read

Aya 92-93: Kuua Kwa Kutokusudia Na Kukusudia

Maana

Wala haiwi kwa muumin kumwua muumin (mwenzake) ila kwa kukosea. Na mwenye kumwua muumin kwa kukosea, basi amwache huru mtumwa mwislamu na atoe diya kwa watu wake ila watakapoifanya sadaka.

Kuua kuko aina tatu:

1. Kukusudia: Ni kudhamiria mtu mwenye akili aliyebaleghe kumwua mwingine moja kwa moja; kama vile kuchinja na kunyonga. Au kwa kusababisha; kama vile kutia sumu kwenye chakula au kumzuilia mtu asile mpaka afe na njaa.

Ukithibiti usawa wa muuaji na muuliwa kidini na kiungwana, na wala muuaji asiwe ni baba wa muuliwa, hapo msimamizi wa aliyeuliwa atakuwa na hiyari ya kumuua kwa kulipiza kisasi au kuchukua fidia ikiwa muuaji atakubali kuitoa. Hiyari ya kulipiza kisasi na kuchukua fidia ni ya msimamizi (walii) katika kuua kwa makusudi. Akichagua fidia, basi muuaji anayo hiyari ya kutoa fidia au ajitolee kuuawa. Kwa hiyo msimamizi hawezi kumlazimisha muuaji kutoa fidia wala muuaji hawezi kumlazimisha msimamizi kuchuka fidia.

Fidia ya kisheria ni Dinar elfu moja ambazo ni sawa na 3.529 Kg za dhahabu.

2. Bila ya kukusudia: Ni kuwa muuaji amekusudia kitendo, lakini akakosea makusudio; kama kumpiga mototo kwa kumtia adabu akafa. Kuua kwa aina hii kunawajibisha fidia sio kisasi. Fidia yake ni Dinar elfu moja; kama fidia ya kukusudia. Tumezungumza kuhusu kuua kwa makusudi na shabihi - kusudio, katika kufasiri (2: 178 - 179)

3. Kukosea: Ni kuwa muuaji alikosea kitendo na makusudio; kama mwenye kupiga mshale mnyama ukampata mtu ukamuua. Hapo mtu siye aliyekusudiwa kufumwa wala kuuliwa. Haya ndiyo makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na mwenye kumwua mwislamu kwa kukosea, basi amwache huru mtumwa mwislamu na diya kwa watu wake ila watakapoifanya sadaka.”

Qur'an na Hadith kwa pamoja zimefahamisha kuwa mwenye kumuua mwislam kwa maksudi , basi ni wajibu kwake atoe kafara ya kumwacha huru mtumwa, kufunga miezi miwili yenye kufuatana na kuwalisha masikini sitini; atakusanya yote matatu. Hili ndilo linaloitwa kafara la kuchanganya.

Ikiwa kuua ni bila ya kukusudia au kukosea, basi atatoa kafara la kumwacha huru mtumwa; akishindwa afunge miezi miwili inayofuatana, akishindwa awal- ishe masikini sitini.

Fidia ya kuua kwa makosa mzigo wake utabebwa na walio baleghe wenye akili na walio na uwezo katika ndugu wa karibu wa upande wa baba; kama vile kaka, ami na watoto wao wanaume. Kiasi cha fidia ni 1000 Dinar. Fidia ni haki ya walii (wasimamizi) wa aliyeuliwa; wakipenda wataidai na wakitaka wataisamehe Ndipo Mwenyezi Mungu akasema, “ila wakiifanya sadaka.”

Mafakihi wanasema limewajibishwa kafara kwa mwenye kuua bila kukusidia ili kuwa ni onyo la uzembe na himizo la kuchukua tahadhari katika mambo yote. Imewajibishwa fidia kwa ndugu zake kwa kumuhurumia aliyekosea. Na kumewajibishwa kuchukuliwa kisasi kwa aliyeua makusdi, ili kumtia adabu kwa kukusudia haramu.

