read

Aya 1-6

Maana

Yamekwishapita maelezo kuhusu (Alif Laam Miim) katika mwanzo wa Sura Baqara. Vile vile maelezo ya hakuna Mola yameelezwa mwanzo wa Aya Kursiy (2: 255).

Amekuteremshia Kitabu kwa haki, kinachosadikisha yaliyokuwa kabla yake.

Makusudio ya Kitabu ni Qur'an; ambayo inasadikisha vitabu vilivyoteremshiwa Mitume waliotangulia.

Kimsingi ni kwamba kusadikishwa yaliyoteremshiwa Mitume waliotangulia, hakulazimishi kusadikisha vitabu vinavyonasibishwa kwao na baadhi ya makundi. Na sisi waislamu tumeamini kauli ya Mtume (s.a.w.), lakini pamoja na hivyo hatuamini kila kilicho katika vitabu vya Hadith zilizoelezwa kutokana naye. Ama yule anayeamini vitabu vilivyotangulia, basi ni juu yake kuamini Qur'an, vinginevyo atakuwa anajipinga yeye mwenyewe. Kwa sababu Qur'an inasadikisha vitabu hivyo. Kwa hiyo kuikadhibisha Qur'an ndio kuvikadhibisha vitabu vingine.

Na aliteremsha Tawrat na Injil kabla yake, ziwe ni uwongozi kwa watu.

Kuisifu Tawrat na Injil kuwa ni uongozi, kunalazimisha kuwa vimeteremshwa kwa haki; kama ambavyo kuisifu Qur'an kuwa ni uwongozi kunalazimisha kuwa imeteremshwa kwa haki. Kwa hivyo basi, kila kimoja katika vitabu vitatu hivyo ni cha haki na ni uwongozi.

Makusudio ya uwongozi hapa, ni ubainisho wa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) wa halali na haramu kupitia katika ulimi wa Mitume Yake. Na, ubainifu huu unamaanisha kujua hukumu za Mwenyezi Mungu. Ama kuzitumia hizo hukumu, kunahitaji aina nyingine ya uwongozi zaidi ya ubainifu. Mimi sikupata tamko jengine la kuelezea aina hiyo isipokuwa neno Tawfiq. Nayo inaashiriwa na neno lake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Kwa hakika wewe huwezi kumwogoza umpendaye, lakini Mwenyezi Mungu humwongoza amtakaye." (28: 56)

Qur'an inalitumia Neno Tawrat kwa maana ya wahyi ulioteremshiwa nabii Musa (a.s.); na neno Injil kwa Wahyi ulioteremshiwa nabii Isa (a.s.). Lakini Qur'an imebainisha kuwa Tawrat na Injil inayozikubali sio zile zilizoko kwa mayahudi na wakristo hivi sasa.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: Miongoni mwa mayahudi wamo ambao huyabadilisha maneno kuyatoa mahali pake. (4:46).

Na kwa wale waliosema: Sisi ni wanasara (Wakristo) tulichukua ahadi kwao, lakini wakaacha sehemu ya yale waliyokumbushwa.
Enyi watu wa Kitabu! Amekwisha wafikia mtume wetu, anayewabainisha mengi mliyokuwa mkiyaficha katika kitabu. (5:14-15)

Wahubiri wa kimasihi wanayajua sana haya, lakini pamoja na hayo wanajisifu na kuwavunga watu kuwa Qur'an inakiri Tawrat na Injil iliyochezewa na mikono ya kugeuza.

Ilivyo, ni kuwa Qur'an yote ni moja na jumla moja; kwa hiyo haifai kuamini sehemu fulani na kukanusha sehemu nyingine.

