read

Aya 18-20: Mwenyezi Mungu, Malaika Na Wenye Elimu.

Mwenyezi Mungu na Malaika na wenye elimu wameshuhudia ya kwamba hakuna Mola isipokuwa yeye; Ndiye mwenye kusimamisha uadilifu. Hakuna Mola isipokuwa Yeye, Mwenye nguvu Mwenye hekima.

Kujishuhudia Mwenyezi Mungu yeye mwenyewe kuwa ni mmoja ni kutokana na vitendo Vyake ambavyo haviwezi yeyote isipokuwa Yeye; Mwenyezi Mungu anasema: "Tutawaonyesha ishara zetu katika upeo wa mbali na katika nafsi zao mpaka iwabainikie kuwa haya ni haki. Je haikutoshi kwamba Mola wako ni shahidi wa kila kitu? (41:53)

Ama ushuhuda wa Malaika kwa umoja wa Mungu ni kwamba wao wana maumbile ya imani. Makusudio ya wenye elimu hapa ni Mitume na wanavyuoni wote wanaomjua Mungu ambao wamekuwa makaimu wa Mitume katika kumlingania Mwenyezi Mungu. Na ushahidi wa mwanachuoni unaambatana na hoja ya kumkinaisha anayetafuta uhakika.

Makusudio ya uadilifu hapa ni uadilifu katika dini na sharia na katika desturi ya maumbile na nidhamu yake, Mwenyezi Mungu anasema: Na hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yake kwa mchezo. (21:16)

Unaweza kuuliza nini makusudio ya kukaririka neno: 'Hakuna Mola isipokuwa yeye,' Katika Aya moja?
Jibu: Inajulikana kuwa katika njia ya Qur'an ni kukariri na kutilia mkazo misingi ya itikadi na misingi muhimu, hasa umoja. Hiyo ni kuondoa shaka.Tumefafanua kukaririka katika kifungu mbali, tulipofasiri Aya 48 Sura ya Baqara.

Imesemekana kuwa makusudio ya kauli ya kwanza ni kujulisha kuwa yeye pekee ndiye anayestahiki kuabudiwa. Na, ya pili ni kujulisha kuwa hakuna yeyote mwenye kusimamia uadilifu isipokuwa yeye.

Dini Ya Mwenyezi Mungu Ni Uislamu

Unaweza kuuliza: Dhahiri ya Aya, Hakika dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni uislam, inafahamisha kuwa dini zote za mitume - hata dini ya Ibrahim - si chochote isipokuwa dini ya Muhammad (s.a.w.w.) na Qur'an tu?

Jibu: Hapana, bali Aya hii inafahamisha kinyume kabisa na hivyo. Kwani dhahiri yake inatamka kwa lugha fasaha kwamba kila dini aliyokuja nayo Mtume miongoni mwa Mitume waliotangulia umbo lake linakuwa na mwito wa kiislamu ambao ameulingania Muhammad bin Abdullah (s.a.w.). Kwa ufafanuzi zaidi angalia hakika hizi zifuatazo:

1. Kabla ya jambo lolote kwanza, uislamu una mambo matatu; Kumwamini Mwenyezi Mungu na umoja wake, kuamini wahyi na Isma yake na kuamini ufufuo na malipo yake. Kila mmoja wetu anaamini kwa imani isiyokuwa na tashwish yoyote kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakupeleka Mtume yeyote isipokuwa kwa misingi mitatu hii. Kwa hali hiyo ndipo Mtume (s.a.w.) akasema: "Sisi Mitume dini yetu ni moja"Akaendelea kusema: "Mitume ni ndugu katika shughuli (zao) baba yao ni mmoja na mama zao ni mbali mbali".

2. Neno uislamu linatumiwa kwa maana nyingi; kama kunyeyekea, usafi na kusalimika na ila na uchafu. Hakuna mwenye shaka kwamba kila dini aliyokuja nayo Mtume katika Mitume wa Mwenyezi Mungu ni safi isiyokuwa na uchafu wowote. Kwa hiyo basi inafaa kulitumia neno uislam kwa dini zote za Mitume.

