mtu mwengine, ila kama atamilikiwa na Mwislam. Hapo atakuwa halali yake yule (Mwislamu) aliyemmiliki hata kama ni mke wa mtu mwengine. Mwislam anaweza kummiliki mwanamke kwa sababu zifuatazo:

Kwanza:

Kuwa mateka wake. Hilo linakuwa kutokana na vita vya kidini baina ya Waislam na washirikina na Waislam wawashinde washirikina. Hapo wake wa washirikina, watoto wao na mali zao, zinakuwa ngawira ya vita. Mwislam akipata mateka wa kike bila ya mumewe, basi mwanamke huyu atatenganishwa naye na awe si mumewe tena, kwa kongamano la madhehebu yote. Wakitekwa wote pamoja (mume na mke) hawatatenganishwa kwa mujibu wa madhehebu ya Hanafi na Hambal ama kwa Shia Imamiya, Shafi na Malik, (wamesema mume na mke hao makafiri) watatenganishwa.

Mwislam akitaka kumwoa mwanamke wa kishirikina aliyemteka, anaweza kufanya hivyo baada ya kuzaa, ikiwa alikuwa na mimba. Au atangoja aingie hedhi moja ikiwa hana mimba. Ikiwa hana mimba wala hatoki hedhi atangoja siku 45 ndipo amwingilie.

Hukumu hizi zilifuatiliwa katika ushindi wa waislam wa kwanza. Wengine wamezitafutia sababu kuwa ati zilikuwa ni kwa sababu ya kuuzuwiya na kuukataza ukafiri, na kuhimiza kukubali uislam. Ama sisi tunasema kuwa hizo ni hukumu za ki-ibada, hatujui hekima yake. Tunachojua ni kuwa zina mifano katika sheria, kuna baadhi ya dini nyengine zimehalalisha kuwaua wanawake na watoto. Lakini Uislam umeamrisha kuwafanyia upole mateka na watumwa wakiwa wa dini yoyote au madhehebu yoyote.

Pili:

Mwislam kummiliki mwanamke ni kumnunua akiwa mjakazi. Hilo ni kuwa mtu awe ana mjakazi aliyemwoza mtumwa wake au mtu mwengine. Kisha akamuuzia mwengine; uuzaji huu utabatilisha ndoa ya mjakazi kwa mujibu wa madhehebu ya Shia Imamiya. Itamhalalishia mnunuzi kulala naye baada ya kusafika kwa kuzaa, hedhi au siku 45.

Sayyid Rashid Ridha mwenye Tafsir Al-manar anasema: "Baadhi ya masahaba kama Ibn Mas'ud wako kwenye rai hii wanayoitumia Mashia, lau si kwamba Ustadh Imam1 hakuichagua ingelikuwa kauli ya Shia Imamiya ni yenye nguvu zaidi kuliko madhehebu yote ya Sunni."
Sayyid Rashid anakiri kwamba kauli ya Shia ina nguvu zaidi kuliko madhehebu ya Sunni lakini pamoja na hivo anaikataa, si kwa lolote ila tu kwamba ustadh wake hakulisema. Ajabu ya watu wa mfano wa Sayyid Rashid ambaye ameilaumu Taqlid (kufuata) na wanaofuata, mpaka akawatoa katika dini sio katika elimu tu. Angalia tafsir yake ya Aya 165-167 ya Sura ya pili (Al-Baqara)

Kwa ujumla ni kwamba Uislam umehalalisha kwa Mwislamu kumwoa aliye na mume (aachike) akiwa ni mjakazi aliyemmiliki kwa kumnunua, au mshirikina aliyemteka katika vita vya kuupigania Uislam na kuulingania.

Unaweza kuuliza: Neno Muhsanat (wanawake walioolewa) ni wingi wa wanawake na maana yake yako wazi, sasa kuna faida gani ya Mwenyezi Mungu kusema katika wanawake

Jibu: Kwanza mara nyingi huwa ni kwa kufafanua na kuyatlia mkazo zaidi mfano "… Na kuwaua kwao Mitume pasi na haki …" (3:181) pamoja na kuwa kuwaua Mitume daima huwa ni pasi na haki.

