read

Aya 256-257: Hakuna Kulazimisha Katika Dini

Maana

Hakuna kulazimishwa katika dini

Lau tungeiangalia jumla hii peke yake, tungelifahamu kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakuweka hukumu yenye aina yoyote ya kulazimisha na kwamba anayolazimishwa mtu katika kauli au vitendo hayaambatani na kitu chochote katika mtazamo wa sharia, si katika dunia wala akhera.

Lakini kauli Yake Mwenyezi Mungu "Uongofu umekwisha pambanuka na upotofu", ambayo ndiyo sababu ya kuacha kulazimisha, inaonyesha kuwa neno katika, hapa lina maana ya juu ya; Yaani uislamu haumlazimishi yeyote kukubali isipokuwa unamlazimisha mpinzani kwa hoja na dalili tu; kama inavyosema Qur'an: "Na sema: (Huu) ni ukweli uliotoka kwa Mola wenu, basi anayetaka na aamini na anayetaka na akufuru ..." (18:29) "... Je, wewe utawashurutisha watu kwa nguvu wawe waumini? (10:99)

Unaweza kuuliza: Hakika dini haiwezekani kufungamana na kulazimishwa, kwa sababu dini ni katika mambo ya moyo yaliyo nje ya uwezo. Sawa na kuleta picha ya kitu akilini. Vinavyoweza kufungamana na kulazimishwa ni kauli na vitendo ambavyo inawezekana kutendeka bila ya matakwa ya msemaji na mtendaji. Kwa hivyo umepita njia gani mpaka ukasema habari ya kukataza kulazimishwa juu ya dini?

Jibu: Hakika kauli Yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.): "Hakuna kulazimishwa katika dini" Imekuja kwa tamko la kuelezea habari. Kama hivyo ndivyo, basi swali litakuwa halina msingi, kwa sababu maana yatakuwa dini ni itikadi na hilo ni jambo linalorudia kwenye kukubali ambako mtu halazimishwi kukubali.

Ikiwa tamko limekuja kwa kukusudiwa kukataza, basi maana yatakuwa ni: Enyi Waislamu msimlazimishe yeyote kusema "Lailaha illa Llahu Muhamadurasuli Llahi." baada ya kuwako hoja na dalili juu ya Tawhid na Utume.

Lakini jibu hili linaweza kuzalisha swali jipya kwamba hayo hayataafikiana na kauli ya Mtume (s.a.w.): "Nimeamrishwa nipigane na watu mpaka waseme: 'Laillahailla Ilah'; wakisema hivyo, basi damu zao na mali zao zimehifadhika na mimi."

Jibu: uislamu unaruhusu kupigana kwa sababu mbali mbali. Miongoni mwa sababu hizo ni: Kujikinga - Mwenyezi Mungu anasema: "Na piganeni katika njia ya Mwenyezi Mungu na wale wanaowapiga, wala msipituke mipaka." (2: 190). Kudhulumiwa - Mwenyezi Mungu anasema : "... Lipigeni (kundi) lile linaloonea (wenzao) mpaka lirudi katika amri ya Mwenyezi Mungu ..." (49:9)

Kupigana ili kuudhihirisha uislamu, ijapokuwa ni kwa ulimi. Hilo ni kwa ajili ya maslahi yanayowarudia wote, sio waislamu peke yao. Na maslahi haya anayakadiria aliye Masum au naibu wake; wala haifai kwa mwislamu yeyote, vyovyote alivyo, kupigana kwa ajili ya kutamkwa tamko la uislamu au kuueneza, isipokuwa kwa amri ya Masum au naibu wake, ambaye ni mujtahid1mwadilifu.

Ni kwa njia hii peke yake ndio inachukuliwa Hadith "Nimeamrishwa nipigane na watu ..."; Yaani mimi nitapigana nao nitakapoona mimi au kaimu wangu kwamba maslahi ya kiutu yanalazimisha kupigana kwa ajili ya 'Lailaha illa llah'.

Hapo inaonyesha kuwa kupigana kwa kujikinga au kuikinga dini na haki, hakungojei idhini ya yeyote. Tumekwisha yaeleza hayo katika tafsiri ya Aya ya 193 kifungu cha 'Uislamu unapiga vita dhulma na ufisadi.'

