read

Aya 253: Kuwafadhilisha Mitume

Maana

Mitume hao tumewafadhilisha baadhi yao zaidi kuliko wengine.

Mwenyezi Mungu alimwambia Mtume Wake Muhammad (s.a.w.) katika mwisho wa Aya iliyotangulia; "Na hakika wewe ni miongoni mwa Mitume," Halafu akafuatisha moja kwa moja na kauli Yake hii: "Mitume hao ..." Kwa hivyo basi, makusudio yanakuwa ni mitume wote ambao miongoni mwao ni Muhammad, sio kundi maalum, kama walivyosema wafasiri wengi.

Mitume wote ni sawa katika asili ya utume kuchaguliwa kwao na katika kufikisha ujumbe, wa Mwenyezi Mungu na kuongoza viumbe Vyake, lakini wanatofautiana katika mambo fulani. Yaani baadhi ya mitume wamekuwa mashuhuri kwa baadhi ya mambo fulani waliyohusika nayo, ambayo wengine hawakuwa nayo, ambayo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewasifu nayo katika Kitabu chake.

Kwa mfano Ibrahim alikuwa mashuhuri kwa kuitwa rafiki wa Mwenyezi Mungu (Khalilullah) kutokana na kauli Yake Mwenyezi Mungu: "….Na Mwenyezi Mungu amemfanya Ibrahim kuwa ni rafiki," (4:125).

Musa naye akawa mashuhuri kwa jina la aliyesema na Mwenyezi Mungu (Kalimullah) kutokana na kauli Yake Mwenyezi Mungu: "... Na Mwenyezi Mungu akasema na Musa maneno." (4:164)

Isa naye akawa mashuhuri kwa, roho wa Mwenyezi Mungu (Ruhullah); kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Hakika Masihi Isa bin Maryam ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na neno lake alilompelekea Maryam. Na ni roho iliyotoka kwake ... " (4:171)

Muhammad naye akawa mashuhuri kwa, mwisho wa Mitume (khatamun nabiyyina) kwa kauli Yake Mwenyezi Mungu: "Na Mtume wa Mwenyezi Mungu na mwisho wa Mitume ..." (33: 40)

Mwenyezi Mungu ametaja baadhi ya Mitume waliofadhilishwa au baadhi ya yanayohusika nao, kwa kauli Yake:

Miongoni mwao yuko ambaye Mwenyezi Mungu alisema naye.

Huyu ni Musa bin Imran kama walivyoafikiana wafasiri

Na wengine akawapandisha vyeo .

Mwenye Tafsiri ya Al Manar amesema: "Wafasiri wamesema huyo ni Mtume wetu ..." Na amesema Razi: "Umekubaliana umma wote kwamba Muhammad ni bora ya Mitume," Ametoa dalili 19 juu ya hilo kwa dalili, Miongoni mwa dalili hizo ni kwamba Ali bin Abu Twalib siku moja alitokeza kwa mbali, Mtume akasema: "Huyu ni bwana wa Waarabu."Aisha akasema: "Siye wewe bwana wa Waarabu? "Mtume akasema: "Mimi ni bwana wa walimwengu na yeye ni bwana wa Waarabu."

Dalili bora zaidi juu ya ubora wa Mtume kwa Mitume wote na watu wema wote ni sharia yake ilivyo na ukunjufu katika utukufu wake na utu wake. 1

Na tukampa Isa mwana wa Maryam dalili zilizo wazi na tukamtia nguvu kwa roho takatifu.

Dalili zilizowazi hapa ni dalili ambazo zinadhihirisha haki; kama kufufua wafu, kuponyesha wagonjwa, kuumba ndege, n.k. Makusudio ya roho takatifu ni roho njema yenye kutakaswa. Imekwishapita tafsiri ya roho katika Aya ya 87 ya Sura hii.

Na kama Mwenyezi Mungu angelitaka wasingelipigana wale waliokuwa baada yao.

Yaani baada ya Mitume kuwajia na hoja zilizowazi na kuzifafanua haki kwa dalili, basi watu wao walihitalifiana baada yao.

Kuna katika wao walioamini na wengine katika wao waliokufuru.