Pili: Huenda mtu akadhania kuwa makusudio ya Muhsanat ni wanawake waislam tu. Ndipo likaja neno katika wanawake ili kubainisha ujumla; na kwamba ndoa ni ya kuheshimiwa tu, iwe kwa mwanamke wa Kiislam au mwengine.

Ni Sharia ya Mwenyezi Mungu kwenu.

Ni kutilia mkazo yaliyotangulia kuhusu walioharamishwa. Kwa maana ya kuwa uharamu wa aina zilizotajwa ni sharia inayotoka kwa Mwenyezi Mungu. Mwenye kuikhalifu, basi Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye atakayemhukumu na kumwadhibu.

Na mmehalalishiwa wasiokuwa hao

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alipomaliza kubainisha walio haramu, anataja desturi ya kijumla, ambayo ni kwamba wasiokuwa wa aina zilizotajwa ni halali kuwaoa kwa sharti ya kuwa ndoa ifuate misingi iliyowekwa na sharia; kama kutoa mahari ya kisharia sio ujira wa ukahaba.

Hiyo ndiyo maana ya kusema: Muwatafute kwa mali zenu kwa kuoa bila ya kufanya zina. Neno kuoa linatosha bila ya kutaja zina, lakini limekuja kwa kutilia mkazo na kuonyesha kuwa mwenye mali anaweza kutoa mali yake katika starehe zisizokuwa za haram. Kwa sababu Uislam kama ulivyoharamisha njia za chumo zisizokuwa za kisheria - kama riba, kughushi na kunyang'anya - pia umeharamisha kutoa mali katika mambo ya haram; kama vile zina au kuingilia uhuru wa wengine.

Sunni na Shia wameafikiana kwamba kauli yake Mwenyezi Mungu: Na mme-halalishwa wasiokuwa hao, inafahamisha kujuzu kuchanganya mtu na shangazi yake au mamake mdogo. Kwa sababu inavyojulikana katika njia ya watu wa sharia ni kutaja ya haram tu, kwa vile inawezekana kuyadhibiti. Ama yenye kuhalalishwa hayadhibitiki.

Hivyo wanayaashiria kwa kusema: "Yasiyokuwa hayo." Lakini Sunni wamesema kuwa imethibiti kutoka kwa Mtume (s.a.w.) kwamba yeye amesema: "Haolewi mwanamke pamoja na shangazi yake wala khala (mama mdogo)."

Khawarij wamesema kuwa inajuzu kuwachanganya kwa hali yoyote, akikataa shangazi, mama mdogo au akikubali.

Shia Imamiya wametofautiana, kuna baadhi wanasema kama walivyosema Sunni. Wengi wao wanasema kuwa ikiwa mke wa pili anayetaka kumwoa ni shangazi au khala wa mke wa kwanza, anaweza kumwoa kwa hali yoyote. Lakini akimwoa shangazi au khala kwanza, haijuzu kuoa mpaka kwa idhini ya shangazi au khala. Wamelitolea dalili hilo kwa riwaya za Ahlul-bait (a.s.)

Ndoa Ya Mut'a

Ambao mmestarehe nao katika wao, basi wapeni mahari yao yaliyo lazimu.
Dhamiri ya 'nao' na 'wao' inawarudia wale ambao ni halali kuwaoa katika kauli yake Mwenyezi Mungu: "… na mmehalalishiwa wasiokuwa hao."

Maana - kwa maafikiano ya wafasiri - ni kwamba mwenye kutaka kumwoa mwanake katika wale walio halali kwake, basi ni lazima atoe mahari ambayo ni lazma, sio sadaka wala hisani.

