read

Aya 43: Msikaribie Swala Mkiwa Walevi

Maana

Enyi mlioamini, msikaribie Swala na hali mmelewa mpaka myajue mnayoyasema; wala mkiwa na janaba - ispkuwa wapita njia - mpaka muoge.

Hapa kuna masuala kadhaa

1. Msemo huu unaelekezwa kwa Waislamu kabla ya kubainishwa hukumu ya kuharimishwa pombe kulikoelezwa katika Sura ya Maida (5: 90 - 91) na katika A'raf (7:32). Zikiungana na Baqara (2:219) ambayo tumeyaelezea hayo kwa ufafanuzi kabisa. Pia tumeeleza hayo katika kitab Fiqhul-Imam Jafar as-Sadiq (a.s.) mlango wa vyakula na vinywaji.

Ilivyo hasa ni kwamba kukatazwa mtu kuswali hali ya kuwa amelewa hakufahamishi kwamba ni halali katika isiyokuwa Swala; kwa mfano ukisema: Usiwaangalie wanawake ukiwa unakwenda njiani hakufahamishi kuwa inafaa kuwaangalia ukiwa ukumbini. Kwa maneno mengine ni kuwa Aya imefahamisha uharamu wa Swala kati- ka hali ya kulewa, na kunyamzia hukumu ya kulewa mahali pengine.

2. Wametofautiana (wafasiri) kuhusu makusudio ya Swala, je ni Swala yenyewe au msikiti ambao Swala iko ndani yake, kwa kuangalia desturi ya kutumia hali kwa mahali; kama kutumia jina la kahawani kwa maana ya mahali panaponywewa kahawa.

3. Lakini wafasiri wengi wameelemea kwenye maana ya kwanza. Na hilo ni wazi zaidi kuliko kuwa ni msikiti.

4. Wametofautiana vilevile kuwa je, makusudio ya kulewa ni kulewa pombe au usingizi? Kwa dhahiri ni kulewa kileo sio usingizi.

5. Baadhi ya wapokezi wamesema kwmba kundi la Maswahaba walikusanyi- ka kwa mmoja wao akawatengenezea chakula na pombe-Kabla ya kubainishwa hukumu ya pombe - Wakala na wakanywa. Walipolewa ukaingia wakati wa Swala; mmoja wao akawaswalisha; akakoroga Swala na akageuza Aya za Qur'an.

Sheikh Muhammad Jawad Balaghi1 katika tafsir yake Alaurrahman amefuatilia na kuthibitisha uongo wa riwaya hizi moja baada ya nyingine.

Kwa ufupi natija ya utafiti wake mkali ni kwamba Tirmidhi amepokea kuwa aliyewaita wenzake ni Abdul-rahman bin Auf na Ali ndiye aliyekuwa Imam. Abu Daud akapokea kuwa aliyealika ni mtu mmoja katika Ansari na Abdul-rahman alikuwa miongoni mwa waalikwa. Ibn Jarir Tabari amesema katika tafsir yake na Suyuti katika Durril-manthur wamesema kuwa Imam wa jamaa alikuwa ni Abdul-rahman bin Auf.

Miongoni mwa mambo yake ya kutokuwa na ubinafsi na kumwelekea kwake Mungu peke yake, alikuwa haweki jina lake katika vitabu vyake alivyovitunga katika maisha yake. Alipoulizwa sababu yake akasema: "Huenda nikakosea katika baadhi ya niliyoyasema, akatusi - yule mwenye marad- hi moyoni mwake - taifa langu kwa sababu yangu, "Alikufa ulama huyu mwaka 1352 A.H.

Vile vile katika Durril-manthur.. imesemwa kuwa Aya imeshuka kwa Abu Bakr, Umar, Ali, Abdul-rahman na Saad, na kwamba aliyewaalika wenzake ni Ali. Katika Musnad ya Ahmad na Nassai kwamba Umar alisema: "Ewe Mola tubainishie kuhusu pombe;" ndipo ikashuka Aya hii.

