read

Aya 48 – 50: Mwenyezi Mungu Hasamehi Kufanyiwa Mshirika

Maana

Hakika Mwenyezi Mungu hasamehi kufanyiwa mshirika lakini husamehe yasiokuwa hayo kwa amtakaye.

Kabla ya kufasiri Aya hii tuanze na mambo mawili yanayoambatana nayo sana:
1. Kushirikisha kunagawanyika kwenye aina mbili: Kushirikisha katika Uungu; kama kuitakidi kuwa kuna waumbaji wangi na wenye kutoa riziki. Na kushirikisha katika twaa; kama kuamini kuwa Mwenyezi Mungu ni mmoja kinadharia tu, lakini anamtii kiumbe katika kumwasi Muumba.

Ukafiri nao pia uko aina mbili: Kumkufuru Mwenyezi Mungu na kumkanusha na kukufuru katika twaa; kama kuamini Mungu mmoja kisha kumwasi kwa kupuuza. Vilevile kukufuru neema na kuacha kumshukuru mwenye kuneemesha.

Makusudio ya kushirikisha katika Aya hii ni aina mbili za kwanza za kushirik- isha na kukufuru; yaani kuamini waungu wengi na kutoamini kabisa.

2. Yakija maneno ya ujumla, yanahukumu kiujumla kwa watu na yakija tena maneno mahsusi, yanawatoa baadhi ya watu waliokuwa katika ujumla. Ikiwa meneno yote mawili yametokea katika chimbuko moja, basi tutauchukulia ule umahsusi kwenye ujumla; yaani tutawatoa wale waliofahamishwa na kauli mahsusi. Kwa ufafanuzi hebu tupige mfano:

Mwenyezi Mungu anasema: "Mwizi mwanamume na mwizi mwanamke ikateni mikono yao." (5:38)

Hapa Aya imefahamsiha kwamba kila mwizi atakatwa mkono, hata kama ni siku za njaa. Kisha ikaja Hadith isemayo: "Mwizi hakatwi katika siku za njaa."

Kwa hiyo kutokana na hali hiyo imepasa tuifunge Aya ya wizi na Hadith ya njaa na hukumu iwe kila mwizi atakatwa mkono isipokuwa siku za njaa. Baada ya utangulizi huu sasa tuzikutanishe Aya tatu ambazo zitatupa ufafanuzi wa makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Hakika Mwenyezi Mungu hasamehe kufanyiwa mshirika."

Mwenyezi Mungu anasema: Sema: "Enyi waja wangu mliojidhulumu nafsi zenu! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu; hakika Mwenyezi Mungu husamehi dhambi zote. Hakika Yeye ni mwingi wa kusamehe, mwenye kurehemu." (39: 53)

Tamko la Aya hii linaonyesha ujumla, na maana yake yako wazi nayo ni kuwa Mwenyezi Mungu husamehe kila dhambi hata ya kushirikishwa Yeye. Lakini Aya tuliyonayo 'Hakika Mwenyezi Mungu hasamehi kufanyiwa mshirika,' tamko lake ni mahsusi, na maana yake yako wazi vile vile, kwamba Mwenyezi Mungu hasamehi kushirikishwa, kwa hiyo imepasa kutoa kushirikisha katika Aya ya (39:53)

Tena ikaja Aya ya tatu isemayo; "Hakika mimi ni mwenye kusamehe sana kwa anayetubia na akaamini na akashika uwongofu." (20:82) Aya hii nayo, imemtoa mwenye kutubia kutoka Aya ya kutosamehewa mwenye kushirikisha; kama ambavyo nayo ilimtoa mwenye kushirikisha kutoka Aya ya kusamehewa dhambi zote.

Kwa hivyo basi, maana yanayopatikana kwa kuzikutanisha Aya tatu na kuziunganisha, ni kwamba mwenye kutubia ushirikina, Mungu humsamehe. Kwa sababu yeye amezikana dhambi zake; na mwenye kufa akiwa msirikina hana uokofu. Kwa sababu ameacha kuitumia nafasi yake na kwamba kusamehewa yeye ni kuchochea ushirikina na kuinyenyekea dhuluma.

