read

Aya 40 – 42: Mwenyezi Mungu Hadhulumu Hata Uzani Wa Chembe

Lugha

Uzani ni uzito hata ukiwa mchache, na chembe ni zile zinazopatikana kwenye miili; na hapa zimekuja kufananisha uchache. Kwenye Aya nyingine uchache umefananishwa na hardali.

Maana

Hakika Mwenyezi Mungu hadhulumu (hata) uzani wa chembe.

Baada ya Mwenyezi Mungu kuamrisha aabudiwe, kuwafanyia wema wazazi wawili na jamaa, kushutumu ubakhili na kutoa kwa ria na mwenye kuficha fadhila za Mwenyezi Mungu na kuwapa kiaga marafiki wa shetani, baada ya hayo anabainisha tena kwa kutilia mkazo kwamba yeye hampunguzii yeyote katika malipo yake hata chembe, hata kama ni uzani wa chembe ya vumbi; bali huzidisha thawabu za wenye kufanya wema, akasema:

Na liwapo ni jema hulizidisha na hutoa kutoka kwake malipo makubwa.

Kusema 'kutoka kwake' ni ishara kwamba yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu, humpa mwenye kufanya wema kwa wema wake kisha humzidishia bahashishi.

Wanafalsafa wana kauli katika hili kuwa, je, Mwenyezi Mungu humpa thawabu mtiifu kwa kuwa ni lazima anastahiki, kiasi ambacho kama hatampa, basi Mwenyezi Mungu atakuwa dhalimu - Mungu ametaka na hilo- au ni kwa njia ya fadhila na hisani tu?

Tuonavyo lililo karibu zaidi ni kuwa Mwenyezi Mungu hutoa thawabu kwenye wajibu kwa njia ya fadhila tu. Kwa sababu hakuna malipo wala shukrani kwenye tendo la wajibu. Ama mambo ya Sunna hutoa thawabu kwa kustahiki. Lakini kwa vyovyote ilivyo ni kuwa thawabu ziko hakuna shaka. Kwa hiyo mzozo wa kuwa sababu yake ni hisani au kustahiki ni mzozo tasa, maadamu sababu iko nje ya uwezo.

Basi itakuwaje tutakapowaletea kila umma shahidi na tukakuleta kuwa shahidi juu ya hawa?

Kesho Mwenyezi Mungu atawakusanya watu kwa ajili ya hisabu na adhabu. Kabla ya chochote ataushuhudiza kila umma na Mtume wao, kwamba amewafikishia ujumbe wa Mola wake na akawafundisha halali na haramu moja kwa moja; au kupitia sahaba zake, au wafuasi wao au wanavyuoni na mafakihi.

Kwa hiyo makusudio ya shahidi wa kwanza ni kila Mtume aliyemtangulia Muhammad na shahidi wa pili ni Muhammad (s.a.w.): Na neno 'hawa' ni umma wa Muhammad.

Umbali zaidi ni ule wa mwenye kusema kwamba neno 'hawa' ni Mitume wote waliotangulia na kwamba Muhammad atatoa ushahidi juu yao na wao watatoa ushahidi juu ya umma wao. Ameweka mbali msemaji huyu, kwa sababu ushahidi unajuzu kutolewa na kusikizwa juu ya ambaye anaweza kupuuza wajibu wake.

Tulipofasiri sura ya Baqara (2:143) tumetaja kwamba Muhammad (s.a.w.) anatoa ushuhuda kwa maulama wa umma wake kwamba yeye amewafikishia Uislam na hukumu zake na ulama wa umma washuhudie kwamba wao wamefikisha risala ya Uislam kwa njia yake.

Sheikh Muhammad Abduh, katika kufasiri Aya hii, amesema kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kesho atalinganisha baina ya itikadi ya kila umma, amali yake na hulka zake, na itikadi ya Mtume wake. Ikiwa ndiyo hiyo hiyo, basi umma utakuwa umeokoka, vinginevyo utakuwu umeangamia.

