read

Aya 10 -13: Hazitawafaa Kitu Mali Zao Na Watoto Wao

Maana

Hakika wale ambao wamekufuru hazitawafaa kitu mali zao na watoto wao kwa
Mwenyezi Mungu; na hao ndio kuni za moto.

Mwenye kufuatilia Aya za Qur'an, yenye hekima, kuhusu kuwazungumzia matajiri, ataziona kuwa zinawataja kwa sifa mbalimbali mbaya kama ifuatavyo:

• Ujeuri, Mwenyezi Mungu anasema.

• Hakika binadamu hupetuka mipaka kwa kujiona amejitosha (96: 6-7)

• Kuhadaika, Mwenyezi Mungu anasema: "Na akaingia katika bustani yake na hali ya kuwa anajidhulumu nafsi yake akasema: "Sidhani kabisa kuwa itaharibika. Wala sidhani kuwa kiyama kitatokea …" (18: 35-36)

• Tamaa Mwenyezi Mungu anasema: Na nikamjaalia awe na mali nyingi… Kisha anatumai nimzidishie .(74: 12-15)

• Kuwa na mawazo potofu kwamba mali itawakinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu anasema: "Na wakasema: 'sisi tunazo mali nyingi na watoto wengi wala sisi hatutaadhibiwa." (34:35)

Mwenyezi Mungu ameziondoa dhana zote hizi kwa kusema kwamba mali na watoto hazitoshelezi kitu, bali mali zitamfanya aliye nazo kuwa kuni kesho; kama vile miti. Wapotofu wanadhani kwamba mali zao na watoto wao wataweza kuwahami hapa duniani, lakini wanapokabiliana na wenye haki ana kwa ana katika uwanja wa vita hubainika unyonge wao.

Kwa sababu Mungu huwapa nguvu wakweli kwa nusura yake na humdhalilisha yule mfisadi aliye mwongo sana.

Wenye Mali

Historia haijajua watu waovu na wadhalimu wakubwa zaidi wakati huu kuliko wenye mali na utajiri waliolundika. Wao ndio wanaoleta fitina, uharibifu na vita; wanapanga kila mbinu kujaribu kuzuia harakati zozote za ukombozi popote pale ulimwenguni.

Wanaanzisha vyama vya vibaraka wao, vikosi vya umoja, wapelelezi na majasusi katika pembe zote za dunia ili waugeuze ulimwengu uwe ni kinyang'anyiro cha shirika la mamilionea.

Wao hawaamini Mungu wala utu au jambo lolote isipokuwa wanaamini hisa ambazo zitany- onya faida kutoka katika jasho la watu, damu yao na mustakbali wao. Dola zao zinajishughulisha kueneza hofu, wasiswasi na ukandamizaji wa kichumi na kisiasa kwa wanyonge. Wanatumia kila mbinu kuwagawaya watu wasiwe na umoja, ili watu wote wawatu- mikie wao.

Kwa ajili hiyo, ndipo uislamu ukaharamisha ulanguzi na utajiri usiofuata sharia na kuwakandamiza wanyonge. Na umewatisha wale wanaolimbikiza mali bila ya kuzitoa sabili na kuita wapetukaji mipaka.

Kama desturi ya watu wa firaun na wale waliokuwa kabla yao; walikadhibisha Aya zetu Mwenyezi Mungu akawatia adabu kwa sababu ya dhambi zao na Mwenyezi Mungu ni mkali wa adhabu.

Yaani wingi wa mali na watoto sio sababu ya kufuzu na kuokoka. Mara nyingi mafukara wameshinda matajiri na uchache ukashinda wingi. Historia imejaa ushahidi wa ukweli huu.

Firaun na watu wake walikuwa wengi wenye jaha, usultani, mali na vifaa, lakini pamoja na hayo Mwenyezi Mungu aliwafedhehesha na kumpa ushindi Musa asiyekuwa na mali wala wingi wa watu; kama ambavyo alimpa ushindi Nuh kwa watu wa zama zake, Ibrahim kwa Namrud, Hud kwa Ad na Saleh kwa Thamud. Kwa hiyo wingi na utajiri sio hoja. Na wanaomkadhibisha Mtume Muhammad (s.a.w.w) nao mwisho wao utakuwa hivyo hivyo.

