read

Aya 78 – 79: Popote Mtakapokuwa Yatawafika Mauti

Maana

Popote mtakapokuwa yatawafika mauti na hata mkiwa katika ngome madhubuti.

Umetangulia mfano wake wakati wa kufasiri 3: 145 kifungu 'Ajali imeandikwa.'

Likiwafikia zuri wao husema: Hili linatokana na Mwenyezi Mungu na likiwafika baya, husema hili linatokana na wewe.

Kila alionalo mtu ni zuri, husema ni zuri na kulifuatishia na neno ‘heri’ ambalo mtu hulipendelea na kulitamani. Na kila alionalo mtu ni baya, husema ni baya, na kuliufuatishia na neno ‘shari’ ambalo mtu hujiepusha nalo na kulikataa.

Kheri inaweza kuwa ya watu wote; kama vile rutuba na fanaka ambayo haimhusu mtu au kundi pekee. Na mara nyingine huwa inamhusu mtu; kama ufanisi wa mtu baina yake na familia yake. Vilevile shari inaweza kuwa ni ya kiujumla; kama vile ukame na ughali wa vitu; au kuwa ni ya mtu binafsi; kama vile kuwa mke mwovu na watoto wake.

Makusudio ya uzuri katika Aya hii ni heri ya kimaumbile ambayo inaenea kwa wote; kama vile mvua na mfano wake. Na ubaya ni shari inayoenea kwa wote; kama vile kahati na mengineyo. Kwa sababu washirikina walipokuwa wakipata neema; kama vile mvua, husema; Mwenyezi Mungu ametukirimu. Na wakipatwa na adhabu; kama vile kahati, husema: Hii imesababishwa na Muhammad; sawa na vile walivyokuwa wakisema wana wa Israil, ambao Mwenyezi Mungu amewaelezea kwa kusema: "Unapowafikia uzuri husema: Huu ni kwa ajili yetu. Na ukiwafikia ubaya humnasibishia ukorofi Musa …" (7:131)

Haiwezekani Kuongeza Zaidi Ya Ilivyo

Sema: Yote yanatoka kwa Mwenyezi Mungu.

Hili ni jibu la anayenasibisha wema kwa Mwenyezi Mungu na uovu kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu. Kwani kahati, mvua, matatemeko na madini vyote hivi na vinginevyo ni katika athari na mambo ya lazima kwa maumbile. Na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ndiye aliyeleta maumbile. Kwa hiyo heri ya maum- bile na shari yake inanasibishwa kwenye maumbile na kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kupitia kuleta kwake maumbile. Yeye, ambaye umetukuka utukufu wake, ndiye sababu ya sababu.

Unaweza kuuliza: Kwa nini Mwenyezi Mungu hakuyafanya maumbile bila ya shari, kwa namna ambayo heri itatakata na kila tatizo na waja wapate raha, wasiwe na tabu?

Swali hili au mushkeli huu umetolewa tangu maelefu ya miaka iliyopita. Zaradasht amejaribu kulitatua kwa kusema kuwa kuna waungu wawili Mungu wa heri (Mozad) na Mungu wa shari (Ahriman).

Wengine wamesema: Hakika Mwenyezi Mungu ameyaumba maumbile haya mkiwa ndani yake mna heri na shari, lakini wakati huo akaumba akili itakayolinganisha maumbile haya kwenye heri yake na utengenevu wake.

Ikiwemo huu ugunduzi ambao umefanya kitu cha mbali kiwe karibu, ukasahilisha jambo zito, yakatengenezwa mawingu ya mvua, na vimbunga vikajulikana kabla ya kutokea na mengineyo yasiyokuwa na idadi.

Amesema Abid Zahid: Hakuna budi na shari ili waasi waadhibiwe, lakini jibu hili linakanushwa na ushahidi uliopo na Qur'an. Kwa sababu desturi ya maumbile haimuhurumii muumin wala dhaifu na matetemeko ya ardhi hayamtengi mwema na mwovu.

Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema: Na iogopeni adhabu ambayo haitawasibu waliodhulumu nafsi zao katika nyinyi, peke yao. (8:25)
Kuna wengine waliosema: Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye na sisi hatujui kitu. Ashaira wamesema swali hili linarudishwa lilivyo. Kwa sababu vitendo vyake Mwenyezi Mungu Mtukufu, havisababishwi kwa malengo fulani. "haulizwi alifanyalo."

Katika kitab Asfar cha mwanachuoni mtukufu aliye mashuhuri kwa jina la Mulla Sadra kuna maelezo, kwa muhtasari: Ni jambo lisilowezekana kuweko ulimwengu usiokuwa na shari. Kwa sababu ulivyo ulimwengu wa kimaumbile kwa mujibu wa hali yake hulazimika kuweko na heri na shari, nguvu na udhai- fu na upole na ugumu. Vinginevyo isingewezekana kabisa kuweko ulimwen- gu; kama isivyowezekana kwa bingwa wa ujenzi kujenga ngome madhubuti kwa udongo tu.

Hilo ni kwamba ni muhali kuweko kitu bila kuweko na vitu vinavyopingana ambavyo daima vinakuwa katika mvutano na msukumano wa daima.

Katika hali hii ndipo yanapatikana maumbile kama vile vimbunga, joto, baridi, mvua, ukame na mengineyo ambayo athari zake za kimaumbile ni heri yake na shari yake. Katika hali hii ndipo mambo lazima yawe katika hali mbili tu. Ama kusiweko ulimwengu ama uweko ukiwa na heri yake na shari yake.

