read

Aya 97 – 100: Ardhi Ya Mwenyezi Mungu Ni Pana

Maana

Waislamu zama za Mtume (s.a.w.) walikuwa na Hijra mbili kutoka Makka. Ya kwanza ilikuwa ni ile ya kuelekea Uhabeshi (Ethopia), na ilikuwa miaka mitano tangu Mtume kuutangaza utume wake. Ya pili ilikuwa ile ya kuelekea Madina iliyokuwa miaka minane baadaye.

Wako Masahaba ambao walifanya Hijra mbili kama Jafar bin Abu Twalib ambaye maisha yake yaliishia kwa kufa shahid baada ya kukatwa mikono yake. Mwenyezi Mungu akamkirimu kutokana na mikono hiyo mbawa mbili atakazoruka nazo katika pepo; na ndio akatiwa 'Attwayyar' (Mrukaji).

Ama sababu ya Hijra (kuhama) ni kujiepusha na kuingia katika maangamivu, kukimbilia mahali pa amani kupanga mipango ya Jihadi na kuipinga batili. Kwa kutokana na Hijra (kuhama) na fadhila zake, uislamu umeshinda maadui zake. Lau si hiyo ungelizimika mwenge wake na kugeuka jivu linalopeperuka. Kwa ajili hii Hijra ikawa wakati huo ni fadhila kubwa na ni kitendo cha fahari cha kwanza ambacho hakikurubiwi na kitu chochote.

Mtume (s.a.w.) alihama kutoka Makka kwenda Madina na akawaamrisha waislamu wahamie huko. Wengi wakamwitikia na wengine wakabaki kwa kung'ang'ania mali zao na masilahi yao. Kwa sababu washirikina walikuwa hawamwachi mwenye kuhama kuchukua chochote katika mali yake.

Washirikina walikuwa wakimwudhi sana anayebaki hapo na kumzuilia na dini yake, akiwa hawezi kujitetea. Lakini alikuwa anaweza kujiepusha na vikwazo hivyo na kuisimamisha dini kwa njia za ukamilifu, kwa kuhama kutoka katika mji ulio na vita na waislam kwenda mji wa uislamu na amani (Madina) aliko Mtume na Sahaba. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu aliwatahayariza wale walioona kuwa ni heri kubaki katika nyumba ya ukafiri na kuipiga vita dini na watu wake. Aliwatahayariza na akawazindua kupitia Malaika kwa kusema:

Hakika wale ambao Malaika wamewafisha hali ya kuwa wamezidhulumu nafsi zao.

Kwa kuacha Jihadi na kuhama kwenda kwenye mji wa kiislamu, wakaridhia kubaki katika nyumba ya ukafiri, udhalili na kuharibu wajibu wa dini, Wataambiwa; mlikuwa katka hali gani? Yaani Malaika wa mauti watawaambia wale walioacha kuhama; mlikuwa vipi? Hili hasa si swali, isipokuwa ni lawama na kusutwa. Ilivyo hasa ni kuwa lawama zinakuwa kwenye tukio maalum, ambalo hapa ni kule kukaa kwao nyuma ya ndugu zao wahamiaji ambao wamemtii Mtume katika kutekeleza mipango ya kuumaliza ushirikina na kuliinua neno la Mungu.

Akiuliza muulizaji; Je, makaripio haya na masuto kutoka kwa Malaika kwa wale waliorudi nyuma yalikuwa wakati wa kukata roho au ni baada yake?

Tutajibu kuwa ujuzi wa haya uko kwa Mola; yeye amelinyamazia hilo. Kwa hiyo na sisi tunalinyamazia vilevile. Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) anasema: "Hakika Mwenyezi Mungu amenyamazia mambo si kwa kusahau, basi msijikalifishe nayo."

Watasema: Tulikuwa ni wanyonge katika ardhi.

Huu ni udhuru na kutafuta sababu kwa waliorudi nyuma. Maana yake ni kuwa waliorudi nyuma wanawajibu Malaika wanaowalaumu kwa uzembe wao katika mambo ya dini. Wanawajibu kwa kusema: Tulikuwa tumeshindwa,tunaonewa katika mji wa makafiri, kusimamia wajibu wa kidini.