Mjadala umekuwa mkubwa kuhusu Aya hii; Je, makusudio ni ndoa ya daima tu, au ndoa ya muda, au zote pamoja? Na kama makusudio ni Mut'a je Aya imekua mansukh (hukmu imefutwa) pamoja na ndoa yenyewe ya Mut'a? vya Hadith, Fiqh na Tafsir ya Sunni na Shia waislam wote wameafikiana kwa kauli moja kwamba Uislam ulileta sharia ya Mut'a ya wanawake, na kwamba Mtume (s.a.w.) aliwaaamrisha sahaba zake hilo; kama inavyoeleza Sahih Bukhar Juz, 7 mlango wa Targhib fin nikah, kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alikuwa katika jeshi la waislam akawaambia: "Mwenyezi Mungu amewapa idhini ya kufanya Mut'a, basi fanyeni …"

Riwaya ya pili ya Bukhari inasema: "Mwanamume yeyote aliyeafikiana na mwanamke wanaweza kuishi pamoja siku tatu, wakipenda wanaweza kuzidisha au wakiamua kuachana wataachana."

Katika Sahih Muslim Juz. 2 mlango wa 'Nikahul-mut'a' Uk. 623 chapa ya 1347 A.H. Kuna Hadith iliyopokewa kutoka kwa Jabir bin Abdillahi Al-ansary amesema: "Tulifanya M ut'a wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu; na wakati wa Abu Bakr na Umar." Katika ukurasa huo huo kuna Hadith nyengine kutoka kwa Jabir, amesema: "… Kisha akatukataza Umar." Kuna Hadith kama hiyo katika Musnad Imam Ahmad bin Hambal. Juz. 3

Arrazi katika kufasiri, ‘ambao mmestarehe nao’ anasema: "Amesema Imran bin Al-hasin, ambaye ni katika mafakihi wa kisahaba na mbora wao: "Hakika Mwenyezi Mungu aliteremsha Aya ya Mut'a na wala Aya hiyo haikufutwa hukmu yake na Aya nyingine; na Mtume akatuamrisha kufanya Mut'a wala hakutukataza. Kisha mtu mwengine akasema kwa maoni yake atakavyo. Hapo anakusudia kuwa Umar alikataza.

Riwaya hizi na mfano wake zinapatikana zaidi katika Sahih za Sunni na Tafsir zao na katika vitabu vyao vya Fikihi. Kwa hiyo basi mzozo wa kuwa je, makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Ambao mmestarehe nao

…" Ni ndoa ya daima tu, au ndoa ya Mut'a tu, au zote pamoja unakuwa ni mzozo tasa usiokuwa na faida yoyote. Kwa sababu, natija inakuwa ni hiyo hiyo haitofautiani na chochote. Ni sawa tuseme kuwa Aya inaenea katika ndoa ya muda, au inahusika na ndoa ya daima tu. Kwa sababu linaloangaliwa ni kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) ameamrisha ndoa ya Mut'a kwa kuafikiana Waislam wote. Na kwamba kila aliloliamrisha Mtume na Mwenyezi Mungu Mtukufu pia ameliamuru kama alivyosema: "Alichowapa Mtume, kipokeeni na alichowakataza jiepusheni nacho." (59:7)

Baada ya kuafikiana Sunni na Shia kwamba Uislam umeweka sharia ya Mut'a, wamehitalifiana katika kufutwa sharia hiyo na kuwa haramu baada ya kuwa halali. Sunni wamesema imeharamishwa baada ya kuhalalishwa, Shia wanasema ilikuwa na itaendelea kuwa halali mpaka siku ya mwisho.

Kimsingi ni kwamba ni juu ya Sunni kuthibitisha kufutwa hukumu hiyo na uharamu wake kutoka kwa Mtume (s.a.w.). Kwa sababu wao wanadai kuondoka kitu kilichothibiti kwa njia ya mkato na yakini. Ama Shia hawalazimiki kuthibitisha kuwa haikufutwa. Kwa sababu wao wanasema linalothibiti kwa yakini haliondoki ila kwa yakini. Mfano watu wawili wameafikiana kuwa fulani alikuwa hai mwaka uliopita, kisha wakatofautiana kuhusu kufa kwake. Hapo atakayetakiwa kuthibitisha ni yule anayedai kuwa amekufa. Ama yule anayesema bado ni mzima, hatakiwi kufanya chochote. Kwa kuwajibisha hukumu ya kubakisha lilokuwa kama ilivyo mpaka ithibiti kinyume.

