read

Aya 34 - 35: Wanaume Ni Wasimamizi Wa Wanawake

Maana

Wanaume ni wasimamizi wa wanawake. Kwa sababu Mwenyezi Mungu amewafadhilisha baadhi yao kuliko wengine.

Mwanamume na mwanamke ni nguzo mbili za maisha. Ni muhali mmoja wao kuwa bila ya mwingine. Maana ya haya ni kuwa kati ya mume na mwanamke kuna aina ya kutofautiana. Lau wangelikuwa sawa katika pande zote, basi wasingelihitajiana na ingelikuwa kuwako na kutakuwako ni sawa. Kwa hivyo basi mwito wa kuwa sawa katika kila kitu unahalifu mantiki ya maisha.

Huenda mtu akasema kuwa mwanamke na watetezi wake wanataka usawa katika haki na majukumu na wala hawataki usawa na mwanamume katika kila kitu; mfano kutunga mimba na kunyonyesha.

Jibu: Tofauti ya viungo inasababisha ulazima wa kutofautiana katika baadhi ya haki na mambo yaliyo wajibu, na hata katika baadhi ya matamanio ya kinafsi. Kwa hiyo basi anayetaka usawa katika haki zote na majukumu yote, atakuwa ameenda mbali sana, sawa na yule anayetaka utofauti katika yote.

Ilivyo hasa ni kwamba mwanamume na mwanamke wanalingana sawa katika haki nyingi; za muhimu zaidi ni usawa mbele ya Mwenyezi Mungu, kanuni, uhuru wa matumizi ya mali, hiyari ya kuchagua mshirika wa maisha n.k. Na wanatofautiana katika baadhi ya haki.

Katika kufasiri Aya 228 Sura Baqara, tumetaja tofauti 14 baina ya mwanamume na mwanamke katika sharia ya kiislam. Ama Aya hii tuliyonayo inafa- hamisha mambo haya yafuatayo:

1. Wanaume ni wasimamizi wa wanawake. Makusudio ya wanaume hapa ni kuwahusu waume wa ndoa; na wanawake, ni wake wa ndoa. Makusudio ya usimamizi sio mamlaka yote, kiasi cha kumfanya mume kuwa ni kiongozi dikteta na mke kuwa ni mwenye kuongozwa asiyekuwa na matakwa au hiyari yoyote, la! Si hivyo, bali makusudio ni kuwa mume ana aina ya usimamizi. Mafakihi wameueleza usimamizi huo, ikiwa ni pamoja na kuifanya talaka iwe mikononi mwa mume, kumtii kitandani na kutotoka nyumbani mke ila kwa idhini ya mumewe. Zaidi ya hayo wako sawa.

2. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametaja sababu mbili za aina hii ya utawala wa mume kwa mke. Ameashiria sababu ya kwanza kwa kusema: Kwa sababu Mwenyezi Mungu amewafadhilisha baadhi yao kuliko wengine. Na sababu ya pili kwa kusema: Na kwa sababu ya mali zao wanazozitoa.

Tuanze na sababu ya kwanza: Dhamiri katika baadhi yao inawarudia wanawake na wanaume pamoja; na makusudio ya baadhi ya kwanza ni wanaume na baadhi ya pili ni wanawake. Unaweza kuuliza kwanini Mwenyezi Mungu hakusema Alayhinna (juu yao wanawake) ambapo ingekuwa wazi zaidi?

Jibu: Lau angelisema hivyo ingelikuwa makusudio ni kufadhilisha wanaume wote juu ya wanawake wote; na hayo siyo makusudio yake. Kwa sababu hili liko mbali na hali ilivyo.

Kuna wanawake kadhaa ambao ni bora kuliko wanaume elfu. Kwa hiyo ndio limekuja neno 'baadhi' peke yake kuashiria kwamba ubora ni wa jinsi fulani kwa jinsi nyingine bila ya kuangalia watu wote.

Mwenyezi Mungu ameficha aina ya ubora kwa kusema: Kwa sababu Mwenyezi Mungu amefadhilisha baadhi yao.

Wafasiri na wengineo wamesema kuwa mwanamume ana nguvu zaidi kuliko mwanamke katika mweko wake wa viungo na kiakili; na wakarefusha maneno na dalili katika hilo. Kuna miongoni mwao waliotunga vitabu mahsusi katika maudhui haya.

Tunayoyashuhudia ni kwamba kazi muhimu katika nyanja za elimu, dini, fani falsafa na siasa zote zinashikiliwa na wanaume na wala sio wanawake. Kama itatokea mwanamke, basi itakuwa ni nadra sana; na unadra unatilia mkazo desturi na sio kama unaikanusha.

