read

Aya 83: Siri Ya Vita Na Kuvitangaza

Maana

Ikiwajia habari ya amani au ya hofu huitangaza.

Walikuwepo katika Masahaba wa Mtume - kama ilivyo katika kikundi au kikosi chochote - wakweli na wanafiki, mashujaa na waoga, wenye nguvu na wadhaifu katika imani, na wenye akili wanaoangalia mambo kulingana na matukio, na wajinga wasiozingatia mambo wala kupima mwisho wake. Qur'an imewaelezea hawa wote, mara nyingine kwa uwazi na mara nyingine kwa ishara.

Wafasiri wameafikiana kwamba Aya hii imeshuka juu ya wale waliokuwa wakisikiliza habari za amani au za hofu, ambazo zilikuwa zikufungamana na nguvu za askari wa kiislam, basi huzitangaza kwa watu. Kisha wafasiri wakatofautiana katika kuwaelezea hao watangazaji: Je, ni wanafiki au ni wale waumini wa juu juu wadhaifu? Kila kikundi kikasema kutokana na vile ilivyotiliwa nguvu kwao.

Ama sisi haikuwa na nguvu kwetu kauli ya kukusudia wanafiki wala wanyonge. Kwa sababu yote yanayofahamishwa na dhahiri ya Aya ni kuwa miongoni mwa jamaa waliokuwa karibu na Mtume (s.a.w.), wakifikiwa na habari ya amani au vita, huizungumzia na kuifuchua kwa watu.

Hakuna kitu kinachodhuru amani ya ndani na ya nje kuliko kufichua siri za kiaskari, hasa ikiwa watangazaji wenyewe wamepata habari juu juu.

Kwa sababu habari nyingi wanazitengeneza maadui na kuzisambaza kwa makusudio ya kufaidika nazo na kueneza fitina na hofu katika safu za waislamu.

Na lau wangeirejesha kwa Mtume na kwa wenye mamlaka katika wao, wangejua wale wenye kuchunguza katika wao.

Dhamiri ya 'wenye mamlaka katika wao' inawarudia waislam. Ama dhamiri ya 'wenye kupeleleza katika wao' wafasiri wametofautiana. Kuna mwenye kusema kuwa inarudia wale waliotangaza habari ya amani au vita. Wengine wakasema kuwa inawarudia wenye mamlaka.

Hilo ndilo lililo dhahiri. Makusudio ya wenye mamlaka ni wale ambao Mtume (s.a.w.) anaowaamini kwa ujuzi wao wa kidini na kielimu, na ambao Mwenyezi Mungu amewakusu- dia aliposema: "Yeya ndiye aliyekusaidia kwa nusura yake na kwa waumini." (8: 62)

Maana yake ni kuwa ingelikuwa bora kwa wale waliotangaza waliyoyasikia katika habari za vita kuacha kuziingilia habari zilizowafikia na wazielezee kwa Mtume na wenye ujuzi katika Masahaba wake, ni wao tu wanaojua habari za vita na mbinu zake na kuvitoa vitu kutoka katika machimbuko yake na kuvirudisha kwenye mashina yake.

Kwa hiyo kauli yake wangelijua wenye kuchunguza katika wao, maana yake ni kwamba wenye ujuzi wanajua hakika ya habari za kutangazwa na lengo lake. Kwa sababu wao ndio wanaofichua hakika kutoka katika chimbuko lake la kwanza na kufanya lile linalowajibisha hekima na masilahi.

Na lau si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake mngemfuata shetani isipokuwa wachache tu.

Makusudio ya fadhila za Mwenyezi Mungu na rehema yake ni kuteremshwa Qur'an na utume wa Muhammad (s.a.w.); na maana yake ni, lau si Kitabu cha Mwenyezi Mungu na sunna ya Mtume wake, mngelibaki juu ya ukafiri na upotevu isipokuwa wachache tu, katika nyinyi; Mfano Qas bin Saida, Waraqa bin Nawfal, Zaid bin Amr na wengine ambao walimwamini Mungu peke yake

kwa hisia safi za ndani kabla ya Mwenyezi Mungu kumtuma Muhammad (s.a.w.). Aina hii ya waumini wanaitwa Hanafiya. Na Hanif, kwa Waarabu, ni yule aliye katika dini ya Ibrahim (a.s.)

فَقَاتِلْ فِي سَبِيلِ اللَّهِ لَا تُكَلَّفُ إِلَّا نَفْسَكَ ۚ وَحَرِّضِ الْمُؤْمِنِينَ ۖ عَسَى اللَّهُ أَنْ يَكُفَّ بَأْسَ الَّذِينَ كَفَرُوا ۚ وَاللَّهُ أَشَدُّ بَأْسًا وَأَشَدُّ تَنْكِيلًا {84}

Basi pigana katika njia ya Mwenyezi Mungu; haikalifishwi ila nafsi yako tu. Na wahimize waumini. Huenda Mwenyezi Mungu akayazuia mashambulizi ya waliokufuru. Na Mwenyezi Mungu ni mkali zaidi wa kushambulia na mkali zaidi wa kuadhibu.