read

Aya 94: Kuudhihirisha Uislam Kunatosha Kuwa Ni Kuuthibitisha

Maana

Enyi mlioamini! Mtakaposafiri katika njia ya Mwenyezi Mungu, basi hakik- isheni, wala msimwambie mwenye kuwapa salamu: Wewe si mwislamu.

Wameafikiana wafasiri na wapokezi wa Hadith sababu iliyowajibisha kushuka Aya hii ni kuwa Mtume alituma kikosi katika Masahaba wakakutana na mtu mmoja mwenye mali; kama kondoo n.k. Wakamdhania ni kafiri; akatamka neno la kufahamisha uislamu wake, katika maamkuzi au tamko la shahada n.k. Baadhi wakaona hiyo ni kutaka kujiokoa na kifo, waka mwua.

Mtume alipolijua hili alihisi taabu na kumlaumu muuaji akasema: Hakika amehifadhika na kuuliwa kwa tamko hilo. Akamwambia - kama inavyoelezwa katika baadhi ya riwaya - "Huoni kuwa umeupiga mapande moyo wake!"

Matamshi ya Aya hayakatai maana haya. Kwani kauli yake, “mtakaposafiri katika njia ya Mwenyezi Mungu, basi thibitisheni.” Maana yake mtakapokwenda kwenye Jihadi pelelezeni; msikimbilie kumua ambaye mnamtilia shaka katika dini yake na uadui wake; wala msimwambie mwenye kuwapa salamu wewe si mwislamu. Kwa sababu kila mwenye kudhihirisha uislamu anayo haki waliyonayo waislam; hasa katika mambo ya kuhifadhi damu na mali ama bati- ni yake inajulikana kwa Mungu peke yake.

Mnataka mafao ya duniani na kwa Mwenyezi Mungu kuna ngawira nyingi!

Inafahamisha kuwa lililowapelekea kuua ni tamaa ya mali aliyokuwa nayo. Hilo ndilo lililowafanya wawaze kuwa kudhihirisha kwake tamko la uislamu kulikuwa na makusudio ya kuokoka. Ni mara nyingi sana mtu kufikiria yale yasiyo ya uhakika. Inakuwa hali ilivyo ni vingine, hata kama anajua ndivyo hivyo. Haya ndiyo maajabu ya mtu. kwa hali yoyote Mwenyezi Mungu amewatanabahisha makosa yao haya na kwamba wao wameharakia ngawira na ngawira za Mwenyezi Mungu na neema zake hazina idadi, ambazo atawabadilishia na mali ya aliyeuwa wa zaidi na zaidi.

Hivyo ndivyo mlivyokuwa nyinyi zamani.

Hili ni jibu lao na kukivunja kitendo chao kwa mantiki ya kiakili na ya hali halisi. Taarifa yake ni kuwa nyinyi hapo mwanzo mlikuwa washirikina, kisha mkaingia katika Uislam kwa tamko lile lile alilolitamka yule aliyeuliwa; na Mtume alilikubali kutoka kwenu. Kwa tamko hili zimehifadhiwa damu zenu na mali zenu. Kwa hiyo ilikuwa ni juu yenu kumkubalia yule mliyemuua kama vile Mtume alivyowakubalia nyinyi. Hivi ndivyo walivyo watu wengi, wanataka wengine waridhie uchache, lakini wao wenyewe hawaridhii.

Na Mwenyezi Mungu akawafanyia hisani

Kwa kuwakubalia uislam na kuwafanya ni katika Masahaba kwa kutamka tu tamko la shahada, wala Mtume hakuyachunguza yaliyo nyoyoni mwenu. Kwa nini hamkufanyia mwingine vile alivyowafanyia Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.)
Basi hakikisheni; hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa mnayoyatenda.

Yaani kuanzia sasa msifanye kitu mpaka muwe na uhakika nacho wala msimwadhibu yeyote kwa tuhuma au dhana. Hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa matukio yenu na ana hisabu kwa mnavyostahiki. Mafakihi wameiingiza Aya hii katika Aya za hukumu1 na wakatoa hukumu mbili za sharia.

1. Wajibu wa kuhakikisha katika kila kitu, hasa katika hukumu za kisharia na zaidi hasa katika damu na mali; ambapo wamewajibisha mafakihi katika mawili hayo kujichunga na kufanya ihtiyat na wakaongezea pia kuhusiana na tupu.

2. Kila mwenye kutamka tamko la uislamu na akasema mimi ni mwislamu, basi hukumu yake ni hukumu ya waislam katika ndoa urithi na mengineyo ambayo yanafungamana na mtu akidhihirisha uislamu tu. Sio kwa undani.

لَا يَسْتَوِي الْقَاعِدُونَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ غَيْرُ أُولِي الضَّرَرِ وَالْمُجَاهِدُونَ فِي سَبِيلِ اللَّهِ بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنْفُسِهِمْ ۚ فَضَّلَ اللَّهُ الْمُجَاهِدِينَ بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنْفُسِهِمْ عَلَى الْقَاعِدِينَ دَرَجَةً ۚ وَكُلًّا وَعَدَ اللَّهُ الْحُسْنَىٰ ۚ وَفَضَّلَ اللَّهُ الْمُجَاهِدِينَ عَلَى الْقَاعِدِينَ أَجْرًا عَظِيمًا {95}

Hawawi sawa waumini waliokaa - wasiokuwa wenye madhara - na wenye kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na nafsi zao. Amewatukuza Mwenyezi Mungu katika cheo wale wapiganao katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na nafsi zao kuliko waliokaa. Na wote Mwenyezi Mungu amewaahidi wema. Na amewatukuza Mwenyezi Mungu wenye kupigana Jihadi kwa malipo makubwa kuliko waliokaa.

دَرَجَاتٍ مِنْهُ وَمَغْفِرَةً وَرَحْمَةً ۚ وَكَانَ اللَّهُ غَفُورًا رَحِيمًا {96}

Ni vyeo kutoka kwake na maghufira na rehema. Na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.
  • 1. Kila Aya inayotolewa hukumu ya kisharia, basi ni katika Aya za hukumu: Kama vile Aya za Hijja, Saumu, ndoa , urithi na vyakula vya haramu. Ziko karibu Aya 500. Mafakihi wa Kishia na Kisunni wameziandikia vitabu maalum. Miongoni mwa vitabu vya Sunni ni Ayatul-Ahkamul cha Al-Jiswas. Na miongoni mwa vitabu vya Shia ni Kanzul Urfan fi Ayatil-Ahkam cha al-Miqdad.