read

Aya 58 – 59: Uaminifu Na Uadilifu

Hakika Mwenyezi Mungu anawaamuru kurudishia amana kwa wenyewe.

Aya mbili zimekusanya wajibu wa kutekeleza amana na uadilifu katika hukumu na kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume na mwenye madaraka katika nyinyi. Zimekuja Hadith kadha na Aya kadhaa katika kuhimiza kuchunga amana na kuitekeleza kwa mwenyewe awe mwema au mwovu. Kwa sababu ni haki yake kama binadamu, sio kwa kuwa ni mwema au mwovu.

Mwenyezi Mungu anasema: "Enyi mlioamini msimkhini Mwenyezi Mungu na Mtume wala msikhini amana zenu …" (8:27)

Mtume anasema: "Hana imani asiyekuwa na uaminifu, wala hana dini asiyekuwa na ahadi…" Lakini hakuna katika Qur'an wala Hadith - kwa tunavyojua - maelezo kamili ya amana. Tunavyofahamu ni kuwa amana ni dhamana iliyoko kwako kwa ajili ya mtu mwingine. Ni juu yako kuichunga na kuilinda na kuirudisha kwa mwenyewe anapoitaka kama ilivyo.
Ukiizuia au kuirudisha pungufu, basi wewe ni mhaini wa hukumu ya Qur'an na Hadith.

Si lazima amana iwe ni kitu kinachoonekana, kama vile mali na kitabu, la inaweza kuwa ni siri, nasaha au kazi. Vilevile si lazima mwenyewe hiyo amana awe mtu hasa; inaweza kuwa ni dini au elimu, bali hata nafsi yako yenyewe ikawa ndiyo yenye amana.

Amana ya dini na elimu ni yale unayoyajua katika halali ya Mwenyezi Mungu na haramu yake na katika heri na shari. Amana hii itathibiti kwa kufanya unay- oyajua. Ama amana ya nafsi yako iliyoko kwako, ni lile lililo la masilahi zaidi kwa dunia ya hiyo nafsi na akhera yake.

Kwa maneno mengine, mwaminifu ni yule anayetekeleza kwa ukamilifu bila ya upungufu, ni sawa aliyewajibisha wajibu huu ni dini, elimu, nchi, jamii au kitu chochote kingine.

Kwa hiyo basi amana sio muonjo ulio katika chakula au kinywaji hiki sio kile, au kuwa ni mwanamke huyu si yule wala sio wasifu unaowapendeza watu; kama upole, bali amana ni mshikamano wa maisha na msimamo wake ambao bila huo maisha hayaendi sawa.

Kwenye maana hayo Imam Ali (a.s.) ameishiria kwa kusema: "Amana ni nidhamu ya umma"; yaani umma hautengenei mambo yake ila ikiwa kila mtu atatekeleza yanayotakikana kwake. Na amesema tena: "Ambaye siri yake haitofautiani na dhahiri yake na vitendo vyake havitofautiani na maneno yake, basi atakuwa ametekeleza amana na amewafanyia ikhlasi waja. Na mwenye kuipuuza amana akawa anafanya hiyana na wala asiepushe nafsi yake na dini yake kwa uhaini basi atakuwa amejiingiza katika fedheha duniani, na akhera atapata udhalili na fedheha. Na hakika hiyana kubwa ni kuuhaini umma, na fedheha kubwa ya utapeli ni kuutapeli umma."

Miongoni mwa dalili za kuutukuza uaminifu ni kauli ya mafakihi: "Mwenye kuu- tangazia vita uislamu na waislamu na akahalalisha damu zao na mali zao si kwa chochote ila kwa kuchukia Tawhid, basi ni halali mali yake na damu yake wala haiwi halali amana yake."

Imam Zainul-abidin anasema: "Lau aliyemuua baba yangu angaliniwekea amana upanga aliomuulia, nisingelimuhini."

Mtu mmoja alimuuliza Imam Arridha; "Yahudi amenihini Dirham elfu; kisha faida yake ikaingia mikononi mwangu, Je, nimlipizie?" Imam akamjibu: "Ikiwa amekudhulumu usimdhulumu."

