read

Aya 85 - 87: Kuunga Mkono Na Maamkuzi

Maana

Mwenye kuunga mkono jema hupata fungu katika hayo. Na mwenye kuunga mkono baya, hupata hisa katika hayo.

Mfumo wa maneno unafahamisha kuwa kuuunga mkono jema ni kuhimiza kupigana, na kuunga mkono baya ni kuvunja moyo wa kupigana. Kila mwenye kuhimiza na mwenye kuvunja moyo ana malipo ya kampeni yake na athari zake. Hilo ni katika kila kuunga mkono jambo la heri na kuunga mkono jambo la shari. Kuna Hadith isemayo: "Mwenye kuanzisha desturi nzuri atakuwa na malipo sawa na ya yule anayeifanya na mwenye kuanzisha desturi mbaya atakuwa na malipo sawa na ya yule anayeifanya."

Uislamu unapongeza kila tendo zuri, liwe litafuatwa na mwingine au limefany- wa na mlahidi au hata bila ya nia ya kitendo chenyewe. La muhimu ni kuwa liwe linaweza kuitwa heri, bora, jema, zuri au mfano wa hayo. Tumelielezea suala hilo katika kufasiri 3: 144 kifungu 'Kila mtu ana alilolinuia,' Pia katika 3: 178 kifungu 'Kafiri na amali ya heri.'

Na Mwenyezi Mungu ni mwenye uweza juu ya kila kitu.

Yaani ana uweza wa kutulipa kila mmoja anavyostahiki humpa thawabu mwenye kuunga mkono mema na kumwadhibu mwenye kuunga mkono maovu.

Na mnapoamkiwa kwa maamkuzi, basi itikieni kwa yaliyo bora kuliko hayo, au mrejeshe hayo hayo.

Uislamu umelifanya neno 'Tawhid' kuwa ni nembo ya itikadi yake; na umefanya Salaam kuwa ni maamkuzi yanayohusiana nao, kuonyesha kuwa mwelekeo wake katika maisha ni kueneza amani (salaam) na kuusimamisha uadui.

Kuongezea kuwa maana ya neno lenyewe Islam ni kuusalimisha uadilifu na wema na heri na amani. Zaidi ya hayo Salaam ni katika majina ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

"Yeye ndiye Mwenyezi Mungu hapana mola isipokuwa Yeye tu; Mfalme, Mtakatifu, Mwenye salama, Mtoaji wa amani, Mwenye kuyaendesha mwenyewe mambo yake, Mwenye nguvu, Jabbar, Mkubwa. Mwenyezi Mungu yuko mbali na hao wanaomshirikisha naye." (59:23)

Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kuhisabu kila jambo.

Ana hisabu kuacha kuitikia salaam na mengineyo katika kuacha haramu na kutenda mambo ya wajibu.

Mafakihi wametoa dalili kwa Aya hii kuhusu wajibu wa kuitikia salaam, ama kwa mfano huo huo, yaani kumrudishia salaam aliyekuamkia kwa herufi hizo hizo bila ya kuongeza au kupunguza; kwa mfano kuongeza: Wa rahmatullah nk. Kuitikia salaam ni 'wajib ainy' (wajibu wa mtu mwenyewe) kama ikielekezwa kwa mtu maalum.
Na 'wajibu kifaya', kama ikielekezwa kwa watu wengi; kwa maana kama baadhi wakiitikia, imetosheleza kwa waliosalia; vinginevyo wote watalaumiwa na kustahiki adhabu. Kuna Hadith isemayo: "Kuamkia ni Sunna na kuitikia ni wajib."

Wafuasi wa Abu Hanifa wamesema makusudio ya neno Tahiya’ katika Aya ni kukirimiwa kwa mali. Mwenye kukupa zawadi kitu, basi ni juu yako kumpa zawadi ya kiasi alichokupa au zaidi1

Njia Mbali Mbali Za Kuthibitsha Marejeo (Ufufuo)

Uislamu umeipa kipaumbile misingi ya mwanzo ya uislamu na kuithibitisha kwa mifumo mbali mbali. Misingi hiyo ni kumwamini Mungu, Mitume na Siku ya Mwisho.

Katika kitabu cha kwanza cha Tafsir Kashif, umewekea kila moja misingi hiyo mlango: Wa kwanza, tumeuzungumzia kwa anuani ya Tawhidi katika kufasiri 2: 21, wa pili, tumeuzungumzia kwa anuani ya 'Leteni Sura mfano wake' kati- ka kufasiri 2: 23, na wa tatu, tumeulezea kwa anuani ya 'vipi mnamkanusha Mwenyezi Mungu' katika kufasiri 2: 28. Mwenye kufuatilia Aya za Qur'an yenye hekima zinazoelezea ufufuo, atakuta aina nyingi, miongoni mwazo ni hizi zifuatazo:

1. Kutolea habari kutokea Kiyama: "Siku itabadilishwa ardhi hii kuwa ardhi nyingine na mbingu; nao watahudhuria mbele ya Mwenyezi Mungu mmoja, Mwenye nguvu." (14:48)

2. Kuelezea pamoja na kusisitiza kwa kiapo na kuondoa shaka; kama ilivyo katika Aya hii tuliyo nayo: “Kwa yakini atawakusanya siku ya Kiama, halina shaka hilo.”