Hii ndio maana ya msemo mashuhuri: "Haiwezekani kuzidisha zaidi ya ilivyo," kama ambavyo inaafikiana kwa ukamilifu na kauli ya wanasayansi kuwa kati- ka kila maumbile kuna sehemu ya nguvu ya sawa na ya kutengua.

Kwa hivyo basi, inatubainikia kuwa kauli ya mwenye kusema; Kwa nini Mwenyezi Mungu hakuumba ulimwengu usiokuwa na shari, ni sawa na mwenye kusema: kwa nini Mwenyezi Mungu hakuumba moto usiokuwa na joto, theluji isiyokuwa na baridi, akili isiyokuwa na utambuzi, uhai usiokuwa na harakati au mauti yasiyokuwa na kutulia. Kwa maneno mengine swali hili linafanana na mtu aliyepagawa anayesema: Kwa nini kitu kikawa hicho hicho na hakikuwa kingine. Katika hali hii ndipo tunapata siri ya undani katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

Basi wana nini watu hao hata hawakaribii kufahamu maneno.

Kwa ufupi ni kuwa si Muhammad (s.a.w.) wala mwingineo mwenye athari yoyote, ya heri au ya shari katika maumbile. Iko riwaya mashuhuri kutoka kwa Mtume kwamba alisema wakati jua liliposhikwa, alipokufa mtoto wake Ibrahim: "Jua na mwezi ni alama katika alama za Mungu, zinakwenda kwa amri yake na kumtii yeye tu, hazishikwi kwa sababu ya kifo cha yeyote au uhai wa yeyote."

Jema likufikalo linatokana na Mwenyezi Mungu na ovu likufikalo lina- tokana na wewe mwenyewe.

Unaweza kuuliza: Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t.) katika Aya ya kwanza ameutegemeza ubaya na uzuri kwake Yeye tu, kwa kusema yote yatoka kwa Mwenyezi Mungu; na katika Aya ya hii ametegemeza mema kwake na mabaya kwa binadamu. Je kuna wajihi gani?

Jibu: Tumetanguliza kueleza katika Aya ya kwanza kwamba makusudio ya uzuri katika Aya ya kwanza ni heri ya maumbile na ubaya ni shari ya maum- bile, na kwamba yote mawili ni dhahiri ya maumbile ambayo ni katika uten- genezaji wa Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo ikasihi kuyanasibisha kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa mazingatio haya. Ama makusudio ya uzuri katika Aya ya pili ni kuokoka mtu katika maisha haya kidini na kidunia. Na makusudio ya uovu ni kutofanikiwa kidini na kidunia.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amekunasibisha kuokoka - katika kuangalia ibara ya wema - Kwake Yeye kwa kuangalia kuwa yeye amempa uzima na utambuzi na akaamrisha kufanya amali kwa ajili ya manufaa ya duniani na akhera. Kwa hiyo akifuata na kufanya amali akafikia kufaulu, hunasibishwa kwake Mwenyezi Mungu. Kwa sababu yeye ndiye aliyemwezesha na akampa ala za kufanyia kazi hiyo tena akamwamrisha. Ndipo Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: Jema likupatalo linatoka kwake.

Vilevile inawezekana kunasibisha kuokoka kwa mtu. Kwa sababu yeye ameacha uvivu na kupuuza akajitahidi na kufanya. Hakuna dalili katika Aya kwamba mtu hana athari kabisa katika kufaulu kwake. Ama kupuuza na kufanya uvivu na asifikie popote kwa sababu ya kupuuza kwake na uzembe, hakuwezi kunasibishwa kwa yeyote zaidi yake yeye mwenyewe.

Kwa sababu ni yeye aliyejiingiza kwa chaguo lake ovu la kupuuza. Kwa kuzingatia hivi ndipo Mwenyezi Mungu akasema: "Na ovu likufikalo linatoka kwako."

Wala haiwezekani kwa hali yoyote kutofaulu kwa mtu kunasibishwe na Mwenyezi Mungu. Kwani Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu, amemwamrisha mtu kufanya na kumhimiza baada ya kumpa zana zote zihitajikazo.

مَنْ يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللَّهَ ۖ وَمَنْ تَوَلَّىٰ فَمَا أَرْسَلْنَاكَ عَلَيْهِمْ حَفِيظًا {80}

Mwenye kumtii Mtume, basi amemtii Mwenyezi Mungu; na mwenye kukataa, basi hatukukupeleka kuwa mlinzi juu yao.

وَيَقُولُونَ طَاعَةٌ فَإِذَا بَرَزُوا مِنْ عِنْدِكَ بَيَّتَ طَائِفَةٌ مِنْهُمْ غَيْرَ الَّذِي تَقُولُ ۖ وَاللَّهُ يَكْتُبُ مَا يُبَيِّتُونَ ۖ فَأَعْرِضْ عَنْهُمْ وَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّهِ ۚ وَكَفَىٰ بِاللَّهِ وَكِيلًا {81}

Na wanasema: 'Tunatii' na wanapotoka kwako kundi moja katika wao huenda njama usiku kinyume cha yale wayasemayo. Na Mwenyezi Mungu anaziandika njama zao. Basi achana nao na mtegemee Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu atosha kuwa ni mwenye kutegemewa.

أَفَلَا يَتَدَبَّرُونَ الْقُرْآنَ ۚ وَلَوْ كَانَ مِنْ عِنْدِ غَيْرِ اللَّهِ لَوَجَدُوا فِيهِ اخْتِلَافًا كَثِيرًا {82}

Je, hawaizingatii Qur'an? Lau kama ingelitoka kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, wangelikuta ndani yake tofauti nyingi.