read

Aya 255: Aya Ya Kursiy

Maana

Mwenyezi Mungu hakuna mola ila yeye aliye hai, Msimamizi wa kila kitu.
Mwanafalsafa mashuhuri wa elimu inayohusika na mambo ya Mungu, aitwaye Mulla Sadra anasema: Neno Allah (Mwenyezi Mungu) linafahamisha kupwekeka dhati Yake Mwenyezi Mungu na sifa Zake. Kufahamisha juu ya kupwekeka katika dhati, ni kwamba jina hili tukufu haliitiwi mtu mwingine kiuhakika wala majazi. Mwenyezi Mungu anasema: "... Basi mwabudu Yeye tu na udumu katika ibada Yake. Je, unamjua (mwingine) mwenye jina lake?" (19:65)

Ama kufahamisha kupwekeka Kwake katika sifa, ni kwamba jina hili linafahamisha juu ya dhati yenye kukusanya kila sifa za ukamilifu na utukufu, kinyume cha majina mengine kama; Mjuzi, Mweza na Muumbaji, ambayo umoja wake haufahamishi isipokuwa umoja wa maana katika elimu, au uweza au utendaji.

Unaweza kuuliza: Hakika sifa za ukamilifu na utukufu ni nyingi na zenye kubadilika kulingana na kueleweka kwake; vipi ifae kusema zimepwekeka na tunaziona zinahisabika na kubadilika?

Jibu: Ukisema huyu ni mtu mjuzi yataeleweka mambo mawili - Sifa na Mwenye kusifiwa; na vyote ni vitu tofauti. Mtu sio ujuzi na ujuzi sio mtu. Hayo ni kwa upande wa kiumbe. Ama kwa upande wa Muumbaji hakuna jingine isipokuwa kuweko kiutukufu; na huko kuweko ndiko ujuzi ndiko uwezo, na ndiko hekima, n.k. Hakuna sifa na mwenye kusifiwa vyote ni vimoja tu; na huku hakukufanana na kitu kingine.

Hakuna mola ila Yeye

Inasemekana maana yake ni hakuna anayepasa kuabudiwa kwa haki isipokuwa Yeye. Lakini kueleweka kwake ni hakuna yoyote mwenye kukusanya sifa za uungu isipokuwa Yeye. Vyovyote iwavyo, maana zote mbili ni zenye kulazimiana.

Aliye hai Msimamizi wa kila jambo

Ukiunasibisha uhai kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, maana yake yanakuwa ni kukua, kuhisi na utambuzi. Lakini ukiunasibisha kwa Mwenyezi Mungu unakuwa ni elimu na uweza.

Makusudio ya kusimamia kila kitu ni kukisimamia katika mambo yake na kukipangilia vizuri. Mwenyezi Mungu anasema: "Akasema: Mola wetu ni Yule aliyekipa kila kitu umbo lake kisha akaongoza." (20:50) Na amesema tena: "....Na ameumba kila kitu akakikadiria kipimo (chake)." (25:2)

Mulla Sadra anasema: Kauli ya Aliye Hai inafahamisha kwamba Yeye ni Mjuzi na Muweza. Na kauli ya Msimamizi wa kila kitu inafahamisha kuwa Yeye ni Mwenye kujisimamia Mwenyewe na kumsimamia mwingine. Kwa hiyo sifa mbili hizi ni zenye kuafikiana katika maana na ni zenye kuingiliana."

Anakusudia kuwa usimamizi hauepukani na uhai; kama vile ambavyo uhai kwa maana ya uwezo na elimu hauepukani na usimamizi.

Mwenyezi Mungu Na Desturi Ya Maumbile

Unaweza kuuliza: Je maana ya kusimamia Mungu juu ya mipango ya vitu vyote, ni kwamba mambo yote ya dhahiri ya kimaumbile mpaka mafungu yake yanasimamiwa na Mwenyezi Mungu moja kwa moja Yeye Mwenyewe bila ya kuweko kati sababu yoyote ya kimaada; kama inavyodhihiri katika Aya isemayo: "Kisha tukamfanya tone la manii, katika makao madhubuti . Kisha tukaliumba tone hilo kuwa pande la damu, na tukaliumba pande la damu kuwa pande la nyama, kisha tukaliumba pande la nyama kuwa mifupa na mifupa tukaivika nyama, kisha tukalifanya umbo jengine. Basi ametukuka Mwenyezi Mungu mbora wa waumbaji." (23:13-14)

Kwa sababu yenye kuja haraka fahamuni katika Aya hii, ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameingilia Yeye Mwenyewe moja kwa moja kwenye makuzi mbali mbali ya tone la manii; na tunajua kuwa nadharia ya kielimu inasema kuwa tone la manii linakuwa na kuzidi kulingana na kanuni maalum?
Katika kujibu hayo, hapana budi kupambanua kati ya jambo lisilokuwa la kawaida, kama vile kufufua wafu na kupatisha kitu bila ya kitu kingine, na matukio yanayo kuwa kulingana na kanuni za kimaumbile, kama kupatwa jua mwezi, n.k. Hili la aina ya kwanza linategemezwa kwake Mwenyezi Mungu moja kwa moja.