Katika riwaya nyingine amesema: "Ikiwa amekuhini usimuhini wala usijiingize katika aliyokufanyia." Siri katika hilo ni kwamba amana ni haki ya mwenyewe kwa sifa ya kuwa ni mtu sio kuwa ni mwislamu wala mshirikina au si mwema wala mwovu. Tutarudia kuelezea uaminifu tutakapofasiri Aya 72 ya Sura ya Ahzab.

Na mutapohukumu baina ya watu muhukumu kwa uadilifu.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuwajibisha kurudisha amana kwa wenyewe, amefuatisha wajibu wa uadilifu katika kuhukmu baina ya watu. Kwa sababu asiyechunga haki za watu, hana haki ya kuwa hakimu. Wajibu wa uadilifu siyo kwa hakimu tu, bali mtawala vile vile, na mtawala mwadilifu ni yule anayejishughulisha na nyanja zote za maisha; kama vile afya maendeleo, chakula na uhuru kwa wote.

Kabla ya kila kitu ni wajibu kutomwacha mtawala mwenye tamaa - mzalendo au asiyekuwa mzalendo - kutawala mambo ya watu. Matukio tuliyoyapitia yamethibitisha kwamba chimbuko la kwanza na la mwisho la matatizo yaliyotufika ni kutokana na kuwarudisha wezi na wasiokuwa na ujuzi kwenye madaraka na vyeo vya juu.

Ama uadilifu wa hakimu unakuwa katika kuwafanyia kwake usawa watesi wawili katika kila kitu na kila mwenye haki kumpa haki yake, bila ya kuangalia dini yake na itikadi yake; urafiki wake na uadui wake au utukufu wake na uduni wake.

Katika Historia ya sheria hakuna sharia iliyojihimu na kulitilia mkazo hilo kuliko sheria ya Kiislam. Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) anasema: "Mwenye kufanywa hakimu amechinjwa bila ya kisu." Anaonyesha kuwa wajibu wa hakimu ni mzito sana. Kwa sababu inabidi kupigana jihadi kwa nafsi yake na kufanya bidii ikiwa haki haiko. Na akasema tena: "Mahakimu ni watatu: wawili watakuwa motoni na mmoja peponi.

Ama yule atakayekuwa peponi, ni yule aliyejua haki akaihukmu, na wale wawili wataokuwa motoni ni aliyewahukumu watu bila ya ujuzi na aliyekuwa anaijua haki, lakini akahukmu kinyume chake."

Hakika mwenyezi Mungu anawapa mawaidha mazuri sana.

Makusudio ya mawaidha hapa ni amri ya kurudisha amana. Neno ‘mazuri’ linatambulisha kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) haamrishi ila ambalo ndani yake mna kheri na masilahi.

Wenye Mamlaka Ni Nani

Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na wenye mamlaka katika nyinyi.

Maneno na mabishano yamekuwa mengi kuhusu makusudio ya 'wenye mamlaka' na sifa zao; kama ambavyo watawala wamejibandika nayo kuwa ni wajibu kuwatii au angalau kuwanyamazia.

Vile vile kundi la mafakihi limetoa dalili kwa Aya hiyo kuwa chimbuko la sharia na misingi yake linathibiti kwa mambo manne:

1. Kitabu cha Mwenyezi Mungu; kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu: "Mtiini Mwenyezi Mungu."

2. Hadith za Mtume; kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu: "Na mtiini Mtume."

3. Ijmai; kutokana na kauli yake: "Na wenye mamlaka"

    4 Kiyasi; kutokana na kauli yake: "kama mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume." Wakadai kwamba maana likisieni lile lisilo na nukuu (nassi) kutoka katika Qur'an na Hadith. Utakuja ufafanuzi wa hilo.

Hakuna tofauti kuwa Qur'an na Hadith ni machimbuko ya msingi ya sharia. Ama Ijmai na Kiyasi wametofautiana katika hoja yake na katika ufahamisho wa Aya juu yake.