Mbali ya kugongana riwaya katika mwalishi, Imam na Maamum, vile vile riwaya zimegongana na kupingana kuhusu Aya iliyovurugwa. Kuna riwaya inayosema kwamba Imam alisema: "Ninaabudu mnachokiabudu." Riwaya nyingine ikasema kuwa alisoma: "Sina dini."

Vile vile riwaya zimetofautiana kuhusu wakati wa kushuka Aya hiyo na sababu yake. Zaidi ya hayo yote mwenye Alaurrahman amethibtishia kuwa mwenye riwaya ya kwanza, ambaye amesema kuwa Imam wa jamaa alikuwa ni Ali, alikuwa ni Kharij na ni katika madui wakubwa wa Ali.

Kwa vyovyote iwavyo ikiswihi kuwa kikundi cha maswahaba walikunywa pombe na kwamba Imam wao alikoroga Swala yake; basi watakuwa ni wale ambao waliwahi kumshirikisha Mwenyezi Mungu, wakaabudu masanamu, wakanywa pombe na kula nyama za haramu katika ujahiliya waliokulia ndani yake na kulelewa,. Na Ali bin Abu Twalib hakuwa katika wao. Yeye alikulia katika malezi ya Mtume (s.a.w.), tangu utoto wake na akamrekebisha vile atakavyo.

Huenda mtu akasema: Kauli yako hii inatokana na mwongozo wa kiitikadi sio mwongozo wa matukio yalivyo.

Jibu: Hukumu ambayo inategemea makuzi ya mtu na malezi yake inatokana na mwongozo wa haki na matukio yalivyo. Sio mwongozo wa mawazo na itikadi.

Wala mkiwa na janaba - ispokuwa wapita njia - mpaka mwoge.

Imesemekana kuwa makusudio ya'mpita njia' ni msafiri; na kwamba maana yake, msikurubie Swala mkiwa mmelewa wala mkiwa na janaba ila katika hali ya safari.
Ikumbukwe kwamba Aya imeeleza hukumu ya wasafiri pale iliposemwa: "Na muwapo wagonjwa au mko safarini." Basi tukifasiri mpita njia kwa maana ya msafiri, italazimika kukaririka katika jumla moja bila ya dharura yoyote.

Pili: Kuna Hadith zilizofasiri 'mpita njia' kwa maana ya kupita msikitini; kwamba ni haramu kwa mwenye janaba kuingia msikitini, ila anayepita tu, isipokuwa Masjidul-haram (wa Makka) na Masjidun nabawi (wa Madina), haijuzu kabisa kuingia katika misikiti hiyo hata kwa kupitia.

Madhehebu mane yamesema kuwa mwili wote utakapoenea maji, basi litakuwa sahihi josho la janaba (janaba limeondoka), bila ya kuangalia kuanzia juu au chini.

Shia Imamia wameligawanya josho la janaba kwenye aina mbili; La mpango (tartib) na la kujivika (irtimasi), mpango kwao ni kujimiminia maji; wakawa- jibisha katika hali hii kuanza kichwa, kisha upande wa kuume na hatimaye kushoto. Lau atafanya kinyume, basi josho limebatilika.

Ama la kujivika ni kuuvika mwili wote ndani ya maji kwa mpigo mmoja; kama vile kuoga baharini, mtoni n.k.

Mgonjwa Na Msafiri Katika Tayammam

Na muwapo wagonjwa au mko safarini au akawa mmoja wenu ametoka chooni, au mkagusana na wanawake, kisha msipate maji, basi tayamamuni na mchanga ulio twahara, mpake nyuso zenu na mikono yenu.

Zimegongana kauli za wafasiri katika Aya hii, mpaka Sheikh Muhammad Abduh akasema: "Nimeangalia tafsiri ishirini na tano, sikupata cha kutesheleza wala kauli ya kuondoa taklifa." Alusy naye katika Rawhul-bayan akasema: "Aya hii ni katika Aya zinazotatanisha."

