read

Aya 15-17: Yaliyobora

Maana

Sema: Je, Niwaambie yaliyo bora kuliko haya kwa wamchao Mungu?

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwanza ametaja kupenda wanawake, mali na watoto; kisha vitu vyote hivi akaviita anasa za dunia, na dunia inaondoka; na akabainisha kwamba kwake ndiko kwenye marejeo mazuri, yaani kwamba mtu baada ya kurejea kwa Mola wake atakuta mambo mazuri zaidi kuliko wanawake, mali na watoto na kuliko dunia yote. Baada ya hapo ndipo anafafanua kwa Aya hii.

Kwa Mola wao ziko bustani ambazo huipita chini yake mito; watakaa humo milele na wake waliotakaswa na wana radhi ya Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu anawaona waja.

Haya matatu ni bora kuliko wanawake, mali na watoto, nayo ni marejeo mazuri. Kwanza ni, pepo ambayo haitakwisha sio kama shamba, farasi na mifugo. Pili ni wanawake waliotakaswa na hedhi, hadathi na uchafu wote. Vilevile wametakaswa na kila kinyaa. Tatu ni radhi ya Mwenyezi Mungu ambayo ni kubwa zaidi kuliko dunia na akhera kwa pamoja. Yote hayo Mwenyezi Mungu ameyafanya ni malipo ya mwenye kuogopa kusimama mbele za Mola wake na akaikataza nafsi (yake) na matamanio.

Wanaofanya subira, na wanaosema kweli na watiifu na wanaotoa na wanaoomba maghufira kabla ya Alfajiri.

Mwenye kusubiri ni yule anayekabiliana na mambo kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu; na kuridhia natija ya makabiliano yake. Msema kweli ni yule anayesema ukweli hata kama unamdhuru. Mtiifu ni yule mwenye kufanya ibada akiwa mtiifu. Mtoaji ni yule anayejitolea mali na kuwatolea watu wake katika njia ya Mwenyezi Mungu. Na, wakati wa kabla ya alfajiri; ni wakati bora kuliko wowote kwa ibada na dua; kama ilivyoelezwa katika Hadith. Kwa sababu wakati huo uko mbali kabisa na shub'ha ya ria; Na, ni wakati ambao usingizi ni mtamu sana; kwa hivyo inakuwa tabu kuamka. Na amali bora zaidi ni ile yenye mashaka na tabu, ingawaje kuhudumia mtu ni bora zaidi kuliko Swala na Saumu.

Matunda Ya Imani

Sifa zote hizi tano (subira, ukweli, utiifu, kutoa na msamaha) ni matunda ya misingi mitatu ya dini; yaani kumwamini Mwenyezi Mungu mmoja aliye pekee, kuamini utume wa Muhammad (s.a.w.w.) na kuamini siku ya mwisho.

Misingi hii siyo kuwa ni mambo tu ya dini, bali inayo matunda na hakika zinazokusanywa na umbile tukufu, na amali yenye kunufaisha katika uhai. Mwenyezi Mungu anasema: "Enyi mlioamini! Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume atakapowaita katika yale yatakayowapa maisha, (8:24)

Kila asili katika asili ya dini inasimama kwa misingi hii. Vilevile kila tawi katika matawi ya dini, ni misingi inayofungamanisha dini na matendo kwa ajili ya maisha. Mwenyezi Mungu anasema: Basi naapa kwa Mola wako tutawauliza wote juu ya yale waliyokuwa wakiyatenda. (15: 92 - 93)

Je, mnadhani mtaingia peponi, bila ya Mwenyezi Mungu kuwapambanua wale waliopigana Jihadi miongoni mwenu na kuwapambanua waliofanya subira? (3:142)

Zimekuja Hadith kadhaa Mutawatir kwamba aina bora ya ibada na utiifu ni kufanya amali kwa ajili ya maisha mema na kwamba kubwa ya madhambi makubwa na maasi ni ufisadi na uadui kwa watu. Mtume anasema: "Karibu zaidi anapokuwa mja na Mola wake ni pale anapotia furaha katika moyo wa nduguye."

Amirul-Muminiin anasema: "Masurufu mabaya siku ya marejeo ni uadui kwa waja." Mjukuu wake, Imam Baqir, naye anasema: "Mwenyezi Mungu ana watu waliobarikiwa, watu wengine wanaishi katika hifadhi zao; nao ni kama tone. Na kuna watu ni vikwazo, wala watu wengine hawaishi katika hifadhi zao; nao ni kama nzige kila kitu wanakitaka."

شَهِدَ اللَّهُ أَنَّهُ لَا إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ وَالْمَلَائِكَةُ وَأُولُو الْعِلْمِ قَائِمًا بِالْقِسْطِ ۚ لَا إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ {18}

Mwenyezi Mungu na Malaika na wenye elimu wameshuhudia ya kwamba hakuna Mola ila Yeye tu. Ndiye Mwenye kusimamia uadilifu. Hakuna mola isipokuwa Yeye, Mwenye nguvu Mwenye hekima.

إِنَّ الدِّينَ عِنْدَ اللَّهِ الْإِسْلَامُ ۗ وَمَا اخْتَلَفَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ إِلَّا مِنْ بَعْدِ مَا جَاءَهُمُ الْعِلْمُ بَغْيًا بَيْنَهُمْ ۗ وَمَنْ يَكْفُرْ بِآيَاتِ اللَّهِ فَإِنَّ اللَّهَ سَرِيعُ الْحِسَابِ {19}

Hakika dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu. Na hawakukhitalifiana wale waliopewa Kitabu ila baada ya kuwajia ilimu. Kwa uhasidi uliokuwa baina yao. Na anayezikataa Aya za Mwenyezi Mungu basi Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.

فَإِنْ حَاجُّوكَ فَقُلْ أَسْلَمْتُ وَجْهِيَ لِلَّهِ وَمَنِ اتَّبَعَنِ ۗ وَقُلْ لِلَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ وَالْأُمِّيِّينَ أَأَسْلَمْتُمْ ۚ فَإِنْ أَسْلَمُوا فَقَدِ اهْتَدَوْا ۖ وَإِنْ تَوَلَّوْا فَإِنَّمَا عَلَيْكَ الْبَلَاغُ ۗ وَاللَّهُ بَصِيرٌ بِالْعِبَادِ {20}

Na kama wakikuhoji, basi sema: "Nimeusalimisha uso wangu kwa kumwelekea Mwenyezi Mungu, na walionifuata" Na waambie wale waliopewa Kitabu na wale wasiokuwa na kisomo na"Je,mmesilimu? Kama wakisilimu basi wameongoka; na kama wakikengeuka, basi juu yako ni kufikisha tu. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwaona waja