read

Aya 95 - 96: Wenye Kupigana Jihad Na Wenye Kukaa

Hawawi sawa waumini waliokaa - wasiokuwa wenye madhara - na wenye kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na nafsi zao.

Mwenye kubaki nyuma asiende katika jihadi kwa udhuru wa kisheria; kama vile upofu, ulemavu na mengineyo, basi amesamehewa, bali atapata malipo mema akiwa ni muumin mwenye ihlasi anayependa ushindi wa dini, na heri ya watu wake; na anayependelea lau angalikuwa mzima akashiriki na wanaopigana jihadi.

Kuna Hadith isemayo: "Mtu yuko pamoja na anayempenda." Yaani, mwenye kumpenda mwenye kupigana jihadi si kwa chochote ila kwa kuwa yeye ni mwanajihadi, basi naye ana malipo ya wapigania jihadi; mwenye kumpenda

mkweli kwa sababu ya ukweli wake basi yeye yuko katika cheo chake; mwenye kumpenda dhalimu katika dhulma yake; basi yeye ni mshirika wake na mwenye kumpenda kafiri kwa ukafiri, basi ni kama yeye. Hii ndiyo hukumu ya wenye kukaa wasiokuwa na siha nzuri.

Ama wale wasiokuwa na udhuru katika wao wataangaliwa. Wakikaa bila ya kwenda kwenye jihadi ambayo wamewajibishiwa wao na wengineo; yaani kuwa vita ni vya wote. Hapo hawatasamehewa, bali watalaumiwa na ni wenye kustahili adhabu.
Kwa sababu wao wameasi, kwa hiyo haifai kuwalinganisha na wapiganaji kwa hali yoyote kwa sababu kulinganisha ni kushirikisha; na hawa hawakushirikiana na wapigana jihadi katika kitu chochote; hata kama ikiwa jihadi ni faradhi kifaya (ya kutosheana), isiyokuwa na haja ya kushiriki wote, lakini bado wapigana jihadi ni bora kuliko waliokaa. Kwa sababu wao wamechagua uvivu - kujiuzulu na vita. Hawa ndio waliokusudiwa na kauli yake Mwenyezi Mungu: "Hawawi sawa waumini waliokaa …"

Kwa hiyo maana yanakuwa ni hawawi sawa mbele ya Mwenyezi Mungu waliokaa, walio wazima na wale wapigania Jihadi ambao haikuwa jihadi ni wajibu kwao tu, bali ilikuwa wajibu kwa wote kwa njia ya kifaya, lakini wao ndio walioziba wajibu huu na wakautekeleza kwa ukamilifu na kuuondoa kwa waliobaki. Ni maana haya ambayo ameyakusudia Mwenyezi Mungu na kuyafafanua kwa kauli yake:

Amewatukuza Mwenyezi Mungu katika cheo, wale wapiganao katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na nafsi zao kuliko waliokaa.

Baada ya Mwenyezi Mungu kukanusha usawa baina yao na baina ya wale waliokaa anabainisha yale yaliyowapambanua wapigania Jihadi; ambayo ni ubora wao katika cheo kuliko waliokaa.

Kwa hiyo inakuwa kauli yake hii ni ufafanuzi baada ya kueleza kwa ujumla. Na siri ya kutukuzwa ni kama tulivyoeleza, kuchukua majukumu ya ulinzi peke yao; sawa na lau adui anashambulia mji, kukatokea kikundi kuwazuiwa kinyume cha kikundi kingine, hapo kimsingi kikundi cha kwanza kitatofautika na kikundi cha pili.

Ingawaje kikundi cha pili hakitaadhibiwa baada ya cha kwanza kusimamia wajibu na kupatikana lengo lililotakikana. Kwa hiyo ndio Mwenyezi Mungu akasema:

Na wote Mwenyezi Mungu amewaahidi wema.

Lakini tena akarudia kutilia mkazo na kuhimiza Jihadi kwa kusema:

Na amewatukuza Mwenyezi Mungu wenye kupigana Jihadi kwa malipo makubwa kuliko waliokaa.

Na akabainisha malipo haya makubwa kuwa Ni vyeo kutoka kwake na maghufira na rehema. Cheo kimoja tu kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni bora kuliko ulimwengu na vilivyomo ndani yake, je itakuwaje vyeo vingi! Ama rehe- ma yake, hakuna kitu bora zaidi kuliko hiyo ila ambaye imetokana naye. Na inatosha kwa maghufira yake kuwa ni kusalimika na adhabu yake na machukivu yake.

Haya ndiyo maghufira, rehema na cheo kwa Mwenyezi Mungu. Mwenye kupa- ta moja tu, atakuwa katika walio juu, sikwambii atakayeyapata yote!