Tawrat ni neno la Kiebrania lenye maana ya sharia; nayo imegawanywa kwenye vitabu vitano:

1. Mwanzo, chenye maelezo ya kuanza kuumbwa ulimwengu na habari za Mitume.

2. Kutoka, ndani yake mna historia ya wana wa Israil na kisa cha Musa.

3. Kumbukumbu la Tawrat, humo mna hukumu za sharia ya Kiyahudi.

4. Walawi, humo mna mambo ya ibada na ndege na wanyama walioharamishwa. Walawi ni kizazi cha mmojawapo wa watoto wa Yakub anayeitwa Lawi.

5. Hesabu, ndani yake mna mkusanyiko wa koo za Wana wa Israil na majeshi yao.

Vitabu hivi vitano ni mkusanyiko wa vitabu vidogo vidogo vipatavyo thelathini na tisa, na wakristo wanaviita Agano la kale.

Ama Injil, asili yake ni neno la kiyunani; maana yake ni bishara (khabari njema). Na Injili kwa wakristo ni nne:

1. Mathayo: Historia ya kutungwa kwake ina kiasi cha miaka 60 (A.D). Na iliandikwa katika lugha ya kiarmenia.

2. Marko: iliyotungwa kwenye mwaka wa 63 au 65 (A.D) kwa lugha ya kiyunani.

3. Luka: iliyotungwa pia kwa lugha ya kiyunani kwa tarehe ile ya Marko.

4. Yohana: vile vile kwa lugha ya kiyunani kwenye mwaka 90 (A.D.)

Rai ya wakristo ilithibiti mwanzoni wa karne ya 5 A.D kwa kutegemea vitabu ishirini na saba katika vitabu vyao. Wakasema kwamba ni ufunuo (wahyi) kutoka kwa Mungu kwa kimaana sio kitamko.

Na wakavipa jina la Agano jipya, likiwa ni mkabala wa lile la zamani wanalolitegemea mayahudi. Kwa hiyo Agano la zamani, ni agano la Musa; na lile jipya ni la Isa, umepita ufafanuzi unaombatana na hayo katika Sura ya pili, Aya ya tatu.

Na ameteremsha upambanuzi.

Yaani upambanuzi baina ya haki na batili. Wametofautiana sana kuhusu makusudio ya upambanuzi; je, ni akili, Zaburi, Qur'an au ni dalili inayopambanua baina ya haki na batili? Sheikh Muhammad Abduh amechagua akili. Mwenye Majmaul Bayan amechagua Qur'an. Tamko la Aya linachukua maana zote mbili.

Hakika wale waliozikufuru Aya za Mwenyezi Mungu wana adhabu kali, na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye nguvu Mwenye kutia adabu.

Wafasiri wanasema kwamba watu wapatao sitini katika wakristo wa Najran, Yemen, walimfikia Mtume mnamo mwaka wa tisa Hijria; mwaka uliojulikana kama mwaka wa ugeni. Kwani wageni wengi walimfikia Mtume kutoka sehemu mbali mbali za Bara Arabu, wakielezea utii na mapenzi yao kwake, baada ya Mwenyezi Mungu kumpa ushindi kwa maadui.

Ugeni wa kinajran ulitoa hoja ya itikadi ya kikiristo ya utatu na uungu wa Isa. Kwa hoja ya kuwa Isa ni mtoto asiyekuwa na baba pamoja na miujiza aliyoifanya ambayo Qur'an imeielezea.

Vilevile wafasiri wanasema Sura ya Al-Imran kuanzia mwanzo wake hadi Aya thamanini ilishuka juu ya wakristo wa Najran na majibu yao: Mwenyezi Mungu akaanza kwa kutaja Tawhid (umoja) ili kukanusha utatu; kisha akataja Qur'an, Tawrat na Injil kwamba vitabu vitatu hivi vinamwepusha Mwenyezi Mungu na mtoto na kugawanyika. Vilevile vinakanusha uungu wa Isa. Kisha Mwenyezi Mungu akataja:

Hakika Mwenyezi Mungu hakifichiki kwake chochote kilichomo ardhini wala kili- chomo mbinguni.