Yafuatayo ni madhumuni ya Aya na rai zilizosemewa Aya hiyo:

1. Hakuna waliotafoutiana katika waislam kwamba kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume kunakuwa ni kufanya amali kwa Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Hadith za Mtume wake na kwamba hiyo ni misingi miwili katika ibara moja: Mwenye kumtii Mtume basi amemtii Mwenyezi Mungu. (4:80)

Alichowaletea Mtume kichukueni na alichowakataza kiacheni. (59:7) Wala hasemi kwa matamanio; hayakuwa haya ila ni Wahyi uliofunuliwa. (53: 3- 4)

Kuanzia hapo ndio wameafikiana waislam kwa kauli moja kukataa kila linalonasibishwa kwa Mtume (s.a.w.) kama linapingana na msingi katika misingi ya Qur'an na hukumu zake. Unaweza kuuliza: Kwa nini kukaririka neno utiifu katika kumtaja Mtume na wala halikukaririka wakati wa kutaja wenye mamlaka?

Jibu: Ni kwa ajili ya kutanabahisha kwamba kumtii Mtume ndio asili kwa dhati yake; sawa na kumtii Mwenyezi Mungu. Kwa sababu hiyo ndiyo ikawa kauli ya kila mmoja wao ni chimbuko katika machimbuko ya sharia, lakini si hivyo katika kuwatii wenye mamlaka. Bali ni tawi la kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume. Hakika wenye mamlaka ni wapokezi wa Mtume.

2. Neno miongoni mwenu, linafahamisha kwa uwazi wazi kwamba hakimu wa waislam anapasa awe ni miongoni mwao, wala haifai kabisa kuwa si miongoni mwao. Hilo linatiliwa nguvu na kauli yake Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu hatawafanyia makafiri njia ya kuwashinda waumini. ( 4:141)

3. Wametofautiana katika makusudio ya wenye mamlaka baada ya kuafikiana kwao juu ya sharti la uislam; kuna waliosema: Ni makhalifa (Khulafau rrashidun). Na waliosema kuwa ni makamanda wa jeshi. Na wengine wakasema ni maulama wa kidini. Sheikh Muhammad Abduh amesema: Wao ni machifu watawala, maulama, viongozi wa jeshi na viongozi wengineo ambao watu wanawarudia katika haja na masilahi. Wakiafikiana hawa juu ya jambo, ni wajibu kuwatii kwa sharti ya kuwa wawe waaminifu na wasihalifu amri ya Mwenyezi Mungu wala Sunna ya Mtume wake. Na wawe na hiyari katika utafiti wao wa amri na kuafikiana kwao.

Shia wamesema kuwa Mwenyezi Mungu ameunganisha kwa herufi ‘Wau’ baina ya kuwatii wenye mamlaka na kumtii Mtume bila ya sharti lolote; na kuunganishwa kwa herufi ‘Wau’ kunahukumia kuchanganya na kushirikiana katika hukumu. Maana ya haya ni kuwa kuwatii wenye mamlaka ni kumtii Mtume na kwamba amri yao ni amri yake.

Hakuna mwenye shaka kwamba daraja hii tukufu haiwi ila kwa anayesifika na kustahiki twaa hii na hakuna kitu kitakachomfanya astahiki hayo isipokuwa kuhifadhika na makosa na maasi (isma). Ndiko pekee kunakokufanya kumtii yeye na kumtii Mtume kuwe sawa.

Arrazi amekiri waziwazi fikra ya Isma kwa kusema kuwa wenye mamlaka ambao ni wajibu kuwatii hapana budi wawe ni maasumin (waliohifadhiwa na dhambi). Na Arrazi - kama anavyojulikana - ni miongoni mwa maulama wakubwa wa kisunni; mwanafalsafa na mfasiri wao. Haya ndiyo aliyoyasema ninamnukuu;"Jua kwamba kauli yake Mwenyezi Mungu, ‘wenye mamlaka inafahamisha kwetu kwamba Ijmai ni hoja.

