read

Aya 71 – 73: Chukueni Hadhari

Maana

Enyi mlioamini! Shikeni hadhari yenu

Aya hii ni miongoni mwa Aya za kuhimiza Jihad, zimetangulia Aya nyingi za namna hiyo na zijazo ni nyingi. Lakini Aya hii inawajibisha kutoka watu wote kwenye vita ikiwa iko haja. Umuhimu huu hasa unafahamisha maadui waliokuwa nao Waislamu wakiwapangia njama. Na waislam hawaachi kuwa na wahasimu wanaowafitini na dini yao. Mpaka leo uislamu na waislamu wanaandamwa na makafiri na mataghuti. Kwa hiyo ni kawaida kwa Mwenyezi

Mungu (s.w.t.) kuwahimiza waislam wawe na hadhari na kujua nguvu za uadui na maandalizi yake ya silaha.

Tokeni, vikosi vikosi au tokeni nyote pamoja.

Tokeni, ni amri ya kutoka kwenda vitani; na kutoka kwa vikosi, ni vikosi maalum vya askari; na nyote pamoja ni jeshi pamoja na wengine kulingana na hali inavyotakikana. Makusudio ni kujiandaa kumkabili adui kwa nguvu zote na kutumia kila njia kuipinga dhulma na uadui; hata kama kujikinga kutapelekea umma wote kushiriki katika vita. Wakubwa kwa wadogo na waume kwa wake. Allama Hilli anasema: "Lau kuna haja ya kutaka msaada kwa wanawake basi itakuwa ni wajibu."

Vita Vya Jana Na Leo.

Zamani vita vilikuwa vya wanaume tu na kuandaliwa na askari na vikosi. Ama leo, sayansi ndiyo imekuwa nguvu katika nyanja zote. Na panga na mishale zimebadilika kuwa mabomu, mizinga nyambiz i, vifaru na meli za kivita.

Vile vile silaha za sumu na mitandao ya upelelezi wa anga, bara na baharini1 kiasi ambacho hajui isipokuwa Mwenyezi Mungu na mabingwa katika elimu ya kuharibu na kuvunja.

Biashara ya vita haikutosheka na uvumbuzi wa elimu wa vifaa vya kuvunja na kuharibu, mpaka wameanzisha vyuo maalum vya elimu ya kuharibu na upangaji wa njama za mapinduzi, kuleta fitina na chuki na kuleta ghasia. Vilevile kupanga namna ya kueneza hofu na wasiwasi, kupuuza maadili na misimamo na kuamini mambo ya uzushi, na mengineyo yanayoandaa nguvu za kuwatawala wanyonge.

Hii ndiyo aina ya silaha anayotupiga nayo vita adui wa dini na wa ubinadamu. Basi tutajikinga naye vipi? Je, ni kwa matusi na shutuma? Au ni kuomboleza na kulia? Au ni kwa chuki.

Hakuna jengine kwa tulivyo hivi sasa ila kumjua ni nani adui yetu na uwezo wake ukoje, na tujihadhari naye na mbinu zake; wala tusimwamini na chochote. Vile vile tujifunze kutokana na makosa yetu, tujiepushe na wahaini na tufanye bidii mkono kwa mkono kwa nguvu zetu zote katika nyanja zote. Kwa namna hii ndipo tutaweza kusimama kumkabili adui; angalau hali isiwe kama tulivyo sasa.

Wavietnam waliweza kuwang'oa wamarekani pamoja na nguvu nyingi walizozikusanya na mabilioni ya madola waliyoyatoa. Kabla ya Vietnam, Cuba ilijikomboa kutoka makucha ya wamarekani ingawaje ndilo taifa kubwa ulimwenguni. Na hivijuzi Korea ya Kaskazini imeteka nyara meli ya kijasusi na wala Amerika haiwezi kuitikisa.

Siri ya hayo - kwa nionavyo - ni kwamba mataifa haya yalikuwa na mwamko na mipango na yalisahihisha makosa yake wakaikata mikono ya wahaini na kuwa- tenga na uongozi na sehemu muhimu. Pia mataifa hayo yaliamini haki yake na misingi yake na kupuuza maisha katika kuipigania.

Wala haiwezekani kwa nguvu za ulimwengu wote kutawala taifa lenye nidhamu na mwamko, liwe la kivietnam au la kiarabu. Tofauti iko katika hali sio asili na katika mwamko na uthabiti katika wanachokiamini na kukiitakidi.

Na hakika katika nyinyi kuna ambaye hukaa nyuma.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anaashiria kwenye kikosi cha siri ambacho kinajiingiza katika safu za watu wema kwa makusudio ya kuharibu na kurudisha nyuma mapambano na uadui.

Unaweza kuuliza kuwa neno, ‘katika nyinyi linaelekezwa kwa waumini, na wanafiki wako mbali zaidi na imani kuliko watu wengine. Sasa imekuwaje kuwafanya ni katika waumini?