Sunni wamekiri kwamba ni juu yao kuthibitisha, na wala sio Shia ndipo waka- toa dalili za kuthibiti kufutwa hukumu hiyo, kwa Hadith za Mtume (s.a.w.), ambazo Shia wamezijadili kwa matini na isnadi na wakathibtisha kwa mantiki sahihi kwamba Hadith hizo zimesingiziwa Mtume (s.a.w.) kwa dalili zifuatazo:

(i) Kwamba Sunni wenyewe wanakubali kuwa zinagongana na kupingana. Ibn Rushdi katika kitabu Al-bidaya Juz, 2 Masuala ya ndoa ya Mut'a anasema: "Baadhi ya mapokezi ni kwamba Mtume (s.a.w.) aliharamisha Mut'a siku ya vita vya Khaybar; nyingine zinasema ni siku ya ushindi wa Makka; na nyingine zikadai ni siku ya vita vya tabuk; nyingine zikasema kuwa iliharamishwa siku ya Hija ya mwisho (Hijjatul-wadaa); nyingine siku ya kulipa Umra, nyingine katika mwaka wa Autas - jina la mahali katika sehemu ya Hijaz palipiganwa vita katika vita vya Mtume (s.a.w.) - kisha anaendelea kusema Ibn Rushdi - imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas kwamba yeye amesema: "Mut'a haikuwa ila ni rehema ya Mwenyezi Mungu aliyowarehemu umma wa Muhammad (s.a.w.) lau si kuikataza Umar asingelazimika kuzini ila mwovu."

(ii) Riwaya hizo za kufutwa hukumu si hoja, hata kama zitakuwa hazina migongano. Kwa sababu ni Khabarul-wahid.Na 'kufutwa hukmu' kunathibiti kwa Aya au Khabar Mutawatir tu, na wala sio Khabarul- wahid.2

Yaliyokuja kwenye Sahih Muslim kwamba waislam walifanya Mut'a wakati wa Mtume na wa Abu Bakr. Kwa hivyo haya yanapingana na kuwa ilifutwa wakati wa Mtume. Vyenginevyo basi khalifa wa kwanza atakuwa ni muhalalishaji wa aliloliharamisha (alilolifuta) Mwenyezi Mungu na Mtume.

Ukweli zaidi unaofahamisha kuwa haikufutwa ni kauli ya Umar mwenyewe: "Mut'a mbili zilikuwako wakati wa Mtume na mimi ninazikataza na nitaadhibu kwazo …" Kila nitakavyotia shaka, lakini siwezi kutia shaka wala sitatia shaka kwamba Umar, lau angelinyamazia basi wasingelitofautiana hata Waislam wawili katika kujuzu Mut'a na uhalali wake mpaka siku ya kufufuliwa. Unaweza kusema: Ni ajabu sana kuwa Umar amesema haya. Kwa sababu ni kuharamisha alilolihalalisha Mwenyezi Mungu; na ni kumpinga Mtume wa Mwenyezi Mungu ambaye 'hatamki kwa matamanio.'

Jibu: Ni kweli, ni ajabu ya maajabu kama ulivyosema: "kumpinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake", lakini waislam wameafikiana kwamba Umar ameyasema hayo. Sijaona hata mmoja aliyekanusha. Bali kuna riwaya nyingine zinazosema kuwa Umar alikataza mambo matatu aliyoyaamrisha Mtume sio mawili. Anasema Al-qawshaji - mwanachuoni wa Kisunni - katika sherehe ya Tajrid mwisho wa utafiti wa Uimam: "Umar alipanda mimbar akasema: 'Enyi watu! Mambo matatu yalikuwako katika wakati wa Mtume na mimi ninayakataza na kuyaharamisha na kumwadhibu atakayeyafanya: Mut'a ya wanawake, Mut'a ya Hija na neno Hayya ala khairil amal."

Amepokea Tabari na Razi kwamba Ali amesema: "Lau si Umar kukataza Mut'a asingelizini ila mwovu." Yako mfano wa hayo soma Tafsir ya Thalabi na ya Suyuti.