Kwa sababu washirikina walitukandamiza na kutuzuia kufanya tuliyokuwa tukiitakidi, Malaika wakajibu udhuru huu. Watasema: - Kwa kuwasuta - Kwani ardhi ya Mwenyezi Mungu haikuwa pana mkahamia humo? Yaani mlikuwa mnaweza kuhamia mji wa kiislamu ambako mtaepukana na udhalili na kuweza kuitekeleza dini kwa uhuru; kama walivyofanya waislamu wengine.

Kama kuna kitu kinachofahamisha zaidi kuhusu malumbano haya, basi ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hamwadhibu yeyote ila baada ya kukamilisha hoja, bali ila baada ya kurundikana hoja kwake; kiasi ambacho kinamwacha mwenye dhambi asiwe na kimbilio ila msamaha wake Mwenyezi Mungu (s.w.t.) na rehema yake ambayo imeenea katika kila kitu, "… Ewe Mola wangu na mimi ni kitu zinienee rehema zako."

Basi hao - yaani waliorudi nyuma - makazi yao ni Jahannam, na ni marejeo mabaya. Isipokuwa wale wanyonge katika wanaume na wanawake na watoto (ambao) hawawezi kufanya hila yoyote wala hawawezi kufuata njia.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuwakemea waliorudi nyuma, aliwavua walio na udhuru kwa ugonjwa au kukosa posho na akawaondolea takilifa ya Hijra. Kwa sababu Mwenyezi Mungu hakalifishi ila uweza wake.

Unaweza kuuliza kuwa kutolewa wanaume na wanawake wenye udhuru kuna mwelekeo maalum. Sasa kuna mwelekeo gani wa kutolewa watoto na inaju- likana kuwa watoto hawakalifiwi na kitu?

Swali hili limejibiwa kuwa maana ya neno Wildan ni watumwa na wajakazi. Ama sisi tunajibu kuwa watoto wengine wanaweza kuhama hasa vijana wado- go, bali baadhi yao wana uwezo zaidi ya watu wakubwa. Kwa ajili hii mtu anaweza akadhania kuwa kuhama ni wajibu kwa kila anayeweza. Hivyo Mwenyezi Mungu ameiondoa dhana hiyo na kubainisha kuwa Hijra ni wajibu kwa kila mwenye uweza ila akiwa ni katika watoto.

Mafakihi Na Wajibu Wa Hijra

Mafakihi wameitolea dalili Aya hii kwamba mwislamu haijuzu kwake kukaa kwenye mji wa ukafiri ikiwa hawezi kuitekeleza dini, hata kama ni mji wake akiwa na milki na masilahi. Lakini hukumu hii siku hizi haina maudhui. Kwa sababu kila mtu katika kila mji anaweza kumwabudu Mwenyezi Mungu kwa namna yoyote atakayo. Akiacha, basi yeye peke yake ndiye mwenye jukumu.

Unaweza kuuliza: Mtu akijua kuwa kukaa kwake katika mji usiokuwa wa kiis;amu kunasababisha kuacha faradhi, si kwa kuwa mtu anamzuia, bali kwa udhaifu wa kukabiliana na msukumo; kama vile mchezo n.k. Je, inafaa kukaa katika mji huu?

Jibu: Akijua kwa yakini kwamba kwenda mahali popote, pawe ni mjini, kikao au sokoni ambako lazima kutamfanya aache wajibu au kufanya haram basi ni wajibu kwake kuepukana nako.

Kwani sababu inayolazimu uharamu basi ni haramu. Mwenyezi Mungu anasema: "… Basi baada ya kukumbuka usikae pamoja na watu madhalimu." (6: 68)

Amirul Mumin (a.s.) anasema: "Hijra (kuhama) bado iko kwenye mipaka yake ya kwanza." Yaani, bado ipo hukumu yake ya wajibu kwa yule ambaye imekuwa uzito kutekeleza hukumu za dini yake ila katika mji wa waislamu.

