read

Aya 56 – 57: Kubadilisha Ngozi Nyingine

Hakika ambao wamezikufuru Aya zetu tutawatia motoni; kila zitakapoiva ngozi zao, tutawabadilisha ngozi nyingine.

Aya hii ni ubainifu wa mwisho wa Aya iliyotangulia. Na Jahannam yatosha kuwaunguza. Makusudio ya Aya hapa ni kila lililothibiti katika dini kwa dharura; mfano ujuzi wa Mwenyezi Mungu na uweza wake, Malaika, pepo moto na mengineyo yanayorudia kwenye misingi ya dini.

Vilevile mfano wa wajibu wa kufunga, Swala, uharamu wa zina, pombe na mengineyo katika masuala ya kifiqhi na ya matawi ya dini.

Hakuna mwenye shaka kwamba kukanusha ni kukufuru; na je kutia shaka ni kukufuru pia.? Hilo tumelifanyia utafiti kwa ufafanuzi, wakati wa kufasiri Aya 115 ya sura Al-imran kifungu 'mwenye kuacha uislam.'

Unaweza kuuliza: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni mwadilifu, hilo halina shaka. Anapoiunguza ngozi ya mwasi inaondoka na kuisha; kisha huumba ngozi nyingine mpya na kuiadhibu, je, huko si kuadhibui ngozi ambayo haikumuasi? Jambo ambalo halijuzu kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu?

Imepokewa Hadith kutoka kwa Imam Jaffar as-Sadiq (a.s.) inayojibu swali hili: "Hakika ngozi ni hiyo hiyo, si nyingine. Akapiga mfano wa tofali unapolivunjavunja mpaka likawa mchanga, kisha ukalichanganya tena na maji na kutengeza tofali jipya. Hapo litakuwa ndio hilo hilo katika mada yake, lakini ni jengine katika sura yake.

Si mbali kuwa 'kubadilisha ngozi' ni fumbo la adhabu na uchungu wake. Katika hali zote ni kwamba linalopatikana kwetu ni kuamini uadilifu wa Mwenyezi Mungu na uweza wake. Ama ufafanuzi hatuna jukumu nao.
Ili waonje adhabu.

Yaani lililosababisha kubadilishwa ngozi ni kuhisi kwao adhabu ya kudumu. Aina hii ya adhabu inahusika na mkanushaji, na msihrikina na ambaye watu humwogopa kwa shari yake.
Nasi daima, kufa na kupona, tuna imani ya Lailaaha illa illah, Muhammad rasuulu llah, na tunamfanyia uadui kila mwovu. Wanavyuoni wanasema: Watakaoingizwa motoni na wasitoke ni watano: Mwenye kudai uungu, kama vile Namrud na Fir'aun, mwenye kukanusha uungu moja kwa moja, mwenye kumfanyia Mungu washirika, mnafiki na muuaji wa nafsi isiyo na hatia.

Kwa dhahiri ni kuwa mnafiki zaidi ni yule anayeleta vita kwa jina la mwenye kulinda amani; mwenye kuwafanya watumwa watu kwa jina la kuchunga uhuru; mwenye kunyang'anya chakula cha watu kwa jina la kunyanyua maisha yao na mwenye kueneza uovu kwa jina la maendeleo.

Na ambao wameamini na wakatenda amali njema

Umetangulia mfano wa tafsir yake katika Sura Al-imran Aya 15. Kwa hiyo haihitaji tafsir.

إِنَّ اللَّهَ يَأْمُرُكُمْ أَنْ تُؤَدُّوا الْأَمَانَاتِ إِلَىٰ أَهْلِهَا وَإِذَا حَكَمْتُمْ بَيْنَ النَّاسِ أَنْ تَحْكُمُوا بِالْعَدْلِ ۚ إِنَّ اللَّهَ نِعِمَّا يَعِظُكُمْ بِهِ ۗ إِنَّ اللَّهَ كَانَ سَمِيعًا بَصِيرًا {58}

Hakika Mwenyezi Mungu anawaamuru kurudisha amana kwa wenyewe. Na mtakapohukumu baina ya watu muhukumu kwa uadilifu. Hakika Mwenyezi Mungu anawapa mawaidha mazuri sana. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kusikia ni mwenye kuona.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنْكُمْ ۖ فَإِنْ تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّهِ وَالرَّسُولِ إِنْ كُنْتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا {59}

Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na wenye mamlaka katika nyinyi. Na kama mkipingana katika jambo, basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake mkiwa mwamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho. Hilo ni bora zaidi na mwisho mzuri.