Swali la pili: Je, haifai - kwa nafasi ya Umar - kuchukua kauli hii, kwamba ni riwaya ya Mtume (s.a.w.) na wala si rai ya Umar dhidi ya Mtume (s.a.w.) ?

Jibu: Ni kweli kabisa kuchukulia hivyo kunafaa sana, lakini kauli ya Umar: "… zilikuwako wakati wa Mtume na mimi ninazikataza …" inakataa kuchukulia huku, Kwani yeye mwenyewe amenasibisha kuhalalisha kwa Mtume na kuharamisha kwake yeye. Lau kauli yake ingelikuwa ni riwaya na siyo rai, basi angelinasibisha kukataza kwa Mtume. Kwa sababu Mtume ndiye anayefaa zaidi kukataza. haiwezekani kwa hali yoyote kuchanganya kauli mbili: "Kwamba Mtume alikataza Mut'a baada ya kuiamrisha na kauli ya Umar kuwa Mut'a ilikuwa wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu na mimi ninaikataza." Na imethibiti kwamba Umar ameyasema haya. Kwa hiyo ni wazi kwamba Mtume hakukataza Mut'a.

Haya ndiyo baadhi ya majibu ya riwaya za 'Naskh'(kufutwa hukumu) zilizolaz- imishwa kwa Mtume. Mwenye kutaka ufafanuzi na arudie Tafsir Alau-Rrahman ya Sheikh Muhammad jawad Al-balaghi; na Al-bayan Fi Tafsir Al-Qur'an ya Sayyid Khui, Naqdhul washi'a ya Sayyid Muhsin Al-amin na Juzuu ya tatu ya kitab Dalail s-swadiq cha Sheikh Muhammad Hassan Al-mudhaffar.

Kwa hakika ni kwamba hakuna tofauti kati ya ndoa ya daima na ndoa ya muda (Mut'a), kuwa haitimii bila ya mahari na Aqdi (kufunga ndoa); na katika uharamu unaoingia kwa ukwe; na katika wajibu wa urithi, kuwaangalia na kuwapa haki nyingine watoto; na katika wajibu wa eda ya mwenye kuolewa.

Katika kitabu chetu Fiqhul Imam Jaafar as-Sadiq (a.s.) tumetaja mambo kumi na tano yaliyo sawa katika ndoa ya daima na ya muda. Na mambo kumi yanayotofautiana.

Wala si vibaya kwenu katika yale mliyoridhiana baada ya (kutoa) kile kilichowalazimu.

Ikipita ndoa kwa mahari maalum yaliyobainishwa wakati wa kufunga ndoa, basi yanakuwa ni haki ya mke; atayatumia kadiri atakavyo. Lakini hiyo haizuwii kuelewana mke na mume kusamehe mahari yote au baadhi hata kuzidisha.

Vilevile halizuwii kuelewana juu ya aina ya matumizi ya mke na kiasi chake, au kuacha kabisa. Vile vile kuelewana kuhusu talaka, kurejeana baada ya talaka au baada ya kwisha muda wa Mut'a na mengineyo ambayo hayatoki katika mipaka ya sharia.

Na asiyeweza miongoni mwenu kupata mali ya kuoa wanawake waungwana waumini; basi (na aoe) katika wajakazi wenu waumini iliyowamiliki mikono yenu ya kuume.

Maana ni kuwa asiyepata mali ya kumwezesha kumwoa mungwana, basi aoe mjakazi mumini.

Na Mwenyezi Mungu anajua sana imani yenu. Baadhi yenu mnatokana na baadhi.

Makusudio ya imani hapa ni dini. Maana ni kuwa haitakikani kwa mumin kuona unyonge kumwoa mjakazi kwa sababu ya rangi yake na kabila yake. Kwa sababu watu wote wanatokana na Adam; na Adam ametokana na mchanga.

Kuzidiana mbele ya Mwenyezi Mungu ni kwa takua tu, si kwa fahari na nasaba. Mjakazi anaweza akawa mtukufu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko muungwana kwa sababu ya wema wake na takua yake.

Basi waoeni kwa idhini ya watu wao na muwape mahari yao kama ada

Watu wao wajakazi, ni wale watu wanaowamiliki

Wawe ni wenye kujistahi si waasherati.