Na ikiwa ni mmoja wa watu walio maadui zenu, naye ni muumin, basi ni kuacha huru mtumwa muumin.

Makusudio ya watu walio maadui ni makafiri wenye vita na waislamu. Dhamiri ya 'naye' inarudia kwa aliyeuawa. Maana yake ni kuwa mwislamu akiua mtu kwa kuitakidi kwamba yeye ni kafiri, kisha ikabainika kuwa yeye ni mwislamu anayekaa kwa watu wake waliomakafiri, hapo hapatakuwa na chochote kwa muuaji zaidi ya kumwacha huru mtumwa; hakutakuwa na fidia. Kwa sababu watu wa aliyeuliwa ni makafiri, wakipewa fidia itawongezea nguvu kuwapiga vita waislamu.

Na ikiwa ni katika watu ambao baina yenu nyinyi na wao pana ahadi, basi ni diya kwa watu wake na kumwacha huru mtumwa muumin. Na ambaye hakupata basi ni kufunga miezi miwili yenye kufuatana.

Yaani ikiwa mwislamu aliyeuawa kimakosa anatokana na watu makafiri, lakini hawana vita na waislam kwa vile wana mkataba wa amani na waislamu, hapa itatolewa fidia kwa watu wake, hata kama ni makafiri, kwa sababu hukumu yao katika hali hii ni sawa na hukumu ya waislamu katika wajibu wa fidia.

Na ni juu ya muuaji kutoa kafara la kumwacha huru mtumwa, akishindwa afunge miezi miwli inayofuatana. Imewekwa sharia hii ya kafara kwa muuaji ili iwe ni toba kwa aliyoyafanya.

Na mwenye kumuua muumin kwa kukusudia, basi malipo yake ni Jahannam, ni mwenye kudumu humo; na Mwenyezi Mungu amemughadhibikia na amemlaani na amemwandalia adhabu kubwa.

Tumeeleza mwanzo wa maelezo namba (1) kuhusu hukmu ya aliyeua makusudi na kwamba yeye atauwawa ila akisamehe walii. Katika Aya hii Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anataja kwamba malipo yake huko akhera ni kukaa milele motoni, ghadhabu na laana ya Mwenyezi Mungu na adhabu kubwa.

Adhabu zote hizi nne ni kutilia mkazo. Makusudio ya ukubwa wa adhabu kutokana na kosa hili ni kuwa ni kosa kubwa la kutisha na kwamba ni katika madhambi makubwa ambayo hayana mfano wake zaidi ya ukafiri. Baadhi ya mafakihi wamesema: Ni udhihirisho zaidi wa ukafiri na maana yake.

Utakuja ufafanuzi wa kuua nafsi kwa dhulma 'Inshaallah' katika kufasiri (5: 32). Na yemetangulia maelezo ya kudumu motoni katika kufasiri (2, 257) kifungu cha 'kudumu motoni.'

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا ضَرَبْتُمْ فِي سَبِيلِ اللَّهِ فَتَبَيَّنُوا وَلَا تَقُولُوا لِمَنْ أَلْقَىٰ إِلَيْكُمُ السَّلَامَ لَسْتَ مُؤْمِنًا تَبْتَغُونَ عَرَضَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا فَعِنْدَ اللَّهِ مَغَانِمُ كَثِيرَةٌ ۚ كَذَٰلِكَ كُنْتُمْ مِنْ قَبْلُ فَمَنَّ اللَّهُ عَلَيْكُمْ فَتَبَيَّنُوا ۚ إِنَّ اللَّهَ كَانَ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرًا {94}

Enyi mlioamini! Mtakaposafiri katika njia ya Mwenyezi Mungu, basi hakikisheni wala msimwambie mwenye kuwapa Salaam: Wewe si mwislam. Mnataka mafao ya duniani na kwa Mwenyezi Mungu kuna ngawira nyingi! Hivi ndivyo mlivyokuwa nyinyi hapo mbeleni, na Mwenyezi Mungu akawafanyia hisani. Basi hakikisheni; hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa mnayoyatenda.