read

Aya 254: Kutoa

Maana

Mwenyezi Mungu amehimiza kutoa mali kwa mifumo mbali mbali. Yameshatangulia maelezo katika tafsiri ya Aya 245; na unakuja tena mfano wake katika Aya hii:

Enyi mlioamini! Toeni katika vile tulivyowapa.

Mwenyezi Mungu anahimiza kutoa pamoja na kuashiria kwamba mali iliyo na watu ni mali Yake aliyoitoa Yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t.); na kwamba kesho fursa itakosekana, kwa hivyo ni juu ya mumin mwenye akili kuchukua fursa kabla ya kupitwa na wakati.

Kabla haijafika siku ambayo hapatakuwa na biashara wala urafiki wala uombezi.

Makusudio ya biashara hapa ni kulipa fidia ili kujikomboa na moto kwa mali; urafiki ni urafiki wa kusameheana na uombezi na kuombewa na mtu mwingine kuepukana na moto.

Maana yake ni kwamba kesho mtu atakuja peke yake hana chochote isipokuwa amali njema. Aya hii ina maana sawa na Aya ya 48 ya Sura hii. Tumeuzungumzia uombezi katika Aya hiyo.

Na makafiri ndio madhalimu.

Wamejidhulumu wenyewe kwa kuacha amali njema ambayo inawaokoa na adhabu. Kwa ujumla ni kuwa neno dhulma na ukafiri yanakuja katika matumizi ya maana mamoja. Mara nyingine hutumiwa ukafiri katika dhulma, kama alivyosema Mwenyezi Mungu (s.w.t.): "... Hakika ushirikina ni dhulma kubwa." (31:13)Na mara nyingine hutumiwa dhulma katika ukafiri, kama alivyosema Mwenyezi Mungu (s.w.t.): "...Lakini madhalimu wanakanusha ishara za Mwenyezi Mungu..." (6:33)

اللَّهُ لَا إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ ۚ لَا تَأْخُذُهُ سِنَةٌ وَلَا نَوْمٌ ۚ لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۗ مَنْ ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِنْدَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ ۚ يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ ۖ وَلَا يُحِيطُونَ بِشَيْءٍ مِنْ عِلْمِهِ إِلَّا بِمَا شَاءَ ۚ وَسِعَ كُرْسِيُّهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ ۖ وَلَا يَئُودُهُ حِفْظُهُمَا ۚ وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ {255}

Mwenyezi Mungu hakuna mola ila Yeye Aliye hai msimamizi wa kila kitu. Hakumshiki kusinzia wala kulala. Ni Vyake vilivyomo ardhini na vilivyomo mbinguni. Na ni nani huyo awezaye kuombea mbele Yake bila ya idhini Yake. Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao; wala wao hawalijui lolote lililo katika elimu Yake ila kwa alitakalo. Elimu Yake imeenea mbingu na ardhi. Wala hakumshindi kuzilinda.
Na Yeye ndiye Mtukufu aliye Mkuu.