read

Aya 80 – 82: Hatukukupeleka Kuwa Mlinzi Juu Yao

Mwenye kumtii Mtume, basi amemtii Mwenyezi Mungu.

Imetangulia tafsir yake katika Aya 59 ya Sura hii.

Na mwenye kukataa, basi hatukukupelekea kuwa mlinzi juu yao.

Kazi ya Mtume inaelezwa na tamko la jina lenyewe; kama ambavyo tamko la jua linavyoelezea maana yake. Ama hisabu ya mateso, ni kazi ya Mwenyezi Mungu, si ya Mtume: Hakika ni kwetu sisi marejeo yao. Kisha ni juu yetu sisi hesabu yao (88: 25 - 28)

Tumezungumzia kwa ufafanuzi maudhui haya katika kufasiri (2:270)

Na wanasema: 'Tunatii' na wanapotoka kwako kundi moja katika wao huenda njama usiku kinyume cha yale wayasemayo. Na Mwenyezi Mungu anaziandika njama zao.

Dhahiri ya Aya inaonyesha kuwa waislamu kwa ujumla wao walidhihirisha utii kwa Mtume (s.a.w.), lakini wao si wote waliokuwa na ikhlasi katika waliyoyadhihirisha, Bali katika wao kulikuwa kuna kikundi kinachomhadaa Mtume na kula njama usiku kinyume na wanayoyadhihirisha. Aya hii ni jawabu tosha kwa wale wanaodai kuwa masahaba wote ni waadilifu na kwamba kusuhubiana na Mtume tu kunamfanya mtu awe msafi wa kila kitu.

Basi achana nao na mtegemee Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu atosha kuwa ni mwenye kutegemewa.

Msemo unaelekezwa kwa Mtume, ukiwa na maana kuwa hekima inapelekea kutowafichua makafiri na kuwataja majina yao. Watafichuka wenyewe. Mfano wa Aya hii ni kama Aya ya 63 ya Sura hii.

Mayahudi Na Muujiza Wa Qur'an

Je hawaizingatii Qur'an? Lau kama ingelitoka kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, wangelikuta ndani yake tofauti nyingi.

Katika kufasiri (2: 23-5) chini ya kifungu 'Siri ya muujiiza wa Qur'an; tumeonyesha siri hii kwa njia ya ujumla. Kwa sababu ufafanuzi utamaliza kitabu chenye ukubwa wa juzuu hii.

Baada ya kwisha kufasiri tumegundua siri za muujiza ambazo hawakuzinduka nazo wanavyuoni wa kiislam waliotangulia; hata wale waliotunga vitabu mah- sus katika muujiza wa Qur'an. Hiyo sio kama imetokana na uzembe, la!

Isipokuwa maajabu na siri za Kitabu cha Mwenyezi Mungu haziishi.

"Sema lau bahari ingelikuwa ni wino kwa (kuandika) maneno ya Mola wangu, bila shaka bahari ingelikwisha kabla ya kwisha maneno ya Mola wangu. Hata kama tungelileta (bahari) kama hiyo kuongezea." (18:109)

Na amesibu kutokana na matamko haya kila mmoja kwa kadiri unavyomsaidia wakati wake na kipawa chake. Kwa sababu zama ni kiungo muhimu katika kufichua maana ya Qur'an na siri zake. Ibn Abbas anasema: "Katika Qur'an kuna maana yatakayofasiriwa na wakati."

Miongoni mwa maana hayo ni yale yaliyoonyeshwa na Aya ya 53 ya sura hii: "Au wao wana fungu katika Ufalme? Basi hapo wasingewapa watu hata kitob- we cha kokwa ya tende."

Tumetaja katika kufasiri Aya 46 utabiri wa Qur'an kuhusu fedheha ya Mayahudi na madhambi yao, wakipata Ufalme. Baada ya karne kumi na tatu utabiri huu umethibitika. Hii ni dalili ya mkato ya utume wa Muhammad (s.a.w.) na ukweli wa ujumbe wake.

Huu ndio muujiza tulioukusudia kusema kuwa wanavyuoni na wafasiri hawakuzinduka nao. Kwa sababu Mayahudi wakati huo walikuwa wakitawaliwa, hawakuwa na chochote, si katika Palestina wala penginepo.

Katika jumla ya dalili za kuwa ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu: Ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Lau kama ingelitoka kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, wangelikuta ndani yake tofauti nyingi."

Miongoni mwa tofauti hizi ni kutokuwepo mpangilio na kunasibiana katika maneno ya watu ki mfumo na kifikra. Hakuna mwanachuoni mwanafasihi au mtu yeyote ila kutakuwepo na kutofautiana nguvu na udhaifu katika ibara zake na fikra zake. Ama Qur'an iko katika daraja moja katika ufasaha wa mpangilio wake na ukubwa wa maana zake.

Siri ya hilo ni kuwa binadamu ana hali na matatizo yanayotofautina na kubadi- lika kwa nyakati mbali mbali bali hata kwa kitambo kidogo tu. Na yeye binadamu anafuatana nazo, wala hawezi kuepukana na hilo kwa hali yoyote ile. Kusema kwake Mwenyezi Mungu, ‘Tofauti nyingi,’ ni ishara ya kuwa mageuzi ya binadamu kulingana na hali yake ni mengi sana yasiyo na idadi.

Tofauti hii inatufasiria tofauti katika mfumo wa binadamu na fikra yake.

Ama dhati takatifu ni moja katika kila kitu milele na milele, haibadiliki kwa hali wala kwa matatizo. "Vipi yatampita Mwenyezi Mungu yale aliyoyapitisha; na yamrudie yale aliyoyaanzisha; na yamzukie yale aliyoyazusha? Ingekuwa hivyo, basi dhati yake ingelitofautiana, na kuwa kwake kungegawanyika;" kama anavyosema Imam Ali (a.s.). Huyu ndiye anayetufasiria kufuatana na kunasibiana katika kitabu cha Mwenyezi Mungu, madhumuni na utendaji kazi wake, kuanzia Alifu mpaka Ye.

وَإِذَا جَاءَهُمْ أَمْرٌ مِنَ الْأَمْنِ أَوِ الْخَوْفِ أَذَاعُوا بِهِ ۖ وَلَوْ رَدُّوهُ إِلَى الرَّسُولِ وَإِلَىٰ أُولِي الْأَمْرِ مِنْهُمْ لَعَلِمَهُ الَّذِينَ يَسْتَنْبِطُونَهُ مِنْهُمْ ۗ وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ لَاتَّبَعْتُمُ الشَّيْطَانَ إِلَّا قَلِيلًا {83}

Ikiwajia habari ya amani au ya hofu huitangaza. Na lau wangeirejesha kwa Mtume na kwa wenye mamlaka katika wao, wangejua wale wenye kuchunguza katika wao. Na lau si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake mngemfuata shetani isipokuwa wachache tu.