Zaidi ya hayo kumsamehe mshirikina sio kuwa Mwenyezi Mungu atamwambia aliyefanya uovu: 'Ahsante sana’ Mwenyezi Mungu ametakata na hayo kabisa.

Unaweza kuuliza, kuwa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: Lakini husame- he yasiyokuwa hayo kwa amtakaye, inafahamisha kuwa dhambi hiyo - isiyokuwa kushirikisha - mtu akiifanya, inawezekana Mwenyezi Mungu akam- samehe kabla ya kutubia.

Kwa sababu kufutiwa dhambi pamoja na kutubia kumethibiti kwa Qur'an na Hadith. Kwa hiyo kauli ya Mwenyezi Mungu husamehe itahusika na muumin mwenye dhambi asiyetubia. Au kwa maneno mengine ni kwamba Aya inafahamisha kuwa kusamehewa dhambi muumin hakufungiki na toba tu, bali huenda Mwenyezi Mungu akasamehe dhambi za waumini bila ya kutubia?
Jibu: Wameafikiana waislamu kwamba mwenye kufa akiwa ametubia Mwenyezi Mungu humtakabalia toba yake, kulingana na Aya za Qur'an na Hadith za Mtume.
Lakini wametofautiana kuhusu mwislamu mwenye dhambi akifa kabla ya kutubia.

Khawarij wamesema: "Atabakishwa milele motoni sawa na Kafiri, ni sawa dhambi yake iwe kubwa au ndogo.

Kikundi kimoja cha Marjaa kinasema kuwa ataingia peponi bila ya kuadhibiwa, kwa sababu maasi hayadhuru imani wala twaa hainufaishi chochote ukafiri; kama wanavyodai.

Shia na Sunni wamesema hatabakishwa milele motoni, na dhambi zake zitaachwa na matakwa ya Mwenyezi Mungu. Akitaka atamsamehe na kumwingiza peponi moja kwa moja; na akitaka atamwadhibu kiasi anachostahili, kisha amtie peponi.

Maoni yetu hayatofautiani sana na kauli ya Sunni na Shia, na tutaeleza kwa mfumo huu: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hataki kusamehe kwa michezo bila ya hekima inayosababishia hilo. Na hekima inayowajibisha kusamehewa, haifungiki na toba tu; inaweza kuwa ni shafaa au jambo jinginelo. Wala si dharura kufahamu kwa ufafanuzi, bali inatosha kujua kwamba Mwenyezi Mungu ni mwenye hekima, basi.

Kwa hivyo, katika mtazamo wa kiakili, hakuna kizuizi cha kusamehewa dhambi kwa Muumin bila ya kutubia. Yametangulia maelezo yanayofugamana na utafiti huu katika kufasiri Aya (2: 81) kifungu cha Madhambi makubwa.

Dalili Ya Umoja Na Utatu

Na mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu, hakika amezusha dhambi kubwa.

Kwa sababu atakuwa ameamini lisilowezekana. Miongoni mwa dalili za kuwa Mwenyezi Mungu ni mmoja na lau kungalikuwa na waungu wawili, basi ama atakuwa mmoja wao ni mweza zaidi wa kupangilia mambo ya ulimwengu, au asiweko.

Kwa hiyo akiwa mmoja ni muweza zaidi, basi wa pili atakuwa hana maana tena; na kama akitokuwapo muweza zaidi, basi hawezi kuwa Mungu, kwa kushindwa kwake kwa upande fulani na kutokuwa na faida ya kuweko kwake.

