read

Aya 31: Madhambi Makubwa

Maana

Qur'an Tukufu imegawanya madhambi kwenye mafungu mawili: Makubwa na madogo. Mgawanyo huu umekuja katika Aya kadhaa. Kama vile Aya hii tuliyo nayo. Kwa sababu makusudio ya; basi tutawafutia makosa yenu ni yale makosa madogo; kama walivyoafikiana wafasiri. Na maana yake ni mwenye kujiepusha na madhambi makubwa hufutiwa madogo.

Aya nyengine zinazoyagawanya madhambi kwenye sehemu mbili ni kama hizi zifuatazo: "Wale ambao wanajiepusha na madhambi makubwa na maovu isipokuwa makosa madogo." (53:32)

"Haiachi dogo wala kubwa ila hulihisabu." (18:49)
"Na amewafanya muuchukie ukafiri na ufasiki na uasi." (49:7)

Hapa inabainika kwa yaliyokatazwa ni mambo matatu: Ukafiri ambao ni ukanushaji na upingaji, ufasiki ambao ni kufanya madhambi makubwa na uasi ambao ni kufanya madhambi madogo.

Kwa hiyo inatubainikia kuwa kauli ya mwenye kusema: Dhambi zote ni kubwa wala hakuna ndogo, kwa vile kumwasi Mwenyezi Mungu katika jambo ni kukubwa, hata kama jambo lenyewe ni dogo, ni wazi kuwa kauli hii inakhalifu dhahiri ya Qur'an. Zaidi ya hayo, hata sharia za kutungwa pia zinagawanya makosa kwenye mafungu mawili: Kosa kubwa na dogo. Hata hivyo inawezekana kukanusha madhambi madogo kwa njia fulani tutakayoionyesha.

Kwa namna yoyote iwayo, ni kwamba Kitabu Kitukufu (Qur'an) hakikuweka mpaka wa kupambanua dhambi ndogo na kubwa. Kwa hiyo wametofautiana Mafaqihi katika maana ya dhambi kubwa. Kundi moja limesema kuwa kila lililokuja katika Qur'an kwa kukutanishwa na kiaga cha akhera hilo ni kubwa na lisilokuwa hilo ni dogo; kauli bora ni ile ya aliyesema: Hakika dhambi zote ni kubwa hizo zenyewe - kama alivyosema mwenye kukanusha dhambi ndogo - isipokuwa zinagawanyika ndogo na kubwa kwa kulinganishwa na nyengine.

Kwa mfano kumwangalia mwanamke wa kando kwa matamanio ni dhambi kubwa hilo lenyewe lakini ni dogo kulinganishwa na kumpiga busu, nako pia ni kudogo kulinganisha na kumwingilia. Au kula kwenye meza iliyo na pombe ni dhambi kubwa, lakini kwa kulinganisha na kunywa pombe yenyewe itakuwa ni dhambi ndogo.

Kwa hakika mtendaji dhambi na vivutio vyake vina athari kubwa katika kuifanya dhambi iwe kubwa au dogo; kama walivyosema Mafaqihi; na uhalifu au kosa la jinai; kama walivyosema wanasheria wapya. Kwa hiyo basi kabla ya kuichukulia dhambi kuwa ni ndogo au kubwa, ni lazima tumwangalie mtendaji kwanza, je amefanya aliyoyafanya kwa kutojua na udhaifu wa matakwa yake; kama vile kughilibiwa na mpotezaji mwenye dhambi; au alifanya kwa haja ya dharura; au ni kwamba yeye ana shauku ya kuwafanyia maovu watu; kama walivyo watu wengi. Zimekuja Hadith mutawatir kutoka kwa Mtume kwamba yeye amesema: "Hakika amali zote huzingatiwa kwa nia tu …"

Hadith nyengine inasema: "Hakuna dhambi ndogo pamoja na kung'ang'ania, wala hakuna dhambi kubwa pamoja na kutubia."

Kutoka kwa Imam as-Sadiq anasema: "Hakika watu wa motoni watawekwa milele motoni, kwa vile nia zao ni kumwasi Mwenyezi Mungu katika dunia milele, kama wangebaki. Na hakika watu wa peponi watawekwa milele peponi kwa vile nia zao zilikuwa ni kumtii Mwenyezi Mungu milele. Kwa hiyo ni kutokana na nia ndio wamewekwa milele hawa na wale." Tumefafanua athari ya nia katika kutafsiri Aya ya 144 Al-Imran.

Litakuwa ni jambo zuri tutaje Hadith iliyopokewa kutoka kwa Imam Jafar as- Sadiq (a.s.) akielezea aina za madhambi makubwa. Imepokewa kwamba Amru bin Ubaid, alikwenda kwa Imam na kumwuliza kuhusu madhambi makubwa katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu, naye akasema: "Kubwa ya madhambi makubwa ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu: "Hakika Mwenyazi Mungu hasamehi kwa kushirikishwa" (4:48).

Na akasema: "Kwa hakika anayemshirikisha Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu amemharamishia pepo na makazi yake ni motoni. " (5:72)

Dhambi kubwa jengine ni kukata tamaa ya rehema ya Mwenyezi Mungu, kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema: "Wala hawakati tamaa ya rehema ya Mwenyezi Mungu ila watu Makafiri." (12:87)

Jingine ni kujiaminisha na hila (adhabu) za Mwenyezi Mungu. Kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema: "Hawajiaminishi na hila (adhabu) za Mwenyezi Mungu ila watu wenye hasara". (7:99).

