read

Aya 51 -52: Wanaamini Sanamu Na Taghut

Lugha

Neno Jibt linatumika kwa maana nyingi. Makusudio yake hapa ni anayeabudi- wa ambaye si Mungu (sanamu) Na Taghut ni aliyepetuka mipaka.

Maana

Je, hawajui ambao wamepewa fungu katika Kitabu wanamini sanamu na taghuti.

Katika Aya zilizotangulia, Mwenyezi Mungu amewataja mayahudi kwa upotevu, upotezaji, kuyaweka maneno pasipo mahali pake na kupindua maneno. Kisha katika Aya hii amewataja kuwa wao wanaamini sanamu na taghuti; yaani masanamu wanayoyaabudu Maquraish. Unaweza kuuliza: Imekuwaje Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kusema kuhusu mayahudi kwamba wao wanaamini sanamu na inajulikana wazi kuwa wao hawaamini masanamu ya Maquraish.

Jibu: mayahudi hawaamini masanamu ya Kiquraish katika nafsi zao, bali waliyakubali kiunafiki kwa kudanganya na kwa ajili ya kubagua na kumfanyia inadi Muhammad (s.a.w.) na aliyemwamini. Wakawaambia waabudu masanamu: "Nyinyi mna njia ya uongofu zaidi kuliko waislamu."

Iliyo sawa ilikuwa ni kwa mayahudi wawasaidie waislamu dhidi ya waabudu masanamu kwa sababu waislam ni watu wa Kitabu na wanaikubali Taurat kinyume na waabudu masanamu. Kwa hiyo mayahudi walikhalifu haki na wakasimama pamoja na washirikina, ndipo Mwenyezi Mungu akawataja kama waabudu masanamu.

Kwa hali hiyo ndipo tunapoipata tafsiri ya Hao wameongoka zaidi katika njia kuliko walioamini. Yaani mayahudi walisema: Washirikina ni waongofu zaidi wa njia kuliko waumini. Kwa hiyo jibu la swali liko ndani ya Aya yenyewe.

Kwa hali hii inatubainikia kuwa ishara ya hao ni ya waabudu masanamu na kwamba herufi lam katika neno Lilladhina ni ya kwa ajili; yaani waliyoyasema ni kwa ajili ya kuwaridhisha wale waliokufuru, ambao ni washirikina wa kiquraish na hawakusema kwa kuamini wayasemayo.
Hao ndio waliolaaniwa na Mwenyezi Mungu nao ni mayahudi waliofanya unafiki wakasadiki masanamu kwa ukaidi na inadi kwa waislam wanaowasadiki Mitume yao; kama vile Musa, Daud, Suleiman, Yahya na Zakariya.

Na ambaye Mwenyezi Mungu amemlaani, hatampatia wa kumsaidia.

Isipokuwa Amerika ambayo ilisheheneza Israil kwa silaha na kuisaidia tarehe 5 June; na Umoja wa Mataifa ukawatetea kwa namna ambayo mwarabu yeyote mwenye ikhlasi au mwislamu yeyote aliye muumin hatasahau hata ukipita muda gani.

Na sisi pamoja na majeraha tuliyo nayo, tunaamini kwa imani isiyo na shaka kwamba Mwenyezi Mungu peke yake ndiye msaidizi mwenye nguvu; na kwamba mwisho wa mambo utakuwa ni wa haki na uadilifu. Kwa hiyo ni juu ya wanaoitafuta haki kuvumilia, kutokuwa na pupa ya kuifikia, na kutotishwa na silaha ya adui kwa vyovyote atakavyokuwa na hatimaye kufaidika na majaribio.

أَمْ لَهُمْ نَصِيبٌ مِنَ الْمُلْكِ فَإِذًا لَا يُؤْتُونَ النَّاسَ نَقِيرًا {53}

Au wao wana fungu katika ufalme? Basi hapo wasingewapa watu hata kitobwe cha kokwa ya tende .

أَمْ يَحْسُدُونَ النَّاسَ عَلَىٰ مَا آتَاهُمُ اللَّهُ مِنْ فَضْلِهِ ۖ فَقَدْ آتَيْنَا آلَ إِبْرَاهِيمَ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَآتَيْنَاهُمْ مُلْكًا عَظِيمًا {54}

Au wanawahusudu watu kwa alichowapa Mwenyezi Mungu katika fadhila yake? Basi tuliwapa watoto wa Ibrahim Kitab na h ekima na tukawapa ufalme mkubwa.

فَمِنْهُمْ مَنْ آمَنَ بِهِ وَمِنْهُمْ مَنْ صَدَّ عَنْهُ ۚ وَكَفَىٰ بِجَهَنَّمَ سَعِيرًا {55}

Katika wao kuna walio mwamini na katika wao kuna waliojie- pusha naye; na Jahanam yatosha kuwaunguza.