Na hili la aina ya pili linategemea desturi ya maumbile na linategemezwa kwa Mwenyezi Mungu, kwa sababu Yeye ndiye aliyeweka desturi ya maumbile pamoja na vilivyomo ndani yake vikiwa ni pamoja na nguvu na viasili. Viasili hivi kwa kupitia njia zake vinafanya dhahiri za maumbile zikiwa ni pamoja na tone la manii. "...Na ameumba kila kitu akakikadiria kipimo (chake)."(25:2)

Yaani anakipitisha katika desturi na kanuni za kitabia. Lau angelikuwa Yeye Mwenyezi Mungu ndiye anayesimamia umbile moja kwa moja bila ya kuweko kati kitu kingine, kusingelikuweko na sababu na msababishaji.

Kwa hivyo basi, inatubainikia kuwa kila mwenye kuamini kwamba kila tukio la kimaumbile linategemea Mwenyezi Mungu moja kwa moja bila ya kuweko kati sababu yoyote yenye kuhisiwa ambayo imegunduliwa na utaalamu au inaweza kugunduliwa, mtu huyo atakuwa mjinga mwenye kukosea katika imani yake.

Na lau ingelikuwa sahihi imani yake hii, kusin- gelikuweko na wajibu wa kitendo chochote na elimu isingelikuwa na faida yoyote; wala uvumbuzi na maendeleo ya mtu yasingekuwa na athari yoyote.

Vile vile amekosa yule mwenye kuitakidi kwamba maumbile ndio kila kitu, kuwa ndiyo sababu ya kwanza na ya mwisho, wala hakuna kitu nyuma yake. Hayo ni makosa. Kwani kama ni hivyo kusingelikuwa na nidhamu wala athari yake na kungelikuwa na migongano na natija ingelikuwa kutokuwepo elimu wala uhai.

Haya tumeyafafanua zaidi katika Aya ya 21 ya Sura hii, kifungu cha Tawhid.

Hakumshiki kusinzia wala kulala.

Mwenyezi Mungu alipobainisha kwamba Yeye ni Hai Msimamizi wa kila jambo, ameendelea kulitilia mkazo hilo kwamba Yeye ni Mwenye kutukuka, haumzuwii usingizi wala kusahau au kitu chochote, katika kupanga kuumba Kwake kwa njia ya ukamilifu. Kwa sababu hilo linapingana na ukubwa Wake na kujitosha Kwake na kila kitu. Imam Ali amesema akimwambia Mola wake: "Sisi hatujui kiasi cha ukubwa wako, isipokuwa tunajua kuwa Wewe ni Aliye Hai wa Milele, Msimamizi wa kila jambo, hakukushiki kusinzia wala kulala; hutazamwi; wala halikuoni jicho, lakini Wewe unaliona; umezithibiti amali na ukazishika barabara."

Ni vyake vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini Makusudio ya vilivyomo ni ulimwengu wote na kila kilichomo ndani yake hakitoki nje ya ufalme Wake na mipangilio Yake. Imam Ali (a.s.) aliulizwa kuhusu: "Hapana hila wala nguvu isipokuwa kwa msaada wa Mwenyezi Mungu."

Akajibu: "Sisi hatumiliki chochote mbele ya Mwenyezi Mungu, wala hatumiliki isipokuwa kile tulichomilikishwa; na anapomilikisha kile ambacho amekimiliki zaidi kuliko sisi, basi ametukalifisha nacho; na anapokiondoa, huwa ametuondolea taklifa."

Na ni nani huyo awezaye kuombea mbele Yake bila ya idhini Yake.

Umekuja mfumo wa swali kwa maana ya kukanusha; yaani hataombea yeyeote mbele Yake isipokuwa kwa amri Yake na hayo ni jibu na kubatilisha kauli ya washirikina kwamba masanamu ndiyo yanayowakurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anawasimulia hao kwa kusema: "...
Na wanasema: hao ndio waombezi wetu mbele ya Mwenyezi Mungu! Sema: 'Je, mnamwambia Mwenyezi Mungu asiyoyajua katika mbingu wala katika ardhi? ..." (10: 18)

Tumekwisha zungumzia uombezi katika Aya ya 48. Baadhi ya ulama wamesema kwamba siku ya Kiyama kutakuwa na aina mbalimbali za watu.
Kama ifuatavyo:- Waliotangulia ambao ni wenye kukurubishwa; watakaokuwa upande wa kuume ambao ni watu wema watakaookoka, watakaokuwa upande wa kushoto ambao ni waovu watakao adhibiwa, na watakaokuwa na msamaha ambao amali zao njema zimechanganyika na maovu.