Tafsiri hii ni miongoni mwa mapinduzi yake juu ya uzushi na kufuata. Nayo haiko mbali sana na hali halisi. Kwani ulinganisho huu kama hautatokea mbele ya Muumba Mtukufu, lakini natija yake itapatikana tu.

Siku hiyo watatamani waliokufuru na kumwasi Mtume ya kuwa ardhi isawazishwe juu yao.

Yaani Makafiri watapofunuliwa pazia siku ya Kiyama, watatamani lau kwamba wao wasingeliumbwa, bora wangekuwa sawa na mchanga; kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Siku ambayo mtu ataona kilichotangulizwa na mikono yake, na Kafiri atasema: Laiti ningelikuwa mchanga." (78:40)
Wala hawatamficha Mwenyezi Mungu na mazungumzo (yao).

Haya ni maneno yanayoanza upya, na maana yake ni kuwa wao hawataweza kuficha dhambi yoyote miongoni mwa dhambi zao walizozifanya na kufichika katika macho ya watu hapa duniani. Kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewazunguuka na amali zao.

Na kwamba Malaika, masikio yao, macho yao, ndimi zao, ngozi zao, mikono yao na miguu yao, vyote vitashuhudia yale waliyoyafanya: "Hata watakapoufikia (moto) yatashuhudia masikio yao na macho yao na ngozi zao kwa yale waliyokuwa wakiyatenda." (41:20). " Siku ambayo zitashuhudia ndimi zao na mikono yao na miguu yao kwa waliyokuwa wakiya- tenda." (24:24).

Ewe Mwenyezi Mungu mhurumie kwa uadilifu wako ambaye hana uwezo. Na mwokoe ambaye hana uokovu zaidi ya msamaha wako.

Unaweza kuuliza:Utaunganishaje baina ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Wala hawatamficha Mwenyezi Mungu na neno lolote" na kauli yake Mwenyezi Mungu: "Na siku ambayo tutawakusanya wote pamoja kisha tuwaambie wale walioshirikisha: Wako wapi washirikishwa wenu mliokuwa mnadai. Kisha hautakuwa udhuru wao isipokuwa kusema: Wallahi Mola wetu hatukuwa washirikina." (6: 22-23)

Jibu: Inawezekana kuwa makusudio yao ni kwamba wao katika itikadi yao hawakuwa washirikina. Tukutane wakati wa kufasiri Sura hiyo ya sita (An'am) inshaallah.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَقْرَبُوا الصَّلَاةَ وَأَنْتُمْ سُكَارَىٰ حَتَّىٰ تَعْلَمُوا مَا تَقُولُونَ وَلَا جُنُبًا إِلَّا عَابِرِي سَبِيلٍ حَتَّىٰ تَغْتَسِلُوا ۚ وَإِنْ كُنْتُمْ مَرْضَىٰ أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ أَوْ جَاءَ أَحَدٌ مِنْكُمْ مِنَ الْغَائِطِ أَوْ لَامَسْتُمُ النِّسَاءَ فَلَمْ تَجِدُوا مَاءً فَتَيَمَّمُوا صَعِيدًا طَيِّبًا فَامْسَحُوا بِوُجُوهِكُمْ وَأَيْدِيكُمْ ۗ إِنَّ اللَّهَ كَانَ عَفُوًّا غَفُورًا {43}

Enyi mlioamini, msikaribie Swala na hali mmelewa mpaka myajue mnayoyasema; wala mkiwa na janaba - ispokuwa wapita njia - mpaka muoge. Na muwapo wagonjwa au mko safarini au akawa mmoja wenu ametoka chooni au mkagusana na wanawake, kisha msipate maji, basi tayamamuni na mchanga ulio twahara; mpake nyuso zenu na mikono yenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwingi wa kusamehe mwenye kughufiria.