read

Aya 29-30: Msiliane Mali Zenu Kwa Batili

Enyi ambao mmeamini! Msiliane mali zenu baina yenu kwa batili.

Jumla kama hii imekwishapita pamoja na tafsiri yake katika Aya ya 188 ya Sura ya Baqara. Tunaunganisha yaliyotangulia na Hadith iliyopokewa kutoka kwa Imam Jafar as-Sadiq (a.s.), kwamba Mwenye deni akiwa anayo mali, akaitumia katika haja yake bila ya kulipa deni, basi amekula mali ya batili bali ni juu yake kulipa deni; hata kama atahitajia sadaka." Inajuzu kwake kutumia mahitaji ya siku moja tu na usiku wake.

Ila itakapokuwa ni biashara kwa kuridhiana baina yenu.

Neno baina yenu ni ishara ya kwamba hapana budi kuridhiana pande mbili. Kusamehewa huku kunafahamisha kuwa biashara haishurutiwi kuwa bidhaa mbili za kubadilishana ziwe sawa sawa bila ya kupungua. Kwa sababu hilo linakurubia kuwa ni muhali. Kwa hivyo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemruhusu mnunuzi au muuzaji kula kinachozidi maadamu pande zote mbili zimekubaliana, lakini kwa sharti ya kutokuwapo kughushiana na kudanganyana.

Unaweza kuuliza: Kama mfanya biashara akiitangaza bidhaa yake na akaipamba; je itakuwa ni kughushi na kula mali ya batili?

Jibu: Hapana, lakini bei ikiwa ni kwa masharti ya sifa maalum; kisha ikawa kinyume, basi mnunuzi anayo hiyari ya kuvunja bei na kurudisha bidhaa kwa muuzaji, naye apewe pesa zake.

Wala msijiue yaani baadhi yenu wasiwaue wengine. Hapo pana ufahamisho wa umoja wa ubinadamu. Kuna Hadith tukufu isemayo: "Waumini ni kama nafsi moja."

Imesemekana kuwa maana ya msijiue, ni kuwa msijiingize katika majanga kwa kufanya mliyokatazwa na Mwenyezi Mungu. Maana hayo yako sahihi, lakini yanatofautiana na dhahiri ya Aya.

Na atakayefanya hilo kwa uadui na dhulma, tutamtia motoni.

Hilo ni ishara ya kujiua, kula mali kwa batili, uadui na kuipetuka haki. Inawezekana kutofautisha baina ya uadui na dhulma; kwamba dhuluma inakuwa kwa mtu mwenyewe kujidhulumu na kumdhulumu mwingine. Ama uadui ni kwa kumfanyia mwingine tu.

Kwa vyovyote ni kwamba, mwenye kusahau, kukosea au kulazimishwa, hasi- fiki na dhuluma wala uadui, isipokuwa mwenye kulazimishwa kuua. Kwa mfano: Dhalimu mwenye uwezo akimwambia mtu: 'Muue huyu au nitakuua wewe.'

Hapo haijuzu kwa mtu huyo kuua hata kama ana hakika kuwa huyo aliyemwamrisha anaweza kumuua. Kwa sababu haifai mtu kujikinga kwa kumwingiza mwengine kwenye madhara. Kwa hiyo kama mtu huyo akitekeleza agizo la dhalimu na akaua, basi naye atauliwa na kulipiziwa kisasi, na yule dhalimu aliyeamuru mauaji atafungwa maisha.

إِنْ تَجْتَنِبُوا كَبَائِرَ مَا تُنْهَوْنَ عَنْهُ نُكَفِّرْ عَنْكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَنُدْخِلْكُمْ مُدْخَلًا كَرِيمًا {31}

Mkijiepusha na (madhambi) makubwa mnayokatazwa, basi tutawafutia makosa yenu (madogo) na tutawatia mahali patukufu