3. Rejea ya Qur'an ni moja, hakuna tofauti kati ya Aya zake, bali hiyo Qur'an inajifasiri yenyewe na kujitolea ushahidi hiyo yenyewe; kama alivyosema Imam Ali (a.s.): "Ikija Aya katika suala fulani au maudhui fulani, basi haifai kuiangalia peke yake, bali ni lazima kufuatilia kila Aya zilizo na uhusiano na suala hilo na maudhui hayo na kuzikusanya katika jumla moja kwa kuunganisha na nyengine, kisha tutoe maana moja katika Aya zinazooana."

Tunapoangalia Aya zinazoelezea uislamu katika uhakika huu, tunakuta kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewasifu Mitume wote kwa Uislamu katika Aya nyingi.

Kwa hivyo tunajua kuwa neno la Mwenyezi Mungu, Hakika dini mbele za Mwenyezi Mungu ni Uislamu linakusanya dini zote za haki. Siri ya hilo ni hayo tuliyoyaeleza kwamba dini zote za Mitume zinadhamini mwito wa kiislamu katika uhakika wake na dhati yake.

Kwa kutilia mkazo imani ya Mwenyezi Mungu, wahyi na ufufuo. Ama tofauti inakuwa kaitka matawi na hukumu, sio katika misingi ya itikadi na imani.

Hebu tuangalie Aya ambazo Mwenyezi Mungu amewasifu Mitume kwa uislamu, tangu zama za Nuh (a.s.) mpaka za Muhammad (s.a.w.w.), Amesema Mwenyezi Mungu kuhusu Nuh: Na wasomee habari za Nuh alipowaambia watu wake Enyi watu wangu! ..., Nimeamrishwa niwe miongoni mwa waislamu. (10: 71-72).

Kuhusu Ibrahim na Yakub anasema: Na Ibrahim akawausia haya wanawe; na Yakub: "Enyi wanangu hakika Mwenyezi Mungu amewachagulia dini hii, basi msife ila mmekuwa waislamu. "(2:132).

Kuhusu Yusuf anasema: "Wewe ndiwe mlinzi wangu katika dunia na akhera, nifishe hali ya kuwa ni Mwislamu…" (12:101)

Kuhusu Musa anasema: "Na Musa akasema: Enyi watu wangu! Ikiwa nyinyi mme mwamini Mwenyezi Mungu, basi mtegemeeni yeye kama nyinyi ni waislamu" (10:84)

Kwa Umma wa Isa anasema: "Na nilipowafunulia wanafunzi (wako) kuwa niaminini mimi na Mtume wangu, wakasema: "Tumeamini na uwe shahidi kuwa sisi ni waislamu." (5:111)

Aya iliyo wazi kuliko zote na inayomuenea wa kwanza na wa mwisho katika Mitume, wafuasi wao na wafuasi wa wafuasi, ni ile isemayo: "Na yeyote mwenye kutaka dini isiyokuwa ya Kiislamu, basi haitakubaliwa kwake, naye akhera atakuwa katika wenye khasara." (3:85)

Ikiwa Mwenyezi Mungu hatakubali isipokuwa Waislamu tu; na huku amekwisha wakubali Mitume kuanzia Adam, Nuh, Ibrahim, Musa, Isa na Mitume wote pamoja na wafuasi wao, basi natija itakuwa kwamba Mitume wote kuanzia Adam mpaka Muhammad (s.a.w.) na wanaowafuata, ni waislamu.

Imam Ali (a.s.) anasema: "Uislamu ni kujisalimisha, kujislaimisha ni yakini, yakini ni kusadikisha, kusadikisha ni kukiri, kukiri ni kutekeleza na kutekeleza ni matendo."

