read

Aya 21-22: Wanaowaua Mitume

Maana

Hakika wale ambao wanazikanusha Aya za Mwenyezi Mungu na wakawauwa manabii pasipo haki na wakawauwa wanaoamrisha mambo ya haki, wabashirie adhabu iumizayo.

Unaweza kuuliza sharia zote za Mwenyezi Mungu na za watu zinaharamisha kuua, bali watu wote wanamuona muuaji ni mkosa, hasa ikiwa aliyeuwawa ni katika watu wema. Kwa hiyo basi kuelezea kuwa muuaji ni mwenye makosa anayestahili adhabu, ni kama kufafanua kilichofafanuka, na hali tunajua kuwa maneno ya Mwenyezi Mungu yako katika mpangilio mzuri?

Jibu: Makusudio hapa ni mayahudi na wakristo waliokuwako wakati wa Mtume (s.a.w.) na wakakataa uislamu. Aya imeonyesha kuwa si jambo geni kwao kukataa na kuwa na inadi na uislamu. Kwa sababu mayahudi waliotangulia waliwaua manabii; kama vile Zakariya na manaswara waliotangulia waliwaua wale waliouonyesha wazi umoja wa Mungu na ubashiri wa Masih, kwa vile tu walikuwa wanaamrisha haki na uadilifu na kuutumia. Kwa hivyo Aya imo katika mfumo wa kukemea; kama ilivyo kuwa ni ya kuhofisha.

Swali la pili: Kuua hakukuwa kwa Ahlul-kitab waliokuwa wakati wa Muhammad (s.a.w.), sasa vipi wananasibishiwa wao pasipo haki?

Jibu: Tumekwishaeleza mara kadhaa kwamba waliokuja nyuma waliridhia yaliyofanywa na wa kale wao na mwenye kuridhia kitendo anakuwa mshirika. Mara nyingi anayoyafanya baba hutegemezewa mwana.

Swali la tatu: Kuwaua manabii hakukuwa haki kwa hali yoyote, sasa kuna faida gani kati- ka msemo huu?

Jibu: Ni kuonyesha kuwa fedheha ya kuwaua mitume si kwa sababu ya vyeo vyao na utukufu wao, bali ni fedheha isiyokuwa na udhuru wowote, na kwamba sio suala la watu au vikundi, bali ni suala zima la haki na ukosefu wa haki.

Hao ndio ambao vitendo vyao vimeharibika katika dunia na akhera

Kuharibika duniani ni kwamba wao wanalaaniwa na kila mtu, kutokana na athari zao mbaya walizoziacha. Ama huko akhera wanangojwa na adhabu.

Kuamrisha Mema Na Kukataza Mabaya

Mafakihi wametaja sharti za kuamrisha mema na kukataza mabaya, kama vile kutohofia mwamrishaji madhara ya nafsi yake, watu wake na mali yake. Lakini baadhi ya mafakihi wamelipinga sharti hili na kuwajibisha kuamrisha mema japo kutapelekea kifo; na wametoa dalili kwa Aya hii. Hoja yao ni kuwa mitume wameamrisha mema na kukataza mabaya, wakauliwa katika njia hii. Kwa ushahidi wa Qur'an tukufu.

Tunavyoona sisi ni kwamba mitume katika tabligh walikuwa wana jambo ambalo wanavyuoni hawana. Wao walikuwa wakiongozwa na wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.); kama wakiuwawa katika njia ya tabligh, watakuwa wameuwawa wakiwa wanatekeleza amri ya Mwenyezi Mungu. Ama wanavyuoni, wanategemea yale waliyoyafahamu katika hukumu. Tunavyofahamu sisi kutokana na dalili hizi ni kwamba mtu yeyote inafaa kwake kunyamaza kwenye mambo mabaya ikiwa hakuna faida ya kidini na tena kuna madhara.

Ama ikiwa dhana yake imeelemea kuwa kutapatikana manufaa ya kidini kwa kuamrisha mema na kukataza mabaya, lakini kuna madhara, basi hapo itakuwa ni wajibu kuamrisha. Kwa hiyo lililopo ni kulinganisha kati ya kukinga nafsi na manufaa ya kuamrisha na kukataza.
Ikiwa manufaa ya dini ndiyo muhimu; kama vile kuumaliza ukafiri, dhulma na ufisadi. Basi hapa itafaa kuyakubali madhara, na huenda ikawa wajibu. Na, ikiwa kujikinga na madhara ni muhimu zaidi kuliko kukataza mabaya; kama kukataza kula najisi, basi hapo itafaa kujikinga na huenda ikawa ni wajibu, kwa hivyo basi suala litakuwa linatofautiana kwa kutafautiana hali.

Na, inatubainikia kwamba kuwalinganisha wasiokuwa Manabii katika suala hili la Manabii ni kuwalinganisha na kitu kilicho tofauti. Tutalirudia suala hili pale litakaponasibika.

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ أُوتُوا نَصِيبًا مِنَ الْكِتَابِ يُدْعَوْنَ إِلَىٰ كِتَابِ اللَّهِ لِيَحْكُمَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ يَتَوَلَّىٰ فَرِيقٌ مِنْهُمْ وَهُمْ مُعْرِضُونَ {23}

Je, huwaoni wale waliopewa sehemu ya Kitabu, wanaitwa kwenye Kitabu cha Mwenyezi Mungu ili kiwahukumu baina yao, kisha baadhi yao wanageuka wanakikataa.

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَالُوا لَنْ تَمَسَّنَا النَّارُ إِلَّا أَيَّامًا مَعْدُودَاتٍ ۖ وَغَرَّهُمْ فِي دِينِهِمْ مَا كَانُوا يَفْتَرُونَ {24}

Hayo ni kwa sababu walisema:Hautatugusa moto isipokuwa kwa siku chache tu, na yakawadanganya katika dini yao yale waliyokuwa wakiyazua.

فَكَيْفَ إِذَا جَمَعْنَاهُمْ لِيَوْمٍ لَا رَيْبَ فِيهِ وَوُفِّيَتْ كُلُّ نَفْسٍ مَا كَسَبَتْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ {25}

Basi itakuwaje tutakapowakusanya siku ambayo hapana shaka kuja kwake na itakapolipwa kila nafsi kwa ukamilifu kile ilichokichuma na wao hawataodhulumiwa.