Jibu: Kwa sababu wao wanahisabiwa kuwa ni katika waumini kidhahiri, na wanachukuliwa kuwa ni katika wao, sawa na mtu anayechukuwa uraia wa nchi akiwa ni kibaraka. Hawa wapo kila mahali na kila wakati.

Ukiwapata msiba husema: Mwenyezi Mungu amenineemesha kwa kutokuwa nao.

Hii ni kuizungumzia hali ya mnafiki ambaye alikuwa akifurahi wanaposhindwa waislam katika vita ambavyo yeye hakuhudhuria pamoja nao. Kila mwenye kufurahi kwa kusalimika na balaa iliyompata ndugu yake katika njia ya Mwenyezi Mungu na kupigania kuinua dini, basi huyo ni mnafiki.

Unaweza kuuliza kuwa kauli yake Mwenyezi Mungu, amenineemesha, ni kukiri kuweko Mwenyezi Mungu, sasa imewezekanaje kumfanya ni katika wanafiki?

Jibu: Yeye ameufanya unafiki kwa kudhihirisha uislamu na kumwamini Muhammad (s.a.w.) na kuficha kukanusha utume wake. Na hili halipingani na kumkubali Muumba.

Si kila anayemwamini Mungu anamwamini Muhammad (s.a.w.), Mwenyezi Mungu ameelezea kuwa kuna katika watu anayemwamini yeye Mwenyezi Mungu na wakati huo huo anamwamini mwingine, au atakayemkurubisha zaidi kwake. "Na wengi wao hawamwamini Mwenyezi Mungu isipokuwa wao ni washirikina." (12:106)

Na iwafikapo fadhila itokayo kwa Mwenyezi Mungu, husema - kama kwamba hapakuwa na mapenzii baina yenu na yeye - laiti ningelikuwa pamoja nao nikafanikiwa mafanikio makubwa.

Baada ya Mwenyezi Mungu kuelezea kuwa mnafiki hufurahi kwa kubaki kwake nyuma, kama waislamu wakishindwa, sasa anaeleza kuwa yeye anajuta kwa kuacha kujiunga nao wanapopata ushindi na ngawira.
Kimsingi ni kuwa ambaye mambo yake ni hayo, si mwislamu kitu, hata kama anadai kuwa ni mwislamu. Na kama angelidhihirisha mapenzi baina yake na waislam angeli- tambua kwamba heri yao ni heri yake na shari yao ni shari yake. Imekuwa mashuhuri Hadith kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.): "Hakika waislam ni kama viungo vya mwili mmoja, na ni kama jengo moja, sehemu moja inasaidia nyingine; na kwamba asiyejishughulisha na mambo ya waislam si katika wao."

فَلْيُقَاتِلْ فِي سَبِيلِ اللَّهِ الَّذِينَ يَشْرُونَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا بِالْآخِرَةِ ۚ وَمَنْ يُقَاتِلْ فِي سَبِيلِ اللَّهِ فَيُقْتَلْ أَوْ يَغْلِبْ فَسَوْفَ نُؤْتِيهِ أَجْرًا عَظِيمًا {74}

Na wapigane katika njia ya Mwenyezi Mungu ambao huuza maisha ya duniani kwa akhera, na mwenye kupigana katika njia ya Mwenyezi Mungu, akauawa au akashinda, tutampa ujira mkubwa.

وَمَا لَكُمْ لَا تُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللَّهِ وَالْمُسْتَضْعَفِينَ مِنَ الرِّجَالِ وَالنِّسَاءِ وَالْوِلْدَانِ الَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا أَخْرِجْنَا مِنْ هَٰذِهِ الْقَرْيَةِ الظَّالِمِ أَهْلُهَا وَاجْعَلْ لَنَا مِنْ لَدُنْكَ وَلِيًّا وَاجْعَلْ لَنَا مِنْ لَدُنْكَ نَصِيرًا {75}

Na mna nini hampigani katika njia ya Mwenyezi Mungu na ya wale wanaoonewa katika wanaume na wanawake na watoto ambao husema: Ewe Mola wetu! Tutoe katika mji huu ambao watu wake ni madhalimu, na tujaalie mlinzi kutoka kwako.

الَّذِينَ آمَنُوا يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللَّهِ ۖ وَالَّذِينَ كَفَرُوا يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ الطَّاغُوتِ فَقَاتِلُوا أَوْلِيَاءَ الشَّيْطَانِ ۖ إِنَّ كَيْدَ الشَّيْطَانِ كَانَ ضَعِيفًا {76}

Wale walioamini wanapigana katika njia ya Mwenyezi Mungu, na waliokufuru, wanapigana katika njia ya shetani. Basi piganeni na marafiki wa shetani; hakika hila za shetani ni dhaifu.
  • 1. Hivi sasa kuna setilaiti karibu 40 katika ardhi za kufanyia upelelezi. Marekani peke yake ina vyombo 30 vya angani na vituo elfu moja vya kufanyia ujasusi.