Na hawa watakubaliwa kuombewa; kama alivyosema Mwenyezi Mungu: " Na wengine walikiri dhambi zao, wakachanganya vitendo vyema na vingine viovu, huenda Mwenyezi Mungu akapokea toba yao. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kusamehe Mwenye kurehemu." (9:102)

Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao.

Maana yake ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.), anajua yaliyokuwa na yatakayokuwa katika waja wake, iwe heri au shari; na anamjua mwombezi na anayeombewa na anayestahiki msamaha na thawabu au adhabu na mateso. Ikiwa mambo yako hivyo, basi uombezi (shafaa) hauna nafasi yoyote isipokuwa kwa amri Yake Mwenyezi Mungu kwenye mipaka Yake anayoridhia.

Wala hawalijui lolote lililo katika elimu Yake ila kwa alitakalo.

Dhamiri katika hawalijui inawarudia waja wote wakiwemo Malaika na Mitume. Makusudio ya elimu ni linalojulikana. Maana yako wazi. Ukipenda kujua zaidi unaweza kuangalia Aya hizi:" Yeye ni mjuzi wa siri; wala hamdhihirishii yoyote siri Yake isipokuwa Mtume aliyem- ridhia ..." (72: 26-27)
"... Utakatifu niwako! Hatuna elimu isipokuwa ile uliyotufundisha ..." ( 2: 32)

Elimu Yake imeenea mbingu na ardhi.

Kauli zimekuwa nyingi na zimegongana kuhusu maana ya neno Kursiy. Baadhi ya kauli hizo ni za kumzungumzia Mwenyezi Mungu bila ya elimu, lakini bora ya kauli ni mbili: Ya kwanza, ni fumbo la utukufu Wake Mwenyezi Mungu na cheo chake yaani enzi. Ya pili, ni elimu; yaani elimu Yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.) imezunguka kila kitu. Mpangilio wa maneno unarudia maana haya.

Wala hakumshindi kuzilinda na Yeye Ndiye Mtukufu aliye Mkuu

Yaani hakumtii mashaka wala uzito wowote kuilinda mbingu na ardhi na kupangilia vizuri yaliyomo ndani yake. Vipi isiwe hivyo! Na hali kuumba nzi na kuumba ulimwengu Kwake ni sawa tu; maadamu Yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t.) "... Akitaka chochote ni kukiambia kuwa, kikawa." (36:82)

Kitu Bila Ya Kitu

Kutengeneza vitu kuko aina mbili: kutegeneza kitu kutokana na maada na kutengeneza bila ya maada. Na kunatofautiana kwa njia nyingi.

1. Anayetengeneza kwa maada anahitaji harakati na zana, lakini asiyetengeneza kwa maada hahitaji.

2. Wa maada anachoka, lakini asiyetumia maada hachoki.

3. Mwenye kutumia maada hawezi kupata kitu bila ya kitu kingine, lakini kwa asiyetumia, hilo sio jambo zito.

Kwa hivyo inabainika kwamba kumlinganisha Muumbaji na Mwenye kuumbwa ni kulinganisha na kisicholingana. Itawezekana vipi kumfananisha mwenye kujitosha na mwenye kuhitajia; atakuwaje sawa na mwenye kushindwa?

لَا إِكْرَاهَ فِي الدِّينِ ۖ قَدْ تَبَيَّنَ الرُّشْدُ مِنَ الْغَيِّ ۚ فَمَنْ يَكْفُرْ بِالطَّاغُوتِ وَيُؤْمِنْ بِاللَّهِ فَقَدِ اسْتَمْسَكَ بِالْعُرْوَةِ الْوُثْقَىٰ لَا انْفِصَامَ لَهَا ۗ وَاللَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ {256}

Hakuna kulazimisha katika dini; uongofu umekwisha pambanuka na upotofu. Basi anayemkataa taghuti na akamwamini Mwenyezi Mungu, hakika yeye ameshika kishiko madhubuti kisichovunjika. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mjuzi.

اللَّهُ وَلِيُّ الَّذِينَ آمَنُوا يُخْرِجُهُمْ مِنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ ۖ وَالَّذِينَ كَفَرُوا أَوْلِيَاؤُهُمُ الطَّاغُوتُ يُخْرِجُونَهُمْ مِنَ النُّورِ إِلَى الظُّلُمَاتِ ۗ أُولَٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ ۖ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ {257}

Mwenyezi Mungu ni mtawala wa wale walioamini; huwatoa gizani na kuwaingiza katika mwangaza, lakini walio kufuru watawala wao ni mataghuti. Huwatoa kwenye mwangaza, na kuwaingiza katika giza, hao ndio watu wa motoni, watadumu humo.