Na sisi tumerejea kiasi tafsiri ishirini za Sunni na Shia. Wengi wa wafasiri wake wamenakili tafsiri kadhaa, tukaona kama alivyosema Sheikh Muhammad Abduh, lakini hatukuona utatanishi wowote au mushkeli wowote, kama alivy- oona Alusy. Baada ya kutegemea maana yake na makusudio, tumejaribu kuifafanua kwa mfumo huu ufuatao:

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametaja katika Aya watu aina nne: Wagonjwa, wasafiri, waliotoka chooni na waliowagusa wanawake (makusudio ya kuwagusa wanawake ni kuwaingilia). Mwenyezi Mungu amewajibisha kwa wote hawa kuelekea kwenye tayammam wakati wa kuyakosa maji.

Katika mambo waliyoafikiana madhehebu yote ni kuwa dhahiri ya Qur'an hai- juzu kuitegemea - hasa katika kutoa hukumu za sheria - ila baada ya kurudia kwenye Hadith za Mtume. Kwa sababu Hadith ni moja ya chimbuko la sharia; kama ambavyo ni maelezo na ubainifu wa Qur'an, kama ilivyosema Qur'an yenyewe: "Analowapa Mtume lipokeeni na analowakataza, basi jiepusheni. Na mcheni

Mwenyezi Mungu kwa hakika Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu." (59:7)

Ikiwa haikupatikana Hadith inayoichambua dhahiri ya tamko la Aya basi ni wajibu kuitumia dhahiri. Vinginevyo itawajibika kufanya amali kwa tutakavy- ofahamu kutoka katika Kitabu na Hadith kwa pamoja. Kwa sababu zinatoka katika chemchemi moja, ambayo ni Wahyi.

Tutazungumzia kila moja ya aina nne zilizotajwa na Aya. Hapo tutapata ufafanuzi wa jibu la swali hili: Kuwa je kuna Hadith inayopingana na dhahiri ya Aya katika moja ya aina hizi nne?

1. Mgonjwa: Dhahiri ya Aya inafahamisha kuwa yeye atatayamum akikosa maji. Wamekongamana kutumia dhahiri hii. Kwa sababu hata ambaye si mgonjwa atatayammum kwa kukosa maji.

Na mgonjwa akipata maji lakini akahofia kuyatumia je, atatayammum? Au atatumia maji hata akiwa anahofia madhara?

Wameafikiana mafakihi kwamba mgonjwa atatayammum hata ikiwa maji yapo akihofia kuyatumia. Wametoa dalili ya Hadith hii: "Hapana madhara wala kudhuriana." Na kwa isemayo kuwa sahaba mmoja alipatwa na janaba naye alikuwa na jeraha kubwa. Akawauliza wenzake wakamwamrisha kuoga alipooga akafa. Mtume aliposikia hilo akasema: "Wamemuua, Mungu awaue (nao)."

Kwa hiyo basi kauli yake Mwenyezi Mungu, ‘kisha msipate maji; ni ya aina zote zilizotajwa katika Aya. Haya ndiyo maana yanayopatikana kwa uasili wa Aya, sio kwa kufuatiza.

Ama maana yanayopatikana kwa kufuatiza kwa kupatikana ambako mafaqihi na maulama wa Usul wanakuita 'ufahamu wa sharti'. Mafhumushart, ni kwamba unawajibisha kila mmoja katika aina nne kutumia maji akiyapata wala haijuzu kwake kutayamammu kwa hali yoyote ikiwa maji yapo; hata akidhurika kwa kuyatumia.

Lakini umekwisha fahamu kutokana na yaliy- otangulia kwamba mafakihi wamekongamana na kwamba Hadith za Mtume, zimefahamisha kuwa mgonjwa atatayammam hata kama maji yapo ikiwa anahofia madhara kwa kutumia maji. Kwa hivyo basi hapana budi kumtoa mgonjwa na maana haya ya kufuatiza: na kubakisha aina tatu ambao ni kutumia maji, yakiwapo, kwa mujibu wa ufahamu huu wa kufuatiza.