Ama kauli ya Mtume (s.a.w.): “Hapana Hijra (kuhama) baada ya kutekwa Makka," makusudio yake ni kuhama kutoka Makka. Hilo linafahamishwa na neno kutekwa Makka.

Na mwenye kuhama katika njia ya Mwenyezi Mungu atapata katika ardhi mahali pengi pa kukimbilia na wasaa.

Riziki haziko nyumbani tu na kuhama hakuwajibishi kukosa. Miji ya Mwenyezi Mungu ni mingi, riziki yake ni pana na neema katika kila mji hazihisabiki, na kwamba mafukara wengi wamejikusanyia mali kule walikohamia kiasi amba- cho walikuwa hawaoti kupata hata sehemu ndogo tu walipokuwa nyumbani kwao.

Lau wale waliorudi nyuma wangelihama, wangelipata riziki na utukufu kiasi cha kuwadhalilisha washirikina waliowapa aina kwa aina za udhalili na vikwazo.

Lakini waliorudi nyuma walilikataa hilo, wakachukua udhalili na utwevu kutoka kwa maadui wa dini yao, si kwa lolote ila ni kuwa shetani aliwatisha na ufukara iwapo watahama wakategemea vitisho vyake na wakaathirika kuacha maghufira ya Mwenyezi Mungu: "Shetani anawatisha na ufukara na anawaamrisha ubakhili; na Mwenyezi Mungu anawaahidi msamaha utokao kwake na fadhila na Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu, Mjuzi" (2: 268).

Na mwenye kutoka nyumbani kwake ili kuhamia kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kisha yakamfikia mauti, basi yamethibiti malipo yake kwa Mwenyezi Mungu.

Kila mwenye kukusudia kwa kujitahidi na kufanya ikhlasi kwa amali yoyote katika amali za twaa kisha akashindwa, basi Mwenyezi Mungu (s.w.t.) humwandikia thawabu kamili kwa fadhila na ukarimu kutoka kwake Mwenyezi Mungu. Tumelifafanua hilo katika kufasiri Aya (3: 144) kifungu, “kila mtu ana alilonuia.”

Imepokewa kuwa Jundub bin Dhumra, aliposikia Aya ya Hijra aliwaambia wanawe; "Wallahi silali Makka mpaka nitoke, kwa sababu ninahofia kufa Makka;" naye alikuwa mgonjwa sana, wakatoka nae wakimchukua kitandani. Alipofika mahali panapoitwa Tan'im akafariki. Ndipo ikashuka Aya hii.

Baina Ya Kuhama Mtume Kutoka Mji Mtukufu Wa Makka Na Kuhama Wapalestina Kutoka Ardhi Takatifu.

Katika maajabu ya sadfa ni kuafikiana - bila ya kukusudia - kufikia kwangu kufasiri Qur'an kwenye Aya ya Hijra mwanzo wa mwaka 1388 A.H. na Israel inakalia ardhi yetu takatifu, watu wetu wanahama wakikimbia mateso na mauaji waliyoyafanya waisrael na wanayoendelea kuyafanya.

Sadfa hii imenifanya nilinganishe tukio la uchokozi wa washirikina katika Makka kwa waislamu na kutolewa kwao mijini mwao, na tukio la uchokozi wa waisrael; au kwa usahihi zaidi uchokozi wa kikoloni kwenye ardhi takatifu na kuwatoa wenyeji mijini mwao.
Kisha nikatoka kwenye mlinganisho huu kufikia Ibra na mazingatio kutokana na jihadi ya Mtume (s.a.w.) na waislamu katika kuhama kwao na kupanga mipango iliyowapeleka waislamu kwenye kilele cha ushindi kwa maadui zao, kuuvunja utaghuti na uchokozi wake na kuwasimamisha mamwinyi wa kiquraish, waliowatoa Makka mbele ya Mtume wakiwa madhalili, wenye kusalimu amri wakimsikiliiza akiwaambia "Mnadhani nitawafanya nini?"