Ikiwa ni majibu ya kauli ya wakristo kwamba Isa alikuwa akijua ghaibu. Tena akaendelea Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kusema:

Yeye ndiye ambaye huwatia sura matumboni jinsi anavyotaka, hakuna Mola isipokuwa Yeye Mwenye nguvu na Mwenye hekima.

Mwenyezi Mungu anayataja haya ili abatilishe kauli ya Wakristo kwamba Isa ni Mungu kwa sababu ya kutokuwa na baba; kwa maana ya kuwa Mungu haumbwi na kuwa tumboni mwa mama. Akipenda anaweza kumuumba kupitia baba na kama akipenda anaweza kumuumba bila ya baba, kwa kiasi kile hekima yake takatifu inavyotaka.

Kwa ufupi ni kuwa kutolea habari baadhi ya mambo ya ghaibu, kufufua baadhi ya wafu na kuzaliwa bila ya baba, hakumaanishi kuwa Isa (Yesu) ni Mungu. Kwa sababu Mungu ni yule anayejua mambo ya ghaibu, hakifichiki kwake chochote katika ardhi au mbinguni, Mwenye kufufua wafu wote sio baadhi, anayeweza kila kitu hata kuumba bila ya kitu kingine. Kwa dhahiri ni kwamba Isa hakuwa akijua ghaibu zote, wala hakuweza kufufua maiti wote na hakuumba yeyote tumboni mwa mama yake bila ya baba au na baba; bali kinyume chake ndio sahihi, kwani yeye ndiye aliyeumbwa ndani ya tumbo la uzazi

هُوَ الَّذِي أَنْزَلَ عَلَيْكَ الْكِتَابَ مِنْهُ آيَاتٌ مُحْكَمَاتٌ هُنَّ أُمُّ الْكِتَابِ وَأُخَرُ مُتَشَابِهَاتٌ ۖ فَأَمَّا الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ زَيْغٌ فَيَتَّبِعُونَ مَا تَشَابَهَ مِنْهُ ابْتِغَاءَ الْفِتْنَةِ وَابْتِغَاءَ تَأْوِيلِهِ ۗ وَمَا يَعْلَمُ تَأْوِيلَهُ إِلَّا اللَّهُ ۗ وَالرَّاسِخُونَ فِي الْعِلْمِ يَقُولُونَ آمَنَّا بِهِ كُلٌّ مِنْ عِنْدِ رَبِّنَا ۗ وَمَا يَذَّكَّرُ إِلَّا أُولُو الْأَلْبَابِ {7}

Yeye ndiye aliyekuteremshia Kitabu ndani yake zimo Aya zilizo waziwazi ambazo ndizo msingi wa Kitabu na nyingine zenye kufichikana. Wale ambao nyoyoni mwao mna upotofu wanafuata zile zinazotatiza kwa kutaka kuharibu na kutaka tafsiri yake. Na hajui tafsir yake isipokuwa Mwenyezi Mungu na waliozama katika elimu. Husema tumeziamini zote zimetoka kwa Mola wetu. Na hawakumbuki isipokuwa wenye akili.

رَبَّنَا لَا تُزِغْ قُلُوبَنَا بَعْدَ إِذْ هَدَيْتَنَا وَهَبْ لَنَا مِنْ لَدُنْكَ رَحْمَةً ۚ إِنَّكَ أَنْتَ الْوَهَّابُ {8}

Mola wetu! Usizipotoshe nyoyo zetu baada ya kutuongoza na utupe rehema kutoka kwako. Wewe ndiwe mpaji mkuu.

رَبَّنَا إِنَّكَ جَامِعُ النَّاسِ لِيَوْمٍ لَا رَيْبَ فِيهِ ۚ إِنَّ اللَّهَ لَا يُخْلِفُ الْمِيعَادَ {9}

Mola wetu! Wewe ndiwe mwenye kuwakusanya watu katika siku isiyo na shaka ndani yake. Hakika Mwenyezi Mungu havunji miadi.