Uongofu umekwisha pambanuka na upotofu.

Makusudio ya uongofu hapa ni imani na upotofu ni ukafiri.

Mwenyezi Mungu amekwisha ibainisha haki kwa uwazi zaidi, na ubainifu na dalili zenye nguvu, mpaka kafiri akaishiwa na hoja au udhuru wowote. Mwenye kuijua njia ya haki na ya uongofu atakuwa amekwisha ijua njia ya upotofu na ya batili. Kwani hakuna kitu kingine baada ya haki isipokuwa upotofu.

Mulla Sadra anasema: Maana ya uongofu umekwisha pambanuka na upotofu ni kuitambua haki kutokana na batili na imani kutokana na ukafiri kwa dalili na hoja pamoja na kuzifahamu na kuziangalia vizuri. Yeyote mwenye kuikubali haki kwa kufuata tu, hana tofauti na mnyama. Hata hivyo mwenye kuwafuata watu wema kwa nia njema na kwa dhamiri nzuri atayapata yale watakayoyapata wao kesho.

Basi anayemkataa taghuti na akamwamini Mwenyezi Mungu, hakika yeye ameshika kishiko madhubuti kisichovunjika.

Kauli zimekuwa nyingi kuhusu tafsiri ya taghuti, baadhi ya wafasiri wamefikisha kauli tisa. Miongoni mwa hizo ni kuwa makusudio yake ni shetani. Nyingine ni dunia iliyo twevu. Iiliyo karibu na ufahamu na yenye kufahamisha kutokana na tamko lenyewe, ni kauli ya Sheikh Muhammad Abduh kwamba taghut ni yule ambaye kwa kumwabudu na kumwamini yeye, ndiyo sababu ya kupetuka mpaka na kutoka katika haki.

Makusudio ya kishiko madhubuti, ni kwenda kwenye njia iliyonyooka ambayo hapotei mwenye kuifuata. Maana kwa ujumla ni kwamba kumwamini Mwenyezi Mungu ni kishiko cha kutegemewa hakikatiki milele na kwamba mwenye kushikamana nacho hapotei.

Katika Sahih Muslim anasema: "Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: Hakika mimi ninaacha kwenu vitu ambavyo kama mkishikamana navyo hamtapotea baada yangu, kimojawapo ni kikubwa kuliko kingine, nacho ni kitabu cha Mwenyezi Mungu kamba yenye kuvutwa kutoka mbinguni hadi ardhini na kizazi changu Ahlul Bait wangu, vitu viwili hivyo havitaachana mpaka vije kwangu kwenye birika." Hadith hiyo pia imepokewa na Tirmidhyi. Lakini hivi sasa vitu vyote hivyo viwili vimeachwa. Ndio Imam Ali (a.s.) akasema: "Utakuja wakati Qur'an haitabaki isipokuwa maandishi yake na Uislamu utabaki jina lake tu."

Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mjuzi.

Anasikia tamko la Tawhid kutoka kwa waumini, na la kufuru kutoka kwa makafiri; na anajua yaliyo katika nyoyo za watu wawili na atamlipa kila mmoja kwa amali zake.

Mwenyezi Mungu ni mtawala wa wale walioamini; huwatoa gizani na kuwaingiza katika mwangaza.

Wafasiri wametofautiana sana katika Aya hii. Baadhi yao wakazalisha mushkeli wa kiitika- di; mpaka Mulla Sadra akasema: "Kuna mushkeli mkubwa ambao ni vigumu kuutatua kwa wenye fahamu." Sheikh Muhammad Abduh amesema: "Hakika baadhi ya tafsiri ni tafsiri za wafasiri wasiokuwa wataalamu ambao hawafahamu mifumo ya lugha ya hali ya juu, au ni tafsiri za wasiokuwa Waarabu ambao zaidi huwa hawafahamu."
Ama sababu ya kutofautiana wafasiri na kuzalisha matatizo ya kiitikadi ni kwamba wao wamefahamu Aya kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni mtawala na mwangalizi wa mambo ya waumini tu; na wala sio kwamba waumini wanamfanya Yeye tu kuwa ni mtawala na mwangalizi wa mambo yao. Hapo kuna tofauti kubwa kati ya maana hizi mbili.

