read

Aya 37 -39: Hufanya Ubakhili Na Kuamrisha Watu Kuufanya

Maana

Ambao hufanya ubakhili na huwaamuru watu kufanya ubakhili.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuamrisha kutoa na kufanya hisani katika Aya iliyotangulia, katika Aya hii anamkemea yule anayefanya ubakhili na akaamrisha wengine wafanye ubakhili. Kila bakhili huwaamrisha watu kufanya ubakhili; bali kila mwovu hupendelea kupata wafuasi, ili asiwe peke yake katika uovu na asisemwe vibaya. Kimsingi ni kwamba mwizi hukiboresha kitendo cha wizi na kukifanya halali, bali hata huongeza kukifanya.

Sijaona kitu kinachokubaliwa haraka na nafsi kama amri ya ubakhili na kuzuia kutoa. Kwa sababu mali ni tamu sana rohoni, wala si rahisi - mara nyingi - kutoa hata kidogo, isipokuwa kwa juhudi kubwa. Kwa hiyo amri ya kuzuwia inaungana na matamanio ya nafsi na kuitikiwa kwa haraka na ni nyepesi.

Sheikh Muhammad Abduh katika kufasiri Aya hii anasema: "Wenye kuamrisha ubakhili wana nguvu ya kutia shaka, hata waliwahi kuniathiri; nikawa ninarudisha pesa mfukoni baada ya kuzitoa. Kwa sababu wasiopenda kutoa walikuwa wakiniambia: Huyu hastahili kupewa na kumpa kitu ni kupoteza; kama utatoa mali mahali pengine itakuwa bora zaidi."

Ukweli ni tulioueleza kwamba amri ya ubakhili inamwathiri mtu anapoitikia matamanio ya nafsi yake, si kwa kauli ya wabakhili na shaka shaka zao. Kwani mtukufu ni yule anayeyashinda matamanio na nafsi yake na kuyalaz- imisha kukubali mambo mazito yakiwa na kheri na utengeneo. Imam Ali (a.s.) anasema: "Amali bora ni ile unayoilazimisha nafsi yako juu yake." Hadith inasema: "Amali bora ni ile iliyo nzito zaidi."

Na wakaficha aliyowapa Mwenyezi Mungu katika fadhila Yake.

Fadhila za Mwenyezi Mungu zinakusanya kila neema, ikiwemo mali na ilimu. Kuficha ilimu ni haramu na kuieneza ni wajibu, lakini kwa mfumo wa kuvutia sio wa kuchukiza na unaokurubisha sio kuweka mbali. Kwa sababu ilimu ni nyenzo na kuitumia ni lengo.

Baadhi ya maulama wamesema: "Tajiri akificha utajiri wake na akajifanya ni fukara mbele za watu basi atakuwa amefanya haramu." Wametoa dalili kwa Aya isemayo: "Na neema ya Mola wako izungumze." (93:11)

Kuna Hadith isemayo: "Mwenyezi Mungu akimneemesha mja neema yoyote hupendelea ionekane athari ya neema yake."

Na tumewaandalia makafiri adhabu yenye kudhalilisha.

Mfumo wa Aya unafahamisha kuwa makusudio ya Makafiri hapa ni wale ambao wameficha fadhila za Mwenyezi Mungu na neema yake. Imepokewa kutoka kwa Imam Jafar as-Sadiq (a.s.) Kwamba yeye amesema: "kuzizungumza neema za Mwenyezi Mungu ni kushukuru na kuacha kuzizungumza ni kufuru."

Mwenyezi Mungu anasema: "Kama mkishukuru nitawazidishia, na kama mkikufuru basi adhabu yangu ni kali sana." (14:7)

Kwa hivyo basi kufuru katika Aya hii inachukuliwa kuwa ni kukufuru neema, sio kumkufuru Mwenyezi Mungu.

Na wale ambao hutoa mali yao kwa kuonyesha watu wala hawaamini Mwenyezi Mungu wala siku ya mwisho.

Imetangulia Aya kama hii na tafsiri yake katika Sura ya Baqara (2:264). Kwa ufupi ni kuwa ambaye anatoa mali yake kwa ria (kujionyesha) na yule anayefanya ubakhili ni sawa mbele ya Mwenyezi Mungu. Na huenda mwenye kujionyesha akawa na hali mbaya zaidi. Kwa sababu yeye ni kama kafiri ambaye hafanyi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Rafiki Wa Shetani

Kila kinachoshawishi kitendo cha uovu, kuhadaa kufanya ufisadi na upotevu, unaweza kukiita shetani; iwe ni mawazo, mtu au kitu chochote. Neno shetani ni nembo ya kila mpotevu aliye mpotezaji. Anaficha hakika yake chini ya nguo za watu wema. Kwa ajili hii ndipo tukawaona watu wengi wanasema na kutenda kutokana na mwongozo wa kishetani na upotevu na wao wenyewe wanahisabu kuwa ni mwongozo kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Aliye karibu zaidi na shetani ni yule ambaye watu humwamini kwa utakatifu wake, na hawajui hakika yake. Hayo ndiyo makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: Na ambaye shetani amekuwa ndiye rafiki yake, basi ana rafiki mbaya na kauli yake: "Na mwenye kufanya shetani ni mlinzi wake badala ya Mwenyezi Mungu, basi amepata hasara iliyo wazi." (4:119).