Kwa ufupi ni kwamba wote wane watatayammam ikiwa wamekosa maji, hili halina shaka. Ama maji, yakiwapo basi atayatumia yule asiyehofia madhara ya kuyatumia. Ama yule anayehofia kuyatumia ataacha na atatayammam.

2. Msafiri: Aya inafamisha kuwa yeye atatayammam akikosa maji, iwe safari yake ni ndefu au fupi. Hivyo ndivyo waliyoafikiana wote. Lakini wametofautiana katika asiyekuwa msafiri ambaye si mgonjwa. Je atayammam na kuswali au atasamehewa kuswali.

Abu Hanifa amesema: Swala itamwondokea. Kwa sababu dhahiri ya Aya ni kwamba tayammam inajuzu katika safari sio mjini.

Madhehebu mengine yote yaliyobakia wameafikiana kuwa mwenye kukosa maji ni wajibu atayammam na kuswali, ni sawa awe msafiri au nyumbani. Kwa sababu kujuzu kutayammam katika safari hakuzuwii kujuzu nyumbani. Zimekuja Hadith mutawatir, kutoka kwa Mtume (s.a.w.) amesema: "Hakika mchanga ulio twahara, humtwahirisha Mwislam hata akikosa maji miaka kumi."

Abu Bakr aliye maarufu kwa jina la Ibn A-arabi katika kitabu Ahkamul-Qur'an Juz, 1 Uk. 176 chapa ya mwaka 1331 A.H alisema: "Hakika Abu Hanifa mara nyingi huacha dhahiri na nukuu (nassi) kwa kukisia."

Unaweza kuuliza: Ikiwa msafiri na aliye mjini wana hukumu moja katika wajibu wa kuyatumia maji yaliyopatikana na kutayammam yakikosekana maji, kwa nini basi Qur'an imetaja safari hasa.

Wamejibu kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameitaja safari kwa sababu ndio aghlabu katika safari kukosa maji.

Ama mtu akiwa mjini ni nadra. Hili ndilo jibu la kudhania na kuonelea ni vizuri katika kauli ya Mwenyezi Mungu. Kwa sababu halitegemei Aya au riwaya mutawatir au hukumu inayotokana na akili. Kwa hivyo sisi tunalinyamazia.

3. Au akiwa mmoja wenu ametoka chooni. Ni kinaya cha kutokwa na mkojo, kinyesi au upepo. Basi mtu akitokwa na kimojawapo katika hivyo na akataka kuswali, ni juu yake kutawadha akipata maji na atatayammam akiyakosa. Hilo ni kwa kongamano la wanachuoni na Hadith (Ijmai na Sunna).

4. Au mkagusana na wanawake, ni kinaya cha kujamii (kumwingilia kimwili) Qur'an, imetumia kwa kinaya katika hilo bila ya kueleza wazi; kama vile: "Basi sasa changanyikeni nao …" (2:187) "Wala msiwakurubie." (2:222) "… Kabla hamjawagusa." (2:237)

Na Shafi amesema: "Makusudio ya kugusa katika Aya ni kule kugusana mwili." Kwa vyovyote iwavyo ni kwamba mwenye kuwa na janaba na akapa- ta maji ni juu yake kuoga akitaka kuswali. Akikosa maji atatayammam badala ya kuoga. Kila linalowajibisha kutawadha, mafakihi wanaliita hadath ndogo na kila linalowajibisha kuoga wanaliita hadath kubwa.

Basi tayammamuni na mchanga ulio twahara

Mchanga ni ardhi. Aya hii iko katika maana ya Hadith tukufu isemayo: "Nimeumbiwa ardhi kuwa ni msikiti na yenye kutwaharisha."

Mpake nyuso zenu na mikono yenu.

Madhehebu yote yameafikiana kuwa kutayammam hakuwi ila katika viungo viwili hivi; na wakatofautiana mpaka wa sehemu zinazopakwa mchanga katika uso na mikono miwili. Madhehebu mane yakasema: "Ni wajibu kupaka uso wote zikiwemo ndevu; sawa na ilivyo katika udhu. Katika mikono, Hanafi na Shafi wamesema ni wajibu kupaka mchanga mpaka kwenye vifundo vya mikono kama udhu."

