read

Aya 64 – 70: Hatukupeleka Mtume Ila Atiiwe

Na hatukumpeleka Mtume ila atiiwe kwa amri ya Mwenyezi Mungu.

Unaweza kuuliza: Habari hii ni kama kufafanua ufafanuzi. Kwa sababu kumtegemeza Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenyewe kunafahamisha kuwa amepelekwa ili atiiwe, vinginevyo kutegemezwa kusingelikuwa na maana. Basi je ubainifu una makusudio gani?

Jibu: Makusudio ni kutoa hoja kwa wanafiki waliomwasi Mtume na kukataa kuhukumiwa naye. Hoja yenyewe ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewabainishia wanafiki na wengineo katika Aya hii kuwa kumwasi Mtume sio kumwasi yeye hasa, bali ni kumwasi Mwenyezi Mungu. Ambapo amekataa mambo yasipitie isipokuwa kwenye desturi yake. Na miongoni mwa desturi ni kufikisha hukumu zake kwa waja wake kupitia Mtume atokanaye na wao.

Kwa hiyo basi mwenye kumpinga katika anayoyafikisha miongoni mwa hukumu za Mwenyezi Mungu, atakuwa amempinga Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo natija ni kuwa wanafiki na kila anayemwasi Mwenyezi Mungu wanastahili adhabu. Kwa sababu wanamwasi na kumkhalifu.Mwenyezi Mungu

Na lau kwamba wao walipojidhulumu wangekujia wakaomba maghufira kwa Mwenyezi Mungu na wakaombewa maghufira na Mtume, wangemkuta Mwenyezi Mungu ni mwenye kutakabali toba mwenye kurehemu.

Wamejidhulumu pale walipojiingiza katika adhabu na maangamizi kutokana na dhambi walizozifanya. Wamemdhulumu Mwenyezi Mungu vilevile kwa kupetuka mipaka yake na kuasi amri zake. Pia wamemdhulumu Mtume kwa kuwa wao wamekataa hukumu yake na kuridhia hukumu ya ubatilifu na kumwonyesha kinyume na dhamira zao.

Pamoja na yote hayo bado Mwenyezi Mungu amewafungulia mlango wa toba. Ni juu yao basi kuuelekea na kutaka maghufira. Wakifanya hivyo atawaingiza kwenye rehema yake. Na wakitofanya, basi hawatapata wa kuwanusuru wala wa kumsaidia zaidi ya Mwenyezi Mungu.

Unaweza kuuliza kuwa kauli yake Mwenyezi Mungu, ‘Na wakaombewa maghufira na Mtume; inapingana na misingi ya kiislam ambayo inapinga kuwe na wasita baina ya Mwenyezi Mungu na watu?

Jibu: Ni kweli kuwa hakuna wasita baina ya Mwenyezi Mungu na waja wake ila katika mambo yanayorudia kwenye haki yake Mwenyezi Mungu Mtukufu na kumkosea Yeye. Ama kukosea haki za watu, basi amri ni yao; na msamaha wake unaombwa kwao si kwengine. Na wanafiki walimwudhi Mtume na kumkosea haki yake. Hivyo ikawa hakuna budi katika toba yao ila kudhihirisha majuto kwake na kumwomba msamaha. Na kila unayemdhihirishia kinyume cha dhamira yako basi umemdhulumu na kumkosea. Bali lau mtu fulani alikudhania sifa nzuri usizo nazo na akakuamini kisha ukamfanya mjinga na tena ukamkimbia, basi wewe ni dhalimu.

Naapa kwa Mola wako! Hawataamini mpaka wakufanye wewe ndiye hakimu katika yale wanayohitalifiana baina yao.
Kwa sababu hukumu zote anazozitamka Muhammad, hazitokani na yeye, isipokuwa zinatoka kwa Mwenyezi Mungu peke yake, na yeye Mtume ni msemaji wake.

Kisha wasione dhiki katika nyoyo zao kwa uliyohukumu na wanyeyekee kabisa kabisa.

Maana yake ni kuwa wao hawatakuwa waumini mpaka wajue kwa yakini kwamba hukumu yake ni hukumu ya Mwenyezi Mungu hasa, na anayekupinga wewe ndio amempinga Mwenyezi Mungu. Ni muhali kwa Muumin wa kweli kuhisi dhiki kwa hukumu anayojua kuwa inatokana na Mwenyezi Mungu.