Yaani sio wazinifu kwa sura ya wazi, kama kahaba mzururaji.

Wala wenye kujifanyia mahawara

Yaani anayeizini kisiri siri.

Watakapoolewa kisha wakafanya uchafu basi itakuwa adhabu yao ni nusu ya adhabu iliyowekwa kwa waungwana.

Yaani mjakazi akizini, adhabu yake ni nusu ya adhabu ya muungwana. Adhabu hiyo ni ile iliyotajwa na Aya hii: "Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume mpigeni kila mmoja wao mijeledi mia." (24:2)

Hayo ni kwa mwenye kuchelea mashaka katika nyinyi.

Mwenyezi Mungu hataki kuwapa mashaka waja wake wala kuingia katika fitna. Mwenye kuona kuwa ana haja na mke, basi aoe mungwana kama ana uwezo; na kama hana basi aoe mjakazi. Kama ataweza kuvumilia bila ya kuwa na mke na akawa salama na dini yake na afya yake, basi ni bora kuvumilia.

Na mkisubiri ni bora kwenu
Aya yote hii ndefu imeelezea hukumu ya mungwana kumwoa mtumwa, na adhabu ya mtumwa kama akizini. Sisi tumefupisha katika kuifasiri, kwa sababu maelezo ya utumwa na hukumu zao yamekuwa hayana umuhimu baada yakufutwa utumwa.

Ajabu ya maajabu ni kwamba dola ya kwanza kutangulia kuleta mwito wa kufutwa utumwa inawafanyia watu wa rangi nyengine kama wanyama nchini kwake na inazisaidia serikali za kibaguzi kila mahali na kufanya mambo ya kuutisha ulimwengu mzima, na mustakbali wa binadamu.

Dalili wazi ya ukweli huu, ni kushiriki kwake kuliunda taifa la Kiisrail na kuisadia kuzifanyia uadui nchi za Kiarabu na kuwafukuza wazalendo katika nchi zao ili kuzichukua. Ama kukusanya kwake mamia ya majeshi huko Vietnam na aina ya ukatili wa mauaji na uharibifu uliyoufanya, haina mfano katika historia . Naona kwamba njia pekee ya kuepuka uovu wa dola hii ni kila mtu wa Mashariki na Magharibi akatae lolote lile linalonasibiana au kuwa na athari na dola hiyo.

يُرِيدُ اللَّهُ لِيُبَيِّنَ لَكُمْ وَيَهْدِيَكُمْ سُنَنَ الَّذِينَ مِنْ قَبْلِكُمْ وَيَتُوبَ عَلَيْكُمْ ۗ وَاللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ {26}

Mwenyezi Mungu anataka kuwabainishia na kuwaongoza Mwendo wa waliokuwa kabla yenu na awatakabalie toba. Na Mwenyezi Mungu ni mjuzi mwenye hekima.

وَاللَّهُ يُرِيدُ أَنْ يَتُوبَ عَلَيْكُمْ وَيُرِيدُ الَّذِينَ يَتَّبِعُونَ الشَّهَوَاتِ أَنْ تَمِيلُوا مَيْلًا عَظِيمًا {27}


N


a


Mwenyez


i


Mung


u


ana


t


aka


kuwa


t


akabali


a


tob


an


awale amba


o


hufua


t


a


ma


t


amanio


wana


t


ak


amkengeuk


emkengeuko mkubwa.

يُرِيدُ اللَّهُ أَنْ يُخَفِّفَ عَنْكُمْ ۚ وَخُلِقَ الْإِنْسَانُ ضَعِيفًا {28}

Mwenyezi Mungu anataka kuwahafifishia. Na mtu ameumbwa hali yakuwa ni dhaifu.
  • 1. Anamkusudia Sheikh Muhammad Abduh
  • 2. Khabarul-mutawatir ni kupokea Hadith kundi lililofikia wingi ambao itakuwa vigumu kuafikiana uongo. Na khabarul-wahid ni ile isiyofikia kiwango cha mutawatir. Hata wapokezi wakiwa ni zaidi ya mmoja.