Dalili bora zaidi ya umoja wake Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni ile aliyoieleza yeye mwenyewe juu ya umoja wa dhati yake, pale aliposema: "Lau wangelikuwako humo (mbinguni na ardhini) waungu wengine, isipokuwa Mwenyezi Mungu bila shaka zingeharibika. Ametakasika Mwenyezi Mungu Mola wa Arshi na yale wanayomsifu. (21:22)

Yaani lau kungelikuwako na Mungu mwengine katika mbingu na ardhi asiyekuwa Mwenyezi Mungu, basi zisingelikuwa sawa na wangeliharibika waliomo na vilivyomo na kusingekuwako na nidhamu. Kwa vile kama kungelikuwa na Miungu wawili angelikuwa kila mmoja ni muweza, na kawaida ya mwenye uwezo ni dhidi ya anavyotaka mwingine.

Kwa hiyo basi mmoja wao akitaka kuumba kitu na mwingine akitaka kinyume chake, hapo ama yatapatikana matakwa yao wote wawili kwa pamoja, jambo ambalo litalazimisha kupatikana na kukosekena kwa wakati mmoja na hilo ni muhali.

Au yatapatikana matakwa ya mmoja wao kinyume cha mwingine, atakuwa huyu mmoja ameshindwa na mwingine. Kimsingi ni kwamba anayeshindwa hawezi kuwa Mungu.

Mwenyezi Mungu anasema: "Mwenyezi Mungu hakujifanyia mtoto wala hakuwa pamoja naye mungu (mwingine). Ingekuwa hivyo basi kila mungu angeliwachukua aliowaumba, na baadhi yao wangeliwashinda wengine. Mwenyezi Mungu ameepukana na sifa wanazomsifu." (23:91)

Kuna mfano mashuhuri unaosema: "Fahali wawii hawakai zizi moja."
Amirul-mumin, Ali alimwambia mtoto wake Hassan (a.s.): "Jua ewe mwanangu, lau Mola wako angelikuwa na mshirika wangelikujia Mitume wake na ungaliona athari ya milki yake na ufalme wake na ungelijua vitendo vyake na sifa zake."

Unaweza kuuliza: Je kusema kuwa Mwenyezi Mungu ni mmoja katika asili tatu: Baba, mwana na roho mtakatifu ni katika umoja au ni katika kuwafanya miungu wengi

Jibu: Ikiwa makusudio ni sifa kama vile mwenye kurehemu, mwingi wa rehe- ma hizo ni katika kumpwekesha, lakini ikikusudiwa mtu basi huo ni Utatu.

Amesema Said Al-Khauri Ashartuni katika kitab Aqrabul-mawarid; "Neno Aqnnim (lililotumiwa katika kueleza utatu) maana yake ni asili na mtu." Kwa hivyo basi litakuwa katika kuwa waungu wengi sio mmoja.

Hayo yanatiwa nguvu na neno baba na mwana ambayo yanahitajia kuweko na idadi na mabadiliko kwa mtu na dhati. Isitoshe, picha na sanamu zilizoko katika makanisa hasa ya bibi Maryam bikira (a.s.) zinaonyesha idadi ya waungu waziwazi, kwa sabaau anaonyesha amempakata mtoto ambaye ni Bwana Masih (a.s.)

Je, huwaoni wale ambao hujitakasa nafsi zao.

Wafasiri wamesema kuwa Aya hii imeshuka kwa mayahudi. Ni sawa iwe ghu- ruri ya mayahudi ndio sababu ya kushuka Aya hii au la, lakini ni picha inayosadikisha madai yao ambayo hayana mfano katika uzushi na uongo.

Mfano kama wasemavyo: 'Sisi ni watoto wa Mwenyezi Mungu na vipenzi vyake.' Au kusema: 'Hataingizwa peponi ila aliye myahudi.' Vile vile 'Sisi ni taifa teule la Mwenyezi Mungu.'

Yaani kuwa Mwenyezi Mungu ni wao tu, peke yao, na kwamba Yeye amewaumba watu wengine wawe ni watwana wao. Hawakutosheka na haya, bali ujinga wao na ghururi yao iliwapelekea kusema: 'Mungu ni fukara na sisi ni matajiri.'