Na hawakuhitalifiana wale waliopewa Kitabu ila baada ya kuwajia elimu kwa uhasidi uliokuwa baina yao

Makusudio ya watu wa Kitabu hapa ni mayahudi. Inasemekana ni manasara. Na, inasemekana ni wote, na hiyo ndio sahihi kwa sababu tamko ni la kiujumla na hakuna dalili ya umahsusi. Linalotilia nguvu kuwa tamko ni la kiujumla, ni kauli yake Mwenyezi Mungu:

"Na kwa wale waliosema: Sisi ni Wanaswara tulichukua ahadi yao, lakini wakaacha sehe- mu ya yale waliyokumbushwa, kwa hivyo tukaweka baina yao uadui na bughudha mpaka Siku ya Kiyama." (5:14)

Kuhusu tofauti ya Mayahudi anasema: "Na Mayahudi walisema: 'Mkono wa Mwenyezi Mungu umefumba'…"Na tumewatilia uadui na bughudha baina yao mpaka siku ya Kiyama." (5:64).

Katika mambo waliyohitalifiana Mayahudi ni uhai baada ya mauti. Baadhi yao wakasema, hakuna ufufuo kabisa, si katika maisha haya wala mengine na kwamba adhabu ya mwenye makosa na thawabu za mtu mwema zinapatikana katika maisha haya ya duniani.

Kikundi kingine kinasema: "Watu wema watafufuliwa mara ya pili hapa duniani ili washiriki katika ufalme wa Masih ambaye atakuja zama za mwisho."

Ama itikadi ya Kikristo iligeukageuka, kabla ya kudumu kwenye utatu. Mwanzo ilikuwa inalingania kwenye ibada ya Mungu mmoja, kisha wakagawanyika makundi mawili: Kundi moja lilikuwa katika shirk na jengine likabakia kwenye Tawhid lakini likatofautiana kuwa je, Isa ana tabia mbili ya kiungu na nyengine ya kibinadamu; au ana tabia ya kiungu tu? Na mengine mengi yaliyoandikwa katika vitabu vya historia za dini. Tofauti hizo za kikristo zimeleta umwagikaji damu wa kufehedhesha kusikokuwa na mfano katika historia ya binadamu.

Tofauti ya mayahudi na manaswara (wakristo) hazikutokana na kutojua uhakika. mayahudi walijua kuwa kuna ufufuo; kama ambavyo wakristo walijua kuwa Isa ni mja miongoni mwa waja wa Mungu, lakini walihitalifiana kwa kutaka ukubwa katika dunia kwa uhasidi na ufisadi.

Vikundi Sabini Na Tatu:

Imetangaa kwamba Mtume (s.a.w.) amesema: "Mayahudi wamegawanyika vikundi sabini na moja, Wakristo vikundi sabini na mbili na umma wangu utagawanyika vikundi sabini na tatu."

Maneno yamekua mengi sana kuhusu Hadith hiyo: Kuna mwenye kusema kuwa ni dhaifu, mwengine anasema hiyo ni Hadith iliyopokewa na mtu mmoja ambayo sio hoja katika maudhui.
Watatu naye anasema kuwa neno "Vikundi vyote vitaingia motoni" ni katika vitimbi vya walahidi kwa kuwatia doa waislamu. Ama wanne amesema kwa tamko hili: "Vikundi vyote vitakuwa katika pepo isipokuwa wazandiki."

Sisi tuna mashaka na Hadith hii, kwa sababu asili ni kuacha kuchukua lolote linalonasi- bishiwa Mtume (s.a.w.) mpaka ithibiti kinyume (ukweli). Lakini kama tukihiyarishwa kati ya kukubali kwa "vyote vitakuwa motoni" na vyote vitakuwa peponi." Tutachagua peponi kutokana na sababu mbili:

Kwanza: Hiyo ndiyo iliyo karibu zaidi na rehema ya Mwenyezi Mungu.
Pili: Kimsingi ni kwamba vikundi vya kiislamu vinavyotofautiana katika misingi (asili) havifiki sabini na tatu, kutofautiana katika matawi, hakupelekei kuingia motoni. Kwa sababu makosa kwenye matawi yanasamehewa yakiwa yametokea pamoja na kujichunga na baada ya kujitahidi.