Dalili ya hilo ni kwamba Mwenyezi Mungu ameamrisha kutiiwa wenye mamlaka moja kwa moja katika Aya hii. Na ambaye Mwenyezi Mungu anaamrisha atiiwe hapana budi awe amehifadhiwa na makosa. Kwa sababu lau asingelikuwa amehifadhiwa na makosa basi itakuwa anakadiriwa kufanya makosa, ambapo Mwenyezi Mungu ameamrisha afuatwe.

Kwa hiyo hilo litakuwa ni kuamrisha kufanywa makosa; na inajulikana kwamba kumfuata mwenye makosa kumekatazwa. Kwa hiyo imethibiti kwamba makusudio ya wenye mamlaka waliotajwa katika Aya hapana budi wawe wamehifadhiwa na makosa."

Hivi ndivyo walivyosema Shia katika kufasiri Aya hii. Tofauti iliyoko kati yao na Sunni ni katika kufuatilia na kumwainisha huyo mwenye kuhifadhiwa na makosa (maasum). Sunni wanasema kuhifadhiwa ni kwa umma. Wamefasiri umma kuwa ni watatuzi. Wengi wao wakasema ni baadhi ya watatuzi. Shia wamesema kuwa makusudio ya wenye mamlaka ni Ahlul-bayt ambao wametakaswa na makosa na kutwahirishwa na uchafu.

Kwa hiyo fikra ya Isma haihusiki na Shia tu, na wala sio waliosema peke yao, bali iko kwa Sunni; kama ambavyo iko kwa Shia. Hivyo kuchukulia kuwa shia tu ndio waliosema kauli hiyo ni kwa ajili ya ukaidi tu, na kueneza utengano.

Shia wametoa dalili juu ya Isma kwa Ahlul-baiti, kwamba ni kipawa cha Mwenyezi Mungu. Anawahusu watu anaowaridhia miongoni mwa waja wake. Haiwezekani mtu kuitafuta mwenyewe Isma kwa namna yoyote atakavyojitahidi; kinyume na sifa nyingine. Kwa hiyo njia ya kujua Isma inajulikana kwa wahyi tu.

Na imethibiti kauli wazi katika Qur'an na Hadith juu ya Isma ya Ahlul-bait. Miongoni kwa hayo ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Hakika Mwenyezi Mungu anataka kuwaondolea uchafu (Enyi) Ahlul-baiti na kuwatakasa kabisa kabisa." (33:33)

Pia kauli yake Mjumbe wa Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Mwenye kunitii mimi ndio amemtii Mwenyezi Mungu; na mwenye kuniasi amemuasi Mwenyezi Mungu; na mwenye kumtii Mwenyezi Mungu, ndio amenitii mimi na mwenye kumwasi ameniasi mimi." Ameipokea Hakim katika Mustadrak na akasema: "Hii ni Hadith sahihi."

Vilevile ameisahihisha Dhahabiy katika Tal-khisu al-mustadrka. Katika kitabu hicho kuna hadith ya Mtume (s.a.w.) amesema: "Ali yuko pamoja na Qur'an na Qur'an iko pamoja na Ali, viwili hivyo havitatengana mpaka vinijie katika Birika."

Vile vile amepokea Tirmidhi katika Musnad yake, Hakim katika Mustadrak yake na Ibn Hajar katika Sawaiq yake kutoka kwa Mtume Mtukufu (s.a.w.) kwamba yeye amesema: "Ewe Mola wangu izungushe haki pamoja na Ali popote aendapo." Pia Imam Ibn Hambal, Tirmidhi, Hakima na Ibn Hajar, wamepokea kauli yake Mtume (s.a.w.): " Mimi nawaachia vitu ambavyo kama mkishika- mana navyo hamtapotea baada yangu, navyo ni vizito viwili: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu Ahlul-bait wangu."