Shia Imamia wamesema ni wajibu kupaka baadhi ya sehemu ya uso, sio uso wote. Kwa sababu herufi 'Ba' ni ya tabiidh (kufanya baadhi); sawa na ile iliyo katika udhu kuhusu vichwa. Kwa sababu kama isingekuwa ya tabiidh basi ingekuwa ya ziada; na asili ni kutokuwa ziada. Wakasema inafaa kupangusa viganja viwili tu. Ufafanuzi uko katika vitabu vya fiqh.

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ أُوتُوا نَصِيبًا مِنَ الْكِتَابِ يَشْتَرُونَ الضَّلَالَةَ وَيُرِيدُونَ أَنْ تَضِلُّوا السَّبِيلَ {44}

Je, huwaoni ambao wamepewa fungu katika Kitabu hununua upotevu na kuwataka mpotee njia?

وَاللَّهُ أَعْلَمُ بِأَعْدَائِكُمْ ۚ وَكَفَىٰ بِاللَّهِ وَلِيًّا وَكَفَىٰ بِاللَّهِ نَصِيرًا {45}

Na Mwenyezi Mungu anawajua sana maadui zenu; na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa mlinzi, na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa msaidizi.

مِنَ الَّذِينَ هَادُوا يُحَرِّفُونَ الْكَلِمَ عَنْ مَوَاضِعِهِ وَيَقُولُونَ سَمِعْنَا وَعَصَيْنَا وَاسْمَعْ غَيْرَ مُسْمَعٍ وَرَاعِنَا لَيًّا بِأَلْسِنَتِهِمْ وَطَعْنًا فِي الدِّينِ ۚ وَلَوْ أَنَّهُمْ قَالُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا وَاسْمَعْ وَانْظُرْنَا لَكَانَ خَيْرًا لَهُمْ وَأَقْوَمَ وَلَٰكِنْ لَعَنَهُمُ اللَّهُ بِكُفْرِهِمْ فَلَا يُؤْمِنُونَ إِلَّا قَلِيلًا {46}

Miongoni mwa mayahudi wako ambao hugeuza maneno kutoka mahali mwake, na husema: tumesikia na tumeasi; na sikia bila kusikilizwa; na (husema) raina kwa kupondoa ndimi zao na kuitukana dini. Na lau kama wao wangesema: Tumesikia na tumetii na usikie na utuangalie, ingelikuwa heri kwao na sawa zaidi. Lakini Mwenyezi Mungu amewaalani kwa kufuru zao, basi hawaamini ila wachache tu.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ آمِنُوا بِمَا نَزَّلْنَا مُصَدِّقًا لِمَا مَعَكُمْ مِنْ قَبْلِ أَنْ نَطْمِسَ وُجُوهًا فَنَرُدَّهَا عَلَىٰ أَدْبَارِهَا أَوْ نَلْعَنَهُمْ كَمَا لَعَنَّا أَصْحَابَ السَّبْتِ ۚ وَكَانَ أَمْرُ اللَّهِ مَفْعُولًا {47}

Enyi mliopewa Kitab! Aminini tuliyoyateremsha yenye kusadikisha mliyo nayo nyinyi, kabla hatujazigeuza nyuso tukazipeleka kisogoni, au tukawalaani kama tuliivyowalaani watu wa Sabato (Jumamosi). Na amri ya Mwenyezi Mungu ni lazima iwe ni yenye kufanywa.
  • 1. Ni miongoni mwa maulama wakubwa wa kishia Imamia. Alikuwa akishinda na kukesha juu ya elimu, utafiti na kutunga. Alikuwa akijua lugha ya Kiibrania na akajua siri za Mayahudi na kufichua aibu zao. Ana vitabu kama Al-huda ila dinil-mustafa, A'ajibul-akadhib, Attawhid wa Tathlith na Rihlatul-madrasiya na vinginevyo.