3. Kutolea dalili uwezekano wa ufufuo kwa kuumbwa mbingu na ardhi: "Je, hawaoni kwamba Mwenyezi Mungu - aliyeziumba mbingu na ardhi na hakuchoka kwa kuziumba - Ana uwezo wa kuwafufua wafu? Ndio, hakika Yeye ni muweza wa kila kitu." (46:33)

4. Kutoa dalili kwa kuumbwa mimea: "Na Mwenyezi Mungu ndiye anayepeleka pepo ziyatimue mawingu na tukayafikisha kwenye nchi iliyokufa na kwayo tukaihuisha ardhi baada ya kufa kwake; kama hivyo ndivyo kufufuliwa." (35:9)

5. Kutoa dalili kwa kuumbwa kwa mara ya kwanza kwa binadamu: "… Hapo watasema: Ni nani atakayeturudisha? Sema: Ni yule aliye- waumba mara ya kwanza …" (17:51)

Kutoa dalili kwa ushahidi uliotokea. Miongoni mwa matukio hayo ni haya yafuatayo: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliwafisha jamaa katika wana wa Israel kisha akawafufua Qur'an yaeleza juu ya hilo

"Na mliposema: 'Ewe Musa! Hatutakuamini mpaka tumwone Mwenyezi Mungu waziwazi,' Yakawanyakuwa mauti ya ghafla na hali mwaona. Kisha tukawafufua baada ya kufa kwenu ili mpate kushukuru." (2: 55 - 56)

Mtu mmoja katika wana Israel alifufuliwa baada ya kuuliwa: "Tukasema: Mpigeni kwa baadhi yake (huyu ng'ombe), Ndivyo hivi Mwenyezi Mungu huwahuisha wafu; na anawaonyesha dalili zake ili mpate kufahamu." (2:73)

Vilevile Mwenyezi Mungu alimfufua Uzair baada ya kufa kwake: "… Mwenyezi Mungu akamfisha kwa miaka mia, kisha akamfufua …" (2: 259)

Pia Mwenyezi Mungu aliwafufua ndege wane wa Ibrahim baada ya kuwakatakata na kuwaweka mafungu : " kisha waite, watakujia mbio …" (2: 260)

Na aliwafufua watu wa pangoni baada ya kuwafisha miaka 309: " … Namna hii tuliwafufua ili waulizane baina yao …" (18: 19)

Amesema kweli Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na hakika tumewapigia watu mifano ya kila namna katika hii Qur'an ili wapate kukumbuka." (39:27)

Je, atakumbuka mjinga anayefahamishwa yule ambaye hashindwi na kitu chochote na yule asiyeweza kitu chochote? Vipi ataamini mnafiki siku watakayotukuzwa wakweli na kudhalilishwa wanafiki? Wala sijui ni madhara gani watakayopata jamii au watu kwa kuamini siku atakayopambanuliwa mwema na mwovu na mahakama watakayokuwa sawa watu wote mbele ya haki na uadilifu?

فَمَا لَكُمْ فِي الْمُنَافِقِينَ فِئَتَيْنِ وَاللَّهُ أَرْكَسَهُمْ بِمَا كَسَبُوا ۚ أَتُرِيدُونَ أَنْ تَهْدُوا مَنْ أَضَلَّ اللَّهُ ۖ وَمَنْ يُضْلِلِ اللَّهُ فَلَنْ تَجِدَ لَهُ سَبِيلًا {88}

Mna nini nyinyi mmekuwa makundi mawili katika (habari ya) wanafiki, na hali Mwenyezi Mungu amewageuza kwa yale waliyoyachuma? Je, mnataka kumwongoza ambaye Mwenyezi Mungu amemuacha kupotea? Na ambaye Mwenyezi Mungu amemuacha kupotea, hatampatia njia.

وَدُّوا لَوْ تَكْفُرُونَ كَمَا كَفَرُوا فَتَكُونُونَ سَوَاءً ۖ فَلَا تَتَّخِذُوا مِنْهُمْ أَوْلِيَاءَ حَتَّىٰ يُهَاجِرُوا فِي سَبِيلِ اللَّهِ ۚ فَإِنْ تَوَلَّوْا فَخُذُوهُمْ وَاقْتُلُوهُمْ حَيْثُ وَجَدْتُمُوهُمْ ۖ وَلَا تَتَّخِذُوا مِنْهُمْ وَلِيًّا وَلَا نَصِيرًا {89}

Wanapenda lau mngekufuru kama walivyokufuru wao mkawa sawasawa. Basi msifanye katika wao marafiki mpaka wahame katika njia ya Mwenyezi Mungu. Wakikataa wakamateni na muwaue popote muwakutapo, wala msifanye katika wao rafiki wala msaidizi.

إِلَّا الَّذِينَ يَصِلُونَ إِلَىٰ قَوْمٍ بَيْنَكُمْ وَبَيْنَهُمْ مِيثَاقٌ أَوْ جَاءُوكُمْ حَصِرَتْ صُدُورُهُمْ أَنْ يُقَاتِلُوكُمْ أَوْ يُقَاتِلُوا قَوْمَهُمْ ۚ وَلَوْ شَاءَ اللَّهُ لَسَلَّطَهُمْ عَلَيْكُمْ فَلَقَاتَلُوكُمْ ۚ فَإِنِ اعْتَزَلُوكُمْ فَلَمْ يُقَاتِلُوكُمْ وَأَلْقَوْا إِلَيْكُمُ السَّلَمَ فَمَا جَعَلَ اللَّهُ لَكُمْ عَلَيْهِمْ سَبِيلًا {90}

Ila wale waliofungamana na watu ambao baina yenu na wao mna ahadi, au wakawajia hali ya vifua vyao vina dhiki kupigana nanyi au kupigana na watu wao. Lau Mwenyezi Mungu angelitaka angewasaliti nao wakapigana nanyi. Watakapojitenga nanyi, wasipigane nanyi na wakawapa amani, basi Mwenyezi Mungu hakuwafanyia njia ya kupigana nao.
  • 1. Rudia Kitab Ahkamul Qur'an cha Qadhi Abu Bakr Al-andalusi