read

Aya 26 - 28: Mwenyezi Mungu Anataka Kuwabainishia

Maana

Mwenyezi Mungu anataka kuwabainishia na kuwaongoza mwenendo wa waliokuwa kabla yenu na awatakabalie toba.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kubainisha katika Aya zilizotangulia aina ya wanawake walio haramu kuwaoa kwa nasaba, ukwe na kunyonya na vile vile walio halali, aliendelea kusema kuwa tumewawekea hukumu hizo na kuwabainishia ili mpate faida ya halali yake kutokana na haramu yake, na kwa twaa yake na maasi na mfuate nyayo za waliowatangulia katika kujiepusha na yaliyoharamishwa na kufuata uongofu na imani. Vile vile aweze kujua mtubiaji hukumu alizoziweka Mwenyezi Mungu, aweze kujikurubisha kwake Mwenyezi Mungu na kuacha aliyoyakataza.

Imesemekana kwamba makusudio ya awatakabalie toba ni kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ameweka sharia hizo ili awajue wanaotubia yale yaliyopita katika zama za ujahiliya na mwanzo wa Uislam - kuoa wake wa mababa, kuoa pamoja dada wawili na mengineyo ya haramu.

Vyovyote iwavyo ni kwamba mwenye kutubia na asiyetubia hawezi kumtii Mwenyezi Mungu na kufuata hukumu zake ila baada ya kuzijua na kum’bainikia. Kwa hiyo ubainifu wa hukumu zake Mungu, ni hisani na neema kutoka kwake. Kwa sababu haamrishi isipokuwa lile lenye heri na masilahi; wala hakatazi ila lililo na shari na ufisadi.

Na wala si lazima Mwenyezi Mungu atubainishie hekima ya kuamrisha Kwake na kukataza Kwake. Sisi hatukalifiwi kujua au kufanya utafiti, letu sisi ni kufuata na kutii, tukiwa ni wenye kuamini kuwa hukumu zake Mwenyezi Mungu Mtukufu ni kwa ajili ya heri yetu ya dunia na akhera.

Na Mwenyezi Mungu anataka kuwatakabalia toba. Na wale ambao hufua- ta matamanio wanataka mkengeuko mkengeuko mkubwa.

Wanaofuata matamanio ni wale wanaotoa mwito wa kujivua na mikazo ya dini na tabia njema, na hufuatana na matamanio ya mwili vyovyote yanavyoelekea.Hawa siku zote wapo; hata wakitofautiana wanatofautiana katika mfumo tu, kulingana na hali zao. Katika karne ya ishirini wamejibandika jina la uhuru na maendeleo. Wamepetuka mipaka katika kuamsha tamaa ya maingiliano ya wanawake na wanaume kwa njia ya filamu, vitabu na picha za uchi. Huu ndio mgeuko na kwenda kombo ambako ameashiria Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa kauli yake: "mkengeuke mkengeuko mkubwa."

Unaweza kuuliza: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amekariri toba katika Aya mbili bila ya kuweko kitu kingine, pale aliposema: "Na awatakabalie toba … na Mwenyezi Mungu anataka kuwatakabalia toba…" Je, kuna makusudio gani katika hilo?

Jibu: Toba ya kwanza imekuja kuwa ni sababu ya kubainisha halali na haramu kwa wanawake bila ya kuangalia amri ya toba. Ama ya pili ni kuelezea amri yake Mwenyezi Mungu Mtukufu na kuwataka watu watubie kwa kuacha mambo ya haramu; mkabala wake ni matakwa ya mfuasi wa matamanio. Kwa mfano unaweza kumwambia mwanao: "Nimekununulia kitabu hiki ili ukisome basi kisome." Umetaja kusoma kwanza kwa kubainisha sababu zinazowajibisha kusoma, na ukarudia mara ya pili kwa sababu wewe unamtaka asome na huku ukimwamuru.

Mwenyezi Mungu anataka kuwahafifishia katika kuhalalisha walio halali katika wanawake; bali hata katika mambo mengine vile vile. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: "Mwenyezi Mungu anawatakia yaliyo mepesi hawatakii yaliyo mazito." (2.185) Wala hakuwawekea uzito katika dini. (22:78) Na kuna Hadith tukufu isemayo: "Nimewajia na dini nyepesi na ya kweli"

Na mtu ameumbwa hali ya kuwa dhaifu katika kukabiliana na mambo yanayosababisha ladha na starehe; hasa starehe ya mwili. Kwa ajili hiyo, ndipo Mwenyezi Mungu akahalalisha kustarehe na wanawake katika mipaka yake tuliyoielezea. Katika ngano la kale inaelezwa kuwa Iblis alimwambia Musa (a.s.): "Mwanamume hakai faragha na mwanamke ila mimi huwa sahibu yake."

Sijamuona yeyote aliyeleta picha ya udhaifu wa binadamu, katika nafsi yake na mwili wake, kuliko Imam Ali (a.s.) aliposema: "Akijiwa na matarajio, tamaa humdhalilisha; Akiingiwa na tamaa, pupa humwangamiza. Akimilikiwa na kukata tamaa, simanzi humuua. Akipatwa na hofu, hadhari humshughulisha. Akipatwa na masaibu, fazaa humfedhehesha na akipatwa na ufukara, mtihani humshughulisha."

Akaendelea kusema tena: "Masikini binadamu! Ajali (yake) imefichwa, ugonjwa (wake) umefunikwa, na amali (yake) imehifadhiwa. Anaumizwa na kunguni, au anauliwa na kikohozi na ananukishwa na jasho." Kama ambavyo Imam ameleta picha ya udhaifu wa mtu; vile vile ameleta picha ya nguvu na ukuu wa mtu; kwa kusema: "Mtu anashiriki kufika mbingu saba zenye nguvu."

Yaani kipawa chake hakisimami katika mazingira yanayomzunguka tu, bali huvuka hadi mwezini, kwenye Zuhura na kwenye Merikh na sehemu nyengine- zo zilizomo ulimwenguni anazitumia kwa haja yake.

Imam ameonyesha udhaifu wa binadamu ili asitegemee nguvu zake na kumhadaa akapetuka mpaka. Na akonyesha nguvu zake ili asisalimu amri kwa unyonge, akaacha kujitahidi na kufanya kazi. Mwenye akili ni yule mwenye kupigania huku akiwa na hadhari ya mambo yaliyofichika na yanayokuja ghafla.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَأْكُلُوا أَمْوَالَكُمْ بَيْنَكُمْ بِالْبَاطِلِ إِلَّا أَنْ تَكُونَ تِجَارَةً عَنْ تَرَاضٍ مِنْكُمْ ۚ وَلَا تَقْتُلُوا أَنْفُسَكُمْ ۚ إِنَّ اللَّهَ كَانَ بِكُمْ رَحِيمًا {29}

Enyi ambao mmeamini! Msiliane mali zenu baina yenu kwa batili. Ila itakapokuwa ni biashara kwa kuridhiana baina yenu. Wala msijiue. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye rehema kwenu.

وَمَنْ يَفْعَلْ ذَٰلِكَ عُدْوَانًا وَظُلْمًا فَسَوْفَ نُصْلِيهِ نَارًا ۚ وَكَانَ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّهِ يَسِيرًا {30}

Na atakayefanya hilo kwa uadui na dhulma, tutamtia motoni. Na hilo kwa Mwenyezu Mungu ni jepesi