Unaweza kuuliza: Kauli Yake Mwenyezi Mungu: "Na kama Mwenyezi Mungu angelitaka wasingelipigana. Si inafahamisha kwamba binadamu ni mwenye kuendeshwa hana hiyari na kwamba kukaririka jumla hii ni kutilia mkazo kunasibika kupigana na matakwa ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.)?

Jibu: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amempa uwezo mja na akambainishia heri na shari na kumkataza hili na kumwamrisha lile. Mwenyezi Mungu anasema: "Na shikamaneni na kamba ya Mwenyezi Mungu nyote wala msiachane..." (3:103)

Mtu akifuata njia ya mshika- mano na kupendana, atakuwa yeye mwenyewe ndiye anayenasibika na huko kufuata, kwa sababu kumetokana na yeye na kwa hiyari yake iliyomfanya aone bora njia hiyo kuliko njia ya kutoelewana; wakati huo huo huko kufuata njia hiyo ya mshikamano kunafaa kunasibishwe kwa Mwenyezi Mungu, kwa sababu Mwenyezi Mungu ndiye aliyemwezesha kuifuata na ndiye aliyemwamrisha kuifuata.

Ama akifuata njia ya chuki na uhasama, basi njia hiyo itanasibika na mtu pekee wala haina- sibiki na Mwenyezi Mungu, kwa sababu mtu ameifuata kwa radhi yake na akaiona ni bora kuliko njia ya maafikiano; wala haifai kuinasibisha kwa Mwenyezi Mungu, kwa sababu Mwenyezi Mungu amemkataza.

Unaweza kuuliza tena: Kwa nini Mwenyezi Mungu amemwezesha mtu kuifanya shari ambapo ilikuwa inatakikana ampe hima ya kuaacha na kufanya heri tu?

Jibu: Lau Mwenyezi Mungu angelifanya hivi, binadamu asingebakiwa na fadhila yoyote wala vitendo visingekuwa na sifa ya heri na shari au vizuri na vibaya. Kwa sababu sifa hizi zinafungamana na matakwa ya mtu na hiyari yake.

Bali lau Mwenyezi Mungu angelimfanya mtu kufanya kitu fulani tu, kusingelikuwako na tofauti ya mtu na mawe au tofauti na unyoya ulio katika mavumo ya pepo. Kwa ajili hii na kwa ajili ya kudumu mtu na utu wake, hakutaka Mwenyezi Mungu kuwalazimisha watu kwenye kitu fulani

"Na kama angelitaka wasingelipigana."

Kwa ufupi kupigana ambako kumepatikana kati ya watu sio kama kumekhalifu matakwa ya Mwenyezi Mungu yanayoitwa Kun fa yakun.
Isipokuwa kumekhalifu matakwa ya Mwenyezi Mungu ya sharia yake, ambayo ni ubainifu na uongozi; na hekima yake imetaka kumpa mtu uwezo wa kutosha wa kufanya heri na shari, ili ajichagulie yeye mwenyewe uongozi na heri na awe ni mtu anayetofautiana na mawe na wanyama.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَنْفِقُوا مِمَّا رَزَقْنَاكُمْ مِنْ قَبْلِ أَنْ يَأْتِيَ يَوْمٌ لَا بَيْعٌ فِيهِ وَلَا خُلَّةٌ وَلَا شَفَاعَةٌ ۗ وَالْكَافِرُونَ هُمُ الظَّالِمُونَ {254}

Enyi mlioamini! Toeni katika vile tulivyowapa. Kabla haijafika siku ambayo hapatakuwa na biashara wala urafiki wala uombezi. Na makafiri ndio madhalimu.
  • 1. Wamesema sana kuhusu sababu za kuzorota kwa Waislamu na udhaifu wao katika nafsi zao; wametunga vitabu vingi kuhusu hilo na wakatoa sababu nyingi sana. Sisi tunaona sababu ya kwanza na ya mwisho ni kupuuzwa sharia ya Kiislamu kwa kinadharia na kimatendo. Na ukoloni ulitambua hakika hii, kwa hivyo kazi walioifanya tangu walipokanyaga miji ya Waislamu ni kuiondoa sharia ya Kiislamu kwenye mashule na mahakama, na badala yake wakaweka sharia za kutungwa. Kwa hiyo wakawaweka mbali Waislamu na dini yao. Qur'an yao na Sunna ya Mtume wao, tutalifafanua hilo kila itakapohitajika.