read

Aya 60 – 63: Wanataka Kuhukumiana Kwa Ubatilifu

Je, huwaoni wale wanaodai kuwa wao wanaamini uliyoteremshiwa wewe na yaliyoteremshwa kabla yako, wanataka kwenda kuhukumiana kwa taghuti na hali wameamrishwa wamkatae.

Je huwaoni, ni msemo unaoelekezwa kwa Mtume (s.a.w.) kwa njia ya swali ukiwa na makusudio ya kustaajabia hali ya wanafiki, walioficha ukafiri na kudhihirisha uislam na kuamini vitabu vya Mwenyezi Mungu. La kustaajabu ni kwamba wao wanajikadhibisha wenyewe; pale walipokataa kuhukumiwa kwenye haki na kwenda kwenye batili; pamoja na kuwa uislam umewaamrisha kujiepusha na upotevu na wabatilifu.

Mwenye Majmaul-bayan, anasema: aligombana yahudi na mnafiki katika waislam, yahudi akasema: "Tukahukumiwe kwa Muhammad." Kwa sababu alikuwa anajua kuwa Muhammad hakubali rushwa wala hafanyi dhulma. Mnafiki akasema: "Si yuko Kaabul-Ashraf," (yahudi) kwa sababu alijua kuwa Ka'ab anachukua rushwa na anadhulumu katika hukumu.
Pamoja na kuwa wafasiri hawathibitishi sababu ya kushuka Aya hii, hatuoni mfano unaofasiri makusudio ya Aya ulio wazi kuliko tukio hili aliolitaja mwenye Majmaul-bayan. Mnafiki alikataa kuhukumiwa na Mtume (s.a.w.), kwa sababu anamkanusha yeye na dini yake. Ama yahudi anaamini uyahudi, lakini pamo- ja na hayo alikataa kuhukumiwa kwa yahudi mwenzake na akataka kuhukumi- wa kwa Mtume (s.a.w.) pamoja na kuwa anamkanusha yeye na dini yake, Siri ilikuwa ni manufaa tu.

Dhahiri hii haihusiki na yahudi tu, yeyote mwenye kupata manufaa katika dini au msingi wowote, haitakikani kumtegemea wala dini yake ila baada ya mitihani. Kwa sababu watu wengi wanakabidhiwa maelfu na kuishi vizuri, si kwa lolote ila kwa kuaminiwa tu. Huenda hao ndio wanaoambiwa na kauli yake

Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na miongoni mwa watu kuna wanaomwabudu Mwenyezi Mungu ukingoni. Ikiwafika kheri hutulia kwayo na ukimfikia msukosuko hugeuza uso wake. Amepata hasara ya dunia na khera." (22: 11)

Imam Ali (a.s.) amesema: "Sifa ni baada ya misukosuko." Mtoto wake, Husein (a.s.) naye anasema: "Watu ni watumwa wa dunia, dini iko juu juu tu ya ndimi zao. Wakipatwa na misukosuko huwa wachache wenye dini." Mtume Mtukufu naye alikuwa akisema katika raha: "Sifa njema ni za mwenye kuneemesha mwenye kuzidisha." Na wakati wa shida husema: "Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu kwa kila hali."

Akionyesha kuwa mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu yuko radhi kwa aliyokadiriwa hata katika hali hii; sawa na mtoto mwema anayebakia kumsafia nia mzazi wake hata katika hali ya kutiwa adabu. Na mjukuu wake Imam Zainul-abidin (a.s.) alikuwa akisema miongoni mwa anayoyasema anapopatwa na shida: "Ewe Mola wangu! Ni ipi katika ya hali mbili ambayo nina haki zaidi ya kukushukuru? Ni ipi kati ya nyakati mbili ambayo ni bora zaidi kukusifu? Je ni wakati wa uzima uliponipa afya; au ni wakati wa ugonjwa uliponipata? Ewe Mola wangu! Jaalia kutoka kwangu kwenye ugonjwa kuwa ni msamaha wako na kusilimika kwangu na shida hii kuwa ni faraja iliyotoka kwako."

Na shetani anataka kuwapoteza upotevu wa mbali.

Hii ni dalili ya wazi kwamba shari inatokana na shetani si kwa Mwenyezi Mungu. Na kila fikra inayokupelekea kufanya shari huitwa shetani. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: Ambaye hutia wasiwasi katika nyoyo za watu katika majini na watu. (114: 5 - 6)

Na kuna Hadith isemayo: "Shetani akikwambia: Ni wingi ulioje wa swala yako! Mwambie, kughafilika kwangu ni zaidi. Na akikwambia ni wingi ulioje wa mema yako! Mwambie maovu yangu ni zaidi. Na akikwambia ni wingi ulioje wa waliokudhulumu mwambie: Nilio wadhulumu ni wengi zaidi."

Kwa dhahiri ni kuwa nafsi ndiyo inayompa picha mtu kwamba yeye ni mfanya ibada sana, mtenda mema na mwenye kudhulumiwa. Wala hahadaiki kwa ubatilifu huu ila mjinga.

Na wakiambiwa njooni kwenye yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu na kwa Mtume utawaona wanafiki wanajizuia na kukupa mgongo.

Kwa sababu wao hawamwamini Mwenyezi Mungu wala Mtume wake wala kitu chochote isipokuwa dunia.