"Ewe Mola wangu! Hakika mimi nakuomba wepesi katika rehema yako na maghufira yako; na wewe wajua kuwa mimi naihitajia. Kwani itakuwaje kama utanineemesha na kunikwasisha? Kwani unahofia maghufira yako yatakwisha na hazina ya rehema yako (itakwisha)? Au ni nini ewe Mola wangu! Au ni kwa kuwa mimi nina dhambi? Ndio, lakini hujui kwamba mimi najua kuwa hakuna kimbilio ila kwako tu na kwamba kunanifurahisha mimi kunisamehe! Ewe Mola wangu! Ikiwa mimi ni muongo kwa niliyosema, basi nifanyie vile ninavyostahiki, na ikiwa ni mkweli kwa niliyoyasema, basi fanya vile unavyostahiki."

Ali Na Abu Bakr

Amesema Razi (ninamnukuu): "Wamesema Shia kuwa Aya hii: Amewatukuza Mwenyezi Mungu wenye kupigana Jihadi kwa malipo makubwa kuliko wenye kukaa. Inafahamisha kuwa Ali bin Abu Twalib ni bora kuliko Abu Bakr.

Kwa vile Ali alipigana Jihadi zaidi ya Abu Bakr…" Kipimo cha utofauti ni kuwa Ali alikuwa ni katika waliopigana Jihadi katika alivyomzidi Abu Bakr, na Abu Bakr alikuwa katika waliokaa. Ikiwa hivyo basi imewajibika kuwa Ali (a.s.) ni bora kuliko Abu Bakr."
Kisha Razi akawajibu Shia kwa kusema: "Tunawaambia: Kuua kwa Ali makafiri kulitokana na Mtume, kwa hiyo itawalazimu kwa hukumu yenu hii ya Aya, kuwa Ali ni bora kuliko Muhammad (s.a.w.). Na haya hayasemwi na mwenye akili. Kama mkisema: Kupigana Jihadi kwa Mtume pamoja na Makafiri ni kukubwa zaidi kuliko kwa Ali, kwa sababu Mtume alikuwa akipigana kutokana na dalili na ubainifu, kuondoa shubha na upotevu, na kwamba jihadi hii ni kamilifu zaidi kuliko hiyo. Basi tunasema: Na sisi tukubalieni kuhusu Abu Bakr kama mfano wake."

Huku ni ni kulala kabisa kwa mwanafalsafa wa wafasiri na wala siwezi kukuita kusinzia. Kwa sababu hizi zifuatazo:-

Kwanza: kila mwenye kumlinganisha Muhammad (swa) na mmoja wa maswahaba zake, katika kuleta dalili na ubainifu, basi atakuwa ametoka katika uislamu, atake asitake. Kwa sababu Muhammad anatoa ubainifu kwa wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu-kama tutakavyoelezana maswahaba wanatoa kutokana na mafunzo yake. Kwa hiyo basi cheo cha kwanza ni cha Mwenyezi Mungu peke yake hana mshirika, cha pili ni cha Muhammad peke yake hana mwenzake na kuwamini wote wawili kuko daraja moja. Kwa vile kumwamina Mungu na mitume yake ni nguzo moja katika nguzo zinazousimamisha uislam, haitoshi moja peke yake. Ukhalifa na uswahaba ni matawi ya kumwamini Mungu na Mitume, na tawi haliwezi kufananishwa na shina.

Pili: Maana yaliyo wazi ya neno wenye kupigana Jihadi katika Aya, ni Jihadi kwa upanga, si kwa kingine kwa kukiri Razi katika tafsiri yake. Lakini yeye ameghafilika na aliyoyasema na akajipinga mwenyewe. Hebu tuiache dhahiri ya Aya na tafsiri zote, tumrudie yule ambaye Qur'an imeteremshwa kwenye moyo wake na tumwulize, ni yupi mbora wa watu? Tumsikilize atajibu nini.

Amepokea Muslim katika sahih yake, kwamba mtu mmoja alimwuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.). "Ni nani mbora wa watu?" Akasema: "Ni mtu anayepigana Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa nafsi yake na mali yake."

Sote tunajua kuwa Ali alipigana zaidi Jihadi; kama alivyosema Razi, kwa hivyo anakuwa mbora wa watu, isipokuwa Mtume (s.a.w.); ambapo hakuna chochote zaidi ya daraja ya utume ila Uungu - kama tulivyobainisha - Na kila mmoja anajua kwa uwazi kwamba Jihadi kwa nafsi ni bora na kubwa kuliko Jihadi kwa mali. Kwa sababu mali hutolewa katika njia ya Jihadi kwa nafsi, lakini nafsi haitolewi katika njia ya mali.