Kuanzia hapa ndipo umekuja mushkeli katika wanavyofahamu wafasiri, kwamba utawala wa Mwenyezi Mungu na msaada Wake unakuwa kwa viumbe vyote katika nidhamu moja; na wala sio kwa waumini tu.

Vyovyote itakavyokuwa, kauli za wafasiri au wengi wao hazioani na mfumo, na kwamba maana yaliyo salama, ambayo hayana matatizo yoyote na yanayoafikiana na kauli Yake Mwenyezi Mungu, Basi anayemkataa taghuti na akamwamini Mwenyezi Mungu, hakika yeye ameshika kishiko madhubuti kisichovunjika ni kuwa waumini hawamfanyi mtawala asiyekuwa Mwenyezi Mungu wala hawamfanyi yeyote kuwa mlinzi wao isipokuwa Mungu pekee Yake; Kwake wanakimbilia, na kwa Kitabu Chake na sunna ya Mtume Wake wanaongoka katika itikadi zao, kauli zao na vitendo vyao.

Wala hawategemei watu wapotevu na mataghuti, hata wawe vipi. Kinyume chake ni makafiri ambao wanawafanya mataghuti ndio watawala wao.

Hapana mwenye shaka kwamba mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu na akaendelea kumtii na kuongoka kwa Aya Zake na ubainifu Wake kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu na msaada Wake atasalimika kutokana na giza la bid'a na upotevu, vilevile matamanio na ujinga. Na atapata mwanga kwa nuru ya maarifa ya kweli na imani sahihi. Hayo ndiyo maana ya Huwatoa gizani na kuwaingiza katika mwangaza.

Lakini waliokufuru, watawala wao ni mataghuti. Huwatoa kwenye mwangaza na kuwiangiza katika giza.

Maana kwa ujumla ni kuwa makafiri wanawafanya watu wapotevu na mataghuti kuwa watawala wao badala ya Mwenyezi Mungu; wanachukua amri zao na kuacha makatazo yao. Hawa wanakwenda katika njia ya kuhiliki na wanawatoa kwenye mwangaza wa akili na maumbile na kuwatia katika giza ukafiri na uzushi.

Kudumu Motoni

Watadumu humo.

Mara nyingi sana Qur'an imetaja kuwa kuna aina ya waasi watakaodumu motoni; na imebainisha kuwa miongoni mwa aina hii ni: Mwenye kumkufuru na akakadhibisha Aya zake. Mwenyezi Mungu anasema: "Na wale ambao wamekufuru na kukadhibisha ishara zetu, hao ndio watakoakuwa watu wa motoni, humo watadumu." (2:39)

Mwenye kumua mumini kwa makusudi, Mwenyezi Mungu anasema: "Na mwenye kumuua Muumin kwa kukusudia, basi malipo yake ni Jahannam, humo atadumu ..." (4:93)

Mwenye kumwasi Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na kuruka mipaka. Mwenyezi Mungu anasema: "Na anayemuasi Mwenyezi Mungu na Mtume, na kuiruka mipaka ya Mwenyezi Mungu, atamwingiza motoni, humo atadumu." (4:14)

Mwenye kuzungukwa na makosa yake; Mwenyezi Mungu anasema: "Ndio wanaochuma ubaya na makosa yao yakawazunguka, hao ndio watu wa motoni, humo watadumu." (2:81)

Hapana mwenye shaka kwamba kwa mujibu wa uadilifu Wake Mwenyezi Mungu, hamwadhibu isipokuwa mwenye kustahili adhabu na adhabu yake inatofautiana kwa ukali na udhaifu kulingana na makosa na maasi. Kosa la mwenye kuhangaika akieneza ufisadi duniani, akaangamiza mimea na viumbe, si sawa na kosa la mwenye kuiba shillingi moja au aliyem- sengenya anayeshindana naye katika kazi.

Pamoja na haya tunaweza kujiuliza kudumu katika moto kusikokuwa na mwisho, kugongwa kichwa kwa macheche yaliyo kama majumba, kuvurumishiwa marungu ya chuma mgongoni na kujazwa tumbo kwa maji ya usaha; kisha mtu asife akapumzika wala asipunguziwe angalau akapumua; mtu huyu ambaye anaumizwa na chawa na kufa kwa kusongwa koo na jasho humfanya anuke; kama alivosema Amirul Muminin Ali (a.s.).