Basi itakuwaje watakapopatwa na msiba kwa yaliyotangulizwa na mikono yao.

Na msiba mkubwa zaidi kwa wanafiki ni kufunuka mambo yao na kufichuka siri yao hadharani, ambapo wanajulikana na watu kwa hiyana, uongo, vitimbi, hadaa, woga na utwevu.

Kisha wanakujia wakiapa kwa Mwenyezi Mungu (wakisema): Hakika sisi hatukupendelea ila wema na mapatano.

Wanamjia Mtume wakinyenyekea wakitoa sababu za uongo; na Mwenyezi Mungu, Mtume wake, na watu wanajua kwamba wanafiki ni waongo na kwam- ba wao wanafanya viapo vyao ni ngao ya fedheha na kuadhibiwa.

Basi achana nao.

Yaani wapuuze, usiwakubalie udhuru kwa sababu wao wanachukulia kukubali kwako huku katika malengo yao. Wala usiwaadhibu kwa sababu wametoa udhuru japokuwa kwa dhahiri.

Na wape mawaidha na waambie maneno yatakayoingia katika nafsi zao.

Mtume (s.a.w.) alikuwa akiwaamuru kumcha Mwenyezi Mungu kwa namna ambayo wanahisi kuwa wao ni wakosaji na kwamba ni juu yao kujisafisha kwa kutubia.

Huu ndio msingi wa uislamu kwa kila mwenye makosa, haumfanyii haraka kumwadhibu wala kumkatisha tamaa, bali hutumia njia zote za kumtengeneza. Mwenyezi Mungu anasema: "Nendeni kwa Firaun, hakika yeye amepetuka mipaka. Kamwambieni maneno laini huenda akawaidhika au ataogopa " (20: 44)

Imam, Amirul-muminin anasema: "Fakihi aliyekamilika ufakihi wake, ni yule asiyewakatisha tamaa watu na rehema ya Mwenyezi Mungu na asiyewavunja moyo kabisa na rehma ya Mwenyezi Mungu na kutowapa amani ya kuokoka na adhabu ya Mwenyezi Mungu."

Chimbuko la hekima hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu: "Sema enyi waja wangu mliojidhulumu nafsi zenu! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu.” (39:53)

وَمَا أَرْسَلْنَا مِنْ رَسُولٍ إِلَّا لِيُطَاعَ بِإِذْنِ اللَّهِ ۚ وَلَوْ أَنَّهُمْ إِذْ ظَلَمُوا أَنْفُسَهُمْ جَاءُوكَ فَاسْتَغْفَرُوا اللَّهَ وَاسْتَغْفَرَ لَهُمُ الرَّسُولُ لَوَجَدُوا اللَّهَ تَوَّابًا رَحِيمًا {64}

Na hatukumpeleka Mtume ila atiiwe kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Na lau kwamba wao walipojidhulumu wangekujia wakaomba maghufira kwa Mwenyezi Mungu na wakaombewa maghufira na Mtume, wangelimkuta Mwenyezi Mungu ni mwenye kutakabali toba na mwenye kurehemu.

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنْفُسِهِمْ حَرَجًا مِمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا {65}

Naapa kwa Mola wako! Hawataamini mpaka wakufanye wewe ndiye hakimu katika yale wanayohitalifiana baina yao. Kisha wasione dhiki katika nyoyo zao kwa uliyohukumu na wanyenyekee kabisa kabisa.

وَلَوْ أَنَّا كَتَبْنَا عَلَيْهِمْ أَنِ اقْتُلُوا أَنْفُسَكُمْ أَوِ اخْرُجُوا مِنْ دِيَارِكُمْ مَا فَعَلُوهُ إِلَّا قَلِيلٌ مِنْهُمْ ۖ وَلَوْ أَنَّهُمْ فَعَلُوا مَا يُوعَظُونَ بِهِ لَكَانَ خَيْرًا لَهُمْ وَأَشَدَّ تَثْبِيتًا {66}

Na lau kama tungewalazimisha kuwa jiueni au tokeni katika miji yenu, wasingelifanya hilo isipokuwa wachache katika wao. Na lau kama wangelifanya yale waliyoagizwa, ingelikuwa heri kwao na uthibisho wa nguvu zaidi.

وَإِذًا لَآتَيْنَاهُمْ مِنْ لَدُنَّا أَجْرًا عَظِيمًا {67}

Na hapo tungewapa malipo makubwa kutoka kwetu.

وَلَهَدَيْنَاهُمْ صِرَاطًا مُسْتَقِيمًا {68}

Na tungewaongoza njia iliyonyooka.

وَمَنْ يُطِعِ اللَّهَ وَالرَّسُولَ فَأُولَٰئِكَ مَعَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللَّهُ عَلَيْهِمْ مِنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاءِ وَالصَّالِحِينَ ۚ وَحَسُنَ أُولَٰئِكَ رَفِيقًا {69}

Na wenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume, basi hao (watakuwa) pamoja na wale aliowaneemesha Mwenyezi Mungu miongoni mwa Manabii na wasadikishaji na mashahidi na watu wema. Na hao ndio marafiki wema.

ذَٰلِكَ الْفَضْلُ مِنَ اللَّهِ ۚ وَكَفَىٰ بِاللَّهِ عَلِيمًا {70}

Hiyo ni fadhila itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na anatosha Mwenyezi Mjuzi.