Ni umbali ulioje kati ya Hadith hii inayonasibishwa kwa Mtume (s.a.w.w.) na kauli ya Ibn Arabi katika kitabu Futuhat: "Haadhibiwi yeyote katika umma wa Muhammad (s.a.w.) kwa baraka za Ahlu bait …"

"Na kama wakikuhoji, basi sema: Nimeusalimisha uso wangu kumwelekea Mwenyezi Mungu na walionifuata"

Mara nyingi mwanachuoni wa haki hupambana na mbishi mwenye batili. Wala hakuna dawa ya huyu isipokuwa kuachana naye. Na, yeyote mwenye kuhasimiana na mshari mwenye vurugu anakuwa mshirika wake katika dhambi.

Imam Ali (a.s.) anasema: "Mwenye kubisha sana hupata dhambi. "Kwa ajili hii, Mwenyezi Mungu amemwamrisha Mtume wake Mtukufu kuachana na wabatilifu, walio wapinzani, kwani hakuna ziada ya ubainifu na hoja. "Hakika ni juu yako kufikisha tu, na ni juu yetu hisabu." (13:40)

Na waambie wale waliopewa kitabu yaani mayahudi na manaswara na wale wasio na kisomo yaani washirikina katika waarabu. Mwenyezi Mungu amewanasibisha na neno wasio na kisomo kwa sababu wengi wao hawakujua kusoma na kuandika. Je mmesilimu? Baada ya kuwajia hoja. Kama wakisilimu basi wameongoka kwani hakuna kitu chochote zaidi ya uislamu, isipokuwa kufuru tu na upotevu. Na kama wakikengeuka basi juu yako ni kufikisha tu na kufikisha ndio mwisho wa kazi ya utume, kwani huko ndiko kunakotimiza hoja. Na Mwenyezi Mungu anawaona waja wote anawatendea wanayostahiki.

Faida tunazozipata kutokana na Aya hii ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemchagua Muhammad (s.a.w.) kuwa Mjumbe Wake na kwamba Yeye Mwenyezi Mungu amemwekea njia ya kuufikisha ujumbe huo ambao ni kutoa mwito kwa hoja na dalili; pamoja na kuidhibiti nafsi na kujiepusha na uhasama wa ubishani.

Kwa njia hii ya hekima hoja inatimia kwa mhalifu, mpinzani na asibakiwe na udhuru wowote au popote pa kukimbilia.

Wafuasi bora zaidi wa Mtume kwenye njia yake, ni watu wa elimu wanaojua dini yake na sharia yake; wenye kulingania kushika mafunzo yake na mwenendo wake.

إِنَّ الَّذِينَ يَكْفُرُونَ بِآيَاتِ اللَّهِ وَيَقْتُلُونَ النَّبِيِّينَ بِغَيْرِ حَقٍّ وَيَقْتُلُونَ الَّذِينَ يَأْمُرُونَ بِالْقِسْطِ مِنَ النَّاسِ فَبَشِّرْهُمْ بِعَذَابٍ أَلِيمٍ {21}

Hakika wale ambao wanazikanusha Aya za Mwenyezi Mungu na wakawauwa manabii pasipo haki na wakawaua wanaoamrisha mambo ya haki, wabashirie adhabu iumizayo.

أُولَٰئِكَ الَّذِينَ حَبِطَتْ أَعْمَالُهُمْ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَمَا لَهُمْ مِنْ نَاصِرِينَ {22}

Hao ndio ambao vitendo vyao vimeharibika katika dunia na akhera wala hawana wa kuwanusuru.