read

Aya 32 - 33: Na Muombeni Mwenyezi Mungu Fadhila Zake

Lugha

Neno Mawali ni wingi wa Maula. Neno hili lina maana nyingi; kama vile bwana aliyemwacha huru mtumwa wake; mtumwa aliyeachwa huru; na maana nyingine ni mwenye kurithi. Haya ndiyo maana yaliyokusudiwa katika Aya hii. Na neno Aymanikum ni wingi wa Yamini kwa maana ya kiapo au kwa maana ya mkono kwa sababu watu hupeana mkono wanapofungiana ahadi.

Maana

Wala msitamani aliyowafadhili Mwenyezi Mungu baadhi yenu kuliko baadhi nyingine.

Dhahiri ya katazo hili inaonyesha kuwa haijuzu kwa mtu kutamani kile ana- chokiona ni kizuri kilicho kwa mwenzake; ni sawa iwe ni kwa husuda,yaani kutaka mwenzake aondokewe na neema hiyo; au hata kwa wivu mzuri, yaani kutaka asiondokewe na neema hiyo na yeye apate kama hivyo.

Lakini dhahiri ya Aya siyo makusudio, kwa sababu wivu mzuri hauna ubaya wala madhara. Ama hasadi ni haramu ikiwa kuna kuhusudiana au kuingilia hekima ya Mwenyezi Mungu. Amesema Mtume Mtukufu (s.a.w.): "Ukifanya hasadi usiitokeze!" Yaani ukihisi katika nafsi yako kutaka mwenzako aondokewe na neema usiyokuwa nayo basi jizuiwe na usiitoe uipige vita isije ikadhihirika nje kwa kauli au kitendo. Ukiweza kufanya hivyo, basi wewe huna jukumu lolote mbele za Mwenyezi Mungu, lakini ukishindwa kufanya hivyo basi wewe ni mwenye dhambi.

Hali hii pekee ndiyo inayokatazwa katika Aya. Kwa sababu kauli ya Mtume (s.a.w.) ni ubainifu na tafsiri yake. Ikiwa inajuzu kwa mtu kutamani mfano wa yaliyo kwa mwengine bila ya husuda, basi kutamani kheri kutakuwa kunafaa zaidi bila ya kuangalia aliyomfadhili Mwenyezi Mungu mtu mwengine. Mwenyezi Mungu anasema katika kusifu hayo: "Na miongoni mwao wako wasemao: Mola wetu tupe mema duniani na (tupe) mema akhera na utulinde na adhabu ya moto." (2:201)

Wanaume wana fungu katika walichokichuma na wanawake wana fungu katika walichokichuma.

Katika tafsir Majmaul-bayan, imeeleza hivi: Ulikwenda ujumbe wa wanawake kwa Mtume (s.a.w.) ukasema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwani Mwenyezi Mungu siye wa wanaume na wanawake? Na wewe si ni Mtume wa wote? Basi kwa nini Mwenyezi Mungu anawataja wao tu, na wala hatutaji sisi? Tunahofia kuwa sisi hatuna maana yoyote na kwamba Mwenyezi Mungu hana haja nasi!" Hapo ikashuka Aya hii.

Maana ya dhahiri ni kuwa kila mtu atapata natija ya amali yake. Kwa hiyo haitakikani mtu kuishughulisha nafsi yake na husuda. Kwa sababu madhara yake yatamrudia mwenyewe duniani na akhera. Imam Ali (a.s.) anasema: "Msihusudiane, kwani husuda inakula imani, kama moto ulavyo kuni." Amesema tena: "Siha ya mwili ni hasadi kuwa chache ."

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewataja wanawake kwa kukumbusha kuwa mke na mume ni sawa kila mmoja wao katika kupata alichokichuma. Mwenyezi Mungu amesema: "… Mimi sitapoteza amali ya mfanya amali miongoni mwenu akiwa mwanamme au mwanamke ni nyinyi kwa nyinyi." (3:195)

Kumwomba Mwenyezi Mungu Bila Ya Kufuata Njia Yake

Na muombeni Mwenyezi Mungu fadhila zake.