Zaidi ya hayo tumeshuhudia mwanamke kabla ya chochote, akijishughulisha zaidi na vipodozi na mavazi ambayo yanaunda uke wake na kudhihirisha uchi wake na kujibadilisha kwa namna ambayo anaweza kumvutia mwanamume na kumwamsha hisia zake. Kwa hali hiyo ndio ukaona kuwa majumba ya mitindo ya mavazi ni kwa ajili ya wanawake tu. Wala hakuna tafsir ya kujishghulisha na uke wake; na mwanamume kujishughulisha na kazi muhimu katika nyanja za maisha ila ni kubainisha umbile na nafsi baina ya mwanamke na mwanamume.

Ama sababu ya pili ya ubora wa mwanamume ambao ameubainisha Mwenyezi Mungu kwa kusema: ‘Na kwa mali zao walizozitoa’, iko wazi kama tulivyoieleza katika sababu ya kwanza. Kwa sababu ambaye anachukua jukumu la kuwakimu wengine, hapana budi kuwa ni bora kuliko yule asiyetakiwa lolote; hata kujikimu yeye mwenyewe tu.

Kwa hakika kauli yake hiyo Mwenyezi Mungu: Na kwa mali zao walizozitoa, imetosha kuwa mume asipomkimu mkewe, hawezi kuwa msimamizi wake; au mke anaweza kutaka talaka kupitia kwa kadhi; na ni juu ya kadhi kumwonya mume.

Ikiwa mume ataendelea kumnyima matumizi, kwa kushindwa au kwa inadi, basi Kadhi atamwamrisha atoe talaka. Kama akikataa kutoa talaka, Kadhi atatoa talaka, kwa sababu Kadhi ni msimamizi wa anayekataa.

Hivi ndivyo asemavyo Maliki, Shafii na kundi la wanavyuoni wa Kishia akiwemo mwenye Urwatul-wathqa na Sayyid Muhsin Hakim. Nasi pia twaunga mkono rai hii. Suala hili tumeliwekea mlango maalum katika kitab Fiqhul-Imam Jafar as-Sadiq kwa kichwa cha habari 'Talaka ya kukosa kukimu.' Humo tume- onyesha dalili na kauli kwa ufafanuzi.

Wanawake wema ni wenye kutii na kujilinda hata katika siri, kwa kuwa Mwenyezi Mungu ameamrisha wajilinde.

Mke mwema ni yule mwenye kuafikiana kinyumba na mumewe, mwenye kujichunga, kulingana na alivyoamrishwa na Mwenyezi Mungu. Hamwasi mumewe katika mambo aliyohalalishiwa na Mwenyezi Mungu, wala hamtii katika mambo aliyoharamishiwa na Mwenyezi Mungu.

Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.): "Mwanamke ni yule anayekufurahisha ukimwangalia; anayekutii ukimwamrisha; na ukiwa mbali naye, hujichunga yeye mwenyewe na mali yako."

Maelezo ya unyumba hayaishi; wala hakuna yeyote anayejua siri iliyoko katika kauli ya asemaye: "Sioi tena hata mkinichinja;" isipokuwa yule aliyeoa tu. Baadhi ya wanawake ni saratani inayoua pole pole, Ikiwa kuna mtu aliye huru mwenye hiyari, basi mtu huyo ni kapera.

Ama mwenye mke hana uhuru wala hiyari isipokuwa wachache sana. Baadhi ya dini zinasema kuwa kesho Mwenyezi Mungu hatawaadhibu kwa moto wala hatawapa thawabu kwa pepo, bali yule mwasi atamwoza kikongwe kilichojishia kinachomchukiza umbo na tabia, na ataozwa mtiifu msichana mzuri anayemfurahisha kiumbo na tabia!

Na ambao mnaogopa unashiza wao, basi wanasihini, muwahame katika malazi na wapigeni.

Makusudio ya unashiza ni kuacha kutekeleza haki za unyumba. Unashiza unaweza kuwa kwa mke tu, au mume tu, au wote pamoja.

Baada ya Mwenyezi Mungu kumtaja mwanamke mwema, sasa anamtaja mwanamke mwasi (nashiza); na akamuhalalishia mume kumwonya mkewe nashiza. Akiendelea amuhame kitandani. Akiwa bado anaendelea ampige kipigo hafifu cha kumtia adabu sio cha kumtesa-kipigo kisichoumiza wala kugeuza rangi ya ngozi;kama ilivyoelezwa katika vitabu vya fiqh.
Ieleweke kwamba; kutoa onyo, kususia kulala naye na kupiga ni ruhusa tu, sio wajibu. Mafakihi wote wameafikiana kuwa kuacha kupiga ni bora; na kwamba anayevumilia maudhi ya mke, wala asimpige ni bora kwa Mungu, kuliko anayempiga; kama walivyoafikiana kuwa kila itakapopatikana njia nyepesi zaidi, basi itumike na kuwa haramu kutumia njia ngumu.

