read

Aya 14: Kupenda Matamanio

Maana

Wametofautiana wafasiri kuwa ni nani anayewafanya watu kupenda matamanio. Baadhi wamesema ni Mwenyezi Mungu na wengine wakasema ni shetani. Lakini ukweli ulivyo, ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amempa mtu tabia ya kupendelea matamanio na shetani naye humtia wasiwasi mtu na kumfanyia nzuri amali mbaya; na ile mbaya anamfanyia aione nzuri. Hata hivyo kupenda wanawake, watoto na mali siko kubaya hasa; na wala Mwenyezi Mungu hakutuharamishia. Vipi isiwe hivyo na hali yeye Mwenyezi Mungu amesema: Waambie nimewahalalishia mema. Na Mtume (s.a.w.) amesema: "Mimi ninapenda vitu vitatu katika dunia yenu: Manukato, wanawake, na kitulizo cha moyo wangu, Swala."

Makusudio ya matamanio hapa ni vitu anavyovipendelea mtu na kuhisi raha anapovipata. Unaweza kuuliza neno matamanio linakusanya maana ya mapenzi; kama ambavyo mapenzi yanakusanya maana ya matamanio. Kwa hivyo basi maana ya Aya yatakuwa kwamba watu wanapenda mapenzi na wanatamani matamanio. Na maneno ya Mwenyezi Mungu hayawezi kuwa katika hali hii ya kutonyooka.

Jibu: Kupenda kitu kuko namna mbili:

Kwanza: ni mtu kupenda kitu, lakini hapendi akipende, yaani nafsi yake inapenda kama ingewezekana asikipende kitu hicho. Kwa mfano mtu kupenda kuvuta sigara inayomdhu- ru. Mwenye pendo hili anataka limwondokee kila siku.

Pili: ni mtu kupenda kitu na yeye mwenyewe yuko radhi; kama mtu aliyezoweya kufanya amali za kheri. Mwenyezi Mungu anasema katika kumzungumzia Nabii Suleiman: Hakika mimi ninapenda pendo la kheri (38:32) Hili ni pendo la hali ya juu na mwenye pendo hilo hataki limwondokee.
Mrundo ni fumbo la wingi. Hadith inasema: "Lau mtu angekuwa na nyangwa mbili za dhahabu, basi angelitamani wa tatu; na wala hawezi kutosheka isipokuwa kwa mchanga."

Kupenda wanawake, watoto na mali, kunapatikana wakati wote bali hayo ni matamanio ya kila nafsi. Ama kupenda farasi, wanyama na mashamba, Mwenyezi Mungu amekuhusisha kukutaja kwa wakati huo kwa sababu ndio vitu vilivyopendelewa zaidi.

Wafasiri wengi kama vile Razi na mwenye Al-manar wamerefusha maneno katika kutaja kila moja katika aina hizi sita za ladha na starehe, lakini wametaja mambo ya dhahiri yanayojulikana na kuhisiwa na wote. Kwa hiyo hatukujishughulisha nayo na tunaonelea ni vizuri tutaje raha katika kifungu kinachofuatia.

Raha

Baadhi ya watungaji wanaona kuwa raha inaweza kukamilika kwa binadamu kama akiwa na nguzo hizi nane: Afya, mke anayeafikiana naye, mali ya kutekeleza haja na jaha itakayohifadhi utukufu. Nafikiri mwenye rai hii ameangalia raha kwa upande wake na haja yake, sio kwa ilivyo hasa. Kama ni hivyo ataziweka wapi hisia za matatizo ya kilimwengu; kama vile hofu, mwisho mbaya na uongo, na matatizo mengineyo yanayousonga moyo.

Kwa kweli kabisa raha kamili bado haijapatikana kwa binadamu; na ninafikiri haitapatikana katika maisha haya, ispokuwa maisha mengine. Ama raha ya upande fulani na wakati fulani imeweza kumpitia mtu, ijapokuwa utotoni. Ni vizuri kufafanua raha ya upande fulani kama ifutavyo:

Kustarehe kuko kwa aina nyingi, kama kustarehe kwa kuangalia miti wakati wa maleleji na mito na maporomoko ya maji, au kusikiliza mashairi, au kustarehe kwa kusoma vitabu, na mengineyo katika mambo ya starehe za kiroho.

Katika starehe za kimaada ni wanawake, mali na watoto. Ama farasi wanyama na mashamba hiyo ni katika jumla ya mali. Lakini starehe hizi zote hazimpi binadamu raha kamili, kwa sababu dunia haimnyookei yeyote kwa kila upande. Akiwa ana uwezo wa kuyamudu maisha, basi atakuwa na matatizo ya nyumbani au katika uzao wake.

Amirul Muumini Ali (a.s.) anasema: "Akipata raha mtu upande mmoja, atapata uchungu upande mwengine, Hawezi kupata mtu starehe ila atapata tabu"

Ama raha ya upande fulani tu yaani katika hali fulani hiyo anaipata mtu. Mfano mzuri ni ule niliousoma katika baadhi ya vitabu. Mtungaji anasema: Familia moja ilitoka kwenda kwenye matembezi; akiwemo mama, watoto, ami, mjomba, baba na babu. Walipofika wanapokwenda, mtoto alielekea kwenye nyasi, mwengine akachuma maua, mama naye akatengeneza sandwichi, ami akatafuna tofaha, mjomba akazungusha gramafoni (kinanda), baba akajinyoosha mchangani akiwa anaangalia kondoo na babu naye akawa anajishughulisha na kuvuta buruma.

Basi ikawa kila mmoja anahisi raha kwa upande wake, lakini raha hiyo ni katika hali hiyo tu, sio katika hali zote.Hekima ya Mungu imepitisha kuwa raha kamili haiwezi kupatikana isipokuwa akhera. Kwa sababu hii ndipo akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu baada ya kutaja wanawake, watoto na mali kuwa kuna kilicho bora zaidi ya hivyo. Nimeona Riwaya kutoka kwa Imam Jaffar Sadiq (a.s.) akizingatiya kuwa tawfiki ya Mungu ni nguzo miongoni mwa nguzo za msingi wa raha. Na, hakika hii nimeijua kwa hisia na majaribio.

قُلْ أَؤُنَبِّئُكُمْ بِخَيْرٍ مِنْ ذَٰلِكُمْ ۚ لِلَّذِينَ اتَّقَوْا عِنْدَ رَبِّهِمْ جَنَّاتٌ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا وَأَزْوَاجٌ مُطَهَّرَةٌ وَرِضْوَانٌ مِنَ اللَّهِ ۗ وَاللَّهُ بَصِيرٌ بِالْعِبَادِ {15}

Sema: Je, niwambie yaliyo bora kuliko hayo kwa kwa wamchao Mungu? Kwa mola wao ziko bustani ambazo hupita chini yake mito; watakaa humo milele na wake waliotakaswa na wana radhi ya Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu anawaona waja.

الَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا إِنَّنَا آمَنَّا فَاغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا وَقِنَا عَذَابَ النَّارِ {16}

Ambao wanasema: "Mola wetu! Hakika sisi tumeamini, basi tughufirie madhambi yetu. Na tuepushe na adhabu ya moto.

الصَّابِرِينَ وَالصَّادِقِينَ وَالْقَانِتِينَ وَالْمُنْفِقِينَ وَالْمُسْتَغْفِرِينَ بِالْأَسْحَارِ {17}

Wanaofanya subira na wanaosema kweli na watiifu na wanaotoa na wanaoomba maghufira kabla ya Alfajiri.