Imekuwa mashuhuri Hadith kutoka kwa Mtume isemayo: "Hakika mfano wa Ahlul-bait wangu kwenu ni kama mfano wa safina ya Nuh, mwenye kuipanda ataokoka." Na Hadithi nyinginezo nyingi. Zote hizo zimeandikwa katika vitabu vya Hadith vya Sunni na sahih zao, na zimepokewa na wategemewa wao.

Shia wamezikusanya na kuziwekea vitabu maalum vya zamani na vya kisasa. Vya zamani ni kama Kitab shafi cha Shariff Murtadha, Tal-khisu shafi cha Sheikh Tusi, Nahjul-haq cha Allama Hilli na katika Hadith za Mujallad wa tatu katika A'yanusha Shia cha Sayyid Muhsin Amin. Vile vile Dalailus-swidq cha Sheikh Mudhaffir na Muraja't cha Sharafuddin.

Kwa ujumla ni kwamba Shia na Sunni wanaamini Isma kwa pamoja kama msingi1 Vile vile wameafikiana Shia na Sunni wengi kwamba wenye mamlaka waliotajwa katika Aya wamehifadhiwa na dhambi.

Pia wanaafikiana kwamba dalili ya kuhifadhiwa kwao ni kwamba Mwenyezi Mungu amewajibisha watiiwe kama alivyowajibisha kutiiwa yeye Mwenyezi Mungu na Mtume. Lakini Sunni wakatofautiana na Shia kuwa makusudio ya wenye mamlaka waliohifadhiwa na makosa, ni watatutuzi wa mambo au ni Ahlul-bait?

Sunni wakasema ni watatuzi wa mambo. Shia wakasema ni Ahlul-bait. Kwa sababu Isma ni kipawa cha Mwenyezi Mungu, hakijulikani ila kwa kauli wazi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Mtume. Na imethibiti kauli kutokana nao juu ya Isma ya Ahlul-bait. Kwa hiyo makusudio ya wenye mamlaka ni Ahlul-bait si wengineyo.

Kwa maneno mengine ni kuwa wenye mamlaka katika Aya ni wenye kuhifad- hiwa na makosa kwa sababu ya wajibu wa kuwatii wao. Kwa sababu ambaye ni wajibu kumtii ni maasum. Vile vile kunathibiti kuhifadhiwa kwa Ahlul-baiti kwa kauli wazi na hakukukuthibiti kwa wengineo.

Na ambaye kumethibiti kuhifadhiwa kwake, basi ni wajibu kumtii. Kwa hiyo natija ni kuwa Ahlul-baiti ndio wenye mamlaka si wengineo. Kama kusema: Msikilize mwenye kunasihi aliye mwaminifu, wala hakuna mwaminifu ila Zaid. Kwa hiyo natija ni msikilize Zaid.

Katika ambayo wameyatolea dalili Shia juu ya kutojuzu kuwafuata watatuzi katika mambo ya kidini ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Lakini watu wengi hawajui." Na kauli yake: "Na wengi wao hawaelewi." (5:103)
Maana ya haya ni kuwa haki haijulikani kwa kuangalia idadi ya watu, wawe wengi au wachache isipokuwa hujulikana kwa kuchukuliwa kutoka katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake na hukumu ya kiakili ya msingi ambayo hakuna wanaotofautiana, - Kwa kuongeza - ninaandika maneno haya katika mwezi Machi 1968 na uchaguzi wa wabunge wa Lebanon umeuma mchanga; watu wanasongamana kwenye masanduku ya kura ili wamchague aliyenunua sauti za watu baada ya mnada, au yule aliyewaahidi watu wake kutekeleza matakwa yao.

Salaam zimfikie yule aliyesifu baadhi ya uchaguzi kwa kusema: "Mtu anaitikiwa pamoja na ukorofi wake. Mwengine anafuatwa kwa sababu ya udugu pamoja na maovu chungu nzima aliyonayo."

Mwengine akasema: "Ni wachungwa mazuzu wanaufata kila sauti ya mchungaji. Ni bendera wanafuata upepo. Hawakupata mwanga wa elimu wala hawakuegemea nguzo thabiti."