Baadhi ya watu wanaweza kudhani kuwa lengo la kwanza la Mtume na wais- lamu ni kuikimbiza tu dini yao kutoka kwa washirikina ambao waliwaingilia kwa kuwaudhi na kuwazuia kutekeleza nembo za dini yao na amali za kidini; sawa na anavyokimbilia Daruweshi msikitini ili aswali vizuri kwa kuepuka fujo na kelele. Hapana! Hijra ya waislamu ilikuwa mbali na kuwa na undani zaidi ya hilo.

Dalili ya hilo ni natija na malengo yaliyotekelezwa na Hijra hiyo. Hijra hiyo zaidi ya kuikimbiza dini, ilikuwa na mipango iliyopangwa vizuri ya uandalizi wa vita; sawa na jeshi linapojitenga kutoka uwanja wa vita kwenda mahali pengine ili kujiandaa kwa shambulio kubwa la kummaliza adui.

Mtume (s.a.w.) baada ya kufika Madina aliwafanya ndugu Masahaba na akazichanganya pamoja nyoyo za mahasimu na akayeyusha vinyongo na vidonge walivyokuwa navyo.

Baada ya kukamilisha kazi hiyo aliwahimiza waislamu jihadi na kuwahimiza kulinda heshima yao na itikadi yao, na kumdhaminia pepo atakayepigana katika njia ya Mwenyezi Mungu, na kupata utukufu na cheo duniani na akhera kwa atakayepona kifo.

Baada ya mafunzo haya kuwaingia, Mtume akaanza kuwaunganisha kijeshi na kuwazoesha vita vidogo vidogo akiwapeleka huku na huko; mara nyingi akiv- iongoza mwenyewe. Waislamu wakawa na amani na raha; na amani ya Maquraish ikaingia kwenye wasiwasi. Hatimaye vita vidogo vikageuka na kuwa vita vikubwa, huku waislamu wakijitolea roho zao na mali zao, mpaka ukaja msaada wa Mwenyezi Mungu na ushindi.

"… Na akalifanya neno la waliokufuru kuwa chini na neno la Mwenyezi Mungu ndilo la juu …" (9: 40). Nadhani ishara hii inatosha kuchukua ibra ambayo ni wajibu kunufaika nayo katika balaa letu na israel na wanaoisaidia .

Mtume (s.a.w.) alihama kutoka Makka kwa sababu ya uchokozi wa washirikina waliokuwa wakimfanyia yeye na masahaba wake. Na wapalestina nao wal- ihama kutoka ardhi takatifu kwa uchokozi wa kizayuni na kutaka kuwatawala wao wanawake wao na watoto wao. Hijra ya waislamu wakati huo ilikuwa ni kujiepusha na maangamizo na kujitenga kutoka uwanja wa vita ili kukusanya nguvu na kujiandaa kwa shambulio la kummaliza adui.

Kwa hiyo basi ni wajibu kuwa kutoka kwa wapalestina mijini kwao kuwe ni kwa makusudio haya na kwa lengo hili; sio kwa kuwaachia wanyang'anyi Baitul- Maqdis waichezee.

Mtume alianza Hijra yake kwa kufanya udugu baina ya masahaba zake. Kwa hiyo ni juu ya viongozi wa kiarabu na waislamu, kuanza kufanyiana udugu na kusafiana nyoyo; wawe wamoja ili waweze kumkabili adui; sawa na alivyofanya Mtume kabla ya kukabiliana na washirikina. Mwenye kuepuka njia hii basi amekutana na waisrael na ametekeleza malengo yao, atake asitake.

Mtume alituma vikosi vidogo kubabaisha washirikina, alivipa vikosi hivyo mahitaji yao. Ni wajibu kwa waarabu na waislamu kuwashujaisha wanaojitolea mhanga na wengineo na kusaidiana nao hadi mwisho, ili kuwatia wasiwasi waisrael. Mtume aliwaandaa waislamu wote kwa vita vikubwa na kuung'oa ushirikina na mizizi yake baada ya kuota mizizi, karibu karne nzima, katika kila sehemu ya ardhi ya Bara Arabu. Na hivyo ndivyo inavyopasa kwa kila kiongozi wa waarabu na waislam.