Ndio ni kweli muumin anaweza kutaka baina ya nafsi yake kuwa kula mchana mwezi wa Ramadhan kuwe halali, lakini pamoja na hayo anafunga na kujizuilia kula kwa kuhofia adhabu ya Mwenyezi Mungu ambayo ni kali na ya mashaka zaidi ya kufunga. Na huenda nafsi yake ikamshinda na maasi, lakini yeye anavumilia na kuilaani, kwa sababu itakuwa imepuuza haki. Hii ndiyo imani hasa.

Na lau kama tungewalazimisha kuwa jiueni au tokeni katika miji yenu, wasingefanya hilo isipokuwa wachache katika wao.

Hakika dini ya Mwenyezi Mungu ina wasaa, nyepesi na ni bora na ya utengenefu. Haimkalifishi yeyote zaidi ya uwezo wake, bila ya manufaa yake ya kidini na ya kidunia. Mwenyezi Mungu anasema: "Wala hakuweka mambo mazito katika dini." (22: 78)

Na amesema tena: "Enyi mlioamini! Mwitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume wake katika yatakayowapa uhai." (8:24)

Unaweza kuuliza: Ikiwa mambo ni hivyo, basi hakuna wajihi wa kauli yake Mwenyezi Mungu (Na lau kama tungewalazimisha kuwa jiueni…) kwa sababu hii ni amri ya lisilowezekana?

Jibu: Hii ni kiasi cha kukadiria tu, na ndio maana limekuja neno "lau" linalofahamisha kuzuilika jambo kwa kuzuilika jengine.

Makusudio ya kukadiria huku ni kubainisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwamba wanafiki hawana udhuru kabisa katika kuzifanyia inadi hukumu zake Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ambazo hakuna mashaka wala kujiangamiza, bali ni rehema kwao. Lakini pamoja na haya yote waliasi.

Ikiwa wanafiki wameasi na kuzigomea hukumu za Mwenyezi Mungu Mtukufu pamoja na wepesi uliomo, basi katika Masahaba wa Mtume (s.a.w.) kuna ambao lau wangeliamrishwa kujiua wangelifanya. Nao Mwenyezi Mungu amewaelezea kuwa ni wachache. Miongoni mwa wachache hao ni Yasir na mkewe, ambao walikufa shahid katika adhabu kwa ajili ya Uislam. Hao ni wazazi wa Ammar aliyeuliwa na kikundi kiovu siku ya vita vya Siffin. Alikuwa katika munajat akimwambia Mwenyezi Mungu kwa kusema: "Ewe Mola wangu! Hakika wewe unajua lau ikiwa mimi ninajua kuwa kukuridhisha ni kuki- ta upanga wangu huu kifuani mwangu na utokeze mgongoni mwangu, ningelifanya."

Na lau kama wangefanya yale waliyoagizwa, ingekuwa heri kwao na uthibitsho wa nguvu zaidi.

Makusudio ya waliyoagizwa, ni kumtii Mwenyezi Mungu katika amri zake na makatazo yake, "… Na anayemtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake hakika amefanikiwa mafanikio makubwa." (33: 71)

Makusudio ya kuthibitisha ni kuthubutisha imani. Imam Ali (a.s.) anasema: "Katika imani kuna zilizo thabiti katika nyoyo na kuna zilizokaa kombo kwenye nyoyo kwa muda maalum."

Na hivi ndivyo alivyofasiri Imam as-Sadiq (a.s.) kauli yake Mwenyezi Mungu: "…Pako mahali pa kutulia pa kupita njia (6:98)

Na hapo tungewapa malipo makubwa kutoka kwetu.

Huu ndio ubainifu wa kheri katika kauli yake: "ingelikuwa kheri kwao" na kila malipo ya Mwenyezi Mungu na thawabu zake ni kubwa, hata yakiwa machache, sikwambii akiyasifu kwa ukubwa.

Na wenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume basi hao (watakuwa) pamoja na wale aliowaneemesha Mwenyezi Mungu miongoni mwa Manabii na wasadikishaji na mashahidi na watu wema. Na hao ndio marafiki wema.

Aya hii ni kutilia mkazo Aya iliyotanguilia na kuhimiza imani na wema ambao utamfanya mtu kuwa ni rafiki wa Mitume, mashahidi na watu wema.

Ni Nani Wasadikishaji?

Sheikh Muhammad Abduh anasema: "Wasadikishaji ni wale walio na maumbile matakatifu, kiasi kwamba wao wanaipambanua haki na batili, heri na shari kwa kuiona tu."