Waambie wale waliokufuru: Mtashindwa na mtakusanywa mtiwe katika Jahannam, nako ni makao mabaya.

Imeelezwa katika Majamaul-bayan kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alipompa ushindi Mtume wake katika vita vya Badr,alipofika Madina Mtume aliwakusanya Mayahudi na kuwaambia: "Tahadharini yasije yakawapata yaliyowapata maquraish katika Badr."

Wakamwambia: "Usihadaike, wewe umekutana na watu wasiojua vita; lau ungelikutana na sisi ungelijua kwamba sisi ni watu;" ndipo Mwenyezi Mungu akateremsha Aya hii. Mwenyezi Mungu alitimiza miadi yake: Waislamu wakawaua Bani Quraydha wahaini na wakawafagia Bani Nadhir wanafiki, wakaichukua Khaybar na wakawatoza kodi wengine.

Hakika ilikuwa ni ishara kwenu katika yale makundi mawili yalipokutana na kundi moja lilipigana katika njia ya Mwenyezi Mungu na jingine kafiri, likiwaona mara mbili zaidi kuliko wao kwa kuona kwa macho.
Mwenyezi Mungu katika Aya hii anawaonyaMayahudi, manaswara, waislamu na wenye busara wote kwa ujumla kuhusu vita vya Badr wakati kilipokutana kikosi cha Mtume ambacho ni Muhammad na sahaba zake na kikosi cha shetani ambacho kilikuwa zaidi ya watu elfu, wakiwa wamejisheheneza silaha za kutosha.

Na kikosi cha Mtume kilikuwa ni theluthi tu ya idadi yao, wakiwa hawana zana zozote zaidi ya farasi wawili, deraya saba na panga nane, lakini pamoja na hayo Mungu aliwaandikia ushindi hao wachache; Mwenyezi Mungu akawaonyesha washirikina kuwa waislamu ni zaidi yao ingawaje ni wachache.

Aya hii iko katika mwelekeo wa Aya inayosema: "Na mlipokutana, akawaonyesha machoni mwenu kuwa wao ni wachache na akawafanya nyinyi ni wachache machoni mwao, ili Mwenyezi Mungu atimieze jambo lililokuwa liwe. Na mambo yote hurejezwa kwa Mwenyezi Mungu" (8 : 44)

Kwa mnasaba huu ni vizuri tutaje nasaha ya Imam Ali (a.s.) kwa khalifa wa pili alipomtaka ushauri katika vita vya Roma; Imam alisema: " Yule aliyenusuru Waislamu wakiwa ni wachache bado yuko hai, hafi, wewe ukienda mwenyewe katika vita na ukakimbia basi waislamu hawatakuwa na ngome wala kimbilio. Wewe mpeleke mtu mwenye uzowefu na umwandalie watu wenye uzoefu na wenye ushauri. Ikiwa Mwenyezi Mungu atakudhihirisha ndivyo unavyotaka, vinginevyo utakuwa ni kimbilio la watu.

زُيِّنَ لِلنَّاسِ حُبُّ الشَّهَوَاتِ مِنَ النِّسَاءِ وَالْبَنِينَ وَالْقَنَاطِيرِ الْمُقَنْطَرَةِ مِنَ الذَّهَبِ وَالْفِضَّةِ وَالْخَيْلِ الْمُسَوَّمَةِ وَالْأَنْعَامِ وَالْحَرْثِ ۗ ذَٰلِكَ مَتَاعُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَاللَّهُ عِنْدَهُ حُسْنُ الْمَآبِ {14}

Watu wamepambiwa kupenda matamanio ya wanawake na watoto na mirundo ya dhahabu na fedha, na farasi wazuri, na mifugo na mashamba. Hivyo ni vitu vya anasa katika maisha ya dunia; na kwa Mwenyezi Mungu ndiko kwenye marejeo mazuri.