Ikiwa hatutalizingatia somo hili kutokana na turathi zetu na Historia yetu na kuwa sote ni askari katika askari wa Mwenyezi Mungu na wa nchi, basi hatutastahiki jina la uarabu na warabu, wala la uislamu na waislam; hata kwa jina za binadamu na ubinadamu; baada ya kuwa hizi ni zama za kujitolea na kutekeleza; na kujikomboa na kila aina ya dhulma na unyonyaji.

Tumalizie kwa kuwapa salaam watoto wetu wapiganaji waliojitolea mhanga ambao wameonyesha mfano mzuri wa kishujaa katika nchi yetu iliyovamiwa, wakauthibitishia ulimwengu wote kwamba sisi tuko katika zama za kujitolea na kupigania uhuru na heshima.

وَإِذَا ضَرَبْتُمْ فِي الْأَرْضِ فَلَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ أَنْ تَقْصُرُوا مِنَ الصَّلَاةِ إِنْ خِفْتُمْ أَنْ يَفْتِنَكُمُ الَّذِينَ كَفَرُوا ۚ إِنَّ الْكَافِرِينَ كَانُوا لَكُمْ عَدُوًّا مُبِينًا {101}

Na mnaposafiri katika ardhi, si vibaya kwenu kama mkifupisha Swala, ikiwa mnaogopa kuwa wale waliokufuru watawaletea balaa. Hakika makafiri ni maadui wenu walio wazi.

وَإِذَا كُنْتَ فِيهِمْ فَأَقَمْتَ لَهُمُ الصَّلَاةَ فَلْتَقُمْ طَائِفَةٌ مِنْهُمْ مَعَكَ وَلْيَأْخُذُوا أَسْلِحَتَهُمْ فَإِذَا سَجَدُوا فَلْيَكُونُوا مِنْ وَرَائِكُمْ وَلْتَأْتِ طَائِفَةٌ أُخْرَىٰ لَمْ يُصَلُّوا فَلْيُصَلُّوا مَعَكَ وَلْيَأْخُذُوا حِذْرَهُمْ وَأَسْلِحَتَهُمْ ۗ وَدَّ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْ تَغْفُلُونَ عَنْ أَسْلِحَتِكُمْ وَأَمْتِعَتِكُمْ فَيَمِيلُونَ عَلَيْكُمْ مَيْلَةً وَاحِدَةً ۚ وَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِنْ كَانَ بِكُمْ أَذًى مِنْ مَطَرٍ أَوْ كُنْتُمْ مَرْضَىٰ أَنْ تَضَعُوا أَسْلِحَتَكُمْ ۖ وَخُذُوا حِذْرَكُمْ ۗ إِنَّ اللَّهَ أَعَدَّ لِلْكَافِرِينَ عَذَابًا مُهِينًا {102}

Na utakapokuwa kati yao, ukawasimamishia Swala, basi kundi moja miongoni mwao wasimame pamoja nawe na washike silaha zao. Watakaposujudu na wawe nyuma yenu; Na lije kundi jingine ambalo halijaswali, waswali pamoja na wewe na washike hadhari yao na silaha zao. Wanataka wale waliokufuru lau kama nyinyi mwasa- hau silaha zenu na vifaa vyenu ili wawavamie mvamio wa ghafla. Wala hapana vibaya kwenu ikiwa mnaona udhia kwa sababu ya mvua au mkiwa wagonjwa kuweka silaha zenu. Hakika Mwenyezi Mungu amewaandalia makafiri adhabu ya kudhalilisha.

فَإِذَا قَضَيْتُمُ الصَّلَاةَ فَاذْكُرُوا اللَّهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِكُمْ ۚ فَإِذَا اطْمَأْنَنْتُمْ فَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ ۚ إِنَّ الصَّلَاةَ كَانَتْ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ كِتَابًا مَوْقُوتًا {103}

Mtakapomaliza Swala, basi mtajeni Mwenyezi Mungu kwa kusimama na kwa kukaa na kwa (kulala) ubavu. Mtakapopata amani, basi simamisheni Swala. Hakika Swala kwa waumin ni faradhi iliyoekewa wakati maalum.