read

Aya 77: Zuieni Mikono Yenu Na Simamisheni Swala

Maana

Mwanzo wa kulingania Mtume (s.a.w.) kwa Mwenyezi Mungu, alilingania akiwa Makka. Wenye nguvu wakamzuia, wakihofia masilahi yao. Wakamwita mwenda wazimu, mchawi na mwongo. Lau si ami yake Abu Twalib kumhami, wangelimmaliza. Waliposhindwa naye, waliingilia kuwatesa wanaomwamini. Na Mtume alikuwa akiwaamuru kuwa wavumilivu na kuizuia mikono yao, kwa sababu ya wingi wa adui na uchache wa wasaidizi.

Maudhi na vikwazo vya washirikina vilipoziidi kwa waumini wanyonge, kikundi kimoja kilisema kumwambia Mtume (s.a.w.) "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu; tupe idhini ya kupigana na washirikina." Akasema: "Nimeamrishwa kufanya subira." Na Mtume alikuwa akiwapa matumaini sahaba zake ya kuenea waislam na kuondoka utawala dhalimu.

Baada ya kupita miaka 13 Makka tangu kuanza mlingano, Mtume alihama kwenda Madina na wakahama pamoja naye wanaojiweza katika waislamu, wakiwemo wale waliotaka idhini ya kupigana na washirikina wa Makka. Idadi ya waislam ilipoongezeka wakawa wanaweza kujilinda. Mwenyezi Mungu akawaamrisha kupigana Jihadi na washirikina ili kujikinga na shari yao.

Kwa sababu hekima yake Mwenyezi Mungu Mtukufu ilihukumia kupita mambo kwa desturi yake na sababu zake; na kutoenea dini yake ispokuwa kwa nyezo za kiubinadamu na kutolazimisha dini kwa nguvu za kiungu; kama inavyonyesha mvua na tufani.

Mambo yalipoiva wakaanza kuogopa wale waliokuwa na hamasa ya kupigana na washirikina walipokuwa Makka kabla hawajaruhusiwa vita. Hii ndiyo hali ya wanaopandwa na mori kwa hisia za mapenzi bila ya kufikiri na kuwaza, wanapandwa na mori na hamasa ya kupigana mpaka wanarukwa na akili; ambapo utekelezaji wake ni kujiua. Lakini inapofikia haja ya kupigana na kuwa ni lazi- ma, basi huanza kurudi nyuma kwa woga.

Si lazima watu wa namna hii wawe ni wanafiki au wasiokuwa na uhakika wa dini yao. Wanaweza kuwa ni katika wanyonge wanaohofia mauti na kuathirika na uhai kwa kuhofia kufa shahid katika njia ya haki.

Aya hii tuliyonayo imeonyesha kikundi cha waislamu waliokuwa na hamasa ya kupigana walipokuwa Makka kisha wakaogopa walipokuwa Madina. Tumetangulia kueleza utangulizi huo, kabla ya kuanza kufasiri Aya hii ili yawe wazi makusudio yake.

Je huwaoni wale ambao wameambiwa: Zuieni mikono yenu, na msi- mamishe Swala, na mtoe Zaka.

Makusudio ya, ‘wale ambao; ni ‘wale waliokuwa na haraka ya vita na hamasa walipokuwa Makka. Na kauli yake Mwenyezi Mungu "wameambiwa …" ni ishara ya kwamba Mtume aliwaamuru kufanya subira na kujizuia kupigana, na kufanya lile waliloamriwa ikiwemo kuswali na kutoa Zaka.

Walipolazimishwa kupigana, mara kundi moja katika wao wakawaogopa watu kama kumwogopa Mwenyezi Mungu au kwa hofu zaidi.

Yaani, zilipokamilika sababu za waislam kupigana baada ya kuhamia Madina, na kukawa na haja sana waliamrishwa kufanya hivyo, lakini wale waliokuwa na haraka walichukia kwa kupenda uhai na kuwa na woga wa kukabiliana na adui na kuogopa kuteseka.

Kusema kwake na wakawaogopa watu kama kumwogopa Mwenyezi Mungu au kwa hofu zaidi ni fumbo la kuwa hofu imefikia kikomo.

Na wakasema: Ewe Mola wetu! Kwa nini ukatufaradhia vita, usituahirishie muda kidogo.

Walitaka muda kwa kupenda sana anasa za dunia.

Na mwelekeo wao wa hili kwa kunyenyekea, unaonyesha kumwamini kwao Mungu. Ilivyo ni kuwa kuasi amri ya Mwenyezi Mungu kwa mauti, hakufahamishi kuwa ni ulahidi; kama ambavyo kuhiyari mauti kuliko kuwa dhalili hakufahamishi kumwamini Mungu.

Tumewaona walahidi wengi wakihiyari kufa kuliko kuishi na madhalimu; kama ambavyo tumewaona waislamu wengi wanajiingiza kwenye vifungo vya udhalili na utumwa, wao wenyewe na watu wao.

Waambie starehe ya duniani ni chache.

Makusudio ya uchache hapa ni kutodumu na kuondoka haraka. Na kila starehe za dunia zitakwisha zaidi ya kuwa zimechanganyika na wasiwasi na machukivu.

Na akhera ni bora kwa wenye kumcha Mungu.

Akhera ndio mwisho wa yote; uchache wa neema yake ni bora kuliko neema za dunia zote; kama ambavyo uchache wa adhabu yake ni mkubwa kuliko adhabu ya dunia yote. Mwenye akili ni yule ambaye anathamini kitukufu cha kudumu, hata kama kitakuja baadaye, kuliko kitu duni kinachokwisha ingawaje ni cha sasa hivi.

أَيْنَمَا تَكُونُوا يُدْرِكْكُمُ الْمَوْتُ وَلَوْ كُنْتُمْ فِي بُرُوجٍ مُشَيَّدَةٍ ۗ وَإِنْ تُصِبْهُمْ حَسَنَةٌ يَقُولُوا هَٰذِهِ مِنْ عِنْدِ اللَّهِ ۖ وَإِنْ تُصِبْهُمْ سَيِّئَةٌ يَقُولُوا هَٰذِهِ مِنْ عِنْدِكَ ۚ قُلْ كُلٌّ مِنْ عِنْدِ اللَّهِ ۖ فَمَالِ هَٰؤُلَاءِ الْقَوْمِ لَا يَكَادُونَ يَفْقَهُونَ حَدِيثًا {78}

Popote mtakapokuwa yatawafika mauti na hata mkiwa katika ngome madhubuti. Na likiwafikia zuri wao husema: Hili linatokana na Mwenyezi Mungu. Na likiwafika baya husema: Hili linatokana na wewe, Sema: Yote yanatoka kwa Mwenyezi Mungu. Basi wananini watu hao hata hawakaribii kufahamu maneno.

مَا أَصَابَكَ مِنْ حَسَنَةٍ فَمِنَ اللَّهِ ۖ وَمَا أَصَابَكَ مِنْ سَيِّئَةٍ فَمِنْ نَفْسِكَ ۚ وَأَرْسَلْنَاكَ لِلنَّاسِ رَسُولًا ۚ وَكَفَىٰ بِاللَّهِ شَهِيدًا {79}

Jema likufikalo linatokana na Mwenyezi Mungu na ovu likufikalo linatokana na wewe mwenyewe. Na tumekupeleka kwa watu kuwa ni mjumbe, na atosha Mwenyezi Mungu kuwa shahidi.