Kweli hakuna mtu anayewashinda kwa utajiri wa kuzusha na kutengeneza mambo yasiyokuwapo. Ni hivi majuzi tu walitangaza na kueneza uvumi, wakapiga kelele Mashariki na Magharibi kwamba waarabu wanajianda kuwashambulia, wakati ambapo wao na mabwana zao wakoloni wanapanga njama za kuvamia na kuwahujumu waarabu.

Baada ya kumaliza kupanga, wakatekeleza bila ya kutazamiwa, wakafanya dhulma na unyama uliowafanya watu wasahau aliyoyafanya Hitler na Jankis khan.

Haya ni madogo sana katika mifano ya madai ya mayahudi. Tumeyaleta kama mfano tu, lakini sio hali yao hasa. Je, inawezekana kuyamaliza yote ya mayahudi? Unaweza kuuliiza: Ikiwa hali ya Israil ni hivi imekuwaje wakaweza kusimamisha dola zaidi ya miaka ishirini sasa?

Jibu: Mataifa ya kikoloni ndiyo yaliyoitengeneza Israel kwa kuhami masilahi yao katika Mashariki ya kati mayahudi hawana dola isipokuwa jina tu. Ama kubakia kwake mpaka leo, kunatokana na kubakia ukoloni ambao umeipigia hema la Oksijeni.

Hivi sasa dola hiyo iko njiani kuisha; hata kama itachukua muda mrefu. Kimsingi ni kwamba mwenye kusimamia kitu huisha, mara tu kiishapo.
Ukiuliza vipi Mwenyezi Mungu amewashakiza mataghuti Makafiri kwa waja wake wanaompwekesha, jibu utalipata kwenye tafsiri ya 3; 138. Kwenye kifungu cha Ushenzi wa 5 Juni

Bali Mwenyezi Mungu humtakasa amtakaye.

Sio yule anayejishuhudia yeye mwenyewe. Kimsingi, Mwenyezi Mungu hamtakasi ila ambaye vitendo vyake vinashuhudia utakaso.
Ingawaje Aya imeshuka kwa mayahudi, lakini inamkusanya kila mwenye kujitakasa kwa sababu tamko ni la kiujumla; na linalozingatiwa ni ujumla sio sababu ya kushuka.

Majaribio yamethibtisha kuwa hakuna yeyote anayejitukuza ila ni kwa sababu ya ujinga wake na ghururi yake. Au kwa kasoro fulani anayojaribu kuificha, kwa ushahidi usiokubalika hata kwake yeye mwenyewe; kwa sababu anajua uongo wake.

Tizama jinsi wamzuliavyo Mwenyezi Mungu uwongo kwa kusema 'Sisi ni taifa teule la Mwenyezi Mungu', ni watoto wa Mungu na vipenzi vyake' na mengineyo mengi: "…Nahatengenekewimwenyekuzuauongo…"(20:61)

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ أُوتُوا نَصِيبًا مِنَ الْكِتَابِ يُؤْمِنُونَ بِالْجِبْتِ وَالطَّاغُوتِ وَيَقُولُونَ لِلَّذِينَ كَفَرُوا هَٰؤُلَاءِ أَهْدَىٰ مِنَ الَّذِينَ آمَنُوا سَبِيلًا {51}

Je, huwajui ambao wamepewa fungu katika Kitabu wanaamini sanamu na taghuti na wakisema kwa ajili ya wale waliokufuru kuwa hao wameongoka zaidi katika njia ya haki kuliko walioamini.

أُولَٰئِكَ الَّذِينَ لَعَنَهُمُ اللَّهُ ۖ وَمَنْ يَلْعَنِ اللَّهُ فَلَنْ تَجِدَ لَهُ نَصِيرًا {52}

Hao ndio waliolaaniwa na Mwenyezi Mungu, na ambaye Mwenyezi Mungu amemlaani, hatampatia wa kumsaidia.