Vilevile kuwaudhi wazazi wawili, kwa sababu Mwenyezi Mungu amekufanya kuwaudhi wazazi ni ujeuri na uovu katika kauli yake: "Na kuwatendea wema wazazi wangu wala hakunifanya niwe jeuri muovu." (19:32).

Pia kuua nafsi aliyoiharamisha Mwenyezi Mungu ila kwa haki, kwa kauli yake Mwenyezi Mungu: "Na mwenye kumuua muumini kwa kukusudia, basi malipo yake ni Jahanam atadumu humo" (4:93).

Miongoni mwa madhambi makubwa ni kuwasingizia wanawake watakatifu kwani Mwenyezi Mungu anasema: "Hakika wale ambao wanawasingizia wanawake wanaojiheshimu, walioghafilika (na zina), wamelaaniwa katika dunia na akhera; nao watapata adhabu kubwa." (24:23)

Jingine ni kula mali ya yatima; kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu: "Hakika wale wanaokula mali ya yatima kwa dhulma, bila shaka wanakula moto matumboni mwao na wataingia motoni" (4:10)

Pia kukimbia vita, kwani Mwenyezi Mungu anasema: "Ambao wanakula riba; hawatainuka, ila kama ainukavyo ambaye amezugwa na shetani kwa wazimu." (2:275)

Na uchawi, kwani Mwenyezi Mungu anasema: "Wakajifunza kwao mambo ambayo kwayo waliweza kumfarikisha mtu na mkewe … Na hakika wanajua kwamba aliyenunua haya hatakuwa na sehemu yoyote katika akhera." (2:102)

Pia zina, kama anavyosema Mwenyezi Mungu: "… Wala hawazini; na atakayeyafanya hayo atapata adhabu. Na ataongezewa adhabu siku ya Kiyama atadumu humo kwa kufedheheka." (25: 68-69)

Vilevile dhambi kubwa ni kiapo cha kuzamisha1 kwani Mwenyezi Mungu anasema: “Hakika wale wanaouza ahadi ya Mwenyezi Mungu na viapo vyao kwa thamani ndogo, hao hawatakuwa na thamni yoyote akhera (3:77)

Pia kufanya hiana, kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema: Na Mwenye kufanya hiyana, atayaleta yale aliyoyafanyia hiyana siku ya Kiyama (3:161)

Na kuzuia kutoa Zaka pia ni dhambi kubwa kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu: "Siku (mali yao) itakapotiwa joto katika moto wa Jahannamu na kwayo vitachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao (waambiwe) haya ndiyo mliyolimbikizia nafsi zenu, basi onjeni (adhabu ya) yale mliyokuwa mkiyalimbikiza." (9:35)

Pia kutoa ushahidi wa uongo na kuuficha ushahidi. Kwani Mwenyezi Mungu anasema: ".. Wala msiufiche ushahidi.

Na atakayeuficha, basi hakika moyo wake ni wenye kuingia dhambini … " (2:283) Jingine ni kunywa pombe. Kwa sababu Mwenyezi Mungu amelinganisha na kuabudu masanamu.

Kuacha Swala makusudi au chochote alichofaradhisha Mwenyezi Mungu. Kwa sababu Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) anasema: "Mwenye kuacha Swala makusudi atakuwa ameepukana na dhima ya Mwenyezi Mungu na dhima ya Mtume wake na atakuwa amevunja ahadi."

Na kuvunja udugu, kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema: "… Na wanakata aliyoamuru Mwenyezi Mungu yaungwe na wanafanya uharibifu katika nchi; hao ndio watakaopata laana na watapata nyumba mbaya." (13: 25).

Hapo Amr bin Ubaid akatoka na kilio huku akisema: "Ameangamia anayesema kwa maoni yake na kubishana nanyi katika fadhila na elimu enyi watu wa nyumba ya Mtume!"

وَلَا تَتَمَنَّوْا مَا فَضَّلَ اللَّهُ بِهِ بَعْضَكُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ ۚ لِلرِّجَالِ نَصِيبٌ مِمَّا اكْتَسَبُوا ۖ وَلِلنِّسَاءِ نَصِيبٌ مِمَّا اكْتَسَبْنَ ۚ وَاسْأَلُوا اللَّهَ مِنْ فَضْلِهِ ۗ إِنَّ اللَّهَ كَانَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا {32}

Wala msitamani aliyowafadhili Mwenyezi Mungu baadhi yenu kuliko baadhi nyingine. Wanaume wana fungu katika walichokichuma na wanawake wana fungu katika walichokichuma. Na muombeni Mwenyezi Mungu fadhila zake. Hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa kila kitu.

وَلِكُلٍّ جَعَلْنَا مَوَالِيَ مِمَّا تَرَكَ الْوَالِدَانِ وَالْأَقْرَبُونَ ۚ وَالَّذِينَ عَقَدَتْ أَيْمَانُكُمْ فَآتُوهُمْ نَصِيبَهُمْ ۚ إِنَّ اللَّهَ كَانَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدًا {33}

Na kila watu tumewawekea wa kuwarithi yale waliyoacha wazazi wawili na jamaa na wale mliofungamana nao ahadi wapeni sehemu yao. Hakika Mwenyezi Mungu ni shahidi wa kila kitu.
  • 1. Kiapo cha kuzamisha ni kiapo cha uongo ambacho kinamzamisha mtu motoni.