Tatu: Hakika Mtume Mtukufu (s.a.w.) - kama tulivyotangulia kueleza - hakutoa dalili na hakubainisha,wala hakuondoa utatanishi yeye mwenyewe; bali yote yanatoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alikuwa akimwelezea Muhammad (s.a.w.) naye akifikisha kwa kunukuu kwa herufi. Muhammad anaambiwa.

"Sema: Ataihuisha yule aliyeiumba mara ya kwanza …" (36:79) "Sema: Je, yuko katika washirika wenu aongozaye katika haki?" (10: 35) "Sema: Hebu leteni Sura moja mfano wake na muwaite muwezao asiyekuwa Mwenyezi Mungu mkiwa mnasema kweli." (10: 38) "Sema: Je, mnawafanya wengine badala yake kuwa ni walinzi na hawajifai wenyewe kwa nafuu wala dhara" (13: 16)

Na Aya nyingine kadha. Jambo la ajabu ni kuwa Razi ameghafilika nazo baada ya kurefusha ufafanuzi na tafsiri zake. Ajabu ya maajabu ni pale aliposema: "Basi na sisi tukubalieni kuhusu Abu Bakr kama mfano wake;" yaani kama mlivyomkubalia Muhammad.

Hapana! tena hapana mara elfu! Si sisi wala mwislam yeyote atakayekukubalia wewe au mwengine kuwa Abu Bakr awe na mfano wa aliyo nayo Muhammad (s.a.w.) (katika kuleta dalili, hoja na kuondoa utatanishi na upotevu. Ila ikiwa Abu Bakr ni Mtume anayeteremshi- wa Wahyi.

Zaidi ya haya cheo cha Ali katika elimu hakikurubiwi na yeyote katika Masahaba. Inatosha kuwa ni ushahidi wa hilo. Hadith mutawatir iliyopokewa kutoka kwa Mtume inayosema: "Mimi ni jiji la elimu na Ali ni mlango wake." Zimehifadhiwa turathi za kiislam kutokana na elimu ya Ali, kiasi ambacho hakikuhifadhiwa kutoka kwa Abu Bakr wala Sahaba mwengineo.

إِنَّ الَّذِينَ تَوَفَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ ظَالِمِي أَنْفُسِهِمْ قَالُوا فِيمَ كُنْتُمْ ۖ قَالُوا كُنَّا مُسْتَضْعَفِينَ فِي الْأَرْضِ ۚ قَالُوا أَلَمْ تَكُنْ أَرْضُ اللَّهِ وَاسِعَةً فَتُهَاجِرُوا فِيهَا ۚ فَأُولَٰئِكَ مَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا {97}

Hakika wale ambao Malaika wamewafisha hali ya kuwa wamezidhulumu nafsi zao, wataambiwa: Mlikuwa katika hali gani? Watasema: Tulikuwa wanyonge katika ardhi. wataambiwa: Kwani ardhi ya Mwenyezi Mungu haikuwa pana mkahamia humo? Basi hao makazi yao ni Jahannam; nayo ni marejeo mabaya.

إِلَّا الْمُسْتَضْعَفِينَ مِنَ الرِّجَالِ وَالنِّسَاءِ وَالْوِلْدَانِ لَا يَسْتَطِيعُونَ حِيلَةً وَلَا يَهْتَدُونَ سَبِيلًا {98}

Isipokuwa wale wanyonge katika wanaume na wanawake na watoto (ambao) hawawezi kufanya hila yoyote wala kufuata njia.

فَأُولَٰئِكَ عَسَى اللَّهُ أَنْ يَعْفُوَ عَنْهُمْ ۚ وَكَانَ اللَّهُ عَفُوًّا غَفُورًا {99}

Basi hao huenda Mwenyezi Mungu akawasamehe; na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwingi wa maghufira.

وَمَنْ يُهَاجِرْ فِي سَبِيلِ اللَّهِ يَجِدْ فِي الْأَرْضِ مُرَاغَمًا كَثِيرًا وَسَعَةً ۚ وَمَنْ يَخْرُجْ مِنْ بَيْتِهِ مُهَاجِرًا إِلَى اللَّهِ وَرَسُولِهِ ثُمَّ يُدْرِكْهُ الْمَوْتُ فَقَدْ وَقَعَ أَجْرُهُ عَلَى اللَّهِ ۗ وَكَانَ اللَّهُ غَفُورًا رَحِيمًا {100}

Na mwenye kuhama katika njia ya Mwenyezi Mungu atapata katika ardhi mahali pengi pa kukikimbilia na wasaa. Na mwenye kutoka nyumbani kwake ili kuhamia kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kisha yakamfika mauti, basi yamethibiti malipo yake kwa Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.