Na kama mkipingana katika jambo, basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Tumetangulia kusema kuwa kauli yake Mwenyezi Mungu mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume - kwa maafikiano ya wote inafahamisha kushikamana na Qur'an na Hadithi; na kwamba kauli yake Mwenyezi Mungu. Na wenye mamlaka katika nyinyi, inafahamisha - kwa shia - wajibu wa kuwatii Ahlul-bait; na kwa sunni wengi inafahamisha kuwatii watatuzi wa mambo.

Sasa tuzungumzie kauli hii, ‘Na kama mkipingana.’ Je inafahamisha wajibu wa kutumia kiasi au iko mbali na hayo? Kabla ya jawabu tutupe swali hili:

Kwa nini Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawajibisha kurudishwa mapingano Kwake na kwa Mtume tu, bila ya wenye mamlaka, ambapo Yeye amewajibisha kuwatii wote watatu?

Jibu: Kwa sababu mzozo huenda ukatokea katika kuwajua hao wenye mamlaka; kama ambavyo limetokea hilo. Sunni wakasema: Ni watatuzi wa mambo na Shia wakasema ni Ahlul-bait. Kwa hiyo katika mzozo huu inabidi kurudia Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Hadith za Mtume wake. Kwa ajili hiyo ndio Shia wakatoa dalili Aya ya tathir 2 na Hadith. Sasa turudie kwenye wajibu wa kutumia kiasi au kutotumia.

(Qiyas), ni kutoa hukumu ya tukio iliyoelezwa wazi na sharia kwa tukio jengine ambalo hukumu yake haikuelezwa wazi; kwa kushirikiana matukio mawili katika sababu zilizotolewa na fakihi. Mfano sheria, imeeleza kuwa nyanya wa upande wa mama anarithi na wala isielezwe wa upande wa baba. Tukamrithisha nyanya wa upande wa baba kwa kuchukulia kiasi cha wa upande wa mama. Kwa sababu wote ni nyanya.

Sunni wamesema kuwa kauli yake Mwenyezi Mungu; Mkipingana katika jambo lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume inafahamisha kusihi qiyasi; kuwa maana yake ni lirudisheni kwenye tukio alilolibainisha Mwenyezi Mungu hukumu yake; yaani linalofanana nalo.

Shia wamesema kuwa Aya iko mbali kabisa na qiasi wala haifahamishi zaidi ya kurudia Qur'an na Hadith katika masuala ya kidini inapotokea tofauti baina ya mafakihi. Na kauli za maimamu walio maasum zinaingia katika hadith. Kwa sababu ni riwaya kutoka kwa babu yao Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.)

Ama njia yao katika ambalo halikuelezwa wazi katika Kitab wala Hadith ni kurudia kwenye hukumu ya akili ya mkato iliyo dhahiri ambayo haiwezi kutofautiana. Mfano ubaya wa mateso bila ya ubainifu; na ambayo wajibu hautimii ila kwalo, basi ni wajib. Kwa hiyo qiasi sio katika kauli hii. Kwa sababu natija zake zote ni za kudhania; na dhana haitoshelezi kitu3.

Katika waliyoyatolea dalili Shia kuhusu kubatilika kwa qiyas ni kwamba mambo ya kawaida, inasihi kuyafanyia qiyas. Kwa vile sababu zake ziko kwenye ukawaida. Ama hukumu za kidini haisihi kufanya qiyas. Kwa sababu sharia imekusanya pamoja vitu vinavyotofautiana; kama katika mambo yanayovunja udhu ambapo imeweka sawa kulala na kukojoa.

Mkiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho.

Mwenye Majmau anasema: "Ni ubainifu wa uwazi ulioje wa kauli hii!" Nasi twasema: Ni uzuri ulioje wa tafsir wa hiyo!

Hilo ni bora zaidi na mwisho mzuri

Yaani kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume, na kuirudisha hukumu ya kutofau- tiana kwa Qur'an na Hadith ni mwisho mzuri. Hii ni ikiwa tutalifasiri neno Taawil katika Aya hii kwa maana ya mwishilio.