Kauli hii iko karibu na kauli ya kisufi kwamba mtu akijitahidi na kuizowesha nafsi yake ataijua haki bila ya kujifundisha. Ilivyo hasa ni kufasiri wasadik- ishaje kuwa ni Maasum (walio hifadhiwa na makosa) waliokamilika na

wanaokamilisha, kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewajaalia katika daraja ya pili kutoka Mitume bila ya kuweko kitu kingine. Na daraja hii haitakuwa kabisa kwa ambaye inajuzu kwake kukosea. Kwa sababu anayeweza kufanya makosa, hawezi kuwa mkamilifu wa mwengine kwenye ukamilifu wa uhakika. Bali atahitajia mkamilifu wa kihakika atakayemrudisha kwenye usawa. Na mkamilifu huyu ni Masum.

Kwa maneno mengine wasadikishaji wako aina mbili:

Wa kwanza, ni yule asiyekusudia kusema uongo, lakini inawezekana kusema akakosa au kutatizika; kama mwenye kuelezea jambo mwenyewe akiamini ni mkweli katika anayoyaelezea, kisha ikabainika kwa habari yake si kweli. Hapo anakuwa mkweli katika makusudio yake na habari yake ni ya uongo. Haya hutokea mara nyingi.

Wa pili ni yule asiyekusudia uongo na wala hawezi kukosea, kiasi ambacho habari yake haikhalifu matukio kwa hali yoyote. Haya ndiyo makusudio ya wasadikishaji katika Aya hii na ya Wenye mamlaka katika Aya 59 ya sura hii. Kwa hiyo inakuwa makusudio ya wenye mamlaka na wakweli ni Ahlul -bait.

Vilevile Sheikh Muhammad Abduh amesema: "Makusudio ya mashahidi hapa ni watu wa uadilifu na wanaochunga haki, ambao wanaitilia nguvu haki kwa kuitolea ushahidi kuwa wao ni watu wa haki na kuwatolea ushahidi wabatili- fu kuwa wao ni wabatilifu."

Hii ni kulifanyia taawili tamko lililo dhahiri bila dalili yoyote. Kwani inavyofa- hamika mashahidi ni wale waliouliwa katika njia ya Mwenyezi Mungu na haki. Ni kweli kuwa iko Hadith isemayo: Wino wa maulama ni kama damu za mashahid. Na kwamba mwenye kufa katika njia ya haki, basi amekufa shahid, au ana thawabu za shahid, lakini kufa shahid ni jambo jengine na kuwa katika daraja ya kufa shahid ni jambo jingine.

Ama watu wema ni wale ambao imekuwa njema itikadi yao na amali zao. Imam Ali (a.s.) amesema; "Kwa imani yanafahamika matendo mema na kwa matendo mema inafahamika imani." Hakuna mwenye shaka kwamba kujua halali ya Mwenyezi Mungu na haramu yake kwa kujitahidi au kwa kufuata ni sharti la msingi katika wema. Kwa sababu kutojua huharibu itikadi na amali.

Hiyo ni fadhila itokayo kwa Mwenyezi Mungu.

Ndio! Radhi ya Mwenyezi Mungu, na kuwa na urafiki na Mitume, wakweli, mashahidi na watu wema, ni kutengenekewa kwa kweli na ni fadhila za kudumu, sio hizi starehe ziondokazo.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا خُذُوا حِذْرَكُمْ فَانْفِرُوا ثُبَاتٍ أَوِ انْفِرُوا جَمِيعًا {71}

Enyi mlioamini! Shikeni hadhari yenu. Tokeni vikosi vikosi au tokeni nyote pamoja.

وَإِنَّ مِنْكُمْ لَمَنْ لَيُبَطِّئَنَّ فَإِنْ أَصَابَتْكُمْ مُصِيبَةٌ قَالَ قَدْ أَنْعَمَ اللَّهُ عَلَيَّ إِذْ لَمْ أَكُنْ مَعَهُمْ شَهِيدًا {72}

Na hakika katika nyinyi kuna ambaye hukaa nyuma, na ukiwapata msiba husema: Mwenyezi Mungu amenineemesha kwa kutokuwa nao.

وَلَئِنْ أَصَابَكُمْ فَضْلٌ مِنَ اللَّهِ لَيَقُولَنَّ كَأَنْ لَمْ تَكُنْ بَيْنَكُمْ وَبَيْنَهُ مَوَدَّةٌ يَا لَيْتَنِي كُنْتُ مَعَهُمْ فَأَفُوزَ فَوْزًا عَظِيمًا {73}

Na iwafikiapo fadhila itokayo kwa Mwenyezi Mungu, husema - kama kwamba, hapakuwa na mapenzi baina yenu na yeye - laiti ningelikuwa pamoja nao nikafanikiwa mafanikio makubwa