Mtume (s.a.w.) amesema: "Asimpige mmoja wenu mkewe kama anavyompiga ngamia; anampiga mchana kisha analala naye usiku. Mbora wenu ni mbora wenu kwa familia yake, na mimi ni mbora wenu kwa familia"

Jambo la kushangaza ni kwamba Tabari ambaye anasifika kuwa ni Sheikh wa wafasiri, amesema katika kufasiri Aya hii kwamba ni amri kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa mume, ikiwa mkewe atamuasi amfunge kwa kamba - kama amfungavyo ngamia - katika nyumba anayolala naye. lililomfanya kufasiri hivi ni kwamba Waarabu wanaiita kamba wanyomfungia ngamia

'Hijaria', kwa hivyo maana ya 'Uhjuruhunna' ni wafungeni kwa hiyo 'Hijara' ni kufunga na sio kuwahama. Jibu zuri sana la tafsir hii, ni kauli ya Zamakhshari; "Na hii ni katika tafsiri nzito kufahamika."

Watakapowatii msiwatafutie njia katika zile njia tatu. Kwa sababu kuonya, kumwacha kitandani, na kipigo ni njia ya kutafuta utiifu. Kwa hiyo lengo lik- itimia hakuna haja ya njia.

Kauli yake hii Mwenyezi Mungu inaonyesha kuwa haifai kwa mume kutafuta sababu za uongo za kumuudhi mke; hata kama mke anamchukia mumewe. Maadam anamtekelezea haki zake za kisharia. Kwa sababu pendo na chuki viko nje ya uwezo wa mtu. Na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hahisabu wala kuad- hibu isipokuwa kauli inayodhihiri au kitendo kinachodhihiri.

Hakika Mwenyezi Mungu ni Mtukufu mkubwa

Arrazi anasema kwamba makusudio ya kauli hii ya Mwenyezi Mungu, kwa ufupi ni:

1. Kuwatisha wanaume wasiwadhulumu wanawake.

2. Mwenyezi Mungu hakalifishi isipokuwa haki.

3. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakalifishi lisilowezekana. Kwa hiyo ni juu ya mume kutowakalifisha wanawake wasioyaweza.

4. Mwasi hakalifishwi akitubia kutokana na uasi wake, basi nashiza akitubia, msimwadhibu.

5. Mwenyezi Mungu hafichui siri, kwa hiyo nyinyi ndio mnatakikana zaidi msifichue dhahiri ya hali ya mke; wala msitafute yaliyo moyoni mwake.

Arrazi ni katika Ashaira, wasemao kwamba Mwenyezi Mungu anamkalifisha mwanadamu asiloliweza. Naye ni mtetezi wa madhahebu haya kwa nguvu zake zote, ametetea katika sehemu nyingi kwenye tafsiri Al-kabir, hasa pale alipofasiri Aya isemayo: "Haikalifishi Mwenyezi Mungu nafsi yoyote ila uweza wake." (2:286)

Lakini hapa ameyasahau madhehebu yake na kurudia kwenye umbile safi ambalo Mwenyezi Mungu amewaumbia watu, Akasema: (Ninamnukuu) "Hakika Mwenyezi Mungu hawakalifishi msioyaweza. Kwa hiyo msiwakalifishe wanawake wawapende kwa sababu wao hawawezi hilo."

Na kama mkihofia ugomvi ulio baina yao, basi wekeni mwamuzi mmoja katika watu wa mume na mwamuzi mmoja katika watu wa mke.

Aya iliyotangulia imeonyesha uasi wa mke; na Aya hii inaonyesha uasi wa mke na mume kwa kutokutekeleza kila mmoja wao haki ya mwingine.

Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Mkihofia ugomvi ulio baina yao’ anakusudia kuhofia kuendelea ugomvi; na dhamiri katika 'mkihofia' na 'wekeni' inaelekezwa kwa makadhi. Amri ya kuwaweka waamuzi wawili ni ya sunna, siyo ya wajibu, lengo lake ni kupatikana suluhu, na kuhifadhi familia kwa kuhofia watoto wasipotee.