Tujiulize je machungu yote haya makubwa kwa mnyonge huyu mwenye kushindwa na chawa, yanaafikiana na dhati ya Mwenyezi Mungu ambaye ni heri tupu na rehema, ukarimu, neema, upole na hisani?" Je inaingilika akilini mtu huyu kuadhibiwa milele au kunyimwa kabisa neema ... Au huko kuwa milele na kila ngozi inapoiva kubadilishwa ngozi nyingine bila ya kupumzika, yote hayo ni ya kujiuliza.

Akisema msemaji: Hakuna adhabu ambayo itazidi ya mwenye kumuua Hussein bin Ali (a.s.) au aliyetupa bomu la Atomic au Haidrojeni kwa watu na akawamaliza wote, au mwenye kuanzisha mambo mabaya, yakadumu na uovu wake ukazidi?

Jibu: Ni kweli kuwa hazidi yeyote katika uliowataja, lakini sio kila asi ni Yazidi wala sio kila bomu ni Atomic na Hadrojeni; wala sio kila desturi inawatawanya watu. Lakini swali halikuwa juu ya hawa, bali swali ni juu ya kudumu walio na daraja nyingine.

Unaweza kusema: Maelezo ya Qur'an na Hadith za Mtume juu ya kudumu milele utazifanyaje?

Jibu: Hakuna katika hizo inayokataa Taawil.

Ukisema tena kuwa, kila kilicho elezwa ikiwa kukielewa kunawezekana kwa dhahiri, basi ni wajibu kudumu juu ya dhahiri yake, kwa hiyo kudumu wakosaji katika moto si muhali.

Jibu: Ndio, lakini lichukuliwe la kudumu muda mrefu badala ya milele, kwa kukusanya kati ya Qur'an na dalili za rehema ambako, hakukataliki wala hakupingwi na sharia na akili.

Utasema mara ya tatu: Hakika mafaqihi hawawezi kuridhika na jawabu hili, kwa sababu wao hawaruhusu kuchukulia kinyume cha dhahiri ya tamko isipokuwa kwa sababu tatu: Kuunganisha na kitu kingine kwa kidesturi, kama vile kuchukulia mahsus kutoka katika jumla; au kisheria, kama kauli wazi yenye kuthibiti kutoka kwa Masum; au kiakili kusikokubali uwezekano wa kinyume, Na sisi hatuna chochote katika hivyo vitatu.

Jibu: Kwanza: Ninadhani kuwa mafaqihi waliozitambua dalili za rehema ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) wataafikiana nami, kwamba inawezekana kuziacha dhahiri za dalili za kudumu milele katika moto kwa baadhi ya wakosaji. Miongoni mwa dalili hizo ni Hadith Qudsi: "Rehema yangu imeshinda ghadhabu yangu." Vilevile Hadith tukufu inayosema: Hakika waombezi siku ya Kiyama ni wengi na mwisho wa waombezi ni mwenye kurehemu wenye kurehemu. Na kwamba rehema yake Mwenyezi Mungu itaenea siku ya Kiyama mpaka ibilisi atakuwa na tamaa na kunyoosha shingo yake.

Katika baadhi ya riwaya ni kwamba Hassan al Basri alisema: "Si ajabu kwa aliyeangamia, kuwa vipi ameangamia. Lakini ajabu ni ya mwenye kuokoka vipi ameokoka." Imam Zainul Abidin (a.s.) akasema: "Ama mimi ninasema; sio ajabu kwa aliyeokoka kuwa ameokoka vipi; isipokuwa ajabu ni kwa aliyeangamia kuwa ameangamia vipi pamoja na ukubwa wa rehema ya Mwenyezi Mungu!"

Tukiiunganisha riwaya hii na Aya inayosema: "Sema! Enyi waja wangu waliojidhulumu! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu; hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote ..." (39:53).
Tunapata ulinganisho mkataa wa kuacha dhahiri ya dalili za kudumu milele motoni.