Imesemekana kuwa makusudio ya neno Taawil hapa ni tafsiri ambapo maana yatakuwa ni tafsir ya Mwenyezi Mungu na Mtume katika mnayopingana ni bora na nzuri kuliko tafsiri yenu. Vyovyote iwavyo neno Taawil linachukua maana zote mbili.

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ يَزْعُمُونَ أَنَّهُمْ آمَنُوا بِمَا أُنْزِلَ إِلَيْكَ وَمَا أُنْزِلَ مِنْ قَبْلِكَ يُرِيدُونَ أَنْ يَتَحَاكَمُوا إِلَى الطَّاغُوتِ وَقَدْ أُمِرُوا أَنْ يَكْفُرُوا بِهِ وَيُرِيدُ الشَّيْطَانُ أَنْ يُضِلَّهُمْ ضَلَالًا بَعِيدًا {60}

Je, huwaoni wale wanaodai kuwa wao wanaamini uliyoteremshiwa wewe na yalioteremshwa kabla yako, wanataka kwenda kuhukumiana kwa taghut na hali wameamrishwa wamkatae. Na Shetani anataka kuwapoteza upotevu wa mbali.

وَإِذَا قِيلَ لَهُمْ تَعَالَوْا إِلَىٰ مَا أَنْزَلَ اللَّهُ وَإِلَى الرَّسُولِ رَأَيْتَ الْمُنَافِقِينَ يَصُدُّونَ عَنْكَ صُدُودًا {61}

Na wakiambiwa njooni kwenye yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu na kwa Mtume, utawaona wanafiki wanajizuia na kukupa mgongo.

فَكَيْفَ إِذَا أَصَابَتْهُمْ مُصِيبَةٌ بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيهِمْ ثُمَّ جَاءُوكَ يَحْلِفُونَ بِاللَّهِ إِنْ أَرَدْنَا إِلَّا إِحْسَانًا وَتَوْفِيقًا {62}

Basi itakuwaje watakapopatwa na msiba kwa yaliyotangulizwa na mikono yao kisha wakakujia wakiapa kwa Mwenyezi Mungu (wakisema): Hakika sisi hatukupendelea ila wema na mapatano.

أُولَٰئِكَ الَّذِينَ يَعْلَمُ اللَّهُ مَا فِي قُلُوبِهِمْ فَأَعْرِضْ عَنْهُمْ وَعِظْهُمْ وَقُلْ لَهُمْ فِي أَنْفُسِهِمْ قَوْلًا بَلِيغًا {63}

Hao ni ambao Mwenyezi Mungu anayajua yaliyo katika nyoyo zao. Basi achana nao na uwape mawaidha na uwaambie maneno yatakayoingia katika nafsi zao.
  • 1. Fikra ya kuhifadhiwa na makosa (Isma) haihusiki na Shia wala Sunni. Wakristo pia wamesema kwamba Baba mtakatifu amehifadhiwa na makosa. Wakomunist wamesema ni Max na Lenin. Wachina wakasema ni Mao tse Tung. Ikhwanul muslimin wakasema ni Hassan Al-banna. Qaumiyyun wa Syira wakasema ni Anton Saada. Namna hii kila kikundi kinasema kuwa rais wake na mwasisi wake aliyeweka misingi anahifadhiwa na makosa (maasum). Tumezungumza kwa urefu kuhusu Isma katika kufasiri sura ya 2: 124.
  • 2. Aya (33: 33)
  • 3. Haya ndiyo waliyo nayo Shia hivi leo. Lakini yaliyokuwepo wakati wa Amirul-mumin kwa Malik Ashtar, ni kwamba kurudisha kwa Mwenyezi Mungu katika Aya ni kuchukua kauli wazi katika Kitab cha Mwenyezi Mungu; na kurudisha kwa Mtume ni kuchukua Hadith zake ambazo Waislam wamekubaliana kuwa ni zake.