Ni sharti kwa mwamuzi awe na uwezo wa kusuluhisha. Kwa sababu (kuna msemo) 'asiye nacho hatoi.' Pia inafaa kuwa si katika jamaa; kwa sababu udugu si sharti katika uamuzi wala katika uwakili. Umetajwa udugu katika Aya kwa kuwa ni bora tu, sio kwa ulazima. Kwa sababu wao wanajua hali kwa undani zaidi, wenye huruma na wanaoweza kuficha siri.

Kazi ya waamuzi wawili ni kutafuta suluhu. Wakishindwa wampelekee Kadhi wamueleze hali ilivyo na maoni yao kwa masilahi ya pande zote mbili, wala hawana haki ya kuwatenganisha ila kwa idhini ya mume, wala mke kuachish- wa ila kwa matakwa yake.

Wakitaka suluhu basi Mwenyezi Mungu atawawezesha.

Wametofautiana wafasiri katika dhamiri ya 'wakitaka' kuwa inawarudia kina nani? Imesemekana kuwa dhamiri ya kutaka inawarudia waamuzi wawili, na dhamiri

'kuwawezesha' inawarudia mke na mume; na maana iwe: Waamuzi wakitaka suluhu, basi Mwenyezi Mungu atawawezesha mke na mume. Lakini hayo yako mbali kabisa. Kwa sababu ilivyo ni kuwa wanalotaka waamuzi ni suluhu, vinginevyo wasingekuwa waamuzi.

Pili: Ni kuwa waamuzi wanaweza kutaka suluhu na tawfiki isipatikane ambapo Mwenyezi Mungu anasema: Wakitaka suluhu atawawezesha, kuonyesha ni wajibu kupatikana Tawfiq (kuwezeshwa) mara tu baada ya kutaka suluhu kutoka kwa waamuzi.

Ilivyo hasa ni kwamba dhamiri zote mbili zinawarudia mke na mume. Maana yake ni ikiwa mke na mume wakiwa na nia safi, kwa kukusudia ndoa yao iendelee na kuilinda familia, basi kazi za waamuzi zitaleta natija; na Mwenyezi Mungu bila shaka atawawezesha mume na mke. Kwani nia ikitengemaa mambo nayo hutengemaa. Na kama nia ya mume na mke ikiwa mbaya basi kazi ya waamuzi nayo haitafaulu, hata kama watakusudia usuluhishi kwa juhu- di zao zote.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametaja uasi wa mke; kisha uasi wa mume na mke na wala hakutaja wa mume tu. Lakini mafakihi wameliingilia hilo na wakasema: "Mume akimwasi mke na akaacha kumtekelezea haki zake atamuonya; akikubali sawa, la si hivyo hawezi kumwacha peke yake kitandani wala kumpiga, kama anavyofanyiwa yeye akiasi; hata kama ataona kufanya hivyo kutaleta manufaa. Kwa sababu kufanya hivyo kunahitaji idhini ya sharia ambayo haiko kwa mke, isipokuwa lake la kufanya ni kwenda kumshtaki kwa Kadhi.

Na ni wajibu wa Kadhi kuthibitisha na kubainisha. Ikimthibitikia uasi wa mume, basi atamkataza, akirudia atamwaziri vile atakavyoona yeye; ikiwa ni kumshutumu au kumpiga au kumfunga gerezani.

Ikiwa ataacha kumtunza mkewe na ana uwezo, inajuzu kwa kadhi kuchukua mali ya mume na amlishe mke; hata ikiwa ni kwa kuuza kitu katika milki yake. Ikiwa hana kitu basi - kuna rai ya kuwa - kadhi anaweza kumlazimisha kutoa talaka,ikiwamkeatatakatalaka. Hayoyametanguliakuelezwanyuma.

وَاعْبُدُوا اللَّهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا ۖ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا وَبِذِي الْقُرْبَىٰ وَالْيَتَامَىٰ وَالْمَسَاكِينِ وَالْجَارِ ذِي الْقُرْبَىٰ وَالْجَارِ الْجُنُبِ وَالصَّاحِبِ بِالْجَنْبِ وَابْنِ السَّبِيلِ وَمَا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ ۗ إِنَّ اللَّهَ لَا يُحِبُّ مَنْ كَانَ مُخْتَالًا فَخُورًا {36}

Na mwabuduni Mwenyezi Mungu wala msimshirikishe na chochote, na watendeeni wema wazazi wawili na jamaa wa ukoo na mayatima na maskini na jirani wa karibu na jirani wa mbali, na rafiki wa ubavuni na msafiri na waliomilikiwa na mikono yenu ya kulia; Hakika Mwenyezi Mungu hapendi mwenye kiburi ajivunaye.