Kwa sababu hazina yake haishi, na neema zake hazihisabiki. Imam Zainul-Abidin katika baadhi ya dua zake anasema: "Ninajua- Ewe Mola wangu - kwamba mengi ninayokuomba ni mepesi kwako; na kwamba chungu ya mambo ninayokutaka unipe si lolote katika ukunjufu wako; na kwamba ukarimu haumdhikishi yeyote kukuomba; na kwamba utoaji wako ni zaidi ya wa yeyote."

Kuna Hadith isemayo: "Mwombeni Mwenyezi Mungu fadhila zake na Mwenyezi Mungu hupenda kuombwa."

Unaweza kuuliza kuwa amri ya kuomba inasababisha ulazima wa kujibiwa na inajulikana wazi kuwa watu wote au wengi wao wanaomba na kuomba, lakini hawajibiwi maombi yao?

Jibu: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kama alivyoamrisha kuomba dua, pia ameamrisha kujishughulisha na kujitahidi; na akasema: "Na kwamba mtu hatapata ila aliyoyachuma." (53:39)

Maana ya haya ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amedhamini kuitikia dua kwa njia ya kujishughulisha na amali, na wala hakudhamini kila ayawazayo mtu kwa kutaka tu na kuomba. Vipi isiwe hivyo? Lau angelifanya hivyo, ungeliharibika ulimwengu. Kisha je, Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mwenye kuamuru au kuamriwa? Na atafanya nini kama atapokea maombi mawili yanayopingana wakati mmoja? Na mwisho utasemaje kwa yule anayeomba na hafuati njia yake?

Kwa hivyo basi amri yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ya kuomba fadhila zake, ni ibara ya pili baada ya amri ya kujitahidi na kufanya amali; na kwamba ni juu ya mtu kuelekea kwenye shughuli zake akimtegemea Mwenyezi Mungu peke yake na kutomwingilia mwengine katika shughuli zake, kutokana na fadhila alizopewa na Mwenyezi Mungu. Hakuna mtu yeyote aliye shughulishwa na mambo ya mwengine ila husongwa katika maisha yake, hudangana na kukosa namna katika mambo yake yote.

Kuna wanafunzi wenzangu fulani niliosoma nao huko Najaf, wakiwa werevu na wenye akili sana. Wakamaliza miaka mingi hapo Najaf, lakini pamoja na hayo hawakufaulu, si kwa lolote isipokuwa walishughulishwa na kuangalia mambo ya watu kuliko nafsi zao na masomo yao. Hakukosea aliyesema: "Mwenye kuchunguza mambo ya watu atakufa na kibuhuti." Tumezungumza kwa ufafanuzi kuhusu dua na kuitikiwa kwake katika kufasiri Aya 186 ya sura ya Baqara.

Na kila watu tumewawekea wa kuwarithi yale waliyoacha wazazi wawili na jamaa na wale mliofungamana nao ahadi wapeni sehemu yao.

Mwenyezi Mungu amewataja warithi wa aina tatu:

(i) Wazazi wawili wakiwemo mababu na mabibi.

(ii) Jamaa wa karibu wakiwemo watoto, akina kaka na akina dada, ami, shangazi na wajomba na khala.

(iii) Mfungamano maalum; kama vile ndoa, umiliki au mfungamano wakudhaminiana. Vile vile mfungamano wa kijumla ambao ni Uislam.