Kama ilivyokuwa shetani ni rafiki yake duniani, basi akhera pia ni rafiki yake vile vile. Kuna Hadith isemayo: 'Mtu yuko pamoja na anayempenda,' Shetani anawagawanya wafuasi wake kwenye mafungu na kuwapa majukumu yao; kama afanyavyo kamanda wa jeshi.

Wengine wanapoteza watu kwa kumwaga damu na kuyaingilia mataifa yenye amani; kama vile mataifa yaliyotengeneza Israel na kuipa mali na silaha kwa ajili ya kuwachokoza Waarabu na miji ya Kiarabu, si kwa lolote ila wawatawale kisiasa na kiuchumi.
Wengine kazi yao ni kuhadaa kwa ufasiki na uovu na kuvunja heshima. Wengine wanawaamrisha kuswali, kujivika nguo ya watu wema na wasiotaka mambo ya dunia, ili waweze kuwapata watu wema.

Ikiwa wameshindwa na wanaomcha Mungu na wakachoka na hila zao, basi huwa radhi kuwahadaa japokuwa kwa tamko la haki atakalolisema mtu kwa matakwa ya Iblis. Kuna riwaya kwamba Iblis alimwambia Isa bin Maryam (a.s.): "Sema: Lailaha illa Ilah," Isa akamwambia nitasema lakini si kwa matakwa yako, bali kwa kuwa ni neno la haki. Basi mlaanifu (Iblis) akawa dhalili. Hekaya hii inaonyesha kuwa imani haiwi kwa tahalili na takbira, wala kwa kufunga na Swala.

Kwani yote hayo yanaweza kuwa ni mitego ya shetani na vitimbi vyake. Isipokuwa imani ya kweli hupimwa kwa namna ya kumjua Mwenyezi Mungu na hekima zake; na kujua milango ya shetani ambayo inaharibu ikhlasi ya muumin na amali yake.

Na ingeliwadhuru nini lau kama wao wangelimwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho na wakatoa katika aliyowaruzuku Mungu.

Mwenyezi Mungu ameunganisha baina ya kumwaini Yeye, kuamini Siku ya Mwisho na kutoa, kwa sababu bakhili anayeng'ang'nia amemtoa katika imani. Maana yake nikuwa kutoa ni dalili ya imani na ubakhili ni dalili ya ukafiri.

Hilo ni kwa sababu muumini anayemtegemea Mungu kikweli kweli hutoa akiwa anaamini badali atakayopata. Na mwenye kuyakinisha badali hutoa bila ya pingamizi; kama alivyosema Imam Ali (as). Ama mwenye imani dhaifu humsikiliza shetani wake anayemwamrisha kuzuia na kumhofisha na ufukara kama akitoa.

Hata hivyo makusudio ya imani hapa ni imani ya utiifu na matendo sio imani ya itikadi; na ukafiri ni ukafiri wa utiifu na matendo sio wa kumkanusha Mwenyezi Mungu.

Miongoni mwa kauli za Imam Ali kuhusu ubakhili ni: "Namsatajabia bakhili anayeharakia ufukara alioukimbia na kuacha umpite utajiri alioutaka Anaishi duniani maisha ya kifukara na akhera anahisabiwa ni tajiri." Maana ya kuwa tajiri anakimbilia ufukara ni kuwa yeye ana hali mbaya kuliko fukara. Kwa sababu tajiri huwa anahofia utajiri wake utamwondokea, lakini fukara huwa na matarajio
ya kuondoka ufukara wake.

إِنَّ اللَّهَ لَا يَظْلِمُ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ ۖ وَإِنْ تَكُ حَسَنَةً يُضَاعِفْهَا وَيُؤْتِ مِنْ لَدُنْهُ أَجْرًا عَظِيمًا {40}

Hakika Mwenyezi Mungu hadhulumu (hata) uzani wa chembe. Na liwapo (jambo) ni jema huzidisha na hutoa kutoka kwake malipo makubwa.

فَكَيْفَ إِذَا جِئْنَا مِنْ كُلِّ أُمَّةٍ بِشَهِيدٍ وَجِئْنَا بِكَ عَلَىٰ هَٰؤُلَاءِ شَهِيدًا {41}

Basi itakuwaje tutakapowaletea kila umma shahidi na tukakuleta kuwa shahidi juu ya hawa.

يَوْمَئِذٍ يَوَدُّ الَّذِينَ كَفَرُوا وَعَصَوُا الرَّسُولَ لَوْ تُسَوَّىٰ بِهِمُ الْأَرْضُ وَلَا يَكْتُمُونَ اللَّهَ حَدِيثًا {42}

Siku hiyo watatamani waliokufuru na kumwasi Mtume ya kuwa ardhi isawazishwe juu yao, wala hawatamficha Mwenyezi Mungu na mazungumzo (yao).