Pili: Sisi tunazungumza mambo ya kiitikadi mkataa, sio masuala ya matawi ya kudhania; na mafaqihi pamoja na kujichunga kwao na nguvu ya imani zao, wanakuwa ni wataalamu wa hukumu za Mwenyezi Mungu za kisharia sio mambo ya itikadi. Bali wengi katika wao wako katika daraja ya kufuata yale yanayorudia sifa za Mwenyezi Mungu na vitendo Vyake.

Ama yale yanayorudia kwenye dalili za kuweko Muumbaji (s.w.t.) ni dalili za mzunguuko na kuendelea. Hata hivyo ni lazima ieleweke kuwa sisi tunaamini kuswihi kufuata katika misingi ya itikadi ikiafikana na mambo yalivyo.

Tatu: Akili huona vibaya kukhalifu ahadi, lakini sio kiaga. Ukimwambia mtu mwingine nitakufanyia wema; kisha uvunje ahadi, basi utakuwa mwenye kulaumiwa mbele za wenye akili. Ama ukamwambia unayemdai haki: Nitachukua haki yangu tu kutoka kwako kisha umsamehe, basi wewe utakuwa mwenye kusifiwa mbele ya Mwenyezi Mungu na watu; hasa akiwa yule unayemdai ni fukara na wewe ni tajiri. Na Mwenyezi Mungu ni tajiri kwa viumbe na adhabu zao. Na wao wana haja sana ya rehema Yake na msamaha Wake.

Swali la nne na la mwisho: Kwa nini unaleta taawil ya Aya za kudumu motoni na ni maana gani unayoyachukulia?

Jibu: Inawezekana kuchukulia maana ya kudumu muda mrefu, lakini sio milele; au kudumu motoni bila ya adhabu; kama hema la Hatimtai2au kuwepo Ibrahim katika moto.

Haya yanatiliwa nguvu na yaliyopokewa katika baadhi ya Hadith kwamba baadhi ya watu wa motoni watakuwa wanacheza na makaa ya moto kama mpira wakirushiana. Hapana mwenye shaka kwamba mchezo huu hauwezi kuwa pamoja na adhabu hata hafifu sikwambii kali yake.

Na Mungu si Mwenye kushindwa kuufanya moto baridi na salama kwa asiyekuwa Ibrahim kama alivyoufanya kwa Ibrahim (a.s.).

Muhhiddin Ibn al Arabi anasema katika al Futuhul Makkiyya J2 uk. 127: "Hatobaki motoni mwenye kumwamini Mungu mmoja katika waliopelekewa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.), kwa sababu moto utarudi kuwa baridi na salama kwa wanaompwekesha Mwenyezi Mungu kwa baraka za Ahlul Bait katika akhera. Ni utukufu ulioje wa baraka za Ahlul Bait!

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِي حَاجَّ إِبْرَاهِيمَ فِي رَبِّهِ أَنْ آتَاهُ اللَّهُ الْمُلْكَ إِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ رَبِّيَ الَّذِي يُحْيِي وَيُمِيتُ قَالَ أَنَا أُحْيِي وَأُمِيتُ ۖ قَالَ إِبْرَاهِيمُ فَإِنَّ اللَّهَ يَأْتِي بِالشَّمْسِ مِنَ الْمَشْرِقِ فَأْتِ بِهَا مِنَ الْمَغْرِبِ فَبُهِتَ الَّذِي كَفَرَ ۗ وَاللَّهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ {258}

Je, hukumjua aliyehojiana na Ibrahim juu ya Mola wake kwa sababu Mwenyezi Mungu alimpa ufalme ? Ibrahim aliposema: Mola wangu ni yule ambaye huhuisha na kufisha. Yeye akasema: Mimi pia na huhuisha na kufisha. Ibrahim akasema: Hakika Mwenyezi Mungu hulichomoza jua mashariki, basi wewe lichomoze magharibi. Akafedheheka yule aliyekufuru, na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu madhalimu.
  • 1. Mujtahid aliye marjaa: yaani kiongozi anayefuatwa katika madhehebu ya Shi'a katika zama za kughibu kwa Imam Mahdi (a.s)
  • 2. Katika baadhi ya riwaya ni kwamba Hatimtai ataingia motoni kwa sababu ya kufuru yake, lakini atakuwa na hema la kumkinga joto kwa sababu ya ukarimu wake. Huyu alikuwa ni mtu aliyepigiwa mfano kwa ukarimu wake wa kupindukia.