Wote hawa wanaingia katika kauli ya Mwenyezi Mungu "Na mliofungamana nao ahadi." Mfungamano wa ndoa ni maarufu.Ama mfungamano wa miliki ni mtu kummiliki mtumwa, kisha akamwacha huru kwa ajili ya Mwenyezi Mungu bila ya kutoa chochote au kuwa ni kafara. Mtumwa huyu huria akifa na akawa hana mrithi basi mrithi wake atakuwa yule aliyemwacha huru. Mfungamano wa kudhaminiana, ni kuafikiana wawili kila mmoja amdhamini mwenzake, au mmoja tu adhamini.

Yakikamilika maafikiano haya kwa masharti yaliyotajwa katika vitabu vya Fiqhi, basi ni juu ya mdhamini kumdhamini mwenzake na pia atamrithi mdhaminiwa ikiwa hana mrithi.

Ama mfungamano wa kiislam makusudio yake ni mafugamano ya kijumla baina ya Mtume na aliyemwamini. Mwislamu akifa na hana mrithi kabisa, basi atarithiwa na Mtume au atakayekuwa katika nafasi yake.

Imepokewa hadith kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwamba yeye amesema: "Mimi ni mrithi wa asiye na mrithi" katika riwaya ya pili anasema: "Mimi ni msimamizi wa asiye na msimamizi." Na katika riwaya ya tatu: "Mimi ni bwana wa huria asiye na mrithi, ninamrithi mali yake na kumwacha huru."

Inatosha kuwa ni dalili ya hayo kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Nabii ni bora zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao" (33:6)

Katika kitab Wasailu-Shia kuna Hadith kadhaa zisemazo kuwa Ali (a.s.) alikuwa akisema: "Mtu akifa na akaacha mali bila ya mrithi, wapeni mali (hiyo) watu wa mjini kwake." Hii haipingani na kauli ya Mtume. Kwa sababu Mtume aliwahi kuwapa haki yake hii mafukara wa mji wa marehemu.

Yamekwishatangulia maelezo kuhusu mafungu ya baba, mama ndugu mume na mke, katika Aya ya 12 ya sura hii.

الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ بِمَا فَضَّلَ اللَّهُ بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ وَبِمَا أَنْفَقُوا مِنْ أَمْوَالِهِمْ ۚ فَالصَّالِحَاتُ قَانِتَاتٌ حَافِظَاتٌ لِلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ اللَّهُ ۚ وَاللَّاتِي تَخَافُونَ نُشُوزَهُنَّ فَعِظُوهُنَّ وَاهْجُرُوهُنَّ فِي الْمَضَاجِعِ وَاضْرِبُوهُنَّ ۖ فَإِنْ أَطَعْنَكُمْ فَلَا تَبْغُوا عَلَيْهِنَّ سَبِيلًا ۗ إِنَّ اللَّهَ كَانَ عَلِيًّا كَبِيرًا {34}

Wanaume ni wasimamizi wa wanawake, kwa sababu Mwenyezi Mungu amewafadhili baadhi yao kuliko wengine na kwa sababu ya mali zao wanazozitoa; basi wanawake wema ni wale wenye kutii na kujilinda hata katika siri, kwa kuwa Mwenyezi Mungu ameamrisha wajilinde Na ambao mnaogopa unashiza wao, basi wanasihini na muwahame katika vitanda na wapigeni. Watakapowatii msiwatafutie njia. Hakika Mwenyezi Mungu ni mtukufu mkubwa.

وَإِنْ خِفْتُمْ شِقَاقَ بَيْنِهِمَا فَابْعَثُوا حَكَمًا مِنْ أَهْلِهِ وَحَكَمًا مِنْ أَهْلِهَا إِنْ يُرِيدَا إِصْلَاحًا يُوَفِّقِ اللَّهُ بَيْنَهُمَا ۗ إِنَّ اللَّهَ كَانَ عَلِيمًا خَبِيرًا {35}

Na kama mkihofia ugomvi ulio baina yao, basi wekeni mwamuzi mmoja katika watu wa mume na mwamuzi mmoja katika watu wa mke. Wakitaka suluhu basi Mwenyezi Mungu atawawezesha, Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye habari.